WIZARA YA KILIMO YAJA NA MWELEKEO MPYA

 

NA AMINA SAIDI,TANGA.

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imezitaka taasisi zote zilizo chini yake kuhakikisha wakulima nchini wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea pamoja na huduma za ugani kwa wakati, ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza na kudorora kwa uzalishaji wa mazao.

​Wito huo umetolewa  na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika mkoani Tanga, yakiwa yameratibiwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) pamoja na wadau wa maendeleo.

​Katika kutilia mkazo usimamizi wa sekta hiyo, Silinde amewaagiza maofisa ugani kote nchini kuanza kuwasilisha taarifa za kila wiki kuhusu mwenendo wa shughuli za kilimo katika maeneo yao, Hatua hiyo inalenga kuiwezesha wizara kufanya ufuatiliaji wa karibu na kuchukua hatua za haraka dhidi ya changamoto zitakazojitokeza kwa wakulima.

​ Naibu Waziri Silinde amewatoa hofu Watanzania akibainisha kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya chakula na kwamba Serikali inaendelea kununua mazao zaidi kutoka kwa wakulima kwa bei ya soko kulingana na maeneo husika.

​”Tuna akiba ya kutosha ya chakula na tutawafikia wananchi wenye uhitaji endapo kutatokea majanga,Hata hivyo, ni wajibu wa kila mwananchi na familia kuweka akiba ya chakula nyumbani,” alisisitiza Silinde.

​Aliongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatatumika kama jukwaa la kuelimisha umma kuhusu mbinu bora na sahihi za uhifadhi wa chakula, ili kujihakikishia usalama wa chakula hata wakati wa changamoto za hali ya hewa.

​Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano Serikalini kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Angela Shangali, amethibitisha kuwa wakala huo umejipanga kikamilifu kuhakikisha chakula kinapatikana nchini kote na kinawafikia wenye uhitaji bila kukwama.

​Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwesa, amewasihi wananchi kuhifadhi kwa umakini chakula walichovuna msimu huu, ili kuwa na akibai imara endapo mabadiliko ya tabianchi na mvua zitaathiri uzalishaji ujao.