Rais wa Paraguay Aondolewa Madarakani, Akamatwa kwa Tuhuma za Ufisadi

Rais wa Paraguay, Santiago Peña, anaripotiwa kuondolewa madarakani na kukamatwa baada ya Bunge la Seneti kupitisha azimio la kumwondoa katika nafasi hiyo kufuatia mgogoro mkubwa wa kifedha uliohusishwa na kuanguka kwa benki ya kidijitali ya Ueno Bank.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maseneta 44 kati ya 45 walipiga kura kumuondoa Peña madarakani, huku mbunge mmoja akiwa hayupo wakati wa upigaji kura.

Peña, ambaye hadi mwaka jana alikuwa na hisa katika kampuni iliyokuwa inamiliki benki hiyo, anakabiliwa na tuhuma za mgongano wa maslahi, kuingilia usimamizi wa sekta ya fedha, matumizi mabaya ya fedha na kuficha taarifa kuhusu mgogoro huo.

Hata hivyo, rais huyo amekanusha kuhusika na makosa yoyote.

Kuanguka kwa Ueno Bank kumeibua taharuki nchini humo, huku takribani wateja milioni tatu wakidaiwa kushindwa kupata akiba zao na fedha za pensheni baada ya Benki Kuu ya Paraguay kuichukua benki hiyo.

Hali hiyo imesababisha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo, hususan katika mji mkuu wa Asunción, huku wananchi wakitaka fedha zao kurejeshwa.

Baada ya kuondolewa kwa Peña, Makamu wa Rais Pedro Alliana aliapishwa kuwa rais wa mpito na kuahidi kuhakikisha wananchi walioathiriwa na mgogoro huo wanalipwa fidia.

Katika hotuba yake kwa taifa siku moja kabla ya kuondolewa madarakani, Peña aliomba radhi kwa wananchi akisema hakukusudia kusaliti imani waliokuwa wameweka kwake.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi wa Peña, Ricardo Preda, ameyataja mashtaka dhidi ya mteja wake kuwa ni ya kizembe na yenye nia za kisiasa.

Peña anatarajiwa kuhojiwa kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, ushawishi usio halali na ubadhirifu wa fedha.

Mgogoro huo sasa umeweka taifa hilo la Amerika Kusini katika kipindi cha sintofahamu ya kisiasa na kiuchumi, huku macho ya wananchi yakielekezwa kwa uongozi mpya na hatua zitakazochukuliwa kurejesha imani katika mfumo wa benki.