Na Matukio daima App Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa juhudi za kusambaza umeme vijijini, akisema hatua hiyo imekuwa chachu ya ukuaji wa viwanda na kuinua uchumi wa wananchi.
Nyongo ametoa pongezi hizo leo Novemba 6, 2026, Wilayani Mafia, wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka kati ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG) na REA, uliolenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya wakala huo katika kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza katika mkutano huo, Nyongo amesema Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa inayokua kwa kasi katika sekta ya viwanda, huku uwekezaji wa viwanda ukizidi kuelekezwa hadi maeneo ya vijijini, hali inayoongeza umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa uhakika.
“Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa Maendeleo, ni Mkoa wa viwanda. Viwanda sasa hivi vinajengwa vijijini. Vijijini wanahitaji umeme. Juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekea Dira ya 2050 pamoja na juhudi za Wabia wa Maendeleo kwa pamoja tumeweza kupeleka maendeleo ya umeme vijijini,” amesema Nyongo.
Awali, Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema Wabia wa Maendeleo wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya sekta ya nishati, ikiwemo usambazaji wa umeme vijijini, uzalishaji wa nishati jadidifu na usafirishaji wa umeme.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali mstaafu Jacob Kingu, amewashukuru Wabia wa Maendeleo kwa mchango wao katika miradi ya kusambaza nishati vijijini, huku akiahidi kuwa Bodi itaendelea kuisimamia Menejimenti ya REA ili kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa na fedha zinazotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema licha ya Serikali kufanikiwa kusogeza miundombinu ya umeme katika vijiji na vitongoji vingi nchini, wakala huo umeweka vipaumbele vitatu vya kimkakati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kunufaika kiuchumi na uwepo wa nishati hiyo.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuongeza idadi ya wateja wanaounganishiwa umeme, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma ya umeme kupitia ujenzi wa vituo vidogo vya kupoza na kusambaza umeme, pamoja na kuimarisha matumizi ya umeme katika shughuli za uzalishaji mali na kuboresha huduma za kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati, Dkt. Rhonda Jordan, ambaye pia ni Mtaalamu Mwandamizi wa Nishati kutoka Benki ya Dunia, amesisitiza kuwa wabia hao wataendelea kushirikiana na Serikali kupanua upatikanaji wa huduma za nishati zilizo salama, za uhakika na endelevu ili kufanikisha malengo ya nchi katika sekta ya nishati.





