NA AMINA SAIDI, MATUKIO DAIMA TANGA.
WAKALA wa Taifa wa Huduma za Ugani nchini (NAESA), kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, imejipanga kutoa mafunzo maalum kwa maafisa ugani katika mikoa 14 inayopata misimu miwili ya mvua, ikiwa ni mkakati wa kuwajengea uwezo wa kutafsiri na kuwafikishia wakulima taarifa za kitaalamu kwa wakati.
Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani kutoka NAESA, Ester Mwaisango, alibainisha hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Mwaisango aliitaja mikoa itakayofaidika na mafunzo hayo kuwa ni pamoja na ile ya Kanda ya Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini, pamoja na maeneo ya Kaskazini mwa mikoa ya Morogoro na Kigoma.
”Wakala tumeandaa mafunzo haya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, na tunaamini yatakuwa na tija kubwa kwa maafisa ugani ili kuwafikishia wakulima taarifa na mbinu bora za kilimo kwa wakati,” alisema Mwaisango.
Aliongeza kuwa mbali na mafunzo hayo, NAESA inaendelea kuratibu na kusimamia shughuli mbalimbali za ugani nchini, ikiwa ni pamoja na usajili wa wakulima kwenye mifumo rasmi ambapo hadi sasa zaidi ya wakulima milioni 5.5 wameshasajiliwa.
Alisema NAESA pia inahusika na usimamizi wa vyuo vya mafunzo ya kilimo, vituo vya mafunzo kwa wakulima, hamasa ya kilimo biashara, pamoja na kuboresha mitaala ya ufundishaji kwa kushirikiana na vyuo vya kilimo.
Katika maadhimisho hayo, NAESA imeshiriki ikiongozana na wakufunzi kutoka vyuo vilivyo chini yake vinavyotoa mafunzo ya uhaulishaji wa teknolojia za kilimo, ambapo wameonyesha teknolojia mbalimbali za usindikaji na uongezaji thamani wa mazao.
Miongoni mwa teknolojia zilizoonyeshwa ni pamoja na uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke kabla ya kukobolewa, lengo likiwa ni kuboresha ubora wa mchele na kupunguza upotevu wa mazao wakati wa usindikaji.
Naye Mwakilishi na Mkufunzi kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Ulenga (kilicho chini ya NAESA), Hamisi Ramadhani, alisema wameona umuhimu wa kuwafundisha wakulima mbinu zinazoweza kuongeza tija na kipato chao.
”Wakulima wengi wamekuwa wakiuza mpunga ukiwa shambani au kupeleka kwenye mashine za kawaida za kukoboa, hali inayowakosesha fursa ya kuongeza thamani ya mazao yao.
“Kupitia teknolojia ya mvuke, wakulima watapata mchele bora usiovunjika na kupata faida kubwa zaidi sokoni,” alieleza Ramadhani.
Alisisitiza kuwa juhudi hizo zinaenda sambamba na azma ya NAESA ya kuleta maarifa, ubunifu, na tija katika sekta ya kilimo, ili kuhakikisha wakulima wanatoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuingia kwenye kilimo biashara chenye manufaa makubwa kiuchumi.
