
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imetangaza nafasi 10 za kazi kwa Watanzania wenye sifa, zikiwemo nafasi tano za Mwandishi Mwendesha Ofisi Daraja la II na nafasi tano za Dereva Daraja la II.
Tangazo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, kufuatia kibali kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Nafasi za Mwandishi Mwendesha Ofisi
Kwa nafasi tano za Mwandishi Mwendesha Ofisi Daraja la II, majukumu yanajumuisha kuchapa barua, taarifa na nyaraka za kawaida na za siri, kupokea wageni na kuwaelekeza sehemu husika, kutunza taarifa na kumbukumbu za matukio, miadi, wageni na ratiba za kazi.
Majukumu mengine ni kutafuta majalada na nyaraka zinazohitajika, kupokea na kusambaza majalada kwa maofisa husika, kutunza majalada na nyaraka, kuandaa maandalizi ya vikao pamoja na orodha ya mahitaji ya vifaa vya ofisi.
Mwombaji wa nafasi hiyo anatakiwa kuwa na Elimu ya Kidato cha Nne au Sita na Stashahada ya Uhazili au Cheti cha NTA Level 6 ya Uhazili. Pia anatakiwa kuwa amefaulu somo la Hatimkato ya Kiswahili na Kiingereza kwa maneno 100 kwa dakika moja na kuwa na ujuzi wa programu za kompyuta za ofisi, ikiwemo Word, Excel, PowerPoint, Internet, E-mail na Publisher.
Nafasi hiyo ina mshahara wa TGS C.
Nafasi za Dereva
Halmashauri pia imetangaza nafasi tano za Dereva Daraja la II.
Majukumu ya dereva ni pamoja na kukagua gari kabla na baada ya safari, kuwapeleka watumishi katika maeneo mbalimbali kwa safari za kikazi, kufanya matengenezo madogo ya gari, kukusanya na kusambaza nyaraka, kutunza taarifa za safari katika daftari la safari na kufanya usafi wa gari.
Mwombaji anatakiwa kuwa na Cheti cha Kidato cha Nne pamoja na Leseni ya Daraja E au C, akiwa na uzoefu wa kuendesha magari kwa muda usiopungua mwaka mmoja bila kusababisha ajali. Pia anatakiwa kuwa na vyeti vya mafunzo vilivyompatia sifa ya kupata madaraja hayo na kuwa amehudhuria mafunzo ya msingi ya uendeshaji magari yanayotolewa na VETA au chuo kingine kinachotambuliwa na Serikali.
Nafasi hiyo ina mshahara wa TGS B1.
Masharti kwa waombaji
Tangazo limeeleza kuwa waombaji wote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 45. Waombaji wenye ulemavu wanahamasishwa kutuma maombi na wanatakiwa kuainisha ulemavu walionao kwenye mfumo wa kuombea ajira.
Waombaji wanatakiwa kuwasilisha CV yenye maelezo binafsi, anuani, namba za simu, barua pepe pamoja na majina ya wadhamini watatu, na kuambatanisha vyeti vya elimu na taaluma vilivyothibitishwa na Mwanasheria/Wakili.
Aidha, “Testimonials”, “Provisional Results”, “Statement of Results” pamoja na hati za matokeo za Kidato cha Nne na Sita hazitakubaliwa. Waombaji waliosoma nje ya Tanzania wanatakiwa kuhakikisha vyeti vyao vimehakikiwa na kuthibitishwa na mamlaka husika.
Mwisho wa kutuma maombi
Mwisho wa kutuma maombi ni Oktoba 1, 2026. Waombaji wanatakiwa kuambatanisha barua ya maombi ya kazi iliyosainiwa pamoja na vyeti vya elimu. Barua hiyo ielekezwe kwa Mkurugenzi Mtendaji (W), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, S.L.P. 3, Mbozi.
Maombi yote yanapaswa kutumwa kielektroniki kupitia Recruitment Portal ya Sekretarieti ya Ajira. Tangazo limeeleza kuwa maombi yatakayowasilishwa nje ya utaratibu huo hayatafanyiwa kazi.
