Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments
Uongozi wa Young Africans Sports Club (YANGA) umetuma salamu za pole kufuatia kifo cha Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, Mama Fatma Karume, aliyefariki dunia Septemba 21, 2026.
Kupitia taarifa iliyotolewa Septemba 22, 2026, Uongozi wa YANGA umesema umepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mama Fatma Karume, akielezwa kuwa mmoja wa viongozi waliokuwa na mchango mkubwa katika historia ya klabu hiyo.
“Huu ni msiba mkubwa kwetu. Tumepoteza Kiongozi mkubwa mwenye busara, hekima na mapenzi makubwa na Klabu yetu. Tutamkumbuka Mama yetu Fatma Karume kwa mengi mazuri aliyofanya ndani ya Klabu yetu, ikiwemo upatikanaji wa Ardhi ya jengo letu la Makao Makuu, Jangwani Jijini Dar es Salaam. Hakika, tumepoteza Mwanachama na moja ya nembo ya Klabu hii,” amesema Rais wa YANGA, Eng. Hersi Said.
Uongozi wa YANGA umetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau wote wa michezo, huku ukiwaombea wafiwa nguvu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Ameen.”
Taarifa hiyo imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Young Africans Sports Club.


