Marekani Yatangaza Hatua Kali Dhidi ya Mashirika ya Ndege ya Iran

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent.

NEW YORK, Marekani: Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema mashirika ya ndege ya Iran yanatarajiwa kukabiliwa na vikwazo vikubwa vya kiuchumi duniani kuanzia Septemba 23, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Donald Trump kuongeza shinikizo kwa Tehran.

Akizungumza na kituo cha CNBC Jumatatu, Septemba 21, 2026, Bessent alisema mashirika yote ya ndege ya Iran yataathiriwa na hatua hizo, akidai kuwa yatazuiwa kupata huduma muhimu katika viwanja vya ndege duniani.

Bessent amesema ndege za Iran zitakapowasili katika viwanja vya ndege, watoa huduma watakabiliwa na vikwazo iwapo wataendelea kuwapatia mafuta, huduma za kutua na kuondoka, pamoja na kuuza tiketi.

Kwa mujibu wa Bessent, kampuni au taasisi zitakazokiuka masharti hayo zinaweza kupoteza uwezo wa kufanya miamala kupitia mfumo wa dola wa Marekani.

Hatua hiyo ni sehemu ya sera ya Marekani ya kutumia vikwazo vya kiuchumi kuongeza shinikizo dhidi ya Iran, huku ikilenga sekta ya usafiri wa anga ya nchi hiyo.