UWEKEZAJI katika miundombinu ya barabara na mifumo ya kidijitali katika Mji wa Serikali Mtumba unatarajiwa kuongeza ufanisi wa utendaji wa Serikali na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi wanapofika Dodoma kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiserikali.
Mji huo wenye kilomita 59 za barabara za lami umejengwa kwa lengo la kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma za Serikali, huku wananchi wakitarajiwa kunufaika na urahisi wa kufika katika ofisi husika wanapohitaji huduma.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya utendaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi wanapofika katika makao hayo ya Serikali.
Msigwa ameyasema hayo Oktoba 28, 2026, alipokutana na waandishi wa habari na wahariri waliotembelea Mji wa Serikali Mtumba kabla ya uzinduzi rasmi wa majengo na miundombinu yake.
“Ujenzi wa mji huo haukuishia katika kuweka majengo ya kisasa kwa ajili ya ofisi za Serikali, bali umehusisha pia miundombinu inayowezesha shughuli za kiutendaji kufanyika kwa ufanisi na kwa mpangilio unaokidhi mahitaji ya Serikali, ” Amesema.
Ameeleza kuwa kilomita 59 za barabara za lami zilizojengwa katika eneo hilo ni sehemu muhimu ya uwekezaji huo, zikilenga kuwezesha wananchi na watumishi wa Serikali kufika katika ofisi mbalimbali kwa urahisi.
Msigwa amesema Serikali pia imeweka mifumo ya Serikali Mtandao inayolenga kupunguza utegemezi wa huduma zinazotolewa kwa njia ya kufika ofisini, ambapo baadhi ya huduma zitaweza kupatikana kwa njia za kidijitali.
Amesema matumizi ya mifumo hiyo yatasaidia kupunguza usumbufu kwa wananchi, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuboresha utendaji wa taasisi za Serikali zilizopo katika mji huo.
Aidha, amesema ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba umezingatia hadhi ya Tanzania, kwa kuweka mazingira ya kisasa na yenye mpangilio yatakayowezesha shughuli za Serikali kufanyika katika mazingira bora.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo unatarajiwa kuwa na manufaa kwa wananchi wanaofika Dodoma kwa ajili ya kufuatilia huduma mbalimbali za Serikali, kwa kuwa watakuwa na nafasi ya kuhudumiwa katika ofisi zinazohusika zilizopo Mtumba.
Msigwa amewataka waandishi wa habari na wahariri kutumia nafasi yao kuueleza umma kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mji huo na namna miundombinu iliyowekwa inavyolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali.
” Matarajio ya Serikali ni kuona wananchi wanaofika Mtumba wanapata huduma kwa urahisi kupitia ofisi zilizopo katika eneo hilo, kuanzia ngazi za juu hadi za chini za kiutendaji, ” Amesema Msigwa
