BOT YAKUTANA NA WATAALAMU WA MATAIFA SABA KUJADILI MATUMIZI YA AKILI UNDE.

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Chuo cha Benki Kuu Tanzania, Mwanza, kimeandaa kongamano la siku mbili linalowakutanisha wataalamu kutoka mataifa saba kujadili matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence — AI) katika kuboresha utendaji kazi wa benki kuu na taasisi nyingine za kifedha, pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Kongamano hilo limefanyika leo Jumatano, Oktoba 28, 2026, katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu Mwanza, likishirikisha wataalamu kutoka Madagascar, Kenya, Malawi, Zambia, Misri na Ghana, pamoja na wawakilishi kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na taasisi nyingine za kimataifa zinazojihusisha na masuala ya fedha na uchumi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema mjadala huo unalenga kuangalia namna akili unde inavyoweza kutumika kuboresha utendaji kazi, kurahisisha utoaji na uchakataji wa taarifa, kuchambua takwimu na kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kiuchumi na kifedha.

“Tumekuwa na wageni kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo wataalamu kutoka nchi sita za Afrika, pamoja na wataalamu kutoka IMF na mashirika mengine ya kimataifa yanayosimamia masuala ya kifedha na kiuchumi,” amesema Tutuba.

Ameeleza kuwa katika kongamano hilo, wataalamu watabadilishana uzoefu kuhusu namna akili unde inavyoweza kusaidia kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku za benki, ikiwemo uchakataji wa taarifa na takwimu zinazotumika kufanya maamuzi ya kiuchumi.

Tutuba amesema Benki Kuu ya Tanzania imeanza kuchukua hatua za kutumia teknolojia hiyo kupitia idara inayojihusisha na akili unde na ubunifu, inayosaidia wataalamu kuchakata na kuchambua taarifa mbalimbali.

Amesema matumizi ya akili unde yanaweza kusaidia Benki Kuu kufuatilia mwelekeo wa uchumi na kubaini mapema changamoto zinazoweza kuathiri ustawi wa sekta ya fedha, hivyo kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kwa wakati.

“Kwa kutumia uzoefu uliopo katika nchi moja na nyingine, wataalamu hawa watajadiliana ili kupata mwelekeo sahihi. Wale wenye changamoto wataziwasilisha na kupata ufumbuzi wa namna bora ya kufanya shughuli zetu kwa kutumia mifumo ya akili unde,” amesema Tutuba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu Mwanza, Dkt. Nicas Yabu, amesema mjadala kuhusu akili unde utatoa fursa ya kutathmini namna mabenki yanavyoweza kutumia teknolojia hiyo kuboresha huduma zao na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja.

Amesema kongamano hilo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wataalamu kuhusu fursa zinazotokana na matumizi ya akili unde katika sekta ya benki na kuimarisha uwezo wa taasisi za kifedha kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mazingira ya sasa ya kiuchumi na kiteknolojia.