MALASUSA KUONGOZA UZINDUZI WA KANISA LA KKKT NSHARA, MBOWE AFUNGUKA KUHUSU CHANGAMOTO ZA UJENZI

NSHARA, HAI, KILIMANJARO. 

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Alex Malasusa, anatarajiwa kuongoza ibada ya uzinduzi wa kanisa la KKKT Usharika wa Nshara, Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, inayotarajiwa kufanyika Novemba 1, mwaka huu.

Akizungumza kuhusu uzinduzi huo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Nshara, Mchungaji Rodrick Mlay, amesema wanamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufikia hatua hiyo muhimu ya kukamilika kwa ujenzi wa kanisa hilo.

Amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza rasmi mwaka 2006 na kwamba umekuwa ukiendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliojitolea kuhakikisha kazi hiyo ya Mungu inakamilika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo, ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Aikaeli Mbowe, amesema ujenzi wa jengo hilo haukuwa kazi rahisi hadi kufikia hatua ya kukamilika.

Katika ibada hiyo, wanatarajiwa kuhudhuria wageni mbalimbali wa kitaifa, maaskofu, wachungaji, waumini wa usharika huo pamoja na wadau kutoka sekta binafsi.

Baada ya ibada ya uzinduzi, shughuli hizo zinatarajiwa kuhitimishwa kwa tamasha.