UJENZI wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma umetajwa kuwa mfano wa upangaji na ujenzi wa miji ya kisasa nchini, kutokana na usanifu wa majengo na uwekaji wa miundombinu ya huduma muhimu chini ya ardhi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema hayo baada ya kushiriki ziara ya wahariri na waandishi wa habari kutembelea Mji wa Serikali Mtumba, ambapo wamejionea maendeleo ya ujenzi wa majengo na miundombinu inayotekelezwa na Serikali.
Balile amesema uwekezaji uliofanyika katika eneo hilo unaifanya Dodoma kuwa na mwonekano wa kisasa, akibainisha kuwa majengo yaliyopo yana usanifu unaovutia na unaoendana na mahitaji ya miji ya kisasa.
“Kwa kweli tumefanya ziara hii kama wahariri na waandishi wa habari, tumeona ujenzi mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika Mji wa Serikali hapa Mtumba, Dodoma. Kwa kweli ni uwekezaji mkubwa na umeleta heshima ya pekee,” amesema.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyomvutia ni namna miundombinu ya umeme, mawasiliano na maji ilivyopangwa, ambapo nyaya na mabomba muhimu yamepitishwa chini ya ardhi badala ya kuonekana juu.
Amesema mfumo huo unachangia kuupa mji mwonekano safi na wa kisasa, tofauti na baadhi ya maeneo ya miji mingine ambako nyaya za umeme na mawasiliano zinaning’inia juu, jambo linaloweza kuathiri mandhari na kuibua changamoto za kiusalama.
Akizungumzia hali ilivyo Dar es Salaam, Balile ametolea mfano wa maeneo ya katikati ya jiji, ikiwemo Barabara ya Samora, akisema kuna maeneo ambayo nyaya zinazoonekana juu zinaweza kuleta hatari, hasa wakati wa mvua.
Amesema uzoefu unaoonekana Mtumba unaweza kuwa somo kwa miji mingine nchini, ikiwemo Dar es Salaam, kwa kuzingatia umuhimu wa kupanga miundombinu tangu hatua za awali za ujenzi ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye.
“Tunadhani kwamba kwa uzuri huu wa mji, ingekuwa vyema mji huu ukageuka somo, hata Dar es Salaam wafikirie kufanya kitu tunachokiona hapa Mtumba. Kwa kweli ni mji mzuri sana,” amesema.
Balile ametoa pongezi kwa Serikali, wahandisi na wataalamu walioshiriki katika kutekeleza mradi huo, akisema mafanikio yanayoonekana ni matokeo ya maamuzi ya kuwekeza katika ujenzi wa mji huo.
Aidha, amezipongeza Serikali za Awamu ya Tano na ya Sita kwa kuendeleza wazo la ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, akieleza kuwa uwekezaji huo unaonesha umuhimu wa kuwa na mipango ya muda mrefu ya maendeleo.
Amesema majengo na miundombinu ya Mtumba yanaonesha namna usanifu wa kisasa unavyoweza kuimarisha mazingira ya kazi na kutoa mwonekano unaoendana na hadhi ya Dodoma kama makao makuu ya nchi.
Ameongeza kuwa miji mingine inapaswa kuzingatia si ujenzi wa majengo pekee, bali pia namna huduma za umeme, maji na mawasiliano zinavyopangwa ili kuhakikisha miundombinu inakuwa salama, nadhifu na yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya baadaye.
Kwa mujibu wa Balile, hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Mtumba inapaswa kuwa chachu ya kuendeleza mijadala kuhusu namna ya kuboresha mipango miji nchini, hususan katika maeneo yenye ongezeko la shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema uwekezaji huo unastahili kutambuliwa kutokana na mchango wa wataalamu na viongozi waliohusika katika kuanzisha na kuendeleza mradi huo, ambao umebadili mwonekano wa eneo hilo.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia na upangaji mzuri wa miundombinu ni mambo muhimu katika ujenzi wa miji inayokidhi mahitaji ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Amesisitiza kuwa uzoefu wa Mtumba unaweza kutumiwa na mamlaka zinazohusika na mipango miji kama rejea katika kubuni na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo nchini.
