Wachimbaji Wadogo Geita Watakiwa Kuchukua Tahadhari Dhidi ya Mvua Kubwa

GEITA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewataka wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha nchini.

Sangu ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita, akisisitiza umuhimu wa wachimbaji kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waweze kuchukua hatua mapema.

Amesema tahadhari hiyo ni muhimu zaidi kwa kuwa shughuli nyingi za uchimbaji zinazofanywa na wachimbaji hao ni za chini ya ardhi, hivyo uwepo wa mvua kubwa unaweza kuongeza vihatarishi katika maeneo ya uchimbaji.

“Niwatake wachimbaji wote kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa, ili kuchukua tahadhari mapema. Uchimbaji wetu ni wa underground, hivyo ni muhimu kujiridhisha kabla ya kuanza kufanya uchimbaji,” amesema Mhe. Sangu.

Ameongeza kuwa endapo kutatokea madhara yoyote katika maeneo ya uchimbaji, taarifa zinapaswa kutolewa mapema kwa OSHA na mamlaka nyingine zinazohusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Waziri Sangu pia amewataka wachimbaji kutumia elimu wanayopewa kuhusu usalama na afya mahali pa kazi, pamoja na kutumia ipasavyo vifaa kinga walivyokabidhiwa, huku akisisitiza umuhimu wa wachimbaji kukumbushana mara kwa mara kuhusu uzingatiaji wa taratibu za usalama.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha makundi mbalimbali ya wafanyakazi, wakiwemo wachimbaji wadogo, yanapatiwa elimu kuhusu usalama na afya mahali pa kazi.

Amesema OSHA imekuwa ikiendesha mafunzo kama hayo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na Wilaya za Bukombe mkoani Geita na Namungo mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa Bi. Mwenda, wachimbaji wadogo wanakabiliwa na vihatarishi mbalimbali kutokana na aina ya shughuli wanazofanya, jambo lililosababisha OSHA kuamua kuwafikia moja kwa moja kwa kutoa elimu ya usalama na afya pamoja na kuwapatia vifaa vya kujikinga (PPE).

Mafunzo hayo yamewashirikisha wachimbaji kutoka Mbogwe na Geita, pamoja na wachimbaji kutoka Uganda, ambapo wamefundishwa namna ya kutambua na kudhibiti vihatarishi katika maeneo ya kazi pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza.

Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Uganda nchini Tanzania, mwakilishi wa Ubalozi huo, Brigedia Jenerali Julius Mbaine, amesema ushiriki wa wachimbaji kutoka Uganda umefungua fursa ya kubadilishana uzoefu na kutambua maeneo ambayo Tanzania na Uganda zinaweza kushirikiana katika sekta ya madini.

Amesema sekta ya madini inaweza kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili, hususan katika uwekezaji, biashara na mnyororo wa thamani wa madini.

“Sekta ya madini inatoa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano. Ubalozi wa Uganda nchini Tanzania uko tayari kusaidia kuimarisha uhusiano wa kitaasisi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, hususan katika kukuza uwekezaji, biashara na mnyororo wa thamani wa madini,” amesema Brigedia Jenerali Mbaine.

Ameongeza kuwa mazungumzo yaliyofanyika kati ya ujumbe wa Uganda na wadau wa madini mkoani Geita yamewapa fursa ya kuelewa zaidi sekta ya madini nchini Tanzania na kubaini maeneo yenye maslahi ya pamoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Geita Mjini, Chacha Mwita Wambura, amepongeza juhudi zinazofanywa na OSHA katika kusimamia usalama na afya mahali pa kazi nchini.

Amesema shughuli za uchimbaji madini zina vihatarishi mbalimbali, hivyo elimu na uzingatiaji wa taratibu za usalama ni muhimu katika kulinda maisha na afya za wachimbaji.

Mafunzo hayo yameandaliwa na OSHA kwa kushirikiana na Mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani humo.