Mikopo ya asilimia kumi yazidi kuinua wananchi Bukoba – HabariLeo

KAGERA: KATIBU Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Proscovia Mwambi, amesema Manispaa ya Bukoba imetoa mikopo ya zaidi ya Sh milioni 800 kwa vikundi 123 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali bila riba.

Amesema vikundi vilivyonufaika ni 68 vya wanawake, 37 vya vijana na tisa vya watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukuza shughuli zao za uzalishaji mali.

Akizindua Mwezi wa Maendeleo ya Jamii, Mwambi amesema idadi ya wanufaika inaweza kuongezeka endapo vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vitashiriki kikamilifu katika kutambua na kutumia fursa zinazotolewa na serikali.

Amesema mikopo hiyo hutolewa bila riba kwa vikundi vinavyokidhi vigezo vilivyowekwa, bila ubaguzi, huku vikundi vinavyorejesha mikopo yao vizuri vikiendelea kupewa fursa zaidi hadi vitakapojitegemea kiuchumi.

Katika hatua nyingine, amesema Manispaa ya Bukoba imesajili vikundi 164 katika mfumo wa manunuzi ya umma wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ili viweze kunufaika na fursa ya asilimia 30 ya manunuzi katika taasisi za serikali kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023.

Amesema kupitia mfumo huo, vikundi viwili tayari vimepata zabuni zenye thamani ya Sh milioni 491, huku vingine vikiendelea kupata fursa hizo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.

Aidha, amesema manispaa hiyo ina wafanyabiashara wadogo 805, ambapo 206 tayari wamepata vitambulisho, huku wafanyabiashara wengine 66 wakinufaika na mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya Sh milioni 105.

Kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Bukoba, Faraja Chaula, amesema maafisa maendeleo ya jamii watatumia Mwezi wa Maendeleo ya Jamii kufuatilia wanufaika wa mikopo ya asilimia 10, kukagua miradi wanayoitekeleza na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha za mikopo.

Amesema mwezi huo pia utatumika kutoa elimu kwa wafanyabiashara wadogo kuhusu fursa za mikopo ya masharti nafuu, umuhimu wa lishe bora, kuchangia chakula shuleni na masuala ya afya ya jamii.

Ameongeza kuwa shughuli nyingine ni kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuimarisha mawasiliano kati ya serikali, wananchi na wadau wa maendeleo.

Kongamano la uzinduzi wa Mwezi wa Maendeleo ya Jamii lilihudhuriwa na mamia ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba, ambao walipata fursa ya kuelimishwa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na semina ya uwekezaji na matumizi sahihi ya fedha kupitia vikundi vyao.

Kaulimbiu ya Mwezi wa Maendeleo ya Jamii mwaka huu ni: “Familia Imara, Jamii na Taifa Imara Kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.”