Video: Dereva wa Basi Satco Adaiwa Kutishiwa kwa Bastola Dodoma

Global Publishers
September 21, 2026
0 views
0 Comments

Tukio la aina yake limetokea katika eneo la Makole jijini Dodoma, baada ya dereva wa basi la kampuni ya Satco, lenye namba za usajili T308 EME, kudaiwa kutishiwa kwa kutumia silaha ya moto na dereva wa gari aina ya Land Cruiser, lenye namba za usajili T881 ENZ.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, basi hilo lilikuwa likitoka katika Stendi ya Mabasi ya Dodoma kuelekea mkoani Geita, ambapo lilipofika eneo la Makole, lilidaiwa kugongana na Land Cruiser hiyo baada ya gari hilo kulipita basi hilo kwa upande.

Mashuhuda hao wanaeleza kuwa baada ya magari hayo kugongana, dereva wa Land Cruiser alishuka na kudaiwa kuwa na bastola, kisha kumfuata dereva wa basi na kumtaka ashuke. Aidha, inadaiwa kuwa dereva huyo alimtaka dereva wa basi kuingia katika Land Cruiser, jambo lililosababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi waliokuwa eneo hilo.

Katika hali hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa karibu walidaiwa kuingilia kati na kumzuia dereva wa basi kuchukuliwa, huku wakitaka vyombo vya usalama kufika eneo la tukio na kuchunguza kilichotokea.

Tukio hilo limeibua maswali kuhusu matumizi ya silaha katika mazingira ya barabarani, huku wananchi wakitaka uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha mgogoro huo, iwapo silaha ilitumika na hatua stahiki zichukuliwe endapo madai hayo yatathibitishwa.