Mashariki ilinifungulia njia kuwa Miss Tanzania – HabariLeo

PWANI:  MISS Tanzania 2022, Halima Kopwe, amesema ushiriki wake katika mashindano ya Miss Kanda ya Mashariki ulikuwa hatua muhimu katika safari yake ya urembo na baadaye kumfungulia milango ya fursa mbalimbali, ikiwamo kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya dunia.

Halima, ambaye alitokea Mtwara na kushindana Miss Tanzania Kanda ya Mashariki, alisema hayo wakati wa uzinduzi wa shindano la kanda hiyo 2026 uliofanyika Kisemvule, Mkuranga mkoani Pwani Septemba 18, 2026.

“Baada ya kuwa Miss Kanda  ya Mashariki na kwenda kwenye mashindano makubwa duniani, nimepata fursa nyingi sana. Maisha yangu yamebadilika kupitia Miss Tanzania,” amesema Halima.

 

Amesema uzoefu wake unaonesha namna mashindano ya urembo yanavyoweza kubadilisha maisha ya wasichana kupitia fursa za ajira, ubalozi na mikataba mbalimbali.

Halima pia aliwashukuru wadau wanaoendelea kuunga mkono tasnia ya urembo, akisema ushirikiano huo unawapa moyo washiriki na waandaaji.