MTOTO WA MIAKA 10 AOKOLEWA BAADA YA KUTAKA KUOZWA SAME

Serikali wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, imemuokoa mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina limehifadhiwa, aliyekuwa ameachishwa shule na familia yake na kupelekwa kwa mwanaume kwa lengo la kumuozesha.

Mtoto huyo, mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Jiungeni, iliyopo Kata ya Ruvu wilayani Same, aliokolewa baada ya Serikali kupata taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu tukio hilo.

Akizungumza  Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alisema baada ya kupokea taarifa hiyo alielekeza maafisa wa Serikali kufanya uchunguzi, ambapo walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 20 katika mazingira ya ndoa.

“Serikali inalaani vikali kitendo hiki cha kikatili cha kumnyima mtoto haki zake za msingi, ikiwemo haki ya kupata elimu na kukua katika mazingira salama,” alisema Kasilda.

Alisema watuhumiwa wamefikishwa mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya hatua za kisheria, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Serikali kuhusu vitendo vya aina hiyo.

Aidha, Kasilda alisema Shule ya Msingi Jiungeni ilijengwa mahususi kusaidia watoto kutoka jamii ya wafugaji wanaoishi katika eneo hilo kupata elimu.

Alisema kuna uwezekano wa kuwepo kwa wanafunzi wengine walioacha shule kutokana na ndoa za utotoni au kwenda kuchunga mifugo, hivyo Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu.

“Msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha watoto wanakwenda shule na sisi tutapambana na wazazi wanaokiuka maelekezo ya Serikali,” alisema.

Kasilda aliwapongeza maafisa wa Serikali pamoja na wananchi waliofanikisha zoezi la kumuokoa mtoto huyo, akisema walilazimika kufanya uchunguzi katika mazingira magumu ya porini ambako mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana huyo.

Pia aliwaonya watu wanaojaribu kutoa rushwa kwa lengo la kuwaachia watuhumiwa, akisema watakaobainika kufanya hivyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayehatarisha usalama, elimu na ustawi wa watoto.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema mtoto huyo atarejeshwa shuleni ili kuendelea na masomo yake.

Ndoa za utotoni zinaweza kuwanyima watoto fursa ya kupata elimu na kuwaweka katika mazingira hatarishi ya ukatili na unyanyasaji, pamoja na changamoto za kiafya na kisaikolojia.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa jamii kulinda haki za watoto, kuhakikisha wanapata elimu na kukua katika mazingira salama yanayozingatia maslahi na mustakabali wao.

VEROTAS PLUMBING SULUHISHO LA MFUMO WA MAJI SAFI NA SALAMA.

 

NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

KAMPUNI ya VEROTAS PLUMBING imeendelea kutoa suluhisho katika ujenzi na uboreshaji wa mifumo ya maji kwa wananchi, kwa kutoa bidhaa zenye ubora zinazolenga kuhakikisha mifumo hiyo inakuwa safi, salama na yenye kudumu.

Huduma hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kupata mifumo bora ya maji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani, maliwatoni na kwenye majengo ya biashara, huku wakizingatia matumizi ya bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa VEROTAS PLUMBING, Veronica Mwita, amesema kampuni hiyo imejikita katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa na huduma zinazowawezesha kuwa na mifumo bora ya maji katika mazingira yao.

Amesema matumizi ya bidhaa bora katika mfumo wa maji ni muhimu katika kuhakikisha maji yanapitishwa katika mazingira salama, huku yakipunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vifaa visivyo na ubora.

“Tunatoa suluhisho kwenye mifumo ya maji kwa kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa zenye ubora ambazo zitawasaidia kuwa na mfumo mzuri, salama na wa kudumu. Tunazingatia mahitaji ya wananchi kuanzia kwenye maliwato hadi kwenye mfumo mzima wa maji wa nyumba,” amesema Mwita.

Aidha, amesema VEROTAS PLUMBING inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchagua bidhaa sahihi wakati wa kujenga au kuboresha mifumo ya maji, ili kuepuka gharama zinazoweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mifumo.

Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia ubora wa bidhaa wanazonunua na kuhakikisha zinafaa kwa matumizi yanayokusudiwa, kwani mfumo bora wa maji una mchango mkubwa katika usafi, afya na ustawi wa familia.

VEROTAS PLUMBING imeendelea kuwahimiza wananchi wanaojenga nyumba mpya au kufanya maboresho katika nyumba zao kutumia wataalamu na bidhaa bora ili kuhakikisha mifumo ya maji inakuwa salama, imara na yenye kudumu kwa muda mrefu.

MAGAZETINI LEO IJUMAA AGOSTI 14/2026:TRA KUVUKA MALENGO KWAMGUSA BALOZI OMARI,MADAKTARI BINGWA WAPIGA KAMBI HOSPITAL YA TOSAMAGANGA IRINGA…

<img alt="" border="0" data-original-height="887" data-original-width="2560" src="https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhphjRvscMWq5RLwwbsy2XGrzPRiJTnqHC7lLtkkWxqFPu8nd8-

PIEfJGtgItjXj0v5KCT2NHLwBaaWyFkaO8H-zRpOA0saATv5F2JNqvWmGSJRJlK27Ex0JQOOQcO85JZEL01qLgsxNKLMgqPB5xhUBoSNHAmJ5miW3G876lM5sPI_bpWee-1WjnhMaKA/s1600/1009271769.jpg” />

SUA YASISITIZA MAWASILIANO YA KISAYANSI KUFIKISHA MATOKEO YA UTAFITI KWA JAMII

 

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  kwa kushirikiana na Kituo cha Umahiri cha Afya Moja (SACIDS Foundation for One Health) na wadau wengine wa utafiti, imeendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wananchi na watumiaji wa mwisho. Hayo yameelezwa wakati wa Warsha ya Mkakati wa Ushirikishwaji wa Utafiti ya Vigoda vya Utafiti vya OR. Tambo, iliyofanyika SUA, Morogoro, 13 Agosti, 2026 ikilenga kuwajengea watafiti uwezo wa kuwasilisha kwa ufanisi tafiti zao ili kuongeza athari zake katika jamii.

Akizungumza katika warsha hiyo, Prof. Gerald Misinzo, Mwenyekiti wa  Kigoda cha Utafiti Barani Afrika cha OR Tambo cha Magonjwa ya Kuambukiza ya virus, amesema mawasiliano ya kisayansi ni nyenzo muhimu katika kubadilisha matokeo ya utafiti kuwa maarifa yanayoeleweka na kutumika katika jamii. Amesema watafiti wanapaswa kuwasilisha taarifa za kisayansi kwa lugha na njia zinazolingana na mahitaji ya walengwa, ili kuongeza uelewa, ushiriki na matumizi ya matokeo ya tafiti.

Prof. Misinzo amesema tafiti zinazofanywa na Kigoda hicho kwa kushirikiana na SACIDS na wadau wengine zinahusu magonjwa mbalimbali yanayoathiri wanyama na binadamu, yakiwemo homa ya nguruwe ya Afrika, Newcastle na magonjwa ya samaki. Amesema ni muhimu matokeo ya tafiti hizo kuwafikia wafugaji, wataalamu, watunga sera na wananchi kwa wakati, ili kusaidia kuchukua hatua stahiki na kupunguza madhara ya milipuko ya magonjwa.

Aidha, Prof. Misinzo amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano katika kufikisha taarifa za utafiti kwa hadhira pana. Amesema mawasiliano ya kisayansi yanapofanyika kwa ubunifu na kuzingatia mahitaji ya walengwa, yanaweza kuongeza uelewa wa jamii, kuimarisha ushirikiano na kujenga uaminifu katika taarifa za kisayansi.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam wa SUA, Prof. Maulid Mwatawala, amesema utafiti haupaswi kuishia katika machapisho ya kitaaluma pekee, bali unapaswa kuwafikia watumiaji wa mwisho. Amesema mafunzo ya mawasiliano ya kisayansi ni muhimu katika kuwajengea watafiti uwezo wa kueleza matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi na inayoeleweka, kushirikisha wadau na kuhakikisha utafiti unaleta suluhisho na mchango chanya katika maendeleo ya jamii.

ASKOFU MIHALI AWATAKA WAZAZI KUENDANA NA DIRA 2050 KWA KUWEKEZA KATIKA ELIMU

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA IRINGA 

Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Romanus Elamu Mihali amewataka wazazi na walezi kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kuwekeza zaidi katika elimu ya watoto akisema elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtoto, familia na taifa kwa ujumla.

Askofu Mihali ametoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Shule ya St. Dominic Savio, ambapo amesisitiza kuwa elimu ni urithi mkubwa ambao mzazi anaweza kumuachia mtoto wake.

Alisema wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa elimu katika kuwaandaa watoto kwa maisha ya baadaye na kuchangia katika ujenzi wa taifa.

“Ili kuendana na Dira yetu ya 2050 inayolenga malezi bora kwa vijana wetu, ningependa kuwasihi wazazi na walezi kuweza kuacha urithi wa elimu kwa watoto wao ili kusaidia kuchochea maendeleo ya Taifa kwa sababu elimu ni maisha.”

Aidha Askofu Mihali amewahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika Shule ya St. Dominic Savio alisema shule hiyo inatoa elimu pamoja na malezi yenye kuzingatia maadili.

Alisema mafanikio yaliyooneshwa na wanafunzi katika mahafali hayo, ikiwemo katika elimu, michezo na nidhamu, ni sehemu ya ushahidi wa ubora wa malezi na elimu inayotolewa shuleni hapo.

“Shule za St. Dominic ni shule bora na nzuri sana kwa watoto wetu Kama ambavyo wao wenyewe watakuwa wameshuhudia kwa yale yaliyotolewa kwa muhtasari katika mahafali haya  ikiwemo michezo, kauli zao na upande wa elimu inaonesha kuwa katika shule hii elimu inayotolewa ni njema na nzuri.”

Hatahivyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkimbizi A, Aghata Kasisi amepongeza uongozi wa Shule za St. Dominic kwa kutoa elimu bora na malezi yanayojenga nidhamu na kujiamini kwa watoto, akisema shule hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu Manispaa ya Iringa.

“Leo nimeshuhudia mahafali ya wanafunzi  wa darasa la saba wanaomaliza masomo yao katika Shule hii nimefurahishwa na kiwango cha elimu kinachotolewa shuleni hapa pamoja na juhudi zinazofanywa na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na uwezo wa kuwasiliana kwa ujasiri”

Naye Diwani wa Kata ya Gangilonga, Kenyata Likotiko  amelipongeza Kanisa Katoliki kwa uwekezaji katika sekta ya elimu kupitia shule za St. Dominic, akisema uwekezaji huo umekuwa chachu ya maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa na umeongeza imani ya wazazi katika shule hizo.

“Nampongeza Padre Ulungi kwa kutimiza miaka 30 ya huduma katika Jimbo la Iringa katika kipindi hicho amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu na jamii,kuanzia kuanzishwa na kuendelezwa kwa shule za St. Dominic ikiwemo matawi yaliyopo maeneo mbalimbali kumechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa na Mkoa wa Iringa kwa ujumla”

Aidha kwa upande wake Mchungaji  wa kanisa la kiinjilisti la kilutheri Dayosisi ya Iringa Yusto Jaffet Kinyowa  amewataka wazazi na walezi nchini kuendelea kuziamini shule  hizo  kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kuwajengea vijana maarifa na msingi mzuri wa maisha alisema elimu inayotolewa katika shule hizo huwasaidia wanafunzi kuendeleza maarifa waliyoyapata katika elimu ya msingi na kuwaandaa kwa masomo ya juu na maisha ya baadaye.

“Shule hizi zinatoa mafunzo ya ziada yanayowajengea wanafunzi uwezo wa kuwasiliana na kujifunza lugha mbalimbali, ikiwemo lugha ya Kichina, stadi hizi ni muhimu kwa vijana katika dunia ya sasa na zinaweza kuwasaidia kupata fursa mbalimbali za kielimu na kiuchumi pia niwashukuru wazazi, walezi, walimu na wanafunzi kwa mchango wao katika kufanikisha elimu, akisisitiza kuwa kuwekeza katika elimu ya msingi na sekondari ni kuwekeza katika taifa la kesho”

Ziara ya Rais Tshisekedi kufungua ukurasa mpya wa biashara, amani

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia leo Agosti 17 hadi kesho Agosti 18, 2026, ikiwa ni mara yake ya tatu kutembelea Tanzania tangu alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 2018.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeeleza kuwa Rais Tshisekedi atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Zanzibar, kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo.

Ajenda hiyo inatarajiwa kugusa biashara na uwekezaji, kilimo, madini, nishati, utalii, elimu, afya, miundombinu na usafirishaji, pamoja na amani, usalama na utangamano wa kikanda.

Ziara hiyo inafanyika wakati uhusiano wa Tanzania na DRC ukiendelea kupanuka kutoka uhusiano wa kisiasa na kihistoria hadi kwenye masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji.

Ziara ya kwanza ya Tshisekedi Tanzania ilikuwa Juni 2019, alipofanya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli.

Viongozi hao walijadili amani, biashara, miundombinu na ushirikiano wa kiuchumi. Tshisekedi pia alitembelea Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni njia muhimu ya kusafirisha mizigo kwenda DRC.

Ziara yake ya pili ilikuwa Oktoba 2022, alipokutana na Rais Samia kujadili namna ya kuongeza ushirikiano katika miundombinu, usafiri, biashara, uwekezaji, teknolojia, ulinzi na usalama, pamoja na masuala ya kijamii.

Katika ziara ya sasa, viongozi hao wanatarajiwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari kesho kuhusu maazimio na makubaliano yatakayofikiwa.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Denis Konga, amesema ziara hiyo inapaswa pia kuangazia usalama Mashariki mwa DRC na changamoto za kiafya, ikiwamo milipuko ya magonjwa, ili kuweka mazingira bora ya mwingiliano wa kibiashara.

“Kongo ni Taifa kubwa, matatizo ya kiusalama na kiafya yakishughulikiwa, fursa za kiuchumi na uwekezaji zinaweza kufunguka zaidi. Haya ni maeneo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika mazungumzo ya ushirikiano,” amesema.

Kwa upande wa uchumi, Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu inayolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia masoko ya nchi jirani. Kwa DRC, Bandari ya Dar es Salaam, reli, barabara na miundombinu ya Ziwa Tanganyika ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.

Takwimu zilizopo zinaonesha mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda DRC yaliongezeka kutoka Dola milioni 150.75 za Marekani (Sh343.02 bilioni) mwaka 2018 hadi Dola milioni 312.8 (Sh749.40 bilioni) mwaka 2023.

Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hamphrey Moshi, amesema ongezeko hilo linaonesha umuhimu wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo.

Amesema Tanzania na DRC zinapaswa kuboresha mikataba ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini, ili kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha wananchi.

“Siyo kuwa na sera tu, tuwe na uwezo mzuri wa kujadili na wawekezaji ili kuhakikisha nchi zetu zinanufaika na madini yetu. Hii si kwa Tanzania na Kongo tu, bali Afrika nzima tuna hili tatizo,” amesema.

Ameongeza kuwa usalama nchini DRC ni muhimu katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Wizara ya Mambo ya Nje imesema Tanzania na DRC tayari zinashirikiana katika miundombinu, nishati, utalii, elimu, afya, huduma za kifedha, biashara, uwekezaji, kilimo, maliasili na ufugaji.

Uhusiano huo pia una umuhimu kutokana na DRC kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi hiyo ilikubaliwa kuwa mwanachama wa saba wa EAC Machi 29, 2022, na kuwa mwanachama kamili baada ya kuwasilisha hati ya kuridhia Mkataba wa EAC Julai 11 mwaka huo.

Kwa DRC, Tanzania ni lango muhimu la biashara kuelekea Bahari ya Hindi kupitia Bandari ya Dar es Salaam, wakati Tanzania ikinufaika na soko kubwa la DRC.

Uhusiano wa nchi hizo una historia ndefu, ukiwa umejengwa katika misingi ya ujirani, biashara, historia ya ukombozi wa Afrika na ushirikiano wa amani na usalama katika eneo la Maziwa Makuu.

Tanzania pia imekuwa ikishiriki katika juhudi za kikanda za kutafuta amani Mashariki mwa DRC, eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na migogoro ya silaha na changamoto za kibinadamu.

SEKTA YA MADINI YAVUTIA UWEKEZAJI WA TRILIONI 9 NDANI YA MIAKA MINNE*

▪️Mikataba ya Msingi 14 ya Madini Yasainiwa

▪️Serikali yasaini Mkataba wa Bilioni 265 na Kampuni ya Henan Yudi Mining ya Mradi wa Graphite Morogoro

▪️Tanzania yawa kivutio kikubwa cha uwekezaji sekta ya Madini Afrika

▪️Rais Samia apongezwa kwa mazingira wezeshi ya uwekezaji

📍MOROGORO: 

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema ndani ya kipindi cha Miaka Minne, (4)  Sekta ya Madini imevutia uwekezaji wa Shilingi trilioni 9, hatua inayoiweka Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji wa Madini Barani Afrika.

Amesema hayo leoAgosti 15, 2026, Mkoani Morogoro wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mikataba ya Ubia wa Uchimbaji wa Madini ya Kinywe baina ya Serikali na Kampuni ya Henan Yudi Mining na kuongeza kuwa, hadi sasa tayari jumla ya mikataba ya Msingi 14 imekwisha sainiwa.

Amesema kuwa mradi huo una mashapo yaliyothibitishwa ya takribani tani milioni 104.28 za kinywe, na unatarajiwa kuwekeza takribani Dola milioni 100 (Shilingi bilioni 265) huku uzalishaji wa kiwango kamili ukilenga kufikia tani 50,000 za kinywe kwa mwaka na kwamba mradi unatakuwa na uwezo wa kuchakata tani milioni moja kwa mwaka wakati huohuo zaidi ya Watanzania 600 wakitarajiwa kupata ajira za moja kwa moja.

Mavunde amesema Serikali inaendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya madini kutoka kuwa mwenyeji wa uchimbaji hadi kuwa mshiriki wa thamani inayozalishwa, ambapo katika mradi huo Serikali inamiliki asilimia 17 ya hisa.

Amesema kinywe ni madini muhimu katika teknolojia za kisasa, ikiwemo utengenezaji wa anode za betri, hivyo mradi huo una nafasi ya kuchangia katika azma ya Tanzania kushiriki zaidi kwenye mnyororo wa thamani wa kinywe duniani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema Serikali ya Wilaya inashukuru juhudi zilizofanyika kufanikisha makubaliano hayo, akieleza kuwa mradi unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na ajira, kuongeza uzalishaji wa madini na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa.

Aidha, Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, amezipongeza pande zote zilizoshiriki katika majadiliano hayo, akisema mradi huo utaongeza uwekezaji wa kibiashara nchini, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.

Balozi Chen amesema China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji wa moja kwa moja nchini Tanzania, huku akieleza kuwa mradi huo unaongeza eneo jingine la ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo na kufungua fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa eneo la mradi na Taifa kwa ujumla.

VETA YAANDAA MTAALA WA MAFUNZO YA MUDA MFUPI WA FANI YA RECYCLING

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeandaa mtaala maalum wa kozi fupi za recycling kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya taka na kuongeza thamani ya taka zinazoweza kurejelewa.

Hayo yameelezwa Agosti 15, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohammed Omari, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Chuo cha VETA wilaya ya Bahi.

Amesema hatua hiyo imekuja baada ya tafiti kubaini kuwa baadhi ya vijana wanaojihusisha na shughuli za taka wanakabiliwa na changamoto za kiafya na kiusalama, hivyo kuhitajika kwa mtaala mahsusi utakaowawezesha kukabiliana na mazingira ya kazi.

Dkt. Omari amesema mtaala huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wadau katika mnyororo wa thamani wa taka, kuanzia ukusanyaji hadi uchakataji, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, sekta binafsi, vyuo vya walimu na waajiri.

Aidha, amesema VETA inaendelea kushirikiana na wataalamu wa sekta mbalimbali kuunganisha ujuzi wa vitendo na mafunzo ya vyuoni. Ametolea mfano ushirikiano na mtaalamu wa samani, Edo Sama, anayerejeleza zaidi ya asilimia 50 ya mbao zilizokuwa zikitupwa na kuzitumia kutengeneza samani, hivyo kuongeza thamani ya taka na kupunguza upotevu wa rasilimali.

Ameongeza kuwa VETA inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, ikiwemo kampuni ya Hans Paul ya Arusha inayotengeneza magari ya utalii, ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo. Amesema hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Serikali wa kushirikisha sekta binafsi katika kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

VETA IMETAKIWA KUENDELEA KUWASHIRIKISHA WATAALAMU WALIOBOBEA FANI MBALIMBALI

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetakiwa kuendelea kuwashirikisha wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali zinazotolewa vyuoni, ili kuwezesha mafunzo kwa vitendo na kujenga umahiri kwa vijana.

Rai hiyo imetolewa Agosti 15, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, akisema ushirikishwaji huo utawawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na jamii.

Amesema vyuo vya VETA havipaswi kujifungia kama kisiwa, wataalamu kutoka Jeshi la Zimamoto, maafisa biashara na sekta nyingine zinaweza kushirikishwa kulingana na mahitaji ya fani.

Mhe. Sekiboko ameipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kupitia ujenzi na uimarishaji wa vyuo vya VETA, hatua inayolenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi na fursa za ajira na kujiajiri.

Aidha, Mwenyekiti huyo amepongeza uanzishwaji wa kampuni tanzu za VETA zinazolenga kuongeza uzalishaji wa bidhaa halisi badala ya vielelezo pekee hatua itawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo, kuongeza mapato ya vyuo na kuwajengea vijana uwezo wa kibiashara.