Ziara ya Rais Tshisekedi kufungua ukurasa mpya wa biashara, amani
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia leo Agosti 17 hadi kesho Agosti 18, 2026, ikiwa ni mara yake ya tatu kutembelea Tanzania tangu alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 2018.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeeleza kuwa Rais Tshisekedi atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Zanzibar, kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo.
Ajenda hiyo inatarajiwa kugusa biashara na uwekezaji, kilimo, madini, nishati, utalii, elimu, afya, miundombinu na usafirishaji, pamoja na amani, usalama na utangamano wa kikanda.
Ziara hiyo inafanyika wakati uhusiano wa Tanzania na DRC ukiendelea kupanuka kutoka uhusiano wa kisiasa na kihistoria hadi kwenye masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji.
Ziara ya kwanza ya Tshisekedi Tanzania ilikuwa Juni 2019, alipofanya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli.
Viongozi hao walijadili amani, biashara, miundombinu na ushirikiano wa kiuchumi. Tshisekedi pia alitembelea Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni njia muhimu ya kusafirisha mizigo kwenda DRC.
Ziara yake ya pili ilikuwa Oktoba 2022, alipokutana na Rais Samia kujadili namna ya kuongeza ushirikiano katika miundombinu, usafiri, biashara, uwekezaji, teknolojia, ulinzi na usalama, pamoja na masuala ya kijamii.
Katika ziara ya sasa, viongozi hao wanatarajiwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari kesho kuhusu maazimio na makubaliano yatakayofikiwa.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Denis Konga, amesema ziara hiyo inapaswa pia kuangazia usalama Mashariki mwa DRC na changamoto za kiafya, ikiwamo milipuko ya magonjwa, ili kuweka mazingira bora ya mwingiliano wa kibiashara.
“Kongo ni Taifa kubwa, matatizo ya kiusalama na kiafya yakishughulikiwa, fursa za kiuchumi na uwekezaji zinaweza kufunguka zaidi. Haya ni maeneo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika mazungumzo ya ushirikiano,” amesema.
Kwa upande wa uchumi, Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu inayolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia masoko ya nchi jirani. Kwa DRC, Bandari ya Dar es Salaam, reli, barabara na miundombinu ya Ziwa Tanganyika ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.
Takwimu zilizopo zinaonesha mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda DRC yaliongezeka kutoka Dola milioni 150.75 za Marekani (Sh343.02 bilioni) mwaka 2018 hadi Dola milioni 312.8 (Sh749.40 bilioni) mwaka 2023.
Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hamphrey Moshi, amesema ongezeko hilo linaonesha umuhimu wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo.
Amesema Tanzania na DRC zinapaswa kuboresha mikataba ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini, ili kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha wananchi.
“Siyo kuwa na sera tu, tuwe na uwezo mzuri wa kujadili na wawekezaji ili kuhakikisha nchi zetu zinanufaika na madini yetu. Hii si kwa Tanzania na Kongo tu, bali Afrika nzima tuna hili tatizo,” amesema.
Ameongeza kuwa usalama nchini DRC ni muhimu katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje imesema Tanzania na DRC tayari zinashirikiana katika miundombinu, nishati, utalii, elimu, afya, huduma za kifedha, biashara, uwekezaji, kilimo, maliasili na ufugaji.
Uhusiano huo pia una umuhimu kutokana na DRC kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi hiyo ilikubaliwa kuwa mwanachama wa saba wa EAC Machi 29, 2022, na kuwa mwanachama kamili baada ya kuwasilisha hati ya kuridhia Mkataba wa EAC Julai 11 mwaka huo.
Kwa DRC, Tanzania ni lango muhimu la biashara kuelekea Bahari ya Hindi kupitia Bandari ya Dar es Salaam, wakati Tanzania ikinufaika na soko kubwa la DRC.
Uhusiano wa nchi hizo una historia ndefu, ukiwa umejengwa katika misingi ya ujirani, biashara, historia ya ukombozi wa Afrika na ushirikiano wa amani na usalama katika eneo la Maziwa Makuu.
Tanzania pia imekuwa ikishiriki katika juhudi za kikanda za kutafuta amani Mashariki mwa DRC, eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na migogoro ya silaha na changamoto za kibinadamu.

