TANZANIA, QATAR ZALENGA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA MADINI KUPITIA STAMICO

*Kampuni za Qatar zaalikwa kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC) 2026*

*Qatar Mining yaonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania; wawekezaji waalikwa TMIC 2026*

**DOHA, QATAR**

Tanzania na Qatar zimeonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Madini, huku Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) likitajwa kuwa muhimu katika utekelezaji wa miradi ya pamoja, ikiwemo kuwawezesha wachimbaji wadogo.

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya ujumbe wa Sekta ya Madini Tanzania nchini Qatar ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Baada ya kukutana na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu wa Qatar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Thirty Five Investment Holding, Dkt. Khalid Mohamed.

Dkt. Kiruswa amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji wa Qatar kupitia STAMICO katika miradi mbalimbali ya madini, ikiwemo kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji, teknolojia na mafunzo ili kuongeza tija na ushiriki wao katika mnyororo wa thamani.

Amesema ushirikiano huo unakuja wakati Tanzania ikiendelea kufungua fursa za utafiti na uwekezaji, akibainisha kuwa utafiti wa kina wa rasilimali za madini umefanyika kwa asilimia 16 pekee ya eneo la nchi.

“Mpaka sasa Tanzania imefanya utafiti wa kina kwa asilimia 16 tu ya eneo lake. Hii ni fursa kubwa kwa wawekezaji kushirikiana na Serikali katika kufanya utafiti na kubaini rasilimali zilizopo,” amesema.

Dkt. Kiruswa pia amezialika kampuni za madini na wawekezaji kutoka Qatar kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC) 2026, utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2026.

Ameeleza kuwa mkutano huo utajadili fursa za uwekezaji, teknolojia, uongezaji thamani na maendeleo ya mnyororo wa thamani wa madini.

Katika mazungumzo mengine, Dkt. Kiruswa amekutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Qatar Mining), Abdulaziz Abubakar ambapo ameonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania.

Ushirikiano huo pia unatarajiwa kwenda sambamba na utekelezaji wa mpango wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) unaolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo, hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum, kupata mitaji, teknolojia, ujuzi na masoko.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Mohamed, amezialika kampuni za madini nchini humo kutumia fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Qatar Mining, Abdulazizi Abubakar, amesema kampuni hiyo iko tayari kuangalia maeneo ya ushirikiano yatakayochangia maendeleo ya Sekta ya Madini na kunufaisha Tanzania na Qatar.