Moshi. Makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao kwa nyakati tofauti walivuliwa au kusimamishwa katika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, wameanzisha mchakato wa kisheria kupinga hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
Makada hao wamefungua maombi katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dodoma, wakitaka kupatiwa kibali cha kuanzisha mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi wa kusimamishwa au kuondolewa kwao katika nafasi za uongozi.
Maombi hayo yaliyofunguliwa chini ya hati ya dharura yamepangwa kusikilizwa Agosti 25, 2026, mbele ya Jaji Amir Mruma.
Katika shauri hilo, waombaji wameitaja Bodi ya Wadhamini ya Chadema kuwa mjibu maombi wa kwanza, Katibu Mkuu wa Chadema mjibu maombi wa pili, huku Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakitajwa kuwa wajibu maombi wa tatu na nne mtawalia.
Waombaji hao wanaowakilishwa na wakili Joseph Kipeche, ni Barnabas Okola, Lembrus Mchome, Joseph Mwakidasi, Mathias Cosmas na Abubakari Mashambo.
Okola ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, ambaye alisimamishwa nafasi yake ya uongozi Julai 9, 2026, lakini baadaye akakata rufaa na kurejeshwa katika nafasi hiyo.
Mchome, kwa upande wake ni mwanasiasa ambaye alivuliwa uongozi na kufukuzwa uanachama wa Chadema Mei 2025, kufuatia mvutano ulioibuka baada ya kuhoji na kupinga uteuzi wa viongozi wa sekretarieti ya chama hicho.
Wengine ni Mwakidasi, aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Muheza; Cosmas, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilindi; na Mashambo, ambaye anatajwa kuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.
Mashambo alisimamishwa na uongozi wa chama kuanzia Julai 10, 2026, kufuatia mivutano na kauli zilizohusu ukosoaji wa mambo ya ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Kwa nini wamekimbilia kortini?
Kwa mujibu wa maombi yao yaliyowasilishwa kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa e-Services Portal, wameomba shauri lao lisikilizwe kwa dharura.
Katika hati zao, waombaji wanadai kuwa Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa Chadema wameanzisha taratibu za kinidhamu dhidi yao na hatua hizo zinaweza kuwaweka katika mazingira ya kuadhibiwa mara mbili kwa tuhuma zinazofanana.
“Wajibu maombi wa kwanza na wa pili wameanzisha taratibu za kinidhamu dhidi ya waombaji. Isipokuwa maombi haya yasikilizwe kwa dharura, waombaji watapata adhabu mara mbili,” wameeleza katika maombi yao.
Waombaji pia wanadai kuwa walisimamishwa na wajibu maombi hao kabla ya kusikilizwa na baadaye walipewa taarifa ya kuwasilisha utetezi wao dhidi ya tuhuma hizo hizo, huku hatua ya kuwasimamisha katika nafasi za uongozi ikiwa tayari imechukuliwa.
Kupitia maombi hayo, wanaiomba Mahakama Kuu iwape kibali cha kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama (judicial review) kupinga uamuzi wa kusimamishwa au kuondolewa kwao katika nafasi za uongozi. Kupata kibali hicho ni hatua ya awali inayotakiwa kisheria kabla ya shauri la mapitio ya kimahakama kuendelea kusikilizwa.
Shauri hilo linakuwa miongoni mwa kesi zinazohusu migogoro ya ndani ya Chadema kufikishwa mahakamani katika kipindi cha hivi karibuni.
Kabla ya shauri hilo, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake wawili, walifungua kesi namba 8323 ya mwaka 2025 katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika shauri hilo, walikuwa wakilalamikia kile walichodai kuwa ni kutokuwepo kwa mgawanyo sawa wa rasilimali, fedha na mali za Chadema kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Juni 10, 2025, Jaji Hamidu Mwanga, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, alitoa amri ya kuzuia Chadema kufanya shughuli za kisiasa nchini na kutumia mali zake hadi shauri hilo litakapomalizika. Inaelezwa kuwa amri hiyo ilidumu kwa siku 309.
Hata hivyo, Aprili 15, 2026, Mahakama ya Rufaa ilifuta amri hiyo, ikisema Mahakama Kuu ilikosea kuendelea na usikilizwaji wa shauri baada ya mawakili wa wadaiwa kujiondoa.
Uamuzi huo uliiondoa Chadema katika zuio la kufanya shughuli zake za kisiasa na kutumia mali zake.
Zuio hilo lilikuwa limeathiri uwezo wa chama hicho kufanya mikutano, kampeni na kutumia mali zake katika kipindi kilichotangulia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Chadema ilidai kuwa utekelezaji wa amri hiyo pia ulisababisha uharibifu wa baadhi ya mali zake na kunyima wanachama haki ya kushiriki katika shughuli za kisiasa.
Baadaye, Mei 28, 2026, Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu alitupilia mbali kesi hiyo kwa maelezo kwamba kulikuwa na dosari za kisheria katika madai yaliyowasilishwa.
Juni 6, 2026, Kamati ya Utendaji ya Chadema Kanda ya Pemba ilimfukuza Said Issa Mohamed kutoka katika chama hicho, kwa madai ya kukiuka Katiba ya Chadema.
Hata hivyo, Mohamed ameendelea kupigania masuala yanayohusu chama hicho mahakamani, baada ya yeye na mwenzake kufungua shauri jipya namba 13832 la mwaka 2026 katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, likiwa na maudhui yanayohusu mgawanyo wa mali na rasilimali za chama hicho.

