_*Waziri Mkuu asema anatosha, kiti kimempata mtu sahihi wa kumsaidia Mheshimiwa Rais.*_
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo (Ijumaa, Agosti 28, 2026) limemthibitisha Mheshimiwa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Ndejembi amepitishwa kwa asilimia 100 ya kura zote 324 zilizopigwa na waheshimiwa wabunge, ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyoionesha kwake kwa kumteua kuwa Makamu wa Rais na katika nafasi nyingine mbalimbali za uongozi.
Pia Mheshimiwa Ndejembi amelishukuru Bunge kwa imani kubwa waliyompa kiasi cha kumpigia kura kwa asilimia mia moja.
Mapema akiwasilisha hoja ya kuthibitisha uteuzi wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Mheshimiwa Deogratius Ndejembi anatosha na ni mtu sahihi wa kumsaidia Mheshimiwa Rais katika nafasi ya Makamu wa Rais,
akiitaja kuwa ni nafasi yenye dhamana na majukumu makubwa katika uongozi wa nchi.
“Majukumu hayo yanahitaji mtu mwenye uzoefu wa uongozi, uelewa mpana wa shughuli za Serikali, uwezo wa kufanya kazi kwa karibu na Rais, busara katika kushughulikia masuala ya kitaifa, pamoja na uwezo wa kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali,” amesema Dkt. Mwigulu.
“Mheshimiwa Rais amemteua Mheshimiwa Deogratius John Pancras Ndejembi kwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine, uzoefu alioujenga katika uongozi wa kisiasa na katika nafasi mbalimbali za Serikali,” ameongeza Waziri Mkuu.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa uzoefu wa uongozi alionao Mheshimiwa Deogratius Ndejembi unadhihirisha kuwa ni mtu sahihi kutumikia wadhifa wa Makamu wa Rais.
“Mheshimiwa Deogratius John Pancras Ndejembi si mgeni katika uongozi wa Umma na katika siasa za nchi yetu. Kabla ya kuwa Mbunge, Mheshimiwa Ndejembi alihudumu kama Mkuu wa Wilaya katika Wilaya ya Kongwa. Mheshimiwa Spika, baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge, Mheshimiwa Ndejembi ameendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na kupewa majukumu mbalimbali ndani ya Serikali.”
“Amehudumu katika nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kabla ya kuhudumu kama Waziri wa Nishati,” ameongeza Waziri Mkuu.
Dkt. Mwigulu amesema katika kipindi ambacho amehudumu ndani ya Serikali, Mheshimiwa Ndejembi ameonesha uwezo wa kubeba majukumu mbalimbali na kufanya kazi katika sekta zenye mahitaji na changamoto zinazotofautiana, akisisitiza kuwa uzoefu huo ni muhimu kwa Makamu wa Rais ambaye, kwa nafasi yake, anatakiwa kuwa tayari kumsaidia Rais katika masuala mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano na kutekeleza majukumu yoyote atakayokabidhiwa kwa mujibu wa Katiba.
“Kwa kuzingatia majukumu ya Kikatiba ya Makamu wa Rais niliyoyaeleza, pamoja na uzoefu wa kisiasa, kiutawala na kiutendaji wa Mheshimiwa Deogratius John Pancras Ndejembi, Serikali inaamini kuwa ana uwezo wa kutekeleza kwa uaminifu na ufanisi majukumu ya nafasi ya Makamu wa Rais na kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuendeleza shughuli za Serikali na maendeleo ya Taifa letu,” amefafanua Dkt. Mwigulu.