Fedelica Myovela mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga
NA MATUKIO DAIMA MEDIA , MAFINGA
HALMASHAURI ya Mji Mafinga imeeleza kuwa ina mali zenye thamani ya takribani Sh bilioni 73, huku mali mpya zenye thamani ya Sh bilioni 3.8 zikinunuliwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2026.
Huku ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa chini ya uwakilishi wa George Sangai ambae ni afisa usimamizi fedha ofisi ya mkuu wa mkoa ikiipongeza Halmashauri hiyo kuwa mkoa unajivunia sana kuwa Halmashauri ya mfano .
“Mkoa unajivunia sana mafanikio makubwa ya Halmashauri ya Mji Mafinga kweli madiwani ,watumishi na mkurugenzi mpo vizuri sana “
Aidha, taarifa za fedha za Halmashauri hiyo zinaonesha mtaji wake umefikia Sh bilioni 80.57.
Mhasibu Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Billiard Mlindoko
Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Billiard Mlindoko, wakati akiwasilisha rasimu ya taarifa za hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani.
Mlindoko amesema taarifa hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali za Mitaa pamoja na Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS).
Amesema Halmashauri pia inatumia mfumo wa MUSE katika shughuli za uhasibu na ufungaji wa hesabu, ikiwa ni sehemu ya matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa fedha za umma.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miongozo ambayo tunaitumia ya Serikali za Mitaa, lakini pia kuna miongozo ya kimataifa inayojulikana kama IPSAS. Pia tunatumia mfumo wa MUSE katika ufungaji wa hesabu,” amesema Mlindoko.
Akizungumzia hatua za uandaaji na uwasilishaji wa hesabu hizo, amesema Halmashauri inatakiwa kuwasilisha rasimu ya taarifa ifikapo Agosti 31 ya kila mwaka.
Baada ya hatua hiyo, Halmashauri hupewa muda wa mwezi mmoja kufanya marekebisho yanayohitajika kabla ya taarifa kamili kuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi.
“Taarifa hii huwa inawasilishwa tarehe 31 Agosti ya kila mwaka na ndiyo maana leo tunawasilisha. Baada ya kumaliza tutaunganisha katika kitabu tunachotakiwa kuwasilisha ili kiwe rasimu,” amesema.
Ameongeza kuwa marekebisho yote yanapaswa kukamilishwa ifikapo Septemba 30, kwa mujibu wa mwongozo, kabla ya taarifa hizo kuwa tayari kwa ajili ya ukaguzi.
Mlindoko amesema taarifa ya hesabu inajumuisha taarifa kuhusu muundo wa Halmashauri, madiwani, kamati mbalimbali za Baraza la Madiwani, vikao, shughuli za kiuchumi pamoja na utekelezaji wa bajeti.
Pia inaonesha huduma zinazotolewa kwa wananchi, miradi ya maendeleo inayotekelezwa, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali.
BAKAA YA FEDHA SH BILIONI 2.7
Akizungumzia taarifa ya hali ya kifedha (financial position), Mlindoko amesema hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha, Halmashauri ilikuwa na bakaa ya fedha ya takribani Sh bilioni 2.7.
Pia ilikuwa ikidai watu na taasisi mbalimbali takribani Sh milioni 115.
“Katika mali za muda mfupi tuna bakaa ya Sh bilioni 2.7, lakini pia kuna watu tunaowadai katika Halmashauri ambapo tuna Sh milioni 115 na mchanganuo wake umeoneshwa katika taarifa hii,” amesema.
Mbali na mali za muda mfupi, amesema Halmashauri ina mali za muda mrefu (non-current assets), zikiwemo majengo, vifaa na mali nyingine zinazotarajiwa kutumika kwa kipindi kinachozidi mwaka mmoja.
Kwa mujibu wa Mlindoko, katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2026, Halmashauri ilinunua mali mbalimbali zenye thamani ya Sh bilioni 3.8.
“Kwa mwaka huu wa fedha ulioishia Juni 30, 2026, tumeweza kununua mali zenye thamani ya Sh bilioni 3.8. Kwa hiyo, mali zetu kwa jumla zimefikia takribani Sh bilioni 73,” amesema.
Ameeleza kuwa taarifa hiyo imeambatanishwa na mchanganuo wa mali zilizonunuliwa katika mwaka husika ili kurahisisha uhakiki na ukaguzi wa hesabu.
MADENI YA HALMASHAURI
Kwa upande wa madeni, Mlindoko amesema Halmashauri ina madeni mbalimbali ya muda mfupi, yakiwemo ya zabuni, watumishi na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Pia yapo madeni yanayohusiana na michango ya mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na fedha za amana zinazoshikiliwa na Halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli na miradi ya Serikali.
“Katika madeni ya muda mfupi tuna madeni ya zabuni, madeni ya watumishi, deni la NHIF na michango ya mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Pia tuna fedha za amana ambazo nazo ni deni kwa sababu fedha hizo zipo kwenye miradi ya Serikali,” amesema.
Mlindoko amesema taarifa za fedha pamoja na viambatanisho vyake zina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha hesabu za Halmashauri zinakaguliwa kwa ufanisi, kwa kuwa wakaguzi huhitaji nyaraka na vielelezo mbalimbali kuthibitisha taarifa zilizowasilishwa.
Rasimu hiyo ya hesabu za mwisho za Halmashauri ya Mji Mafinga kwa mwaka wa fedha 2025/2026 inapaswa kujadiliwa na Baraza la Madiwani kabla ya kukamilishwa na kuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi.
Hesabu hizo zinaonesha hali ya kifedha ya Halmashauri, ikiwemo mali, madeni, mtaji na utekelezaji wa bajeti pamoja na majukumu mbalimbali yaliyotekelezwa katika mwaka husika.
Uandaaji na uwasilishaji wa taarifa hizo ni sehemu ya taratibu za uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma, zinazolenga kuweka wazi namna rasilimali za Halmashauri zilivyokusanywa, kutumika na kusimamiwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Hata hivyo chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi kupitia mwenyekiti wake wilaya George Kavenuke akimpongeza mhasibu huyo na kushauri semina ya fedha kwa madiwani kutolewa zaidi.
Reginant Kivinge Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Mji Mafinga alisema mafanikio hayo yanatokana na ushirikino mzuri wa madiwani ,watumishi chini ya mkurugenzi Fedelica Myovela .
Hata hivyo alisema mafanikio makubwa zaidi yataendelea kuonekana iwapo madiwami na watumishi kila mmoja kutimiza wajibu wake .
Katika baraza hilo la madiwani mkurugenzi wa Halmashauri hiyo aliwakilishwa na kaimu mkurugenzi Peter Ngussa ambae alisema Halmashauri hiyo imejipanga kuendelea kutekeleza malengo yake na mipango ya serikali kupitia Dira 2050.
TAZAMA VIDEO YA BARAZA BOFYA LINK HII










