Mo Dewji kuwekeza Sh661 bilioni Msumbiji

Maputo. Bilionea wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohammed Dewji, maarufu Mo ameahidi kuwekeza Dola 250 milioni (Sh661.93 bilioni), nchini Msumbiji na ahadi ya kuajiri raia 20,000 wa nchi hiyo.

Mo alitoa ahadi hiyo baada ya kukutana na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo mjini Maputo Jumanne ya Agosti 18, 2026, akisema mazungumzo yao yalikuwa na tija na tayari amebaini fursa kadhaa za uwekezaji nchini humo.

“Tumekuwa na mazungumzo yenye tija na tumedhamiria kuwekeza Dola 250 milioni nchini Msumbiji na kuajiri watu 20,000,” amesema Mo.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikuelekeza fedha hizo zitaelekezwa katika sekta gani wala ratiba ya kuanza kwa uwekezaji huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ureno (Lusa), taarifa iliyotolewa na Ikulu Msumbiji inaeleza ahadi iliyotolewa na Dewji inaendana na shughuli za MeTL, inafungua fursa za uwekezaji katika maeneo ya kimkakati pamoja na kuanzishwa kwa minyororo mipya ya uzalishaji, usambazaji na huduma nchini humo.

Taarifa hiyo ilisema mkutano huo umefanyika wakati Serikali ya Msumbiji ikitafuta kuongeza uwekezaji binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi, uendelezaji wa viwanda na uundaji wa ajira, huku ikiimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika.

MeTL ni miongoni mwa biashara za binafsi zinazomilikiwa na Watanzania, ikiwa na shughuli katika kilimo, uzalishaji viwandani, usafirishaji na ugavi, nishati, biashara na huduma za kifedha.

Kampuni hiyo inaajiri takribani watu 37,000 na tayari ina shughuli katika zaidi ya nchi 12 za Afrika, ikiwamo Msumbiji.

Taarifa hiyo ikiwa ahadi hiyo itatekelezwa, ajira 20,000 zitakazotengenezwa zitaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wafanyakazi wa kundi hilo nchini humo.

Msumbiji imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kuvutia mitaji binafsi nje ya miradi ya gesi asilia katika mkoa wa Cabo Delgado ambako uasi umesababisha kuchelewa mara kadhaa kwa utekelezaji wa miradi hiyo.

Dewji, mwenye umri wa miaka 51, alichukua uongozi wa biashara iliyoanzishwa na baba yake, Gulam miaka ya 1970 kama kampuni ya biashara na baadaye akaipanua kuwa kundi lenye shughuli za uzalishaji wa nguo, mafuta ya kula, unga, vinywaji na usindikaji wa mazao ya kilimo.

Jarida la Forbes linakadiria utajiri wake kuwa Dola 2.1 bilioni (sawa na Sh5.56 trilioni) jambo linalomfanya kuwa mtu wa 14 kwa utajiri barani Afrika na Mtanzania pekee aliyeorodheshwa kwenye orodha hiyo.

Dewji aliwahi kuwa mbunge wa Singida Mjini kwa vipindi viwili, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 pia alikuwa Mtanzania wa kwanza kusaini Giving Pledge akiahidi kutoa angalau nusu ya utajiri wake kwa shughuli za kijamii.

Mbali na biashara, Dewji anamiliki asilimia 49 ya Simba Sports Club Company Limited, klabu ya soka ya Dar es Salaam na Agosti mwaka huu aliahidi takribani Dola 11.3 milioni (takribani Sh29.9 bilioni) kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na kituo cha mazoezi cha klabu hiyo eneo la Bunju, ikiwa ni pamoja na idhini ya Bodi ya Wadhamini.