Tanzania, DR Congo kuimarisha ushirikiano, kuondoa vikwazo

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi na kukubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo makuu saba.

Maeneo hayo yamejikita katika, miundombinu, biashara, usafirishaji, kilimo, madini, reli na uvuvi, kuimarisha sekta binafsi na kuondoa vikwazo mipakani.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ndogo Zanzibar leo Agosti 18, 2026 Rais Samia amesema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na DRC unatoa nafasi muhimu ya kuimarisha maeneo mengine ya kimkakati.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukishirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uchukuzi na miundombinu. Takwimu mpaka mwaka jana zinaonyesha kwamba nchi yetu hufanya biashara ya Sh794 bilioni, na DRC,” amesema.

Rais Samia amesema, bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi ya DRC, wakati nchi hizo mbili zimeendelea kushirikiana kupitia ushoroba wa kati ambao ni mtandao jumuishi wa usafirishaji unaounganisha DRC na masoko ya kimataifa kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili Ikulu Ndogo ya Zanzibar, Agosti 18, 2026.

“Ni kwa msingi huo, leo katika mazungumzo yetu na Mheshimiwa Rais Tshisekedi tumeupa umuhimu mkubwa mradi wa miundombinu jumuishi ya uchukuzi (Multimodal Transportation Project),” amesema Rai Samia.

Amefafanua kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa katika kuunganisha bandari, reli, barabara, na usafiri wa majini, na hivyo kupunguza gharama na muda wa usafirishaji wa mizigo kupitia Ziwa Tanganyika.

Amesema ushirikiano huo pia utaongeza ufanisi wa ushuru wa kati na kuchochea biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na DRC, pamoja na nchi nyingine jirani.

Samia amesema kwa sasa jitihada za kuendeleza miundombinu ya reli na vituo vya mizigo zinaendelea vyema ikiwemo mwendelezo wa SGR kuelekea maeneo ya magharibi, ambayo baadaye itaunganisha na nchi za Burundi na DRC.

Amesema wanaendelea pia na uboreshaji wa bandari kwenye Ziwa Tanganyika, ikiwemo Kigoma, Tarema, Moba, na Kalemi.

“Mtakumbuka hivi karibuni nikiwa Kigoma nilizindua meli kwa ajili ya kutoa huduma kwenye Ziwa Tanganyika, meli nne na bado tuna jenga nyingine nne ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo pia.”

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ikulu Ndogo ya Zanzibar,  Agosti, 2026.

Amesema asilimia takribani 60 ya mizigo inayopita bandari ya Dar es Salaam ni kutoka DRC, kwa hiyo ni lazima wawe na vyombo vingi vya kusafirisha kwenye maji vitakavyoweza kubeba na kupunguza mzigo Dar es Salaam.

Ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya DRC kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Kalemi-Manono, ambayo itakapokamilika itaunganisha zaidi mataifa hayo na kuchochea shughuli za kiuchumi kwenye nchi mbili na ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.

Sambamba na hayo, kwenye mazungumzo yao pia wawili hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, kuboresha huduma za mipakani, na kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu kadri fursa zinazojitokeza.

“Na tunashukuru Mheshimiwa Rais wa DRC ameeleza jinsi wanavyoishirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa reli kule kwao, lakini na barabara pia, na hata huduma za bandari kama tunavyofanya sisi hapa ili kuharakisha utekelezaji wa miundombinu hiyo,” amesema

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema,”Nimemweleza    Rais wa DRC kwamba, Tanzania inazalisha kwa wingi bidhaa za kilimo, uvuvi, na mifugo, hivyo nawakaribisha kufanya biashara katika maeneo hayo pia.”

Amesema Tanzania na DRC zina utajiri wa rasilimali za madini, na hivyo wamekubaliana kushirikiana katika maeneo hayo, kubadilishana uzoefu na ujuzi, jinsi ya uchimbaji, uongezaji thamani na hata masoko ya madini.

Pia amesema wamewaalika waungane katika kituo cha madini kilichopo nchini kwa ajili ya nchi za Afrika Mashariki na Kati.

“Waungane nasi tubadilishane ujuzi, lakini pia utafiti katika kituo kile.”

Amesema pia katika mazungumzo yao pia  wamegusia masuala ya amani na usalama, ambayo ni nguzo muhimu katika mustakabali wa maendeleo ya mataifa hayo.

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi amesema wamechunguza maeneo kadhaa ambayo tayari wanashirikiana, lakini ambayo wanapaswa kuyaimarisha, na katika maeneo mengine ambayo bado hayajachunguzwa.

“Ndiyo maana kumefanyika uamuzi wa kuifufua tume ya pamoja, tume mchanganyiko, niseme, ili kazi ifanyike kwa kina zaidi, kwa mpangilio na kwa ufanisi,” amesema.

Rais huyo wa DRC amesema ndio maana wamesisitiza zaidi masuala ya amani, usalama na utulivu.

“Pia tumetazama masuala ya kibiashara, masuala ya kubadilishana, kupitia ujenzi wa miundombinu, na kuweka mifumo inayowezesha mabadilishano hayo ya kibiashara. Na naweza kuwaambia kwamba naondoka hapa nikiwa na furaha kubwa na nina matumaini makubwa kuhusu mustakabali mzuri wa ushirikiano kati ya nchi zetu mbili,” amesema Rais Tshisekedi.

Amesema, “Huu ndiyo hasa aina ya ushirikiano unaopaswa kuwa kati ya nchi za Kiafrika. “Tuna ardhi, Afrika, bara ambalo limejaa fursa nyingi za maliasili, lakini pia lina nguvu nyingine ambayo mimi naiona kama muhimu zaidi ambayo ni rasilimali watu.”

Amesema takriban asilimia 60 ya idadi ya watu wa Afrika imeundwa na vijana ambao ni dhamana ya mustakabali thabiti. “Kwa sababu vijana wanapaswa kuelekeza tu na kuingia kazini. Kazi hiyo tutaiweka sawa tu pale tutakapotimiza kinachotia moyo yaani kufaulu kubadilisha maliasili zetu wenyewe hapa barani,” amesema.

 “Tumechoka sasa kuwa ardhi ya uchimbaji tu, ambapo tunaona madini yetu yanatoka ardhini yakiwa mabichi na kwenda kubadilishwa thamani mahali pengine, kupata thamani iliyoongezwa mahali pengine, wakati barani tunaweza kufanya hayo,” amesema

Rais Tshisekedi amemshukuru Rais Samia kumpa rambirambi kuhusu ugonjwa wa Ebola ambapo pia huo ni uthibitisho wa uimara huo wa Afrika.

“Ningependa kueleza ndugu zetu Watanzania kuhusu Ebola,tupo kwenye mlipuko wa 17 na kwa hiyo tumepitia milipuko yote 16, hivyo  msiruhusu kabisa jambo hili likutisheni,”

Amesema  wana uzoefu unaotambuliwa duniani kote katika kudhibiti na kukabiliana na ugonjwa huo.

Watano wafariki dunia akiwamo mtoto mchanga, wanane wajeruhiwa Lushoto

Tanga. Watu watano akiwemo mtoto mchanga wa miezi sita, wamefariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Coaster kutumbukia bondeni katika eneo la Vuga, Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga.

Ajali hiyo imetokea leo, Agosti 18, 2026, saa 7:30 mchana katika barabara ya Mombo–Lushoto.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, gari hilo lilikuwa likitokea Tanga Mjini kuelekea Ngwashi, likiendeshwa na Ally Dione.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema watu watano wamepoteza maisha katika ajali hiyo, huku miili yao ikiwa bado haijatambuliwa.

Amesema waliokufa ni wanaume wawili wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 hadi 45, wanawake wawili wenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 25 na 35, pamoja na mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na miezi sita.

Aidha, watu wanane wamejeruhiwa na wamelazwa katika Kituo cha Afya Soni, Wilaya ya Lushoto, kwa ajili ya matibabu.

Mchunguzi amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa ajali hiyo inadaiwa kusababishwa na uzembe wa dereva, aliyeshindwa kulimudu gari, hali iliyosababisha kuacha barabara na kutumbukia bondeni.

“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi, kutambuliwa na taratibu nyingine za kisheria,” amesema.

Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo na mazingira kamili ya ajali hiyo.

Jeshi hilo limetoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuwa makini na kuhakikisha wanaendesha kwa umakini ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Aidha, limewakumbusha watumiaji wote wa barabara kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja.

Madeleka aeleza namna alivyokamatwa Mahakama Kuu

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kumwachia kwa dhamana, Wakili Peter Madeleka ameeleza namna alivyokamatwa katika viunga vya Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi eneo la Mikocheni.

Madeleka alikamatwa Agosti 14, 2026 na kushikiliwa kwa siku tatu katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa tuhuma za kudharau amri za Mahakama Kuu zilizotolewa Julai 17 na Agosti 13, 2026.

Akizungumza leo Jumanne, Agosti 18, katika ofisi za Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Madeleka amesema alikamatwa akiwa anatimiza majukumu yake ya kikazi mahakamani.

“Walinikamata baada ya kujitambulisha kuwa ni askari wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na walinitaka niambatane nao. Nilipowaambia kuwa nipo mahakamani kuna kesi inaendelea; na kuwaomba niambatane nao hadi kwa jaji kutoa taarifa, walikataa,” amesema wakili Madeleka.

Amesema alipelekwa katika ofisi ya Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu na kuambiwa tuhuma zinazomkabili ni kudharau Mahakama.

Madeleka amesema baada ya kuelezwa tuhuma hizo, alipewa fursa ya kuwasiliana na familia na mawakili wake, ambao walihakikisha anapata dhamana.

Amesema alikaa mahabusu kwa saa kadhaa kabla ya kuhamishiwa kituo kingine usiku akiwa chini ya ulinzi, na Agosti 15 kurejeshwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Wakili Peter Madeleka akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 18, 2026 katika ofisi za Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) aliyekaa kushoto ni Wakili Maduhu William. Picha na Sute Kamwelwe.

Kuhusu amri inayodaiwa kuidharau, Madeleka amesema hana taarifa kuhusu amri hiyo wala hakumbuki kama Mahakama ilitoa amri yoyote Agosti 13, 2026.

Amesema kifungu cha 114 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16) kinaeleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa mtu anayekiuka amri ya Mahakama.

Hata hivyo, Wakili Madeleka amewashukuru polisi kwa kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo, akisema unaweza kusaidia kufikisha suala hilo mahakamani ili sheria ipate nafasi ya kutafsiriwa.

“Namuomba Mkurugenzi wa Mashtaka anipeleke mahakamani ili kukuza sheria yetu,” amesema Wakili Madeleka.

Amesema hajawahi kumdharau jaji au hakimu wala kufikishwa katika kamati ya maadili na kutiwa hatiani kwa kosa hilo.

Hivyo, amesema haoni kama amewadharau majaji, akisema anatambua maadili ya taaluma yake na mamlaka ya mhimili wa Mahakama.

“Kesi hii ni nzuri sana ambayo wananchi wanapaswa kuifuatilia kwa ukaribu, kwanza katika macho ya sheria, je, kesi ya kudharau Mahakama inapelelezwaje na polisi?” amehoji.

Akizungumzia hilo, Wakili William Maduhu amesema walihangaika usiku na mchana kwa siku tatu kuhakikisha Madeleka anaachiwa, huku akisema iwapo kuna kesi dhidi yake, wanaamini itapelekwa mahakamani.

Jumatatu Agosti 17, Wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Paul Kisabo alisema Madeleka alipewa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni kwa siku alizopangiwa na polisi.

Makosa matatu yasababisha daladala 203 kufungiwa VTS

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeanza kufunga vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari (VTS) katika daladala zinazofanya safari za mijini, hatua inayolenga kudhibiti ukiukwaji wa masharti ya leseni na kuboresha huduma kwa abiria.

Hadi Agosti 12, 2026, jumla ya daladala 203 jijini Dar es Salaam zilikuwa zimefungiwa vifaa hivyo kutokana na ukiukwaji wa masharti ya uendeshaji, huku gharama za ufungaji zikibebwa na wamiliki wa magari husika.

Akizungumza na Mwananchi Agosti 13, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Latra, Salum Pazzy, amesema hatua hiyo imeanza Dar es Salaam kutokana na ukubwa wa changamoto za usafiri wa daladala katika jiji hilo.

Amesema makosa yanayoongoza katika hatua hiyo ni upandishaji wa nauli kinyume cha viwango vilivyowekwa, kukatisha safari kabla ya kufika mwisho wa ruti na kutumia njia ambazo hazijaidhinishwa.

“Tumefanya tathmini na kuona ni busara kuanza kufunga vifaa kwenye magari ya mijini yenye changamoto hizo, hasa Dar es Salaam, kwa sababu kuna daladala nyingi na changamoto hii ni kubwa zaidi,” amesema Pazzy.

Kwa mujibu wa Latra, VTS haitumiki kudhibiti mwendo wa magari pekee, bali pia kufuatilia utekelezaji wa masharti ya leseni na kusaidia kubaini ukiukwaji unaojitokeza mara kwa mara.

Pazzy amesema matumizi ya teknolojia yameanza kuleta matokeo, kwa kuwa madereva na wamiliki wanapotambua mwenendo wa gari unaweza kufuatiliwa, huongeza utii wa sheria na kuboresha huduma kwa abiria.

Amesema masharti ya leseni yanataka watoa huduma kuzingatia nauli zilizowekwa, njia zilizoidhinishwa, usafi wa magari, matumizi ya sare na kuwafikisha abiria katika maeneo yaliyokusudiwa.

Pia, daladala zinatakiwa kuonesha wazi viwango vya nauli na njia zinazotumika ili abiria ajue kiasi anachopaswa kulipa na aweze kudai haki yake anapotozwa zaidi.

Pazzy amewataka abiria kutoshiriki katika ukiukwaji wa nauli kwa kuacha kulipa kiasi kinachotakiwa kwa mujibu wa viwango rasmi. Pia amewataka wamiliki wa daladala kuajiri madereva na makondakta wanaotambulika na Latra ili kuongeza uwajibikaji katika huduma za usafiri wa umma.

Mkazi wa Dar es Salaam, Eliya Dachi, amesema baadhi ya daladala za Mwenge-Mbezi huongeza nauli wakati wa jioni kutoka Sh800 hadi Sh1,000.

“Wao hawajali, muda ukifika jioni nauli inabadilika. Wanataka watu walipe Sh1,000 hata kama mtu anashukia njiani,” amesema Dachi.

Matilda Joseph, mkazi wa Kivule, amesema wakazi wa maeneo hayo wanapata changamoto ya usafiri kutokana na daladala nyingi zenye ruti ya Fremu 10 huishia Kivule Sokoni.

Kwa upande wake, dereva wa daladala za Gongo la Mboto, Colnell Mushi, amesema mfumo huo unaweza kusaidia, lakini Latra inapaswa kuhakikisha hatua zinazochukuliwa zinategemea ushahidi wa kutosha.

“Isije kuwa ni uonevu kwa madereva na makondakta. Tunataka ushahidi wa kutosha ili mtu asiadhibiwe kwa sababu ya malalamiko binafsi,” amesema.

Wadau kujadili maendeleo ya kidijitali, data ikipewa kipaumbele

Zanzibar. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa tamasha la data Africa 2026, tukio litakalowakutanisha zaidi ya washiriki 300, mashirika zaidi ya 100, kutoka nchi 30 litakalofanyika katika Hoteli ya Verde, Zanzibar.

Tamasha hilo litakalofanyika siku tatu limeandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania Data Lab (dLab) na Pollicy Uganda, ikiwa ni pamoja na  ushirikiano wa karibu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu ya Zanzibar.

Linatarajia kuonyesha namna taasisi, wabunifu na jamii za Afrika zinavyovuka hatua ya mijadala na kuanza kujenga suluhisho halisi kwa kutumia data, teknolojia za kidijitali na Akili Unde (AI).

Akizungumza kuhusu tamasha hilo leo Agosti 18, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Data Lab, Dk Mahadia Tunga amewahimiza wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi na kwa fahari katika tukio hilo.

“Data inasaidia kubaini vipaumbele vya maendeleo na kuhakikisha kuwa rasilimali zetu chache zinatumiwa kwa ufanisi barani kote. Data Tamasha Africa ni jukwaa kuu la kukutana, kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa, na kujadili kwa uwazi changamoto tunazoshirikiana kwa sababu hakuna mafanikio yanayokuja bila vikwazo,” amesema Dk Mahadia.

Kwenye tamasha hilo lenye kauli mbinu isemayo: “Kujenga na Data / Building with Data,” washiriki wataonesha suluhisho za Akili Unde (AI) zilizobuniwa Afrika, mifumo ya data inayotokana na mahitaji ya jamii, ubunifu katika huduma za kidijitali na teknolojia zinazolenga kutatua changamoto halisi za maendeleo barani Afrika.

Tamasha hilo litawakutanisha wanasayansi wa data, watunga sera, watafiti, wabunifu, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, vijana na wabunifu wa sanaa.

Pia litatoa nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kuanzisha ushirikiano mpya.

Kwa Zanzibar, kuwa mwenyeji wa Data Tamasha Africa 2026 kunaimarisha nafasi yake kama kitovu kinachokua cha ubunifu wa kidijitali, maendeleo yanayoongozwa na data na utawala wa kidijitali Afrika Mashariki.

Naye Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uvumbuzi, Mudrik Ramadhan Soraga amesema Zanzibar imejipanga kikamilifu kuwa mwenyeji wa tukio hilo.

Pia amesema kuandaa jukwaa hilo kutainua hadhi ya Zanzibar kimataifa kama kitovu cha uvumbuzi wa kidijitali, huku likiwavutia wawekezaji katika Tehama, elimu, biashara na huduma za jamii.

“Tunataka kuona data na teknolojia zikitumika kama zana za kuongeza tija, uwajibikaji na maendeleo endelevu,” amesema Soraga.

*MKAKATI WA TAIFA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA WAANZA KUTEKELEZWA MKINGA*

📌*Mitungi ya gesi ya kilo sita 3,255 kuuzwa kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 17,500*

📍*Mkinga, Tanga*

Serikali imeanza kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, kupitia mradi wa usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku.

Kupitia mradi huo, jumla ya mitungi 3,255 ya gesi ya kilo sita itasambazwa na kuuzwa kwa wananchi wa Mkinga kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 17,500 kwa mtungi.

Mwananchi anayehitaji kunufaika na mpango huo anatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA). Mtungi huo utauzwa ukiwa tayari kwa matumizi, ukiwa na gesi pamoja na vifaa muhimu.

Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi, salama na rafiki kwa afya na mazingira, huku ukipunguza utegemezi wa nishati zinazoweza kuwa na madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

Wananchi wa Mkinga wameishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, wameipongeza REA kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha unawafikia walengwa, hususan wananchi wa kipato cha chini.

Wamesema mradi huo utawasaidia kupata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, jambo litakalosaidia kuboresha afya, kuhifadhi mazingira na kuongeza ubora wa maisha ya wananchi.

*Mwisho*

Wimbi la magonjwa ya upumuaji linavyoathiri watoto

Dar es Salaam. Madaktari wamesema kati ya asilimia 50 hadi 70 ya watoto wanaofikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu katika kipindi hiki husumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa upumuaji, huku hali ya baridi na vumbi ikitajwa kuchangia kuongezeka kwa matatizo hayo.

Wamesema mbali na watoto, watu wazima nao wameendelea kupata changamoto za mafua na kikohozi katika kipindi hiki.

Magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayoathiri pua, koo, mirija ya hewa na mapafu, yanaweza kusababishwa na virusi, bakteria, vumbi au moshi.

Takwimu za Wizara ya Afya za Julai 2025 hadi Machi 2026 zinaonesha maambukizi ya mfumo wa upumuaji yalikuwa miongoni mwa magonjwa yaliyoongoza kwa wagonjwa waliofika katika huduma za afya.

Kwa watoto walio chini ya miaka mitano, maambukizi hayo yaliathiri wagonjwa milioni 4.46, sawa na asilimia 36.8, huku kwa wenye miaka mitano na zaidi, walioathirika wakiwa milioni 3.46.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, maambukizi ya mfumo wa upumuaji pia yaliongoza kwa magonjwa yaliyowasumbua wagonjwa waliolazwa, yakifuatiwa na maambukizi ya njia ya mkojo kwa asilimia 9.4 na maambukizi ya ngozi kwa asilimia 3.1.

Takwimu hizo zimetajwa katika Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2026/27.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Agosti 18, 2026, Daktari wa Watoto, Sagumo Chotta amesema watoto walio chini ya miaka mitano wanaathirika zaidi kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

“Matatizo mengi ambayo wazazi wanawaleta watoto hospitalini kwa kipindi hiki ni mafua na kikohozi. Hilo ndilo tatizo kubwa kwa watoto, ingawa wapo baadhi wanaoathirika na nimonia,” amesema Dk Chotta.

Amesema watoto wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa kutokana na kukaa katika mikusanyiko, ikiwamo shuleni na wakati wa kucheza.

“Karibu asilimia 50 hadi 70 ya watoto wanaofikishwa hospitali hivi sasa ni kutokana na matatizo hayo. Kundi hili ni rahisi kuambukizwa kwa kuwa huwa kwenye mikusanyiko, hata wanapokuwa shuleni,” amesema.

Dk Yusuph Mneka amesema mazingira yasiyo safi nyumbani pia yanaweza kuwaweka watoto katika hatari ya kupata maambukizi yanayosababishwa na bakteria, virusi na fangasi.

“Watoto chini ya miaka miwili wanaofikishwa hospitalini sasa, wengi wanaumwa mafua ambayo huwafanya kushindwa kupumua. Kila kundi linakuja na changamoto yake,” amesema.

Ili kudhibiti hali hiyo, Dk Mneka amesisitiza umuhimu wa wazazi kuhakikisha watoto wanapata chanjo, wanazingatia usafi na kuwapeleka hospitalini wanapoonesha dalili za ugonjwa.

Akizungumzia changamoto hiyo, Dk Jida Said amesema matatizo ya mfumo wa upumuaji hayaishii kwa watoto, bali hata watu wazima wanakabiliwa nayo hivi sasa.

“Virusi vya mafua na kifua vinawaathiri sana pia watu wazima na hii inatokana na hali ya hewa ilivyo sasa,” amesema.

Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ramadhani Omary amesema kipindi hiki kina ni cha baridi na vumbi, hali inayoweza kuchochea magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

“Sasa hivi ni msimu wa vumbi na baridi. Katika kipindi cha baridi na vumbi, magonjwa ya macho na kifua hujitokeza, kwa hiyo hali hii ya hewa inachangia,” amesema.

Wakati huo huo, utafiti uliochapishwa Juni mwaka huu na watafiti wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) umeonesha kuwa kuishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko mara kwa mara kunaongeza hatari ya kupata magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji.

Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Kisayansi la GeoHealthJuni, 2026, uliongozwa na Dk Ibrahim Msuya kwa kushirikiana na watafiti kutoka IHI na Chuo Kikuu cha Cork nchini Ireland.

Watafiti hao, wametumia taarifa za picha za satelaiti kuhusu unyevunyevu wa ardhi pamoja na takwimu za afya kutoka kaya 1,500 katika mitaa 15 yenye viwango tofauti vya kipato jijini Dar es Salaam.

Matokeo yanaonesha wakazi wa maeneo yenye mafuriko mengi walikuwa na uwezekano wa hadi mara tisa kuugua magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji ikilinganishwa na wanaoishi katika maeneo makavu.

Aidha, kila ongezeko la unyevunyevu wa ardhi lilihusishwa na ongezeko la takribani asilimia 18 la hatari ya kupata magonjwa hayo.

Utafiti huo pia ulibaini msongamano wa watu katika kaya na matumizi ya maeneo ya pamoja ya kutupa taka, ukihusishwa na ongezeko la hatari ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Watafiti wamependekeza mipango bora ya miji na uboreshaji wa makazi kupewa kipaumbele katika kudhibiti magonjwa hayo, sambamba na hatua nyingine za afya ikiwamo kupunguza uvutaji wa sigara.

PATRICK VIEIRA ATEULIWA KUWA KOCHA MKUU WA SENEGAL

 

Senegal imemteua Patrick Vieira, mshindi wa Kombe la Dunia la 1998 akiwa na Ufaransa, kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa, Shirikisho la Soka la Senegal limetangaza Jumanne.

Vieira anachukua nafasi ya Pape Thiaw, aliyefutwa kazi baada ya Kombe la Dunia lililopita.

Vieira, ambaye ni raia wa zamani wa Ufaransa, ameripotiwa kufikia makubaliano na Shirikisho la Soka la Senegal, FSF, ya kuiongoza timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne.

Mkataba huo unatarajiwa kujumuisha maandalizi ya Senegal kuelekea Kombe la Mataifa ya Afrika la 2027, AFCON, pamoja na mchakato wa kufuzu na maandalizi ya Kombe la Dunia la 2030.

Lengo la haraka la Vieira linadaiwa kuwa kuiongoza Senegal kufika angalau fainali ya AFCON 2027, huku kwa muda mrefu akitarajiwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu Kombe la Dunia la 2030 na kujenga kikosi kitakachoiweka Senegal miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa soka barani Afrika.

Shirikisho hilo limesema uteuzi wa Vieira, aliyezaliwa Senegal, ni “hatua ya kimkakati” inayolenga “kuanzisha mfumo wa kiufundi wa kiwango cha juu, unaoendana na malengo ya michezo ya nchi”.

Kwa mujibu wa taarifa ya BSN Sports, Vieira anatarajiwa kulipwa kati ya faranga milioni 35 na 45 za CFA kwa mwezi, sawa na takriban dola 61,600 hadi 79,200 za Marekani.

Vieira alizaliwa mjini Dakar mwaka 1976 na akawa mmoja wa viungo mashuhuri zaidi wa kizazi chake. Alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya soka la klabu katika Arsenal, ambako alikuwa nahodha na alisaidia klabu hiyo kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya England, ikiwemo msimu maarufu wa 2003 hadi 2004 ambao Arsenal haikupoteza mchezo wowote.

Pia aliwahi kuchezea Juventus, Inter Milan na Manchester City kabla ya kustaafu soka la ushindani.

Akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa, Vieira alicheza mechi 107 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia la FIFA mwaka 1998 nchini Ufaransa. Pia alishinda Mashindano ya Ulaya mwaka 2000 akiwa na Ufaransa.

Uhusiano wake na Senegal ni wa karibu, kwa kuwa alizaliwa Dakar na ameendelea kudumisha uhusiano na nchi hiyo.

Vieira pia ana uhusiano na Diambars, akademi ya soka na mradi wa kukuza vipaji nchini Senegal ambao umetoa wachezaji kadhaa wenye vipaji.

Wazazi sita ‘wabanwa’ kwa watoto kutokwenda shule

Simanjiro.Wazazi na walezi sita katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kushindwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo shuleni.

Hatua hiyo imetangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, jana Agosti 18, 2026, alipozungumza katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.

Makota amesema hatua ya kuwafikisha wazazi hao mahakamani inalenga kuimarisha uwajibikaji wa wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto walio katika umri wa kwenda shule wanahudhuria masomo kwa mujibu wa sheria na taratibu za elimu.

Amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakikosa masomo mara kwa mara bila sababu za msingi, hali inayoweza kuathiri maendeleo yao kielimu na kuongeza uwezekano wa kuacha shule.

“Ninyi madiwani, hata wapiga kura wenu wakija kuwaomba dhamana kwa sababu ya kukamatwa kwa utoro wa watoto wao, msikubali kuwaunga mkono, kwani watazoea kuwazuia watoto kwenda shule,” amesema Makota.

Amewaasa madiwani kuacha tabia ya kuwatetea wazazi wasiotaka watoto wao kwenda shule, kwani inachangia kuongeza utoro na kushuka kwa kiwango cha taaluma shuleni.

“Bahati nzuri, watoto wa jamii ya kifugaji wana akili mno shuleni. Sasa madiwani, msiunge mkono utoro, waelezeni kabisa wapiga kura wenu kuwa elimu ni maendeleo,” amesema.

Diwani wa Naberera, Marco Munga, amesema wazazi na walezi wa eneo hilo wameshapitisha sheria ndogo ya kutoa Sh50,000 na faini ya Sh200,000 mtoto asipokwenda shule.

Munga amesema faini hiyo imelenga kudhibiti utoro kwa kuwabana wazazi na walezi wa wanafunzi kuwatoza fedha ili watoto wao waende shule, wasiende kuchunga mifugo.

“Suala la kudhibiti mimba shuleni, tumewaelekeza wazazi na walezi kuwapima mabinti mara kwa mara ili wazingatie masomo na kuachana na tabia mbaya,” amesema Munga.
Diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi, amesema inatakiwa kujengwa shule nyingine ya msingi ili kuepuka msongamano wa shule mbili za Serikali kwenye eneo hilo.

“Shule zetu mbili za msingi, Songambele na Tanzanite, hivi sasa zina mrundikano mkubwa wa wanafunzi, hivyo tunapaswa kujenga shule nyingine ya msingi,” amesema Salome.

Diwani wa Ngorika, Albert Msole, amesema miundombinu inapaswa kuboreshwa katika Shule ya Sekondari Nyumba ya Mungu ili ikidhi vigezo vya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.

“Mwenyekiti, pamoja na madarasa ya Shule ya Sekondari Nyumba ya Mungu ambayo tuliyojenga, tunapaswa kuboresha miundombinu ili kukidhi vigezo vya elimu ya juu,” amesema Msole.

KANISA LA EBENEZER MBALIZI LAGEUKA FARAJA KWA WAZEE WASIOJIWEZA

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Kanisa la Ebenezer Assemblies of God Africa (EAGA) lenye makao yake makuu mjini Mbalizi wilayani Mbeya, limewagusa wahitaji ambao ni wazee wasiojoweza ndani na nje ya Kanisa hilo kwa kuwasaidia mahitaji ya vyakula.

Mahitaji yaliyotolewa kwa familia tano za wazee hao ni mahindi, maharage, sabuni na fedha kwa ajili ya kujikimu jambo ambalo limeonekana bayana kuwa la mfano kwa Kanisa na jamii kwa ujumla kutokana na kugusa maisha ya wananchi kwa ujumla ikizingatiwa msaada kama huo kwa jamii sio mara ya kwanza kufanywa na Kanisa hilo.

Akizungumza kwenye kilele cha ibada iliyofanyika jumapili iliyopita (Agosti 16, 2026) kanisani Ebenezer, Askofu mkuu wa Kanisa la Ebenezer Assemblies of God Africa Mchungaji Peter Jackson Hasunga anayechunga Kanisa hilo la Mbalizi alisema ameamua kwa kushirikiana na wazee wa Kanisa na waumini kwa ujumla kuwa na sadaka kwa ajili ya kusaidia wasiojiweza kama MUNGU alivyoagiza kuwajali wahitaji na wasiojiweza kwenye shida zao.

Askofu Hasunga aliwataka watu wengine kwenye Kanisa na jamii hasa wenye uwezo kiuchumi kujitoa kusaidia wasiojiweza na yatima ili kushiriki nao katika adha na magumu wanayokumbana nayo.

Wanufaika wa msaada huo walitumia ibada hiyo kumshukuru MUNGU kwa Mchungaji wao kiongozi Peter Hasunga na viongozi wengine kanisani hapo kwa kuwa na moyo wanaosema ni wa kujali na upendo kwa wananchi kwa ujumla.

Awali akihubiri kwenye ibada hiyo, Askofu mkuu wa Kanisa la EAGA aliwataka waumini hao kumwishia MUNGU na kuwa na maisha ya utakatifu na uaminifu ili kutoandamwa na laana za Shetani ikiwemo kuhakikisha wanakuwa waaminifu kwenye sadaka ya fungu la kumi.

Kanisa la YESU kwa ujumla linapaswa kuwa mfano mwema kuanzia ndani ya Kanisa kwa kuwa na kudumisha maisha ya utakatifu na upendo na baadaye hata nje ya Kanisa yaani katika jamii kuhakikisha Kanisa hilo linakuwa majibu na faraja kwa wananchi kama ambavyo Kanisa la Ebenezer Assemblies of God Africa EAGA Mbalizi limefanya kwa kutoa mahitaji kwa familia za wazee wasiojiweza.