Sababu wanaume kuvutiwa na wanawake wenye maumbo makubwa

Dar es Salaam. Mjadala kuhusu aina ya mwili unaovutia zaidi umeibua mitazamo tofauti huku baadhi ya wanaume wa Kiafrika wakisema wanapendelea wanawake wenye maumbo makubwa, hasa wenye makalio na nyonga pana.

Tafiti zinaeleza kuwa mvuto wa makalio unaweza kuhusishwa na jinsi ubongo unavyotambua umbo la mwili kwa ujumla pamoja na ishara zinazoweza kuhusishwa na afya na uwezo wa uzazi.

Hata hivyo, watafiti wanaonya kuwa hakuna sababu moja inayoweza kueleza mapendeleo hayo, kwa kuwa mvuto huathiriwa na utamaduni, mazingira, malezi na ladha binafsi. Mvuto hauwezi kuelezwa na uwiano wa kiuno na nyonga au ukubwa wa makalio pekee, kwa kuwa ukubwa wa mwili, umbo lote na mazingira ya kitamaduni pia vina mchango.

Mazingira na tafsiri ya uzuri

Kwa baadhi ya jamii za Afrika, mwili mkubwa kihistoria umehusishwa na afya, uwezo wa kuzaa na hali nzuri ya maisha. Mtazamo huo unaweza kuhusishwa na mazingira ambayo upatikanaji wa chakula haukuwa wa uhakika, hivyo mtu mwenye mwili mkubwa alionekana kuwa na uwezo wa kupata lishe ya kutosha.

Brian Geofrey, mmoja wa wachangiaji wa mjadala uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa X hivi karibuni, anasema mazingira yanaweza kuathiri namna jamii inavyotafsiri uzuri.

“Katika maeneo ambako lishe imekuwa changamoto, mwili wenye unene unaweza kuonekana kama ishara ya mtu anayepata chakula cha kutosha na mwenye afya,” anasema.

Mtazamo huo haupo Afrika pekee. Katika baadhi ya jamii duniani, miili mikubwa imewahi kuhusishwa na afya na ustawi, ingawa mitazamo ya uzuri imebadilika kadiri mazingira, uchumi na mitindo ya maisha ilivyobadilika.

Mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, Said Seif anasema anavutiwa zaidi na wanawake wenye maumbo makubwa.

“Napenda wanawake wenye maumbo makubwa kwa sababu naona wana mvuto wa asili. Makalio na umbo la mwili ni sehemu ninayoangalia na kunivutia, ingawa kila mwanaume ana ladha yake,” anasema Said.

Paul Beda, mkazi wa Tabata jijini humo anasema kwake mwanamke mwenye maumbo makubwa anaonekana mwenye mvuto na kujiamini.

“Ni aina ya mwonekano ambao nimeuzoea na kuupenda tangu zamani. Hata hivyo, si lazima kila mwanaume awe na mtazamo huo, kwa sababu uzuri na mvuto hutofautiana kati ya mtu na mtu,” anasema.

Andu Mwakalyelye anaona mvuto huo unaweza pia kuhusishwa na namna jamii inavyotafsiri afya na uzuri.

“Kwa sisi ni ishara ya afya na uzazi,” anasema, akisisitiza kuwa kila mtu ana mapendeleo yake.

Hata hivyo wapo baadhi ya wanaume ambao hawavutiwi na ukubwa wa umbo la mwanamke.

“Mimi napenda mwanamke asiye na mwili mkubwa, huyu ninamfurahia zaidi kuliko mwenye umbo kubwa na mnene,” anasema mkazi wa Morogoro Jafari Juma.

Utafiti uliohusisha wanaume 221 uliochapishwa mwaka 2009 na jarida la PubMed la nchini Uingereza, uliangalia uhusiano kati ya uwiano wa kiuno na nyonga, ukubwa wa matiti na mvuto.

Ulibaini kuwa mapendeleo ya umbo la mwanamke yanaweza kutofautiana kulingana na utamaduni na mazingira, hivyo hakuna kipimo kimoja cha mwili kinachopendwa na wanaume wote.

Matokeo ya utafiti huo ulioongozwa na Profesa wa Saikolojia ya Kijamii kutoka Chuo Kikuu cha Anglia Ruskin (ARU) Uingereza, Viren Swami yalionyesha kuwa wanaume wa makundi tofauti hawakuwa na mtazamo mmoja kuhusu umbo la mwanamke.

Wanaume 51 wa Afrika Kusini walionyesha upendeleo zaidi kwa michoro ya wanawake Waafrika wenye uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga ya 0.75 na matiti makubwa, huku kwa wanawake weupe wakiwa na uwiano huohuo wakipendelea zaidi matiti madogo.

Kwa upande mwingine, Waafrika 56 wanaoishi Uingereza na wanaume 114 weupe wa Uingereza walionyesha upendeleo tofauti, wakivutiwa zaidi na wanawake Waafrika wenye uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga ya 0.75 na matiti madogo, huku kwa wanawake weupe wakipendelea uwiano huo ikiwa imeambatana na matiti makubwa.

Watafiti walihitimisha kuwa mvuto wa umbo la mwili hauwezi kuelezwa kwa kipimo kimoja pekee, kwa kuwa mazingira ya kitamaduni na asili ya mwanamke vinaweza kuathiri mapendeleo ya wanaume.

Utafiti pia ulibaini uhusiano mkubwa kati ya mvuto na mtazamo wa afya kwa ujumla, michoro ya wanawake iliyotathminiwa kuwa ya kuvutia zaidi pia ilionekana kuwa ya afya zaidi.

Hata hivyo, watafiti walionya dhidi ya kutafsiri uwiano wa 0.75 moja kwa moja kama “makalio makubwa”, kwa kuwa kipimo hicho kinaonyesha uwiano kati ya kiuno na nyonga, si ukubwa wa makalio pekee.

Utafiti mwingine ulipendekeza kuwa mwonekano wa mwili wenye curves, ikiwamo ukubwa wa makalio, unaweza kuwa na mchango mkubwa katika mvuto kuliko kuangalia uwiano wa kiuno na nyonga pekee.

Utafiti huu ulioandikwa na Ronald Hübner na Emily Sophie Ufken na kuchapishwa katika jarida la Scientific Reports Oktoba 4, 2024, ulishirikisha watu 98, wakiwemo wanaume 33, ambao walipewa michoro ya miili ya wanawake yenye tofauti katika upana wa mwili na kiwango kikubwa cha mikunjo ya mwili kwa maana ya umbo.

Matokeo yalionyesha kuwa umbo ilikuwa kiashiria bora zaidi cha mvuto wa mwili kuliko uwiano wa kiuno na nyonga. Watafiti walibaini kuwa umbo pamoja na upana wa mwili vilieleza takribani asilimia 92 ya tofauti katika alama za mvuto, wakati kiuno na nyonga pamoja na upana wa mwili vilieleza takribani asilimia 63.

Hata hivyo, utafiti haukupima moja kwa moja ukubwa wa makalio, bali umbo na mikunjo ya mwili kwa ujumla.

Mwili mkubwa si kipimo cha afya

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanatahadharisha dhidi ya kuhusisha moja kwa moja ukubwa wa mwili na afya.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Jane Solomon, anasema mwili mkubwa si ushahidi wa moja kwa moja kwamba mtu ana afya njema.

“Ni muhimu kutenganisha suala la mvuto na afya. Mtu anaweza kuwa na mwili mkubwa na akawa na afya njema, lakini pia uzito uliopitiliza unaweza kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali,” anasema.

Anataja shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo kuwa miongoni mwa matatizo yanayoweza kuhusishwa na unene uliopitiliza, ingawa hatari hutofautiana kati ya mtu na mtu. Kwa upande mwingine, anasema kuwa mwembamba pia hakumaanishi mtu hana afya.

“Afya ya mtu haiwezi kuamuliwa kwa kumtazama tu. Tunahitaji kuangalia hali yake kwa ujumla na, inapohitajika, kufanya vipimo vinavyoweza kutoa picha sahihi zaidi,” anasema.

Hatari iliyofichika kumrusha mtoto hewani wakati wa kumbembeleza

Dar es Salaam. Mtoto anapolia, kukosa utulivu au kutaka kucheza, wazazi na walezi hutumia njia mbalimbali kumtuliza au kumfurahisha. Baadhi humbeba na kumtikisa taratibu, huku wengine wakimrusha hewani wakiamini ni mchezo unaomfurahisha mtoto.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Regency, Rahim Danji amesema shingo ya mtoto bado haijakomaa kikamilifu, hivyo haipaswi kupewa msukumo mkubwa au mtikisiko mkali.

Amesema shingo ina pingili zinazounganisha kichwa na sehemu nyingine ya mwili, lakini kwa watoto wadogo mifupa hiyo huwa bado katika hatua za ukuaji.

“Pingili ya kwanza ya shingo inayoshikamana na fuvu la kichwa kwa mtoto huwa bado haijakomaa vizuri. Hivyo, kumrusha mtoto hewani na kumshika kwa namna inayosababisha kichwa kutikisika kunaweza kuleta madhara,” amesema.

Mtaalamu huyo amesema kichwa cha mtoto ni kizito ikilinganishwa na mwili wake, huku misuli ya shingo ikiwa bado dhaifu. Hali hiyo humfanya mtoto awe katika hatari zaidi pale anapopigwa mtikisiko mkali au kuanguka bila kutarajiwa.

Amesema miongoni mwa madhara yanayoweza kutokea ni kuumia kwa shingo, kichwa au uti wa mgongo.

Amesema hali mbaya zaidi, mtikisiko mkali unaweza kuathiri ubongo na kusababisha majeraha makubwa, hasa iwapo mtoto ni mchanga.

Dk Gaudence Mathew kutoka Kituo cha Huduma za afya cha Decca Polyclinic kilichopo mkoani Dodoma amesema kitendo cha kumurusha mtoto hewani kinaweza kusababisha ubongo wa mtoto kutikisika na kusababisha changamoto mbalimbali ikiwamo kupata ugonjwa wa kifafa na degedege.

“Kitendo hicho pia kinaweza kumsababishia maumivu mtoto katika sehemu mbalimbali za mwili,”amesema.

Amesema mwili wa mtoto ni laini na haujakomaa, hivyo mtoto akibembelezwa kwa mtindo huo wa kurushwa na bahati mbaya akaanguka huweza kusababisa mivunjiko katika maeneo mbalimbali ya mwili na kumsababishia maumivu au hata ulemavu.

“Watoto hawatakiwi kubembelezwa kwa kutumia nguvu au kurushwa rushwa juu ni vyema mzazi kuisoma vyema saikolojia ya mtoto wake ili kufahamu pale anapolia nini hasa ni tatizo na kumbembeleza kwa taratibu na inavyoshauriwa na wataalamu,”amesema.

Mtaalamu wa malezi, Irene Mwakalinga anawashauri wazazi na walezi kuwa, mtoto anapolia ni vyema kabla ya kuanza kumbembeleza kuchunguza nini sababu ya kilio chake.

“Mtoto anapolia, mzazi anapaswa pia kutafuta sababu ya kilio hicho. Anaweza kuwa na njaa, nepi kuwa chafu, kuchoka, kuwa na joto au baridi, au kuwa anahitaji kubebwa. Kutambua hitaji lake kunaweza kusaidia kumtuliza bila kutumia nguvu,”amesema Mwakalinga.

Amesema pale inapolazimika kumbembeleza mtoto ni vyema kutumia njia salama badala ya kuwatingisha kwa nguvu au kuwarusha hewani, hatua inayoweza kuwaweka katika hatari ya kupata majeraha.

“Kumwimbia au kuzungumza naye pia ni njia inayoweza kumsaidia mtoto kutulia. Sauti anayoifahamu kutoka kwa mzazi au mlezi inaweza kumsaidia kupunguza msisimko na kumfanya ajisikie yuko katika mazingira salama,”ameeleza.

Amesema njia nyingine ni kumpapasa mgongoni kwa upole, hasa baada ya kunyonya.

Amesema mzazi anaweza kumbeba mtoto akiwa amemshikilia vizuri na kumpapasa taratibu.

Bandari ya Tanga yapaa, wadau wataka bandari kavu

Tanga.  Maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yameongeza ufanisi na kusababisha ongezeko la shehena, meli na abiria, hali iliyowafanya wadau kujadili uanzishwaji wa bandari kavu ili kupunguza msongamano na kuboresha huduma.

Maboresho hayo yanahusisha kuongeza kina cha bandari kutoka mita tatu hadi 13 pamoja na kupanua na kuboresha eneo lake, uwekezaji ulioongeza uwezo wa kuhudumia meli na shehena.

Leo Jumanne Agosti 18, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, bandari ililenga kuhudumia tani 1,643,363, lakini hadi Juni 2026 imehudumia takribani tani milioni 1.7.

Amesema pia ilipangiwa kuhudumia meli 364, lakini imehudumia 616, sawa na asilimia 196 ya lengo. Kwa abiria, amesema ililenga 59,990 na kufikia 110,356 hukju mapato, lengo lilikuwa Sh85 bilioni, lakini imekusanya Sh 138 bilioni.

Baadhi ya wadau waliokutana kwa ajili ya kujadili mpango wa bandari kavu katika bandari ya Tanga .Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dk Batilda Burian, kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TPA, Josephat Lukindo na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salim. Picha na Mbonea Herman.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Joseph Lukindo amesema kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano, Bandari ya Tanga inalenga kufikisha uwezo wa kuhudumia tani milioni 4.5 ifikapo 2030/31, sawa na ukuaji wa asilimia 19.8 kwa mwaka.

Amesema bandari kavu itasaidia kuongeza maeneo ya kuhifadhi na kusafirisha shehena nje ya bandari, kupunguza msongamano na kuongeza kasi ya mzunguko wa magari na mizigo.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mohamed Salim amesema ukuaji wa shughuli za Bandari ya Tanga umeongeza mahitaji ya maeneo ya kuhifadhia shehena nje ya bandari.

Amesema maeneo hayo yanaweza kutumika kama “port extension” yakipata ridhaa ya TPA na kuendelezwa na wawekezaji.

Salim amesema Tasac imekutana na wadau Tanga kuhakikisha changamoto za msongamano zinazoshuhudiwa Dar es Salaam hazijirudii, huku akisisitiza kuwa lengo si kuwanyima wadau fursa za biashara, bali kuweka utaratibu unaoendana na ukuaji wa bandari.

TMA yatahadharisha mvua, reli hatarini

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imezitaka mamlaka zinazosimamia miundombinu ya usafiri, ikiwamo reli, kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za vuli zinazotarajiwa kuwa juu ya wastani hadi wastani katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026.

TMA imesema msimu huo wa mvua unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El -Nino yenye nguvu, huku mvua za juu ya wastani hadi wastani zikitarajiwa katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Victoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Akitoa utabiri huo leo Jumanne, Agosti 18, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026 katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria, kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine Oktoba.

Amesema vipimo vya joto la bahari katika eneo la Nino 3.4 vimefikia nyuzi joto 2.2 Agosti na vinatarajiwa kuongezeka hadi nyuzi joto 3.6 ifikapo Desemba.

Dk Chang’a, amesema hali hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali na mafuriko katika baadhi ya maeneo, hali inayoweza kuathiri sekta mbalimbali, ikiwamo miundombinu.

Amesema reli ya mwendokasi (SGR), reli ya kawaida (MGR), barabara, madaraja na shughuli za bandari ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua hizo kutokana na mmomonyoko wa udongo na mafuriko.

“Katika reli, mvua kubwa zinaweza kusababisha mmomonyoko na kusomba udongo unaoshikilia miundombinu ya reli, hali inayoweza kuharibu njia za SGR na MGR, kuchelewesha huduma za usafiri na kuongeza gharama za matengenezo,” amesema.

Kwa upande wa barabara na madaraja, TMA imeonya kuhusu uwezekano wa kingo za barabara kuporomoka, barabara kukatika na madaraja kuathiriwa na maji, jambo linaloweza kutenga maeneo na kuvuruga usafirishaji wa abiria na mizigo.

“Shughuli za bandari nazo zinaweza kukumbwa na ucheleweshaji katika upakiaji na upakuaji wa mizigo kutokana na hali mbaya ya hewa,” amesema Dk Chang’a.

Amesema katika Ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo ya Kaskazini Magharibi, yakiwamo mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba.

Kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa Morogoro, Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba.

Visiwa vya Unguja na Pemba navyo vinatarajiwa kuanza kupata mvua katika kipindi hicho.

“Mvua hizo zinatarajiwa kuimarika zaidi Novemba na katika baadhi ya maeneo kuendelea hadi Januari 2027, huku maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua yakitarajiwa kuanza kupata mvua mapema kuliko ilivyozoeleka,” amesema.

TMA imezitaka pia sekta nyingine kuchukua tahadhari mapema, zikiwamo kilimo, afya na mifugo, kutokana na uwezekano wa athari zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu huo.

Akizungumzia hatua za kukabiliana na athari hizo, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Menejimenti ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amesema tayari wamepokea taarifa ya TMA na wanaifanyia kazi.

“Ndiyo, nimepata taarifa ya TMA, tunaifanyia kazi. Wiki ijayo tutaeleza nini tutafanya kukabiliana na hili na wananchi wachukue tahadhari gani,” amesema.

Shekilango ilivyopata sura mpya baada ya mabasi kuondolewa

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, eneo la Shekilango, pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kuelekea Magomeni, Dar es Salaam, lilizoeleka kuona msongamano wa mabasi ya kampuni mbalimbali yakiwa yameegeshwa na kupakia abiria wanaosafiri kwenda mikoa tofauti nchini. Sasa eneo hilo limebadilika baada ya mabasi hayo kuondolewa.

Mabasi hayo hayaonekani tena yakiwa yameegeshwa katika eneo hilo kama ilivyokuwa awali, isipokuwa yanapita kuelekea maeneo mengine au kuegeshwa kwa muda mfupi kupakia mizigo na abiria kabla ya kuondoka.

Hata hivyo, ofisi za kampuni za mabasi zilizolipamba eneo hilo kiasi cha kulifanya lionekane kama kituo cha mabasi bado zimefunguliwa na zinaendelea na shughuli za ukatishaji tiketi kwa abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali.

Mawakala nao bado wanaendelea kuzengeazengea huku na kule  kusaka abiria kama ilivyo kawaida yao.

Nje ya baadhi ya ofisi hizo, ikiwemo za mabasi ya Katarama, BM, Happy Nation na Abood, ambazo mara nyingi hufurika abiria na kuwapo pilikapilika za hapa na pale, vifurushi vya mizigo ya abiria vimepangwa huku vikiwa vimeandikwa majina ya wahusika.

Hali hiyo inaonyesha kuwa shughuli za usafirishaji bado zinaendelea katika eneo hilo, licha ya mabasi kuondolewa kwenye vituo vyao.

Basi la kampuni ya Abood likiwa limesimama katika kituo chake kilichopo eneo la Shekilango, karibu na Ubungo Plaza, eneo hilo aghalabu hujaa mabasi mengi yakiwa yamejipanga ya kampuni hiyo, hasa nyakati za asubuhi na jioni kupakia abiria kwenda mikoa tofauti.

Mabadiliko hayo yamekuja baada ya tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alilolitoa Agosti 11, 2026 ambapo  aliwataka wamiliki wa mabasi kuondoa magari yao katika vituo vilivyopo maeneo hayo na kuanza kutumia Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis.

Kwa mujibu wa Chalamila, taarifa alizonazo zinaonyesha kuwa ni kampuni sita pekee zilizokuwa na vibali vya kuendesha vituo vya mabasi katika eneo hilo.

Alisema kampuni hizo zitaendelea na shughuli zake hadi vibali vyao vitakapoisha, kisha zitaungana na nyingine katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli.

Chalamila alidai kuwa kuendelea kwa mabasi hayo kupakia abiria katika eneo hilo au kuja katikati ya Jiji la Dar es Salaam kunasababisha foleni na kuwaondolea watoa huduma wengine wa usafiri wateja zikiwamo daladala, bodaboda na mabasi ya mwendokasi.

Agizo hilo halikuwafurahisha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), ambao walidai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa bila kuwashirikisha, hivyo hawakutendewa haki.

Hata hivyo, walisema hawana mpango wa kushindana na Serikali na kuahidi wanamtafuta Chalamila wafanye naye mazungumzo na kutoa tamko lao.

Mwananchi ilitembelea eneo hilo leo, Jumanne Agosti 18, 2026, kujionea hali ilivyo baada ya utekelezaji wa maelekezo hayo na kushuhudia mabadiliko makubwa ya mandhari.

Tofauti na ilivyozoeleka, eneo hilo sasa halina msongamano wa mabasi yaliyokuwa yakishusha na kupakia abiria. Ingawa, shughuli ndani ya ofisi za kampuni hizo zinaendelea kama kawaida.

Abiria bado wanaonekana kufika katika ofisi hizo kukata tiketi, huku mawakala wakizunguka huku na kule kuwatafuta wasafiri kwa ajili ya safari za mikoa mbalimbali.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Habari kwa Umma wa Taboa, Mustapha Mwalongo, amesema wameutekeleza uamuzi huo, ingawa bado wanaendelea kutafuta nafasi ya kukutana na mkuu wa mkoa ili kuzungumza kuhusu suala hilo.

“Tangu Agosti 13 hadi sasa, nazungumza na wewe tunafanya jitihada za kumtafuta mkuu wa mkoa ili tuzungumze naye kuhusiana na jambo hili, lakini hatujafanikiwa. Barua tulishatuma. Naamini tukishafanya mazungumzo naye tutatoa msimamo wetu,” amesema Mwalongo.

RAIS WA KONGO MHE FELIX ANTOINE APOKELEWA NA RAIS DKT SAMIA IKULU NDOGO ZANZIBAR

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, akipokelewa na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Ikulu Ndogo Zanzibar,Agosti 18, 2026.

 

Mwili wa mwanamume wakutwa porini karibu na eneo la Jeshi Makuburi

Dar es Salaam. Mwili wa mwanamume umekutwa katika eneo la Makuburi, Dar es Salaam, ukiwa hauna jeraha lolote linaloonekana, huku jitihada za kuutambua zikishindikana hadi saa tano kamili leo.

Mwili huo umekutwa katika eneo linalodaiwa kuwa chini ya uangalizi wa jeshi, hali iliyosababisha Polisi, wanajeshi pamoja na wataalamu wa Red Cross kufika eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi na hatua za awali za utambuzi.

Mashuhuda wamesema taarifa za kuwepo kwa mtu huyo katika eneo hilo zilianza kusambaa tangu saa moja asubuhi, baada ya baadhi ya watu kumuona akiwa amelala.

Mmoja wa mashuhuda, James Pancras, amesema aliposogea eneo hilo alimkuta mwanaume huyo akiwa amelala, hajitambui.

“Nilisogea na kumkuta mwanamume huyo akiwa amelala,” amesema Pancras.

Shuhuda mwingine, Anamaria Jilala, amesema alitoa khanga yake kumfunika mwanaume huyo baada ya kuombwa msaada, akisema mwonekano wake haukuonesha dalili za jeraha.

“Nilipita hapa, nikaambiwa kuna mtu amefariki, nilitoa khanga yangu kumsitiri, lakini ukimuangalia ni mtu tu mwenye afya, hana jeraha lolote, ni kama amelala,” amesema Jilala.

Mwananchi imeshuhudia vikosi vya ulinzi na usalama katika eneo la tukio vikitaka watu kumtazama mwanamume huyo kwa lengo la kubaini iwapo kuna anayemfahamu, lakini hawakuruhusiwa kupiga picha.

Hata hivyo, hadi saa tano kamili asubuhu, hakuna mtu aliyemtambua kabla ya mwili huo kuondolewa.

Mjumbe wa Kata ya Makuburi, Kondo Juma Kondo, amesema hana taarifa kuhusu marehemu huyo, akieleza kuwa alifika eneo hilo baada ya kupigiwa simu na kupewa taarifa kuwa kuna mwili.

“Nimepigiwa simu kwamba kuna mwili hapa, ndiyo nimefika na kukuta hivi, sina ninachokijua zaidi kuhusu huyu mtu,” amesema Kondo.

Mwananchi ilishuhudia Kondo akifanya ukaguzi wa awali wa mwili huo, ikiwamo kuangalia iwapo ulikuwa na kitu chochote kinachoweza kusaidia katika utambuzi, lakini hakukuwa na kitu kilichobainika.

Mwanamume huyo alikuwa amevaa gambuti, suruali nyeusi na fulana nyekundu kuukuu, huku Polisi, wanajeshi na Red Cross waliendelea na hatua za ukaguzi wa eneo na mwili huo.

Hata hivyo, wakati wa kuondoa mwili huo, walimvua gambuti na miguu yake kukutwa ikiwa na matope, huku utambulisho wa marehemu pamoja na chanzo cha kifo ukisubiri hatua zaidi za mamlaka.

AFISA WA FIFA AFUTWA KAZI BAADA YA KUKOSOA MPANGO WA INFANTINO

 

Alikuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa mipango ambayo baadae ilifutiliwa mbali ya rais wa FIFA Gianni Infantino, ya kuuza hisa za Kombe la Dunia na michuano mingine kwa wawekezaji binafsi.

Katika taarifa, msemaji wa FIFA alithibitisha tu kwamba “ushirikiano wa kikazi kati ya FIFA na Kevin Lamour katika nafasi ya Afisa Mkuu wa Uendeshaji umekamilika tarehe 17 Agosti 2026.”

“FIFA inamshukuru Kevin kwa miaka yake miwili ya huduma na inamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadaye.”

Mwezi uliopita, Bwana Lamour alisema kuwa mipango ya kuuzia wawekezaji binafsi hisa iliwahadaa wafanyakazi wa FIFA na kuutaja mradi huo kama “mradi wa mtu mmoja.”

DC Magoti awaahidi ajira vijana wa Mgambo Kisarawe

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani wani, Petro Magoti, ametoa matumaini kwa vijana wa wilaya hiyo wanaoshiriki mafunzo ya awali ya Jeshi la Akiba, maarufu Mgambo, kuwapa kipaumbele cha kwanza katika fursa mbalimbali za ajira pindi watakapohitimu kozi hiyo.

Magoti ametoa ahadi hiyo jana, Agosti 17, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya Mgambo katika Kijiji cha Kazimzumbwe.

Amewataka vijana hao kuzingatia mafunzo na nidhamu ya kijeshi, akisisitiza suala la ajira lipo chini yake.

Askari wanafunzi wa Jeshi la akiba wakiwa wamekaa wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Kisarawe katika ufunguzi wa mafunzo Augosti 17,206. Picha na Jumanne Bakana.

Pia, amewataka vijana hao kuwa na nidhamu, kudumisha uzalendo na kujituma kwa kufuata maelekezo ya wakufunzi.

“Wenzenu waliomaliza mafunzo mwaka jana walikuwa 152 na wote tuliwaajiri. Kisarawe ni moja ya wilaya ambayo askari wetu wa Jeshi la Akiba mnapitishwa kwenye uzalendo na mafunzo ambayo hayana mfano katika wilaya nyingine.

“Ndiyo maana, askari wetu wa Jeshi la Akiba wameendelea kuliliwa kila mahala. Tuliwaajiri hadi tukachukua wenzetu wa Jeshi la Akiba Mafia. Hata jana kuna kampuni imeomba vijana 18, kwa hiyo naomba niwahakikishie, kuweni na nidhamu, kuweni waadilifu, kuweni wazalendo, suala la ajira tuachieni,” amesema Magoti.

Askari wanafunzi wa Jeshi la akiba wakiwa wamekaa wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Kisarawe katika ufunguzi wa mafunzo Augosti 17,206. Picha na Jumanne Bakana.

Naye Kaimu Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Kisarawe, Stafu Sajenti Neema Ochieng, amesema mafunzo hayo yalianza Julai 8, 2026, kukiwa na  vijana 85, kati yao wa kike wakiwa 22.

Ochieng amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea washiriki kujiamini na kujitoa kwa Taifa lao.

“Mafunzo haya yamelenga kuwajengea washiriki ujuzi, maarifa, uzalendo na namna ya kudumisha ulinzi wa Taifa lao,” amesema Ochieng.

Kwa upande wake, Diwani wa Kazimzumbwe wilayani Kisarawe, Siza Dilunga, amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuendelea kuwatafutia vijana ajira kutoka katika kampuni mbalimbali.

“Ninakushukuru wewe mkuu wa wilaya kwa jitihada zako ambazo umekuwa ukiwapambania vijana, wananchi wa Kazimzumbwe na Kisarawe kwa ujumla. Umetoka kutuambia namna ambavyo unazungumza na kampuni kuja kutoa ajira kwa vijana wetu,” amesema Dilunga.

MZOZO WA UKRAINE: URUSI YAIONYA UINGEREZA – KUNANI?

 

Urusi imeishutumu Uingereza kwa “kuchochea mzozo wa Ukraine” kufuatia uthibitisho kwamba ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa Uingereza zilitumika kushambulizi maeneo yaliyolengwa nchini Urusi.

“Kwa kufanya hivyo, Uingereza inashiriki kama msaidizi na mhusika mwenza katika uhalifu wa umwagaji damu na mashambulizi ya kigaidi,” ilisema taarifa kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Uingereza.

“London bila shaka italazimika kuwajibikia hatua yake,” ilisema taarifa hiyo, huku ikiongeza kuwa kadiri inavyozidi kujihusisha na mgogoro huo, “ndivyo gharama itakayolipa itakavyokuwa kubwa zaidi.”

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi (MoD) amembia BBC kuwa Uingereza inasimama “bega kwa bega” na Ukraine.

“Urusi haipaswi kuwa na shaka yoyote kuhusu azimio la Serikali hii la kupinga uchokozi wa wake, iwe ni nchini Ukraine au dhidi ya Uingereza na washirika wetu,” alisema msemaji huyo katika taarifa.

Uingereza iliongeza kuwa “imejitolea kutoa vifaa ambavyo Ukraine inahitaji ili kujilinda dhidi ya uvamizi haramu wa [Rais wa Urusi Vladimir] Putin”.

Ndege hizo zisizo na rubani zilizotengenezwa na kampuni mbili tofauti za Uingereza zimetumika kushambulia kwa mafanikio vituo vya kijeshi na viwandandani ya Urusi, ikiwemo mitambo ya kusafisha mafuta na maghala ya kampuni ya mauzo ya mtandaoni ya Wildberries.

Ukraine imekuwa ikilenga mara kwa mara kampuni hiyo —ambayo inajulikana kama toleo la Urusi la Amazon—na kusema kuwa vituo saba kati ya 10 vikubwa zaidi vya usafirishaji na uhifadhi bidhaa vya Wildberries “vimesambaratishwa”.