Mchengerwa ataja vipaumbele sita kupunguza vifo vya mama, mtoto

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ametaja mambo sita yanayopaswa kupewa kipaumbele na nchi za Afrika Mashariki na Kusini, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuimarisha mifumo ya afya.

Mchengerwa amesema hayo leo Jumanne, Agosti 18, 2026, katika Mkutano wa Nne wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Afya wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, unaojadili usalama wa afya, kujitegemea katika sekta hiyo na kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi, mama na mtoto.

Mkutano huo umewakutanisha mawaziri na wawakilishi kutoka nchi 14 za eneo hilo.

Amesema kipaumbele cha kwanza ni kuipa afya ya msingi, usalama wa afya na afya ya mama na mtoto katika mipango ya maendeleo na bajeti za kitaifa.

Amesema Tanzania inalenga kuendelea kupunguza vifo vya mama kuelekea lengo la kimataifa la vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000, akisisitiza kuwa, mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila uwekezaji wa kutosha.

Waziri wa Afya Zanzibar, Saada Mkuya akizungumza wakati wa mkutano wa nne wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Afya wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, unaojadili namna ya kuimarisha usalama wa afya na kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi, mama na mtoto.

“Ni muhimu kuimarisha bajeti zetu na si kuziimarisha katika tarakimu pekee, bali kuhakikisha wakati wote tunapotoka hapa kwenye mabaraza yetu ya mawaziri katika kila nchi tunazungumzia umuhimu wa kuwekeza kwenye sekta ya afya,” amesema.

Kipaumbele cha pili, amesema ni kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, maandalizi na mwitikio wa magonjwa katika mipaka ya nchi, badala ya kusubiri mlipuko utokee.

“Ugonjwa hautambui masuala ya boda, hautambui mipaka, hautambui kama hapa ni Tanzania, Kenya au Uganda,” amesema Mchengerwa.

Ametolea mfano mlipuko wa Ebola Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akisema hali hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa nchi jirani.

AmesemaTanzania hushirikiana na Uganda na DRC kwa kutoa wataalamu, dawa na rasilimali nyingine wakati wa milipuko, huku ufuatiliaji ukiendelea katika vituo vya mipakani.

Kipaumbele cha tatu amesema ni kutekeleza mpango wa afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto kwa kuweka malengo yanayopimika, muda wa utekelezaji na mifumo ya uwajibikaji.

Mchengerwa amesema kipaumbele cha nne ni kutafuta fedha za ndani zinazotabirika na bunifu, pamoja na kuimarisha ununuzi wa pamoja na uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya barani Afrika.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe

Mchengerwa ametaja pia uwajibikaji kuwa kipaumbele cha tano, akitaka ahadi zifuatiliwe, matokeo yapimwe na nchi zibadilishane uzoefu.

Kipaumbele cha sita amesema ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na milipuko na changamoto nyingine za afya.

Waziri wa Afya Zanzibar, Saada Mkuya amesema afya ya mama na mtoto ni miongoni mwa ajenda kuu, huku nchi zikihimizwa kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya afya, rasilimali watu na miundombinu.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dk Raji Tajdin amesema Afrika inazalisha takriban asilimia moja pekee ya mahitaji yake ya chanjo, akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa ndani.

Dk Tajdin amesema Afrika inakabiliwa na zaidi ya magonjwa 200 yanayoibuka na kuibuka tena, huku mabadiliko ya tabianchi yakiongeza hatari mpya za kiafya.

“Hatupaswi kusubiri mlipuko ndipo tuanze kukimbizana. Tunahitaji maandalizi,” amesema Dk Tajdin.

Babu adai kupigwa ngwara na mwalimu Bahi

Bahi. Mvutano kati ya mzee mwenye umri wa miaka 86, anayemtuhumu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamantwa kwa madai ya kumpiga ngwara, umeingia sura mpya baada ya Serikali ya Kijiji kueleza ilivyopokea na kushughulikia malalamiko hayo.

Tukio hilo linamhusisha mzee Joseph Ndega, maarufu Shamba, anayedai mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ramadhan Kipenya, kumpiga ngwara Agosti 4, 2026, baada ya kufika shuleni hapo kuulizia adhabu walizopewa wajukuu zake pamoja na wanafunzi wengine.

Kwa mujibu wa Shamba, aliamua kwenda shuleni baada ya wajukuu zake kurudi nyumbani wakilalamika kupigwa viboko vingi.

Amesema alipofika na kumsogelea mwalimu mkuu, alikasirika na kumshambulia.

“Watoto walirudi wanalia, wakasema wamepigwa sana, nikaamua kwenda kuwasikiliza na kujua chanzo. Lakini, aliponiona akapatwa na hasira. Baada ya kumsogelea akanipiga ngwara, tukaanguka wote, ndipo akanipiga makofi mawili,” amesema.

Shamba anasema hakufikisha malalamiko yake kwa viongozi wa ngazi za juu kwa sababu alielekezwa kuwa suala hilo lilipaswa kumalizwa katika ngazi ya kijiji.

Ameongeza kuwa anaamini tabia ya kupiga wanafunzi imekuwa ikijitokeza shuleni hapo, na ndiyo iliyomsukuma kufuatilia suala hilo baada ya wajukuu wake kupewa adhabu.

Akijibu tuhuma hizo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamantwa, Ally Kipenya, amekana kumpiga Mzee Shamba.

“Kwa sasa niko benki, kwa hiyo siwezi kulisema sana jambo hili, ila kifupi halipo na sijawahi kufanya hivyo. Labda watu wangesikia huko, nikitoka nitakutafuta,” amesema.

Hata hivyo, baada ya mazungumzo hayo, Kipenya hakupatikana tena kwa simu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpamantwa, John Makolokolo, amekiri kuwepo kwa mvutano huo, lakini amekanusha madai kuwa mwalimu mkuu alimpiga mzee Shamba.

Amesema baada ya mzee Shamba kufika kijijini kulalamikia adhabu za wajukuu wake, Serikali ya Kijiji ilimuita mwalimu mkuu kwa mahojiano.

“Mwalimu mkuu alituambia siku hiyo alimkuta mzee Shamba anavutana na mwalimu wa zamu, ndipo akamshika mkono na kumtoa eneo hilo ili kuzuia mvutano. Hapo ndipo hali ilipotulia,” amesema Makolokolo.

Kuhusu madai ya wanafunzi kuchapwa viboko vingi, Makolokolo amesema si kweli kuwa walimu wana utaratibu huo, akisema adhabu zinazotolewa ni za kawaida.

Amesema siku hiyo wajukuu wa Shamba waliitwa na Serikali ya Kijiji ilimtuma mtendaji pamoja na ofisa maendeleo wa kijiji, ambao waliwakagua na kutoa taarifa kuwa hawakuona alama zilizoashiria walipigwa viboko kupita kiasi.

Makolokolo amesema Shamba amekuwa akihusika katika migogoro kadhaa katika maeneo tofauti, hasa anaposikia wajukuu wake wamepewa adhabu.

Kibwagizo cha wimbo wa ‘kilio cha mtu mzima’ kilivyotumika kesi ya ardhi

Arusha. “Mali ya baba inanitoa roho, bora nikae pembeni, niinusuru roho yangu mimi…” Hicho ndicho kibwagizo cha wimbo ‘Kilio cha Mtu Mzima’ wa OTTTU Jazz Band kilichotumiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Mbulu, Mosses Ntumengwa, kuanza uamuzi wa mgogoro wa ardhi uliowakutanisha ndugu wawili waliokuwa wakigombea shamba waliloachiwa na baba yao.

Kwa kutumia ujumbe wa wimbo huo unaogusia migogoro na maumivu yanayoweza kujitokeza katika kugawana au kugombea mali ya wazazi, Ntumengwa alionyesha namna mali ya familia inavyoweza kugeuka chanzo cha uhasama na kuvunja undugu.

Katika shauri hilo, Baraza limemtangaza Tlaka’ari Bura kuwa mmiliki halali wa ekari 11 za ardhi zilizopo Kitongoji cha Labom, Kijiji cha Mighaw, Kata ya Endahagichan, huku ndugu yake, Matle Bura, akitangazwa kuwa mvamizi wa eneo hilo.

Mwenyekiti Ntumengwa amefananisha mgogoro huo na maudhui ya wimbo huo na kueleza kuwa  ujumbe wake unafundisha kuwa mali au ardhi zilizoachwa na wazazi baada ya kufariki dunia kamwe zisifikishe mahali ndugu kupoteza utu, undugu, upendo na hata kugharimu maisha kwa sababu ya ugomvi, chuki na mifarakano kutokana na mali hizo.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa wadaawa katika shauri hilo ambao ni ndugu wa damu, Baraza liliwapa nafasi ya kumaliza mgogoro huo kwa njia ya suluhu ili amani na upendo vidumu kati yao, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa.

Mwenyekiti huyo amesema kutokana na sababu hiyo Baraza halina namna nyingine bali kuwaamua wadaawa kwa mujibu wa sheria, ili baada ya hukumu wachukue kapu na kuvuna wenyewe kila walichokipanda katika ushahidi wao.

“Kwani Baraza halina mikono, jembe na shamba la kulima pale ndugu wanapogombana ili mwishoni lichukue kapu na kuvuna. Na hii ni kulingana na methali ya Waswahili isemayo “ndugu wakigombana shika jembe ukalime, wakipatana chukua kapu ukavune,”ameeleza Mwenyekiti huyo.

Katika maombi hayo ya ardhi namba 7/2026,Tlaka’ari alidai mbele ya Baraza kuwa baba yao, Bura Gitiye alimpa eneo hilo Septemba 20,1991 na alilitumia kwa kilimo cha mahindi, maharage na alizeti toka mwaka  1991 hadi 2026, (miaka 35).

Amedai mgogoro ulianza mwaka 2024 baada ya ndugu yake kuvamia eneo hilo kwa kulima na trekta na kuwa mgogoro huo ulipelekwa kwenye ofisi za Kijiji cha Mighaw kwa ajili ya suluhu, lakini ilishindikana na ukaibuka tena mwaka 2025 .

Amedai mwaka jana mdaiwa alifyeka vichaka na kutengeneza boma huku akidai kuwa eneo hilo alipewa na wazee jambo ambalo sio la kweli, na kuwa mgogoro huo uliwahi kupelekwa kwenye Baraza la Kata ya Endahagichan kwa ajili ya suluhu lakini ilishindikana.

Mdai aliliomba Baraza kuwa atamkwe yeye ndiye mmiliki halali wa eneo hilo, Baraza litoe zuio la kudumu na amri stahiki kwa mdaiwa, wafanyakazi wake wote na wale wote wanaofanya kazi chini yake kutoingilia tena eneo la mgogoro.

Kwa upande wake mdaiwa, aliwasilisha utetezi wake mbele ya Baraza hilo huku akiomba maombi haya yatupiliwe mbali, na eneo la mgogoro litamkwe kuwa ni   la kurithi na wadaawa katika shauri na kuwa mdaiwa afidiwe gharama zake alizozitumia.

Mashahidi wa Tlaka’ari walieleza Baraza kuwa walishuhudia baba yao akimpatika Tlaka’ari eneo hilo na amekuwa akilitumia kwa muda mrefu bila mgogoro.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mwenyekiti  amesema  Tlaka’ari amethibitisha  madai yake ya umiliki wa eneo  hilo kuwa alilipata baada ya kupewa na baba yake mzazi.

Baraza lilisema ushahidi huo uliungwa mkono na ndugu zake, Askwari Bura na Charles Bura, waliodai kushuhudia baba yao akimpa Tlaka’ari eneo hilo, pamoja na Kwaslema Matle aliyethibitisha kuwa Tlaka’ari alikuwa akilitumia eneo hilo kwa muda mrefu.

Kuhusu Matle, Baraza lilisema ushahidi wake haukuwa na nguvu, huku mashahidi wake wakitoa maelezo yaliyokinzana kuhusu chanzo cha umiliki.

“Baada ya kuona na maoni ya wazee wa baraza ambao wameona maombi hayo ya mdai yakubaliwe na mdai atamkwe kuwa mmiliki halali na mdaiwa atamkwe kuwa mvamizi na abakie eneo alilokuwa akilitumia.”

 “Baraza hili linatoa amri zifuatazo, maombi ya mdai yana mashiko na yanakubaliwa, mdai anatamkwa kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo la mgogoro. Mdaiwa anatamkwa kuwa ni mvamizi kwenye eneo la mgogoro mali ya mdai na kwa kuwa wadaawa nia ndugu moja, kila upande utabeba gharama zake,”amesema Mwenyekiti.

Mwili wa mtoto wa miaka saba wakutwa shimoni Tabora

Tabora. Mtoto Yusra Juma (7), mkazi wa Mtakuja, Kata ya Malolo, Manispaa ya Tabora, amekutwa amefariki dunia ndani ya shimo la kuchimbwa mchanga, huku Jeshi la Polisi likisema uchunguzi wa awali umebaini alinyongwa na watu ambao hawajafahamika.

Akizungumza kuhusu tukio hilo leo, Jumanne Agosti 18, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Twaha Lulengelule amesema: “Tukio hili limetokea jana majira ya saa nane mchana baada ya kutoka shuleni, tunaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliofanya kitendo hiki.”

Amesema mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mawiti iliyopo Malolo Manispaa ya Tabora.

Kamanda Lulengelule amesema kifo cha mtoto huyo kilibainika baada ya bibi yake kuona muda umeenda bila kurejea nyumbani ndipo akatoka kufuatilia na hatimaye kuukuta mwili wake kwenye shimo.

Wananchi katika kata ya Malolo wakiwa eneo la tukio alipouawa mtoto Yusra.

“Ufuatiliaji wa bibi yake ndio uliosababisha kuupata mwili wa mtoto huyo mapema, uchunguzi wa madaktari unaeleza kuwa, mtoto huyo amefariki kwa kukosa hewa baada ya kushikwa shingo,” amesema.

Diwani wa Malolo, Manispaa ya Tabora, Naomi Kasanga amelaani tukio hilo akisema ni la kinyama na halikubaliki katika jamii.

Ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na tukio hilo na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

“Mtoto huyu ametuumiza sana, kwanza mdogo halafu sasa hana hatia kabisa, kwa nini mtu amuue kinyama hivi,” amesema Kasanga.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtakuja, Hamisi Ibrahim amelaani tukio hilo akisema ni la kinyama na halivumiliki katika jamii.

Amesema mauaji hayo ni miongoni mwa matukio mabaya yanayohitaji hatua za haraka za kisheria.

“Hatupaswi kuwa na mazingira ya kuogofya kiasi hiki, lazima amani iwepo, watoto hawa ni hazina yetu lazima waishi kwa amani, kifupi tumeumizwa sana,” amesema.

Beatrice Katatula, mkazi wa Malolo amesema tukio la Yusra sio la kwanza kwa Kata ya Malolo kwa sababu miezi kadhaa nyuma alipoteza maisha mtoto mwingine katika mazingira ya kinyama.

“Mpaka tunaogopa sasa jamani maana hatuwezi kwenda na watoto kazini, na ni lazima pia waende shule, sasa kama shule njiani tena usalama hakuna, hii inatuumiza na kutuvuruga kwa kweli,” amesema.

WRRB, MIKOA NA HALMASHAURI KUIMARISHA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA

 

Na Matukio Daima Media DODOMA

BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri nchini ili kuimarisha utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS), kuongeza tija kwa wakulima na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, ameyasema hayo leo Agosti 18, 2026, wakati akizungumza na Maafisa Biashara katika Kikao cha Tatu cha Wizara ya Viwanda na Biashara na Maafisa Biashara, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Bw. Bangu amesema utekelezaji wenye tija wa mfumo huo katika mikoa na halmashauri unahitaji ushiriki wa karibu wa Maafisa Biashara, hususan katika usimamizi wa shughuli zinazohusiana na maghala pamoja na minada ya mazao inayofanyika katika maeneo yao.

Amesema Maafisa Biashara wana nafasi muhimu katika kuhakikisha taarifa sahihi kuhusu mahitaji ya maghala katika maeneo yao zinapatikana, sambamba na kufuatilia hali, matumizi na uhitaji wa maghala katika halmashauri na mikoa ili kuwezesha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa WRRB, Bw. Dionis Musseru, amesema utoaji wa elimu kwa umma umeendelea kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau katika mfumo huo, ambapo hadi sasa mazao 11 yanauzwa kupitia WRS.

Tatoa yatishia kupaki malori | Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akianzisha operesheni ya kukamata malori yanayoegeshwa kwenye  hifadhi za barabara, Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) kimetishia kusitisha shughuli za usafirishaji endapo Serikali  haitashughulikia changamoto zinazowakabili.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tatoa, Elias Lukumay, alipokuwa akizungumzia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, la kuanzisha operesheni dhidi ya malori yanayoegeshwa kwenye hifadhi za barabara.

Agosti 11, 2026, Chalamila aliliagiza Jeshi la Polisi kupitia Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa, kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuajiri vijana watakaosaidia katika operesheni ya kuwakamata madereva wa malori wanaokiuka utaratibu kwa kuegesha katika maeneo yaliyotengwa kwa matumizi mengine.
Chalamila alisema hatua hiyo inalenga kukabiliana na uholela katika Jiji la Dar es Salaam na kuhakikisha maeneo ya barabara yanatumika kwa mujibu wa utaratibu. Alisema agizo hilo pia linawahusu wamiliki wa mabasi.
Hata hivyo, Tatoa imeeleza operesheni za kukamata malori si suluhisho la kudumu, ikitaka Serikali ikae pamoja na wadau wa sekta hiyo ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam leo Agosti 18, 2026, Lukumay amesema wamiliki wa malori wanakabiliwa na kero mbalimbali, zikiwemo kukamatwa kwa magari, madereva kuvamiwa na kupokonywa namba za magari na malalamiko kuhusu mizani ya Iringa na Mikumi.

Amesema wamiliki wa malori hawapingi usimamizi wa Serikali, bali wanataka utekelezaji wa sheria uende sambamba na mazungumzo yatakayosaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika shughuli zao.

“Mnatupitisha kwenye njia ngumu kila kukicha, kero ni zilezile. Naamini katika njia ya maelewano kama itashindikana, hapo tuko tayari kuyapaki haya malori mpaka hapo tutakapokubaliana,” amesema Lukumay.

Amesema kusitisha shughuli za malori kunaweza kuathiri sekta nyingine zinazotegemea usafirishaji wa bidhaa, hususan Bandari ya Dar es Salaam, biashara ya mafuta na shughuli za wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Lukumay, sekta ya usafirishaji pia ni chanzo cha ajira kwa madereva, wapakuaji na makundi mengine yanayohusika katika mnyororo wa usafirishaji.

Amesema Serikali na wamiliki wa malori wanapaswa kujenga utaratibu wa mazungumzo ya kudumu ili kuepusha migogoro na kuhakikisha shughuli za usafirishaji zinaendelea bila kuathiri uwekezaji na maeneo mengine ya  kiuchumi.

Lukumay amezitaka mamlaka husika kupunguza utegemezi wa operesheni za kukamata malori na badala yake kuweka mfumo wa ushirikiano unaozingatia sheria, usalama wa barabara na masilahi ya sekta ya usafirishaji.

Akisimulia changamoto wanazokutana nazo hadi kulazimika kuegesha malori katika hifadhi za barabara, mmoja wa madereva, Elias Mwaningo, amesema tatizo kubwa ni ukosefu wa maeneo maalumu ya kuegesha.

Mwaningo alitoa kauli hiyo mbele ya Chalamila wakati mkuu huyo wa mkoa alipofanya ziara katika maeneo ya Kurasini na kushuhudia malori yakiwa yameegeshwa kwenye hifadhi ya barabara.

“Changamoto ni nyingi. Tunaleta mizigo mingi, lakini kasi ya kuipokea kwenye ICD ni ndogo, kiasi kwamba msongamano wa malori unakuwa mkubwa na tunakosa hata sehemu ya kwenda kujisaidia haja ndogo,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwaningo, madereva pia wanakabiliwa na changamoto katika maeneo wanapopeleka mizigo, ikiwemo vitendo vya rushwa na ucheleweshaji wa upakuaji.

Amesema wakati mwingine gari linaweza kukaa hadi wiki bila kuruhusiwa kushusha mzigo, huku magari yaliyowasili baadaye yakipewa kipaumbele cha kushusha mizigo.

 “Kuna wakati gari inamaliza hadi wiki hairuhusiwi kwenda kushusha mzigo, badala yake anachukuliwa aliyefika leo kwenda kushusha bila kujali kuna wengine waliojipanga kwenye mstari,” amesema.

TBS YALENGA VIFAA BORA NA MATUMIZI SALAMA YA UMEME KUPITIA MEPS

  Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeweka Viwango vya Chini vya Ufanisi wa Nishati (MEPS) kwa vifaa vinavyotumia umeme, hatua inayolenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya nishati na kuwasaidia wananchi kupata vifaa bora na vyenye ufanisi mkubwa.

Ameyasema hayo leo Agosti 18, 2026 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Candida Shirima, wakati akifungua mafunzo kuhusu viwango vya ufanisi wa nishati na uwekaji wa alama za ufanisi kwa vifaa vya kupikia vya majumbani vinavyotumia umeme, yaliyofanyika katika Ofisi za TBS Makao Makuu, Ubungo, Dar es Salaam.

Alisema viwango hivyo vimeweka kiwango cha chini cha ufanisi ambacho vifaa vya umeme vinapaswa kufikia ili kupunguza matumizi makubwa yasiyo na tija ya umeme.

“Viwango vinawezesha ubora wa vifaa, matumizi madogo ya umeme na uwezekano wa kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema.

Dkt. Shirima alisema matumizi bora ya nishati ni muhimu katika kupunguza gharama kwa wananchi, kulinda mazingira na kusaidia Serikali kupunguza mahitaji yasiyo ya lazima ya nishati.

Alisema TBS tayari imeandaa viwango hivyo, imejenga uwezo wa kufanya vipimo na inaendelea kusimamia udhibiti wa vifaa vinavyotumia nishati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia wa Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, alisema Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na ya gharama nafuu kwa ajili ya kupikia.

Mlay alisema matumizi ya umeme katika kupikia (eCooking) yana nafasi kubwa katika kuongeza matumizi ya nishati safi, kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa umeme nchini.

Alisema hadi sasa asilimia 28.6 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, huku Serikali ikiendelea na juhudi za kuongeza kiwango hicho kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa 2024–2034.

Mlay alisema MEPS si kikwazo kwa biashara, bali ni chombo cha kuboresha ubora wa bidhaa, kulinda watumiaji na kupunguza gharama za matumizi ya umeme.

Aidha, alisema uwekaji wa lebo za ufanisi wa nishati utawawezesha wananchi kulinganisha bidhaa na kuchagua vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi zaidi.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na TBS kwa kushirikiana na Modern Energy Cooking Services (MECS), chini ya ufadhili wa UKAid, yakihusisha wazalishaji, waagizaji, wasambazaji, wauzaji na wadau wengine wa vifaa vya kupikia kwa kutumia umeme.

Hichilema ashinda tena urais Zambia, Mundubile aibua shaka

Dar es Salaam. Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema wa Chama cha United Party for National Development (UPND), ameshinda muhula wa pili wa urais baada ya kupata kura 2,965,326, sawa na asilimia 60.5, katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 13, 2026.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zambia (ECZ), Hichilema amemshinda mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile wa National Reconciliation Party for Unity and Prosperity (NRPUP), aliyepata kura 1,856,217, sawa na asilimia 37.8.

Ushindi huo unampa Hichilema fursa ya kuendelea kuongoza Zambia kwa kipindi kingine cha miaka mitano, baada ya kuingia madarakani mwaka 2021 akimshinda aliyekuwa Rais Edgar Lungu.

Hata hivyo, uchaguzi huo umeacha maswali kadhaa kuhusu mwenendo wa mchakato, baada ya ECZ kusimamisha kwa muda uhesabuji kura kufuatia mashambulizi dhidi ya maofisa wa uchaguzi na wizi wa baadhi ya karatasi za kura. Uhesabuji uliendelea baada ya tume kusema hali ya kiusalama imedhibitiwa.

Mundubile ameeleza kutoridhishwa na mchakato huo, akitaka kumbukumbu za kura zilindwe na zihesabiwe kwa uwazi. Pia kumekuwa na taarifa za madai ya vitisho vya kiusalama dhidi yake, ingawa baadhi ya madai hayo hayajathibitishwa kwa uhuru.

Uchaguzi huo ulikuwa na wagombea zaidi ya 10, akiwamo Harry Kalaba, Fred M’membe, Kelvin Fube Bwalya na Richard Silumbe.

Uchaguzi na changamoto za demokrasia

Mchambuzi wa siasa, Absalom Kibanda, amesema malalamiko ya upinzani baada ya uchaguzi si jambo geni katika siasa za Zambia, akisema historia ya nchi hiyo imekuwa na mabadiliko ya madaraka kupitia uchaguzi.

“Zambia kumwondoa madarakani Rais ishazoeleka tangu alipoondolewa mwasisi wa Taifa hilo Kenneth Kaunda. Hichilema naye alimwondoa Rais Edgar Lungu, hivyo kushinda kwa kiongozi aliyekuwepo  madarakani na malalamiko ya upinzani yasingeepukika,” amesema.

Kibanda amesisitiza kuwa malalamiko ya uchaguzi yanapaswa kutazamwa kwa kuzingatia ushahidi na taratibu za kisheria, badala ya kuhitimisha moja kwa moja kuwa mchakato wote haukuwa halali.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Conrad Masabo, amesema uchaguzi huo unaonyesha safari ya demokrasia ya Afrika ambayo, licha ya changamoto, inaendelea kujengwa.

“Demokrasia siyo mpinzani kushinda uchaguzi, bali ni mifumo ya kisheria ya uchaguzi ya nchi husika kufuatwa kikamilifu,” amesema.

Amesema hatua ya ECZ kusimamisha uhesabuji kwa muda ili kushughulikia changamoto za kiusalama inaonyesha umuhimu wa taasisi za uchaguzi kuchukua hatua pale mchakato unapokumbwa na matatizo.

Hata hivyo, amesema madai yoyote ya kuingiliwa kwa uchaguzi kutoka nchi nyingine yanapaswa kuwasilishwa pamoja na ushahidi ili yaweze kutathiminiwa.

Mtihani wa muhula wa pili kwa Hichilema

Hichilema aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya kushiriki katika mbio za urais mara kadhaa. Kabla ya siasa, alikuwa mfanyabiashara na mwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwamo kilimo.

Alipoingia madarakani, Zambia ilikuwa ikikabiliwa na mzigo mkubwa wa deni, baada ya kutolipa deni lake la taifa mwaka 2020. Serikali yake iliongoza mchakato wa marekebisho ya deni, ikaongeza ushirikiano na taasisi za fedha za kimataifa na kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, hususan shaba.

Pia ilipanua huduma za kijamii, ikiwamo elimu ya sekondari bila ada.

Hata hivyo, gharama za maisha, ajira, umaskini na changamoto za nishati bado ni miongoni mwa masuala yanayowakabili wananchi.

Kwa hiyo, ushindi wa Hichilema unamweka mbele ya mtihani mwingine mkubwa: kuhakikisha mafanikio ya kiuchumi yanaonekana katika maisha ya Mzambia wa kawaida.

Muhula wake wa pili pia utapimwa katika eneo la demokrasia na uhuru wa kisiasa, ambako Serikali yake imewahi kukabiliwa na ukosoaji kutoka kwa wapinzani na mashirika ya kiraia kuhusu mazingira ya kisiasa, madai ambayo Serikali imekuwa ikiyakanusha.

Kwa Hichilema, ushindi huu si mwisho wa safari ya kisiasa, bali mwanzo wa muhula mwingine ambao utapima uwezo wake wa kuunganisha utulivu wa uchumi, maendeleo na demokrasia.

Bado kiza kimetanda mtoto wa siku moja aliyeibwa Dareda

Babati. Sakata la kuibwa mtoto wa siku moja katika Kituo cha Afya Dareda Kati, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, bado halijapatiwa ufumbuzi huku mama mzazi akiendelea kusubiri kwa matumaini ya kupatikana kwa mtoto wake.

Mtoto huyo alidaiwa kuibwa Agosti 8, 2026, saa 3 usiku baada ya watu wawili waliojitambulisha kuwa madaktari na muuguzi wa kituo hicho kumchukua, wakisema wanakwenda kumpatia chanjo, lakini hawakurejea naye.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Jumanne, Agosti 18, 2026, mama wa mtoto huyo, Rahma Mpinga (19) amesema ni siku 10 sasa zimepita tangu tukio hilo litokee, mtoto wake bado hajapatikana.

“Bado naamini mtoto wangu atapatikana kwa sababu hao watu waliomchukua mtoto wangu na kusema  wanaenda kumpa chanjo lakini hawakurudi, labda wamekaa naye tu, watamrudisha, nasubiri sijakata tamaa,” amesema.

Rahma amesema baada ya watu hao kumchukua mtoto wake, waliwaeleza wanawake wengine waliokuwa na watoto katika kituo hicho kuwa, wajiandae kwa sababu watoto wao pia wangepatiwa chanjo.

Hata hivyo, amesema watu hao hawakurejea na mtoto wake wala hawakurudi kuwachukua watoto wengine wawapeleke kupata chanjo kama walivyoahidi.

Amesema baadaye walipata taarifa kuwa watu hao waliondoka na mtoto huyo kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah na tangu wakati huo hawajaonekana.

Tukio hilo limemwacha Rahma katika hali ya huzuni, huku ndugu yake, Mwajuma Hamis akisema amekuwa akimsikitikia kutokana na hali anayopitia.

“Huyu ndugu yangu alikuwa na mtoto mmoja wa kiume, kisha akabahatika kupata mtoto mwingine wa kike ambaye ameibwa siku moja baada ya kuzaliwa,” amesema.

Mwajuma amesema Rahma amekuwa mtu kusononeka na kulia mara kwa mara tangu mtoto wake alipochukuliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Ahmed Makarani, amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kuwatafuta watu wanaodaiwa kuhusika.

“Pamoja na taarifa ambazo tayari tunazo, tunatoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa kuhusuiana na tukio hili azitoe katika kituo chochote cha polisi au ofisi ya Serikali,” amesema.

Kamanda Makarani amesema taarifa kutoka kwa wananchi zinaweza kusaidia vyombo vya dola kuwabaini wahusika na kumtafuta mtoto huyo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Dk Madama Hosea amesema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini waliohusika na tukio hilo na kuhakikisha mtoto anapatikana.

Dk Hosea amesema madaktari na wauguzi wa Kituo cha Afya Dareda Kati huvaa sare zao wanapokuwa kazini, huku akisema hakuna utaratibu wa kutoa chanjo nyakati za usiku.

Dola ya Marekani yadhoofika, wawekezaji wakisubiri uamuzi wa Fed

Dar es Salaam. Dola ya Marekani imeendelea kuwa dhaifu dhidi ya sarafu kuu duniani, huku wawekezaji wakipunguza matarajio ya kuongezwa kwa viwango vya riba na Benki Kuu ya Marekani (Fed) katika kipindi cha karibuni.

Kwa mujibu wa Reuters, dola ilipanda kidogo leo Jumanne, Agosti 18, 2026, lakini imeendelea kuwa karibu na viwango vyake vya chini vya hivi karibuni.

Inaelezwa kwamba mabadiliko hayo yamechangiwa na takwimu zinazoashiria udhaifu wa uchumi wa Marekani, ikiwamo hali ya soko la ajira na mfumuko wa bei uliokuwa hafifu kuliko ilivyotarajiwa.

Kutokana na hali hiyo, wawekezaji wameanza kuona uwezekano mdogo wa Fed kuongeza viwango vya riba katika mkutano wake wa Septemba.

Hata hivyo, matarajio hayo hayamaanishi kuwa benki hiyo tayari imefanya uamuzi wa kutopandisha riba.

Dola inapodhoofika, euro na pauni zimeendelea kushikilia nguvu karibu na viwango vyao vya juu vya hivi karibuni.

Mzozo wa Marekani, Iran waongeza wasiwasi

Pamoja na mabadiliko ya matarajio kuhusu sera ya fedha ya Marekani, mzozo unaoendelea kati ya Marekani na Iran umeongeza presha katika masoko ya fedha na nishati.

Mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu yamekwama, huku Iran ikisema iko tayari kuchukua msimamo mkali zaidi wa kijeshi na Marekani ikikataa kuongeza muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Hali hiyo imeongeza hofu kuhusu usafirishaji wa mafuta katika Mashariki ya Kati, hasa kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu kwa biashara ya kimataifa ya mafuta na gesi.

Reuters imeripoti kuwa harakati za meli katika eneo hilo zimeendelea kuwa chache, huku Iran ikisema mlango huo utaendelea kufungwa hadi Marekani itimize masharti ya makubaliano ya muda yaliyofikiwa Juni.

Bei ya mafuta ghafi ya Brent jana ilifikia karibu dola 91 kwa pipa, ikiongezeka kwa siku ya tatu mfululizo kutokana na kupungua kwa matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano ya amani kati ya Washington na Tehran.

Hali hiyo inaiweka Fed katika mazingira magumu. Kwa upande mmoja, udhaifu wa baadhi ya viashiria vya uchumi unaweza kutoa sababu ya kutopandisha riba.

Kwa upande mwingine, kupanda kwa bei ya mafuta kunaweza kuongeza mfumuko wa bei na kuifanya Fed kuwa makini zaidi katika kulegeza sera ya fedha.

Dhamana za Marekani nazo zatikisika

Wakati dola ikidhoofika, soko la dhamana za Serikali ya Marekani limekumbwa na presha.

Mavuno ya dhamana ya Hazina ya Marekani ya miaka 30 yalipanda hadi asilimia 5.327, kiwango cha juu zaidi tangu mwaka 2007. Mavuno ya dhamana yanapopanda, bei ya dhamana hushuka, hali inayoonyesha wawekezaji wanahitaji faida kubwa zaidi ili kuendelea kushikilia madeni ya muda mrefu.

Wawekezaji pia wana wasiwasi kuhusu ongezeko la deni na mahitaji makubwa ya serikali ya Marekani ya kukopa, mambo yanayoongeza shinikizo kwenye soko la dhamana na gharama za muda mrefu za kukopa.

Kwa sasa, wawekezaji wanaelekeza macho kwenye mawasiliano ya Fed, ikiwamo kumbukumbu za mkutano wake na mkutano wa Jackson Hole, wakitafuta ishara kuhusu mwelekeo wa sera ya fedha.

Masoko yanaendelea kupima mambo mawili kwa wakati mmoja: udhaifu wa baadhi ya viashiria vya uchumi wa Marekani unaoweza kupunguza haja ya kuongeza riba, na hatari ya mzozo wa Mashariki ya Kati kusababisha kupanda zaidi kwa bei ya mafuta na mfumuko wa bei.

Mchanganyiko huo umeifanya dola kubaki chini ya presha, huku wawekezaji wakisubiri ishara mpya kuhusu mwelekeo wa uchumi wa Marekani, sera ya Fed, bei ya mafuta na hatima ya mzozo wa Marekani na Iran.