TACAIDS YAWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inaendelea kuimarisha mikakati madhubuti ya kupambana na VVU na UKIMWI kupitia ushirikiano wa kisekta, kuhamasisha vyanzo vya fedha vya ndani, kusogeza huduma karibu na jamii ikiwemo Vituo vya Maarifa kwa madereva wa malori na kuwajengea uwezo vijana na wanawake ili kufikia lengo la kutokomeza kabisa janga hili ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ilipokutana kwa lengo la kupokea taarifa ya wasilisho la hali ya Maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa Vijana na Mkakati wa Kupunguza Maambukizi Mapya kwa Vijana, kilichofanyika tarehe 20 Agosti, 2026 Bungeni Jijini Dodoma.

Waziri Kabudi ameipongeza Kamati kwa namna ilivyoshauri na kupendekeza  uboreshwaji wa masuala  mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, kuongeza nguvu kufikia vijana hasa walioko vijijini, elimu zaidi katika maeneo ya starehe ikiwemo kumbi za miziki na makongamano ya vijana lengo ni kuhakikisha jamii inafikiwa kwa ukubwa wake.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt. Johannes Lumbulung Lukumay ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna inavyoratibu masuala ya Afua za UKIMWI nchini huku akieleza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha Utekelezaji wa Afua hizo unafanikiwa bila mkwamo wowote.

“Ni vyema sasa kuendelea kuwajengea uwezo vijana katika mikoa yenye ushamiri mkubwa wa maambukizi na kuratibu utoaji wa elimu na upimaji wa hiari katika maeneo ya kazi na sekta ya usafirishaji hususan kwa madereva wa malori wa masafa marefu,” alisema Dkt. Lukumay

Vilevile ameipongeza Serikali kwa namna ilivyowekeza nguvu kuhakikisha janga hili linatokomezwa pamoja na kubuni program na miradi mbalimbali ikiwemo ya TIMIZA Malengo Awamu ya Tatu, inayoendeshwa na kauli mbiu isemayo; “Tusonge na Samia kutokomeza UKIMWI, ambavyo vinaleta mwamko wa jamii kujitokeza kupima afya zao na kuendelea kuchukua tahadhari juu ya maambukizi mapya ya VVU.

Pia wajumbe wa kamati hiyo  wamepongeza na kuishukuru Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa Dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zinazosaidia kuimarisha kinga ya mwili, kuzuika VVU kujizalisha mwilini na kushusha kiwango cha Virusi hadi kutokuonekana ili kuzuia maambukizi mapya kwa jamii.

Akifafanua hoja za wajumbe wa kamati hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Adam Mrisho amesema, ofisi yake imeendelea kuweka mikakati madhubuti na hatua za makusudi katika kuhakikisha utekelezaji wa Afua za UKIMWI unafanyuka vyema na kuyafikia makundi yote hususan vijana.

“Tume imejipanga kuhakikisha elimu inaendelea kuifikia jamii ili kuwa na utayari wa kupima na kuhamasisha matumizi ya dawa kwa watakao gundulika kuwa na maambukizi ya VVU pamoja na kuimarisha mashirikiano na sekta binafsi” alieleza Dkt. Mrisho

Jitihada zingine ni kuwezesha wahudumu ngazi ya jamii wapatao elfu tisini kwa kuwapatia elimu ya kutoa huduma za kinga na huduma za JIPIME, hivyo kusaidia kuwafikia vijana waliopo vijijini na kuongeza mwitikio wa masuala ya UKIMWI.

Pia mikakati mingine ni kuviwezesha na kuboresha vituo 32 vya maarifa vinavyotoa elimu ya kinga, huduma za ARVs, upimaji na kuhakikisha vijana wanapewa elimu za masuala ya UKIMWI hususani madereva wa malori ya masafa marefu kupitia vituo hivyo vilivyopo nchini. 

TBS YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA UDHIBITI WA UBORA WA BIDHAA

 

Na Matukio Daima Media 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara,Kilimo na Mifugo imeipongeza TBS kwa kutekeleza majukumu yake ya udhibiti ubora kwa ufanisi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Deogratias Mwanyika kwaniaba ya kamati wakati wa kikao cha Kamati cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu,katika,

ofisi za Bunge Jijini Dodoma mapema leo.

Mhe.Mwanyika amesema juhudi zinazofanywa na TBS katika kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania zinaonekana hata hivyo ametoa rai kwa TBS kuendelea kutoa elimu na kuongeza jitihada sambambana na kuwa na programu maalum za kushughulikia bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi.

Naye Mhe. Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga(Mb) ameishukuru kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo ili kuendelea kurahisisha utendaji kazi wa TBS.

Vile vile Mhe.Kapinga amesema lengo la Wizara kupitia TBS ni kuhakikisha kunakuwa na bidhaa zenye ubora na usalama katika soko zinazozalishwa ndani na zinazotoka nje ya nchi.

Wakili Madeleka kortin, asomewa mashtaka matano

Dar es Salaam. Wakili wa Mahakama Kuu, Peter Madeleka amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matano ya kuidharau Mahakama.

Madeleka amefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi Agosti 20, 2026 na kusomewa kesi ya jinai yenye mashtaka matano na wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato akishiriana na Mosei Kaima na Veronica Chacha, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Mshtakiwa huyo anatetewa na wakili Maduhu William. Akimsomewa shtaka na wakili Kato, alidaiwa Julai 27,2026 eneo la Mawasiliano, Wilaya ya Ubungo akiwa kama wakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi namba 4521/2026 kati ya Jamhuri dhidi mshtakiwa Wendy Ishengoma na wenzake wanne wakati kesi hiyo inaendelea katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi, mshtakiwa anadaiwa kutoa au kuchapisha maneno mitandaoni au katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Jambo TV kuhusiana na kesi hiyo.

Ilidaiwa kitendo hicho kilionesha kudharau amri ya Mahakama iliyotolewa Julai 27,2026 na Jaji aliyekuwa akiendesha kesi hiyo.

Shtaka la pili, anadaiwa Julai 28,2026 katika eneo hilo akiwa wakili wa utetezi katika kesi hiyo, anadaiwa alitoa maneno na kuchapisha maelezo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Jambo Tv kuhusiana na kesi hiyo.

Wakili Peter Madeleka akiwa Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Agost 20, 2026 akishtakiwa kwa Mashitaka matano ya kudharau Mahakama kwa kusambaza maneno ya kesi zinazoendelea mahakamani. Picha na Said Powa

Shtaka la tatu, Madeleka anadaiwa Agosti 7, 2026 katika eneo la Mikocheni wilaya ya Kinondoni, akiwa wakili wa utetezi katika kesi hiyo (Wendy na wenzake) wakati kesi ikiwa bado inaendelea Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi alitoa maneno na kuchapisha katika vyombo vya habari mbalimbali ikiwemo Jambo TV kuhusu kesi hiyo.

Ilidaiwa kitendo hicho kilionesha kutokuheshimu amri ya Mahakama iliyotolewa na Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo Julai 27,2026.

Vilevile, anadaiwa kuwa Agosti 7,2026 katika eneo la Mikocheni wilaya ya Kinondoni, akiwa kama wakili wa utetezi katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Wendy Ishengoma na wenzake wakati kesi ikiwa bado inaendelea katika Mahakama Kuu, alitoa na kuchapisha kauli kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Jambo TV ambayo inadaiwa kupotosha mwenendo wa kesi.

Alidaiwa kauli hiyo ilisomeka kama “Mawakili wa Serikali walikuwa wanaomba vielelezo vilivyotolewa mahakamani vikahifadhiwe kwenye ofisi ya Taifa ya Mashtaka” huku akijua kauli hiyo ni ya uongo.

Shtaka la tano, Madeleka anadaiwa Agosti 13, 2026 ndani ya Wilaya ya Ubungo, akiwa kama wakili wa utetezi katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi, wakati kesi ikiwa bado inaendelea Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi, alitoa na kuchapisha kauli kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Jambo TV kuhusu kesi hiyo.

Ilidaiwa kitendo hicho kilionesha kutoheshimu amri ya Mahakama iliyotolewa Julai 27, 2026 na Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo.

Mshtakwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, alikana kuhusika na tuhuma hizo.

Upande wa jamhuri, ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomewa hoja za awali (Ph).

Hakimu Makube alitoa masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, ambayo alimtaka awe na wadhamini wawili watakaosiani bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Pia wadhamini hao wanatakiwa wawe na utambulisho wa barua kutoka serikali za mitaa au taasisi zinazotambulika kisheria mwenye vitambulisho vya taifa.

Mshtakiwa amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na kuachiwa kwa dhamana.

Hakimu Makube aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 9, 2026 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali(Ph)

MAONESHO YA UCHUMI PARACHICHI MARATHON YAZINDULIWA RASMI NJOMBE

Mkuu wa mkoa wa Njombe amezindua maonesho ya Uchumi Parachichi marathon  yatakayokwenda kwa siku tatu  na Kuwataka wananchi kuacha tabia ya kutupa parachichi zilizochini ya kiwango[Reject] kwani kuna viwanda vingi mkoani Hapa.

Akizindua maonesho hayo akiwa katika stendi ya zamani mjini Njombe Mtaka amesema kufunguliwa kwa viwanda kumefunga hoja ya parachichi mbovu na hivyo walime kwa kujiamini na kujipatia kipato.

Awali mratibu msaidizi wa Uchumi Parachichi marathon Ichikael Malisa amesema maonesho hayo mbali na kuhusisha masuala ya kimechezo lakini pia wanasisitiza suala la lishe Bora pia.

Kwa upande wao wakazi wa Njombe akiwemo Tumsifu sanga ambaye ni mjasiriamali anaye uza parachichi ndani ya soko kuu amesema tunda hilo kwa sasa linachangamoto katika soko huku Diwani wa kata ya Njombe mjini Deo Mazao Sanga na Mratibu wa Mbunge wa Jimbo la Njombe mjini Chrispin Kalinga kwa Niaba ya Mbunge wakikiri kuwa maonesho hayo ni fursa kubwa kwa uchumi wa wananchi.

Kilele cha maonesho hayo ni Agosti 23 siku ya Juma pili huku mkuu wa mkoa akiagiza kuandaliwa kwa nyama choma kwa siku zote za maonesho ili kutia hamasa kwa wananchi.

Muuza magari ageuka mwana wa mfalme

Dar es Salaam. “Unaweza ukalala maskini na kuamka tajiri,” Kauli hiyo inaweza kuelezea kwa ufupi mabadiliko ya maisha ya Clément Vandenkerckhove, raia wa Ubelgiji aliyewahi kufanya kazi kitengo cha mauzo katika kampuni ya magari, kabla ya kutambuliwa rasmi kuwa mtoto wa Prince Laurent wa Ubelgiji.

Vandenkerckhove, mwenye umri wa miaka 26, sasa ametambuliwa kisheria kama mwanamfalme wa Ubelgiji baada ya Prince Laurent, mdogo wake na Mfalme Philippe, kukiri na kuthibitisha  kuwa ndiye baba yake mzazi.

Hatua hiyo imehitimisha miaka kadhaa ya sintofahamu kuhusu uhusiano wa Vandenkerckhove na familia ya kifalme ya Ubelgiji.

Kwa mujibu wa jarida la Soir Mag, Prince Laurent alikamilisha mchakato wa kisheria wa kumtambua Vandenkerckhove mbele ya msajili wa kiraia Februari mwaka huu. Vandenkerckhove pia alihudhuria na kusaini nyaraka hizo.

Ikulu ya Ubelgiji imethibitisha kuwa Prince Laurent amemtambua kisheria Vandenkerckhove kuwa mwanawe, lakini imeeleza kuwa suala hilo ni la kifamilia na haikutaka kutoa maelezo zaidi.

Kutokana na kutambuliwa huko, Vandenkerckhove amepewa hadhi ya mwanamfalme, ingawa hatarajiwi kuwa na majukumu rasmi ya kifalme.

Vandenkerckhove ni mtoto wa Prince Laurent na Iris Vandenkerckhove, anayefahamika zaidi kwa jina la Wendy Van Wanten, mwanamitindo, mwimbaji na mwigizaji maarufu nchini Ubelgiji.

Prince Laurent ni mdogo wa Mfalme Philippe na ana watoto wengine watatu aliowapata na mkewe, Princess Claire wa Ubelgiji, ambaye alimuoa mwaka 2003.

Licha ya kupata hadhi ya mwanamfalme, Vandenkerckhove hataingia kwenye mstari wa kurithi kiti cha ufalme wala kuwa na majukumu rasmi ya kifalme.

Kwa mujibu wa New York Times, Profesa Christian Behrendt, mtaalamu wa sheria za katiba kutoka Chuo Kikuu cha Liège nchini Ubelgiji, amesema hadhi hiyo imetokana na amri ya kifalme ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Profesa Behrendt, mtu anaweza kuingia kwenye mstari wa urithi wa kiti cha ufalme endapo amezaliwa katika ndoa iliyopitishwa na serikali kupitia amri maalumu.

Hivyo, ingawa Vandenkerckhove sasa anatambuliwa kama mwanamfalme, hana nafasi ya kumrithi Mfalme Philippe, ambaye ni baba yake mkubwa.

Prince Laurent alitangaza Septemba mwaka jana kwamba Vandenkerckhove ni mwanawe wa damu, akisema uamuzi huo ulifanyika kwa kuzingatia uelewano na heshima kwa wote waliohusika.

Uhusiano wao umeendelea kuonekana hadharani. Juni mwaka huu, Vandenkerckhove alichapisha picha akiwa na Prince Laurent pamoja na picha nyingine akiwa na Frans Vancoppenolle, ambaye amekuwa mwenza wa muda mrefu wa mama yake, katika ujumbe wa kuadhimisha Siku ya Baba.

Vandenkerckhove alizaliwa Agosti 2000 kutokana na uhusiano wa zamani kati ya Prince Laurent na Iris Vandenkerckhove.

Wawili hao walikuwa na uhusiano katika miaka ya 1990, kabla ya Prince Laurent kumuoa Princess Claire mwaka 2003.

Kwa muda mrefu, utambulisho wa baba wa Vandenkerckhove ulizungumziwa katika vyombo vya habari nchini Ubelgiji, lakini familia hiyo haikuthibitisha rasmi madai hayo hadi Prince Laurent alipotoa tamko mwaka jana.

Kabla ya kutambuliwa rasmi, Vandenkerckhove aliishi maisha ya kawaida na hata kufanya kazi hiyo.

“Nataka uhusiano na baba yangu.”

Kwa Vandenkerckhove, kupata cheo cha kifalme si jambo pekee lenye umuhimu. Zaidi ya hadhi hiyo, ameeleza umuhimu wa kujenga uhusiano wa karibu na baba yake baada ya miaka mingi ya kutokuwa na uhakika kuhusu nafasi yake katika familia ya kifalme.

Taarifa zinaeleza kuwa Prince Laurent amekuwa akitenga muda kwa ajili ya mwanawe huyo na wawili hao wameendelea kujenga uhusiano wao kupitia mazungumzo na muda wanaotumia pamoja.

Vandenkerckhove pia hajaonyesha haraka ya kubadili jina lake la ukoo kuwa la kifalme, huku akiendelea kujitambulisha kwa jina la familia ya mama yake.

Imeandikwa na Anitha Bosco kwa msaada wa mtandao.

Sababu makada watano kuiburuta Chadema, Msajili wa vyama kortini

Moshi. Makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao kwa nyakati tofauti walivuliwa au kusimamishwa katika nafasi za uongozi ndani ya chama hicho, wameanzisha mchakato wa kisheria kupinga hatua zilizochukuliwa dhidi yao.

Makada hao wamefungua maombi katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dodoma, wakitaka kupatiwa kibali cha kuanzisha mapitio ya kimahakama kupinga uamuzi wa kusimamishwa au kuondolewa kwao katika nafasi za uongozi.

Maombi hayo yaliyofunguliwa chini ya hati ya dharura yamepangwa kusikilizwa Agosti 25, 2026, mbele ya Jaji Amir Mruma.

Katika shauri hilo, waombaji wameitaja Bodi ya Wadhamini ya Chadema kuwa mjibu maombi wa kwanza, Katibu Mkuu wa Chadema mjibu maombi wa pili, huku Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakitajwa kuwa wajibu maombi wa tatu na nne mtawalia.

Waombaji hao wanaowakilishwa na wakili Joseph Kipeche, ni Barnabas Okola, Lembrus Mchome, Joseph Mwakidasi, Mathias Cosmas na Abubakari Mashambo.

Okola ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, ambaye alisimamishwa nafasi yake ya uongozi Julai 9, 2026, lakini baadaye akakata rufaa na kurejeshwa katika nafasi hiyo.

Mchome, kwa upande wake ni mwanasiasa ambaye alivuliwa uongozi na kufukuzwa uanachama wa Chadema Mei 2025, kufuatia mvutano ulioibuka baada ya kuhoji na kupinga uteuzi wa viongozi wa sekretarieti ya chama hicho.

Wengine ni Mwakidasi, aliyekuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Muheza; Cosmas, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilindi; na Mashambo, ambaye anatajwa kuwa Katibu wa Chadema Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Mashambo alisimamishwa na uongozi wa chama kuanzia Julai 10, 2026, kufuatia mivutano na kauli zilizohusu ukosoaji wa mambo ya ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Kwa nini wamekimbilia kortini?

Kwa mujibu wa maombi yao yaliyowasilishwa kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa e-Services Portal, wameomba shauri lao lisikilizwe kwa dharura.

Katika hati zao, waombaji wanadai kuwa Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa Chadema wameanzisha taratibu za kinidhamu dhidi yao na hatua hizo zinaweza kuwaweka katika mazingira ya kuadhibiwa mara mbili kwa tuhuma zinazofanana.

“Wajibu maombi wa kwanza na wa pili wameanzisha taratibu za kinidhamu dhidi ya waombaji. Isipokuwa maombi haya yasikilizwe kwa dharura, waombaji watapata adhabu mara mbili,” wameeleza katika maombi yao.

Waombaji pia wanadai kuwa walisimamishwa na wajibu maombi hao kabla ya kusikilizwa na baadaye walipewa taarifa ya kuwasilisha utetezi wao dhidi ya tuhuma hizo hizo, huku hatua ya kuwasimamisha katika nafasi za uongozi ikiwa tayari imechukuliwa.

Kupitia maombi hayo, wanaiomba Mahakama Kuu iwape kibali cha kuwasilisha maombi ya mapitio ya kimahakama (judicial review) kupinga uamuzi wa kusimamishwa au kuondolewa kwao katika nafasi za uongozi. Kupata kibali hicho ni hatua ya awali inayotakiwa kisheria kabla ya shauri la mapitio ya kimahakama kuendelea kusikilizwa.

Shauri hilo linakuwa miongoni mwa kesi zinazohusu migogoro ya ndani ya Chadema kufikishwa mahakamani katika kipindi cha hivi karibuni.

Kabla ya shauri hilo, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake wawili, walifungua kesi namba 8323 ya mwaka 2025 katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Katika shauri hilo, walikuwa wakilalamikia kile walichodai kuwa ni kutokuwepo kwa mgawanyo sawa wa rasilimali, fedha na mali za Chadema kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Juni 10, 2025, Jaji Hamidu Mwanga, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, alitoa amri ya kuzuia Chadema kufanya shughuli za kisiasa nchini na kutumia mali zake hadi shauri hilo litakapomalizika. Inaelezwa kuwa amri hiyo ilidumu kwa siku 309.

Hata hivyo, Aprili 15, 2026, Mahakama ya Rufaa ilifuta amri hiyo, ikisema Mahakama Kuu ilikosea kuendelea na usikilizwaji wa shauri baada ya mawakili wa wadaiwa kujiondoa.

Uamuzi huo uliiondoa Chadema katika zuio la kufanya shughuli zake za kisiasa na kutumia mali zake.

Zuio hilo lilikuwa limeathiri uwezo wa chama hicho kufanya mikutano, kampeni na kutumia mali zake katika kipindi kilichotangulia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Chadema ilidai kuwa utekelezaji wa amri hiyo pia ulisababisha uharibifu wa baadhi ya mali zake na kunyima wanachama haki ya kushiriki katika shughuli za kisiasa.

Baadaye, Mei 28, 2026, Jaji David Ngunyale wa Mahakama Kuu alitupilia mbali kesi hiyo kwa maelezo kwamba kulikuwa na dosari za kisheria katika madai yaliyowasilishwa.

Juni 6, 2026, Kamati ya Utendaji ya Chadema Kanda ya Pemba ilimfukuza Said Issa Mohamed kutoka katika chama hicho, kwa madai ya kukiuka Katiba ya Chadema.

Hata hivyo, Mohamed ameendelea kupigania masuala yanayohusu chama hicho mahakamani, baada ya yeye na mwenzake kufungua shauri jipya namba 13832 la mwaka 2026 katika Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, likiwa na maudhui yanayohusu mgawanyo wa mali na rasilimali za chama hicho.

Majaji Wakuu wa nchi 17 kujifungia Z’bar, kujadili utoaji haki

Unguja. Majaji Wakuu wa nchi 17 wanachama wa Jumuiya ya Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), wanatarajiwa kukutana Zanzibar Oktoba mwaka huu, katika mkutano unaolenga kujadili changamoto za kisheria na kubadilishana uzoefu wa utoaji wa haki.

Mkutano huo wa mwaka wa SEACJF utafanyika Oktoba 5 hadi 9, 2026, katika Hoteli ya Verde, mjini Unguja, na unatarajiwa kuwashirikisha takribani watu 150, wakiwemo majaji, mawakili, wadau wa sheria na wanafunzi.

Nchi zinazotarajiwa kushiriki ni Lesotho, Eswatini, Angola, Botswana, Kenya, Malawi, Mauritius, Zambia, Namibia, Afrika Kusini, Seychelles, Uganda, Msumbiji, Zimbabwe, Tanzania na Zanzibar.

Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, Agosti 20, 2026 na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Jaji Abdalla amesema mkutano huo utatoa fursa kwa nchi wanachama kujadili changamoto mbalimbali za kisheria, kukuza mageuzi ya sheria na kubadilishana maarifa, huku wakijadili pia matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuboresha utoaji wa haki.

“Mkutano huu ni jukwaa muhimu linalowakutanisha pamoja Majaji Wakuu na waalikwa wengine kujadili mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazozikabili Mahakama za nchi za Afrika,” amesema.

Amesema jukwaa hilo pia litatumika kuweka mikakati na kubadilishana uzoefu kuhusu shughuli za kimahakama na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazokabili sekta hiyo, kwa lengo la kuimarisha utawala wa sheria na kurahisisha upatikanaji wa haki.

Jaji Abdalla amesema Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto katika usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji, huku baadhi ya mashauri yakichukua muda mrefu kumalizika mahakamani.

Amesema hali hiyo inaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji, hivyo mkutano huo utawapa fursa ya kujifunza kutoka kwa nchi nyingine kuhusu namna bora ya kushughulikia mashauri ya aina hiyo kwa ufanisi.

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, huku Makamu wa Rais wa Botswana, Ndaba Nkosinathi Gaolathe, akitarajiwa pia kuhudhuria mkutano huo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Balu Lada Balu, amesema mkutano huo utatoa fursa ya kukuza ushirikiano wa kitaaluma miongoni mwa nchi wanachama hususan katika masuala ya sheria na utoaji haki.

Baba aliyehukumiwa kifo kwa kumuua bintiye, aachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani imemwachia huru Abutwalib Salum, aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua binti yake mwenye umri wa miaka mitano na mwenye ulemavu wa viungo, ambaye mwili wake ulipatikana mtoni.

Mahakama hiyo imefuta hukumu ya mauaji na kutengua adhabu ya kifo baada ya kubaini kasoro katika ushahidi uliotumiwa kumtia hatiani Salum, hususan maelezo ya ziada yaliyodaiwa kuwa ungamo lake ambayo hayakusomwa mahakamani baada ya kupokelewa kama kielelezo.

Uamuzi huo ulitolewa Agosti 18, 2026 na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye, Khamis Ramadhan Shaaban na Cyprian Mkeha, katika rufaa namba 370 ya mwaka 2023.

Majaji hao walisema utaratibu sahihi wa kupokea hati kama ushahidi unahitaji hati hiyo kukubaliwa, kutangazwa kuwa kielelezo na hatimaye kusomwa mahakamani.

Kwa kuwa hatua ya mwisho haikufanyika, Mahakama ya Rufani ilisema kasoro hiyo ilikuwa kubwa na ilimnyima Salum fursa ya kuelewa kikamilifu maudhui ya ushahidi uliotumika dhidi yake na kuandaa utetezi wake.

Kutokana na hali hiyo, mahakama iliondoa maelezo hayo kwenye rekodi na kuchambua ushahidi uliobaki. Katika kesi ya msingi, Jamhuri ilidai kuwa Februari 12, 2021, katika Kata ya Igumbilo, Manispaa ya Iringa, Salum alimuua binti yake, Khadija Abutwalib.

Sophia Hassan, aliyekuwa mlezi wa mtoto huyo, alieleza kuwa kutokana na ulemavu wake, Khadija hakuweza kutembea vizuri. Alidai Salum alimwomba amsaidie kumlea mtoto huyo kwa malipo na aliishi naye kwa miezi mitatu.

Alisema Februari 6, 2021, Salum alidaiwa kumchukua Khadija nyumbani kwake wakati yeye hayupo na hakumwona tena hadi alipopata taarifa za kupatikana kwa mwili wa mtoto na kwenda kuutambua.

Ushahidi mwingine ulieleza kuwa mwili wa mtoto huyo ulipatikana mtoni, huku daktari aliyefanya uchunguzi akieleza kuwa mwili ulikuwa umeharibika kwa kuoza baada ya kukaa majini kwa siku kadhaa na hivyo hakuweza kubaini chanzo cha kifo.

Pamoja na ushahidi huo, upande wa mashtaka uliwasilisha maelezo ya ziada yaliyodaiwa kuwa ungamo la Salum, akidaiwa kukiri kumtupa mtoto wake mtoni kwa sababu hakuweza kuendelea kumtunza.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa ilimtegemea ushahidi huo pamoja na ushahidi wa kimazingira, ikiwamo kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, kumtia Salum hatiani na kumhukumu kunyongwa.

Hata hivyo, baada ya Mahakama ya Rufani kuondoa maelezo hayo kwenye rekodi, ilibaini ushahidi uliobaki haukutosha kuthibitisha kwamba Salum alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na mtoto huyo.

Majaji walibaini kuwa shahidi wa kwanza hakumwona Salum akimchukua Khadija, bali alieleza alichoambiwa na watu wengine ambao hawakuitwa mahakamani kutoa ushahidi.

Mahakama ilisema watu hao walikuwa mashahidi muhimu ambao wangeweza kueleza mazingira na wakati ambao Salum alidaiwa kumchukua mtoto.

Kutokana na kasoro hizo, majaji walihitimisha kuwa ushahidi haukuthibitisha kosa la mauaji dhidi ya Salum.

“Kwa hivyo, tunaruhusu rufaa, tunaifuta hukumu na kubatilisha adhabu iliyotolewa dhidi ya mrufani,” majaji wameeleza katika uamuzi wao.

Mahakama ikaamuru Salum aachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

Wazee waombwa wasinyamaze, wasiwe wanaharakati

Dodoma. Wazee nchini wameombwa kutokwepa wajibu wao wa kukemea maovu bila kujikita katika kuwalaumu vijana kwa kila jambo kabla hawajawapa elimu.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi Agosti 20, 2026 na Mwenyekiti wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania Mkoa wa Dodoma, Peter Mavunde wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano mkuu wa chama hicho, unaotarajia kufanyika jijini hapa Agosti 29, 2026.

Mavunde amesema wazee hawana sababu ya kuogopa jambo lolote katika kushauri au kuonya, isipokuwa wasiwe wanaharakati.

“Wazee tuna wajibu wa kuwalea vijana na kuwafundisha mila, tamaduni na uzalendo kwa Taifa lao, hatupaswi kukaa kimya tunapoona mambo yanaharibika, tukumbuke kuwalea vijana badala ya kuwalaumu,” amesema Mavunde.

Mavunde ambaye alizungumza kwa niaba ya rais wa chama hicho, Thadey Mchena, amesema umri mkubwa siyo kwamba mtu amepoteza maarifa, bali anaweza kutumika kama hazina na kisima cha maarifa ya kusaidia nchi.

Amesema mkutano huo ambao mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, utakuwa ni fursa kwa wazee wanaume kujadili masuala yanayowahusu na kuweka mikakati ya kushiriki katika maendeleo ya jamii.

Amesema chama hicho kinalenga kuwaunganisha wazee wanaume kushiriki katika malezi ya vijana kimaadili, kutunza tunu za taifa na kuchangia shughuli za maendeleo na ustawi wa jamii.

Amesema mkutano huo pia utajadili upatikanaji wa huduma za afya na matibabu, ikiwemo changamoto za baadhi ya wazee kukosa matunzo kutokana na kukosa rasilimali na watoto wao kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia.

Kwa mujibu wa Mzee Mavunde, Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia na jitihada za kulinda na kuimarisha ustawi wa wazee nchini, akisema msisitizo huo unapaswa kuungwa mkono kwa utekelezaji wa sera na sheria zinazolinda masilahi yao.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Alhaj Idd Maalim amesema wamejipanga kuishauri Serikali na kufikisha kilio cha wazee ambao wanapitia magumu mengi.

Hata hivyo, Maalim amesema nyingi ya changamoto hizo zinajulikana ikiwemo suala la tiba kwa afya zao, hasa ambao hawakuwahi kuwa watumishi na wasio na uwezo.

Mkutano huo wa siku sita utakuwa wa kwanza tangu chama hicho kilipopata usajili na wanategemea kuwa na washiriki wasiopungua 200 kutoka mikoa yoyote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mo Dewji kuwekeza Sh661 bilioni Msumbiji

Maputo. Bilionea wa Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohammed Dewji, maarufu Mo ameahidi kuwekeza Dola 250 milioni (Sh661.93 bilioni), nchini Msumbiji na ahadi ya kuajiri raia 20,000 wa nchi hiyo.

Mo alitoa ahadi hiyo baada ya kukutana na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo mjini Maputo Jumanne ya Agosti 18, 2026, akisema mazungumzo yao yalikuwa na tija na tayari amebaini fursa kadhaa za uwekezaji nchini humo.

“Tumekuwa na mazungumzo yenye tija na tumedhamiria kuwekeza Dola 250 milioni nchini Msumbiji na kuajiri watu 20,000,” amesema Mo.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikuelekeza fedha hizo zitaelekezwa katika sekta gani wala ratiba ya kuanza kwa uwekezaji huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ureno (Lusa), taarifa iliyotolewa na Ikulu Msumbiji inaeleza ahadi iliyotolewa na Dewji inaendana na shughuli za MeTL, inafungua fursa za uwekezaji katika maeneo ya kimkakati pamoja na kuanzishwa kwa minyororo mipya ya uzalishaji, usambazaji na huduma nchini humo.

Taarifa hiyo ilisema mkutano huo umefanyika wakati Serikali ya Msumbiji ikitafuta kuongeza uwekezaji binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi, uendelezaji wa viwanda na uundaji wa ajira, huku ikiimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika.

MeTL ni miongoni mwa biashara za binafsi zinazomilikiwa na Watanzania, ikiwa na shughuli katika kilimo, uzalishaji viwandani, usafirishaji na ugavi, nishati, biashara na huduma za kifedha.

Kampuni hiyo inaajiri takribani watu 37,000 na tayari ina shughuli katika zaidi ya nchi 12 za Afrika, ikiwamo Msumbiji.

Taarifa hiyo ikiwa ahadi hiyo itatekelezwa, ajira 20,000 zitakazotengenezwa zitaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wafanyakazi wa kundi hilo nchini humo.

Msumbiji imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kuvutia mitaji binafsi nje ya miradi ya gesi asilia katika mkoa wa Cabo Delgado ambako uasi umesababisha kuchelewa mara kadhaa kwa utekelezaji wa miradi hiyo.

Dewji, mwenye umri wa miaka 51, alichukua uongozi wa biashara iliyoanzishwa na baba yake, Gulam miaka ya 1970 kama kampuni ya biashara na baadaye akaipanua kuwa kundi lenye shughuli za uzalishaji wa nguo, mafuta ya kula, unga, vinywaji na usindikaji wa mazao ya kilimo.

Jarida la Forbes linakadiria utajiri wake kuwa Dola 2.1 bilioni (sawa na Sh5.56 trilioni) jambo linalomfanya kuwa mtu wa 14 kwa utajiri barani Afrika na Mtanzania pekee aliyeorodheshwa kwenye orodha hiyo.

Dewji aliwahi kuwa mbunge wa Singida Mjini kwa vipindi viwili, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 pia alikuwa Mtanzania wa kwanza kusaini Giving Pledge akiahidi kutoa angalau nusu ya utajiri wake kwa shughuli za kijamii.

Mbali na biashara, Dewji anamiliki asilimia 49 ya Simba Sports Club Company Limited, klabu ya soka ya Dar es Salaam na Agosti mwaka huu aliahidi takribani Dola 11.3 milioni (takribani Sh29.9 bilioni) kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na kituo cha mazoezi cha klabu hiyo eneo la Bunju, ikiwa ni pamoja na idhini ya Bodi ya Wadhamini.