Vikundi vya michezo kunufaika mikopo asilima 10 – HabariLeo

MOROGORO: MBUNGE wa Jimbo la Mvomero, mkoani Morogoro, Sara Msafiri, amevitaka vikundi ambavyo vitashiriki kwenye tamasha la michezo kwenye jimbo hilo vitakuwa vya kijasiriamali na vitasaidiwa usajili ili vipate kunufaika na fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Msafiri amesema hayo wakati akizindua Tamasha la Sara Festival litakalohusisha mashindano ya mpira wa miguu ,ngoma za asili na riadha kwa kushirikisha vijiji vyote 130 vilivyopo katika kata 30 katika halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema lengo la tamasha hilo si tu kuibua vipaji vya vijana bali ni njia sahihi ya kuhimiza vijana kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa vijana ,wanawake na makundi maalumu.

“Kikundi cha ngoma , timu za mpira wa miguu pamoja na riadha za kutoka vijiji vyote 130 vilivyopo ndani ya wilaya yetu kitakachoshiriki pia kitageuzwa kuwa ni cha ujasiriamali na kitasaidiwa kusajiliwa na halmashauri kinufaike na asilimia 10,” amesema Msafiri.

Msafiri amewataka washiriki wa tamasha hilo kuhakikisha wanatumia fursa ya kujitangaza vizuri kwa sababu litakuwa jukwaa kubwa litakalofuatiliwa na watu wengi na hivyo kuwafungulia njia ya kushiriki matamasha ya kitaifa na kimataifa

Mbunge huyo ametolea mfano kuwa ngoma za kabila la Waluguru zimekuwa zikiwavutia watu wengi kutokana na kuendelea kudumisha mila zenye kusisitiza maadili, desturi na utamaduni wa Mwafrika

Naye, Mwenyekiti wa Chimbuko Band na Kikundi cha Ngoma ya Asili ya Mdundiko kutoka Kijiji cha Tangeni, John Mkude amesema kikundi hicho kinazaidi ya miaka 50 na kimekosa kuungwa mkono wa ufadhili kutoka kwa wadau na kujikuta wakibaki katika hali duni ya kiuchumi.

Mkude amesema kikundi hicho kina wanachama 37 na kinafanya shughuli za utumbuizaji kwenye halfa za kijadi asili na kuingiza kipato kwa ajili ya kugawana ili kukidhi mahitaji ya kifamilia pekee.

Kwa upande wake Msanii na Mweka hazina wa kikundi hicho, Benard Shaban amempongeza Mbunge kwa kuanzisha tamasha hilo ambalo litawasadia wasanii wa ngoma za asili kutangaza vipaji vyao na kwa makundi mengine.

‘Ugatuzi wa madaraka muhimu kufanikisha Dira 2050’ – HabariLeo

DODOMA: NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (anayeshughulikia afya), Jafar Seif, amesema ugatuzi wa madaraka ni miongoni mwa misingi muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuziimarisha Serikali za Mitaa ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akifungua mkutano wa mwaka wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa(TaOA) Dk Seif alisema kufikiwa kwa malengo ya Dira 2050 kutategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa Serikali za Mitaa kusimamia na kutekeleza mipango ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika maeneo yao.

Alisema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kiutendaji pamoja na usimamizi wa fedha za umma, ikiwemo utaratibu wa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo moja kwa moja katika taasisi za Serikali za ngazi za chini.

Taasisi zinazofikiwa na utaratibu huo ni pamoja na shule, zahanati, ofisi za kata na vijiji, hatua inayolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia alisema Serikali za Mitaa zina nafasi muhimu katika kuhakikisha malengo ya maendeleo yanafikiwa kutokana na kuwa ndizo zilizo karibu zaidi na wananchi na zinaelewa kwa undani mahitaji na changamoto zinazowakabili.

“Fursa ya kufikia Dira ya Taifa 2050 inahitaji Serikali za Mitaa zenye uongozi bora na uwajibikaji, mipango madhubuti ya maendeleo na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma,” amesema.

Aidha, Dk Seif amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji katika ngazi mbalimbali za Serikali.

Alisema kuimarishwa kwa mifumo ya kiutendaji katika Serikali za Mitaa kutasaidia kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa tija na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Kigoma yatarajia kuuza kilo milioni 15 za tumbaku – HabariLeo

KIGOMA: Zaidi ya kilo milioni 15 za tumbaku zinatarajiwa kuuzwa na wakulima kwa kampuni za ununuzi wa zao hilo mkoani Kigoma kwa msimu huu wa kilimo.

Kaimu Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Elisha Chao, amesema hayo akiwasilisha taarifa ya bodi hiyo kwa wajumbe wa kikao cha wadau wa kahawa mkoa Kigoma kilichofanyika mjini Kigoma jana.

Chao amesema hadi sasa kilo milioni 15 zimenunuliwa na bado kuna tumbaku ipo sokoni na wanunuzi wanaendelea na taratibu za ununuzi kwenye masoko hayo.

Amesema mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji kutokana na soko lililokuwepo msimu uliopita na bei iliyokuwepo na kwamba TTB inasimamia kwa karibu kuhakikisha tumbaku iliyiozalishwa inaunuliwa yote.

Akizungumza katika mkutano huo Mkoa wa Kigoma Balozi ,Simon Sirro, ametaka wadau wa zao la tumbaku nchini kusimamia taratibu za kilimo na uuzaji wa zao hilo ili kuhakikisha mkulima ananufaika na kuwa na maendeleo.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma amesema uzalishaji wa zao la tumbaku mkoani humo umeendelea kuongezeka, kutoka tani 4,452 mwaka 2021/2022 hadi tani 14,213 mwaka 2024/2025.

Amesema ongezeko hilo la uzalishaji limechochea pia kuongezeka kwa mapato ya Serikali, kutoka Sh bilioni 15.4 mwaka 2023/2024 hadi Sh bilioni 26.9 mwaka 2025/2026.

Wabuni vigae vya ukutani kwa kutumia chupa za plastiki – HabariLeo

TANGA; Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimeendelea kujipambanua kama kitovu cha tafiti na bunifu zinazotoa majibu ya moja kwa moja kwa changamoto zinazoikabili jamii, huku kikisisitiza mfumo wa vitendo kwa wanafunzi wake kabla ya kuhitimu.

Akizungumzia juhudi hizo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa, amesema chuo kimeimarisha mfumo ambapo kila muhula wanafunzi wanafanya miradi ya vitendo chini ya usimamizi wa wahadhiri na kuiteetea kama sehemu ya mitihani yao.

“Kila muhula wanafunzi wanasimamiwa na kufanya miradi chini ya usimamizi wa walimu, na wanazitetea kama sehemu ya mitihani yao,” anaeleza Profesa Liwa, akisisitiza kuwa mbinu hiyo inawafanya wahitimu kuwa na uelewa mpana katika kutatua changamoto za kiutendaji.

Katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira inayotokana na taka ngumu, Chuo Kikuu cha Ardhi kimeleta tija kupitia uvumbuzi mpya wa kutengeneza vigae vya ukutani (wall tiles) vinavyotokana na chupa za plastiki.

Mwanamapinduzi wa wazo hili ni Isabellah Edwin Sam, mwanafunzi wa mwaka wa nne chuoni hapo, ambaye alibaini kuwa chupa za plastiki za rangi zimekuwa zikitupwa kwa wingi kutokana na bei yake kuwa chini, hali inayochochea uchafuzi mkubwa wa mazingira.

Ili kupunguza kadhia hiyo, Isabellah alibuni mbinu ya kuchakata taka hizo na kuzigeuza kuwa vigae imara vinavyoweza kutumika katika ujenzi wa kuta, hususan katika maeneo ya bafu na vyoo.

Akizungumzia ubora wa uvumbuzi wake, Isabellah ameeleza kuwa bidhaa hiyo ni thabiti na inaendelea kuboreshwa zaidi.

Amesema hatua inayofuata ni kuwasilisha vigae hivyo katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya kupata uthibitisho rasmi kabla ya kuanza kutumika kwa wingi katika soko la ujenzi.

Vijana wasisitize kwa na maono ya maisha – HabariLeo

SHINYANGA: VIJANA wametakiwa kuwa na maono ya maisha na kutumia mitandao ya kijamii kutafuta fursa za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kuangalia machapisho na kutuma ujumbe usio na staha.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, wakati akifungua Jukwaa la Vijana la Halmashauri ya Msalala lililowakutanisha zaidi ya vijana 250.

Nkinda amesema kila kijana anapaswa kuwa na maono yake binafsi na kuyafanyia kazi ili kufikia malengo, akisisitiza kuwa simu za mkononi na mitandao ya kijamii zinaweza kuwa nyenzo muhimu za kupata fursa za kielimu na kiuchumi.

“Unaamini kijana mwenzangu, Tanzania ya kesho ni mimi na wewe. Hivyo tuilinde kwa amani na upendo na tutumie vizuri simu zetu za mkononi kupata fursa za kimaendeleo,” amesema Nkinda.

Amesema Serikali inataka kuona vijana wakiwa na maono yanayojenga, akitoa mfano kwa wanafunzi kuzingatia masomo yao na kuweka malengo ya taaluma wanazotaka kufikia, ikiwamo udaktari, uongozi na sekta mbalimbali za uchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Rose Manumba, amesema jukwaa hilo ni fursa kwa vijana kukutana, kubadilishana mawazo na kujenga uzalendo kwa kuwa kila mmoja ana nafasi katika ujenzi wa taifa.

Naye Ofisa Vijana kutoka Halmashauri ya Bariadi na mwezeshaji wa jukwaa hilo, Godwin Misana, amesema uadilifu ni msingi muhimu kwa kijana anayelenga kufanikiwa.

Amesema kijana anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kitaaluma au kufanya vizuri kazini, lakini bila uadilifu anaweza kupoteza fursa, hivyo amewataka vijana kutanguliza uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika maisha yao.

Kamati ya Bunge yasifu ufanisi Wizara ya Viwanda na taasisi zake – HabariLeo

DODOMA; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ikiongozwa na Mwenyekiti wak, Deodatus Mwanyika, imeipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake ya udhibiti ubora kwa ufanisi.

Mwanyika amesema kuwa juhudi zinazofanywa na TBS kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania zinaonekana, sambamba na kuendelea kutoa elimu na kuongeza programu maalumu za kushughulikia bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi.

Aidha, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imepongezwa kwa maboresho na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kusisitizwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kuhusu mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS), ili wakulima na wadau wengi zaidi wanufaike.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema wizara hiyo imepokea pongezi hizo pamoja na maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara nchini.

Bunifu MUHAS suluhisho za changamoto za afya – HabariLeo

TANGA: Ubunifu wa wanafunzi na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umeendelea kuibua matumaini kwa wananchi katika kutafuta suluhisho za changamoto mbalimbali za afya zinazowakabili katika maisha ya kila siku.

Kupitia banda la MUHAS katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika katika Shule ya Sekondari Usagara, wananchi na wanafunzi wanapata nafasi ya kujionea bunifu zinazolenga kuboresha huduma za afya na kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma muhimu.

Miongoni mwa bunifu zinazooneshwa ni MoyoGuard, BiliMeasure, Siku Smart, Biosafe, Robospine, QR Dharura na Bridging Silence, ambazo zimeibua hamasa miongoni mwa wageni kutokana na kulenga changamoto zinazogusa maisha ya wananchi.

Maonesho hayo pia yamekuwa darasa kwa wanafunzi wanaotembelea banda hilo, ambapo wanapata fursa ya kuona kwa vitendo namna maarifa wanayopata shuleni na vyuoni yanavyoweza kubadilishwa kuwa bidhaa au teknolojia yenye manufaa kwa jamii.

Kwa wananchi, ubunifu huo unaonesha umuhimu wa kuwekeza katika vijana na kuwapa mazingira bora ya kutumia vipaji, elimu na teknolojia kutengeneza majibu ya changamoto zinazowazunguka.

Wiki hiyo inaendelea hadi Agosti 24, 2026, ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii, hususan vijana, kutambua nafasi ya elimu, ujuzi na ubunifu katika kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea na kutatua changamoto zake.

Kamati yapongeza polisi kuimarisha usalama – HabariLeo

DODOMA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Jijini Dodoma leo.

Ayoub amesema wizara inaendelea kuimarisha amani na usalama wa raia pamoja na mali zao.

Amebainisha kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kufanya doria, misako na operesheni katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ulinzi shirikishi.

Aidha, amesema wizara kupitia Jeshi la Polisi imendelea kuimarisha usalama barabarani kupitia ukaguzi wa vyombo vya moto, mafunzo kwa madereva na matumizi ya teknolojia ikiwemo Global Positioning System (GPS) na kamera za usalama barabarani katika maeneo muhimu ili kufuatilia mienendo ya Madereva na Wanaokiuka Sheria za barabarani.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa mtandaoni kupitia matumizi ya vifaa vya kisasa, mafunzo kwa watendaji na matumizi ya teknolojia ili kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Najma Murtaza Giga akizungumza kwa niaba ya Kamati amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa linayofanya katika kulinda amani na usalama wa wananchi.

Amesema wananchi bado wana imani na Jeshi hilo na wanatambua kazi kubwa inayofanywa na Jeshi hilo katika kuhakikisha wanachi wanaendelea kuishi kwa amani huku akieleza kuwa changamoto zinazojitokeza haziwezi kutatuliwa na Jeshi la Polisi pekee bali kwa ushirikiano na wadau mbalimbali

Kadhalika, amesema Kamati iko tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi pale watakapohitaji jambo lolote linalohitaji msukumo wa Kamati hiyo.

Aidha, amemshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Naibu Waziri pamoja na Viongozi wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya.

TBS yapongezwa udhibiti usalama, ubora wa bidhaa – HabariLeo

DODOMA; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda,Biashara,Kilimo na Mifugo imeipongeza TBS kwa kutekeleza majukumu yake ya udhibiti ubora kwa ufanisi.

Pongezi hizo zimetolewa na  Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deogratias Mwanyika wakati wa kikao cha Kamati cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu,katika, ofisi za Bunge jijini Dodoma mapema  leo.

Mwanyika amesema juhudi zinazofanywa na TBS kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania zinaonekana  na kutoa rai kwa TBS kuendelea kutoa elimu na kuongeza jitihada sambambana na kuwa na programu maalumu za kushughulikia bidhaa zinazoingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameishukuru kamati hiyo na kuahidi kufanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati,  ili kuendelea kurahisisha utendaji kazi wa TBS.

Amesema lengo la wizara kupitia TBS ni kuhakikisha kunakuwa na bidhaa zenye ubora na usalama katika soko zinazozalishwa  ndani na zinazotoka nje ya nchi.