Mafuta, gesi, utalii kivutio cha Saudi Arabia Zanzibar

Unguja. Zanzibar imefungua milango kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Saudi Arabia, huku sekta za mafuta, gesi, utalii, nishati na uchumi wa buluu zikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa za uwekezaji.

Hatua hiyo imekuja baada ya Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Zena Saidi kuongoza ujumbe wa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi hiyo katika ziara yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kutafuta fursa mpya za uwekezaji Zanzibar.

Akizungumza katika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Zanzibar na Saudi Arabia lililofanyika visiwani hapa leo Alhamisi, Agosti 20, 2026, Balozi Zena amesema ziara hiyo ni mwendelezo wa mikutano iliyoanzia Dar es Salaam Agosti 17 na kwamba, ujumbe huo ulitembelea viwanda vya kuzalisha umeme na vya kusindika nyama kwa ajili ya soko la nje.

Amesema kwa muda mrefu uwekezaji kutoka Saudi Arabia kwenda Zanzibar umekuwa hafifu, hivyo jukwaa hilo limeandaliwa kuchochea uwekezaji zaidi.

“Tunataka sasa uwekezaji kutoka Saudi Arabia ufanyike. Wenyewe wana hamasa kubwa, hasa katika masuala ya usalama wa chakula na nishati,” amesema.

Balozi Zena alisema wawekezaji hao wanatafuta maeneo nje ya Saudi Arabia kwa ajili ya kilimo na ujenzi wa matanki makubwa ya kuhifadhia mafuta kwa matumizi ya kawaida na nyakati za dharura.

Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema Zanzibar imejiandaa kupokea uwekezaji huo, hasa katika uchumi wa buluu na utalii.

Amesema utafiti wa mafuta na gesi unaendelea vizuri na unaonesha matumaini, huku akitaja pia nishati ya jua na upepo kuwa maeneo yenye fursa.

Aidha, amesema Zanzibar imeanza kutekeleza Sera ya Halal Tourism, inayolenga kuvutia watalii kutoka Saudi Arabia, hasa familia.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Saleh Saad Mohamed amesema baadhi ya wawekezaji tayari wameonesha nia ya kubaki Zanzibar kwa ajili ya kutembelea maeneo ya uwekezaji.

Ametaja makazi, teknolojia, usafirishaji na bandari kuwa miongoni mwa sekta zinazovutia wawekezaji hao, huku Mangapwani ikitajwa kuwa eneo la kuvutia kwa maghala ya kuhifadhia mafuta.

Kwanini maboresho ya mifumo NMB ni muhimu kwako

Dar es Salaam. Ongezeko la wateja kutoka milioni 1.8 mwaka 2011 hadi zaidi ya milioni 10 kwa sasa limetajwa kuwa moja ya sababu iliyoifanya Benki ya NMB kufanya maboresho ya mfumo mkuu wa benki ili kuendana na mahitaji hayo.

Maboresho hayo ni zaidi ya kubadilisha mfumo wa kiteknolojia unaolenga kuongeza kasi, usalama, uthabiti na uwezo wa benki kutoa huduma mpya kwa wateja.

Akizungumza katika mahojiano maalumu leo Alhamisi, Agosti 20, 2026, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema mfumo huo umejengwa kuendana na ukuaji wa benki na kuifanya teknolojia isiwe kikwazo katika utoaji wa huduma.

“Kilichofanyika si uboreshaji wa mfumo pekee bali ni uwekezaji katika usalama, uthabiti, kasi, ubunifu na uwezo wa NMB kukua pamoja na Watanzania. Mfumo mpya umejengwa kuhimili ukuaji wa benki, kuongeza ufanisi wa miamala na kuwezesha kizazi kipya cha huduma za kidijitali na kifedha,” amesema.

Kwa sasa NMB ina zaidi ya matawi 250, mawakala zaidi ya 80,000, ATM zaidi ya 750 na zaidi ya QR Codes 130,000 zinazotumika kupokea malipo; ukuaji uliofanya mfumo uliokuwa ukitumika tangu mwaka 2011 kutotosheleza mahitaji ya benki hiyo kwa sasa na miaka ijayo.

“NMB sasa imehamia kwenye mfumo mpya wa Core Banking unaolenga kuongeza uwezo wa kushughulikia miamala, kuimarisha uthabiti wa huduma na kuwezesha benki hiyo kuanzisha bidhaa mpya za kifedha,” amesema.

Kwa mteja, umuhimu wa maboresho hayo unatarajiwa kuonekana katika huduma zenye kasi na uthabiti zaidi, pamoja na kuimarika kwa huduma za kidijitali kupitia NMB Mkononi, USSD, ATM na mawakala.

Zaipuna amesema mfumo huo pia utawezesha benki kuanzisha bidhaa na huduma mpya kwa haraka zaidi, huku ukiboresha usalama na ufanisi wa miamala.

“Kwa mteja, maboresho haya yanamaanisha huduma za kasi zaidi, salama zaidi, zinazotegemeka zaidi na zinazoweza kuendana kwa karibu zaidi na mahitaji yake,” amesema.

Kwa wafanyabiashara, kampuni na taasisi, mfumo huo umeongeza uwezo wa kushughulikia miamala mingi kwa wakati mmoja, malipo na ukusanyaji wa fedha pamoja na huduma za mishahara.

“Kwa kampuni kubwa mfumo huu una uwezo wa kuratibu ulipaji wa mishahara kwa zaidi ya wafanyakazi 20,000 wa kampuni moja,” amesema.

Zaipuna amesema hadi maboresho hayo yanafanyika kulikuwa na maandalizi ya zaidi ya miaka miwili tangu mwaka 2023 na ulihusisha majaribio ya mara kwa mara, uhakiki wa mifumo, tathmini za vihatarishi na ushirikishwaji wa wataalamu wa ndani na nje ya benki.

Hatua ya mwisho ya uhamishaji wa mfumo ilianza Julai 31, 2026,  baadhi ya huduma zilisitishwa kwa muda ili kuruhusu uhamishaji wa taarifa kufanyika kwa usalama.

“Hatukuchagua njia rahisi, tulichagua njia salama na yenye uwajibikaji zaidi kwa wateja wetu,” amesema Zaipuna.

Amesema mfumo huo mpya unaweka msingi wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa NMB wa 2026-2030, unaolenga kuifanya benki hiyo kuwa ya kisasa, salama na inayoendeshwa zaidi na teknolojia.

“Hatua hii inaweka msingi muhimu wa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa NMB 2026-2030, unaolenga kuendeleza NMB kuwa benki ya kisasa, salama, inayozingatia mteja, inayoendeshwa na teknolojia na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” amesema.

MAKAMU WA RAIS DKT NCHIMBI AKUTANA NA BALOZI MTEULE WA TANZANIA NCHIN MALAYSIA MEJA JENERALI MBARAKA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, Mazungumzo yaliyofanyika mkoani Dodoma, leo tarehe 20 Agosti 2026.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amempongeza Balozi Mkeremy kwa imani aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuliwakilisha Taifa katika nchi ya Malaysia. Amesema nchi hiyo yenye uchumi mkubwa, ina ushirikiano wa kimkakati na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya kibiashara na majukwaa ya kimataifa.

 

Makamu wa Rais amemsihi Balozi Mkeremy kufanya kazi kwa jitihada na ubunifu kuhakikisha anaimarisha zaidi urafiki wa Tanzania na Malaysia kwa kuongeza fursa na kukaribisha wawekezaji wengi zaidi nchini. Pia, amemsisitiza kuhamasisha watanzania waishio Malaysia (Diaspora) kuwekeza nchini Tanzania.

 

Amemsihi Balozi Mkeremy kufahamu vema Dira ya Taifa 2050 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025 – 2030 ili kutambua mambo ya uhusiano wa kimataifa yaliyopewa kipaumbele na yanayohitaji msisitizo wa kipekee kuyatekeleza.

 

Kwa upande wake Balozi mteule wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwakilisha Taifa nchini Malaysia. Aidha, amemshukuru Mhe. Makamu wa Rais kwa nasaha zake na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

 

Huku ndiko vita ya binadamu na mbu ilikohamia

Vita kati ya binadamu na mbu imeingia hatua mpya, huku mbinu za zamani za kuwadhibiti zikikabiliwa na usugu wa viuatilifu na wanasayansi wakitafuta silaha mpya za kuzuia wadudu hao kueneza malaria, dengue na chikungunya.

Agosti 20 kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mbu, ikiwa ni kumbukumbu ya ugunduzi wa Sir Ronald Ross mwaka 1897 kuhusu uhusiano kati ya mbu na maambukizi ya malaria.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2024 kulikuwa na wagonjwa wa malaria milioni 282 na vifo 610,000 duniani kote.

Afrika ilibeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa huo, ikichangia asilimia 94 ya wagonjwa na asilimia 95 ya vifo, huku takribani watoto 438,000 wakifariki kutokana na malaria.

Katika vita hiyo, binadamu wamekuwa wakitumia silaha mbalimbali, ikiwemo vyandarua vilivyotiwa dawa, unyunyiziaji wa dawa ndani ya nyumba na udhibiti wa mazalia ya mbu.

WHO inapendekeza matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa na unyunyiziaji wa dawa kwenye kuta za ndani za nyumba. Vyandarua humzuia mbu kumfikia mtu na vinaweza kumuua au kumdhoofisha anapogusana na dawa.

Tangu mwaka 2000, zaidi ya vyandarua bilioni tatu vimesambazwa katika nchi zilizoathirika na malaria.

Lakini vita hiyo haijawa rahisi. Mbu wameanza kujenga usugu dhidi ya baadhi ya viuatilifu, hasa pyrethroids, hali inayowalazimu wanasayansi kutafuta silaha mpya za kukabiliana nao.

Kwa mujibu wa WHO, usugu dhidi ya viuatilifu umeonekana katika nchi 48, hali inayoweza kupunguza ufanisi wa baadhi ya mbinu zinazotumika kuwadhibiti.

Moja ya majibu ya kisayansi ni matumizi ya vyandarua vyenye mchanganyiko wa dawa mbili, pyrethroid na chlorfenapyr, ambavyo tayari vimetumika katika nchi 17 za Afrika.

Utafiti mwingine unahusu mbu waliobadilishwa vinasaba, wakiwemo mbu dume wenye sifa zinazoweza kupunguza uwezo wao wa kuzaliana.

WHO inaunga mkono utafiti huo, lakini inasisitiza tathimini ya usalama wa afya, mazingira na ikolojia kabla ya teknolojia hizo kutumika kwa kiwango kikubwa.

Kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu aina ya Aedes, wanasayansi wanachunguza pia matumizi ya bakteria aina ya Wolbachia, anayeingizwa kwenye mbu ili kupunguza uwezo wao wa kusambaza virusi.

Nchini Tanzania, vita hiyo inaendelea kwa kutumia mchanganyiko wa mbinu zinazolenga kuzuia mbu kuzaliana na kuwafikia binadamu.

Mtafiti Kiongozi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Kituo cha Amani kilichopo Muheza, Tanga, Dk William Kisinza, amesema hatua muhimu ni kuhakikisha maambukizi ya malaria yanazuiwa kwa kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa huo.

Amesema njia za kuzuia mbu zimeainishwa na wataalamu wa afya na miongozo ya WHO, ikiwemo matumizi sahihi ya vyandarua vilivyowekwa dawa, hasa nyakati za usiku.

Amesema njia nyingine ni kupulizia dawa zenye mabaki ya muda mrefu kwenye kuta za ndani za nyumba, maarufu kama Indoor Residual Spraying (IRS).

“Njia nyingine ambayo hata Serikali ya Tanzania na nchi zingine zinaitumia ni viuadudu. Kuna tafiti zimeonyesha viuadudu ni mbinu sahihi zaidi, ambapo hapa nchini tuna kiwanda Kibaha,” amesema.

Ameongeza kuwa viuadudu vinaweza kutumika kwenye mazalia ya mbu na kuwaua kabla hawajafikia hatua ya kuwa mbu waliokomaa.

“Viuadudu vinaua kabla mbu hawajawa pevu. Hiyo maana yake wanaua lava, hayo ndiyo matumizi sahihi,” amesema.

Vita dhidi ya malaria havilengi mbu pekee. Binadamu pia wameanza kutumia chanjo kama silaha ya kupunguza madhara ya ugonjwa huo.

WHO imeidhinisha chanjo mbili za malaria, RTS,S na R21/Matrix-M, kwa matumizi kwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye malaria.

Hata hivyo, WHO inasisitiza kuwa hakuna njia moja inayoweza kumaliza malaria.

Vyandarua, unyunyiziaji wa dawa, udhibiti wa mazalia, chanjo na mbinu nyingine zinapaswa kutumika kwa pamoja kulingana na mazingira na kiwango cha maambukizi.

Njia nyingine inayotumika ni IRS, ambapo dawa yenye mabaki ya muda mrefu hunyunyiziwa kwenye kuta za ndani za nyumba ili kuua au kuzuia mbu.

WHO pia imeanza kupendekeza matumizi ya spatial emanators, vifaa vinavyotoa kemikali hewani kwa lengo la kuzuia, kuvuruga au kuua mbu.

Udhibiti wa mazalia nao huhusisha kuondoa au kutibu maeneo yenye maji yanayoweza kuwa mazalia ya mbu.

Mbinu hizo zimeanza kuonyesha matokeo nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa tamko la Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, lililotolewa Aprili 25, 2026, vifo vya malaria vilipungua kwa asilimia 50, kutoka 2,460 mwaka 2020 hadi 1,231 mwaka 2025.

Maambukizi katika jamii nayo yalishuka kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025.

Wagonjwa waliothibitika kuwa na malaria katika vituo vya afya wamepungua kwa zaidi ya nusu, kutoka milioni sita mwaka 2020 hadi milioni 2.8 mwaka 2025.

Serikali ilitenga Sh20 bilioni katika mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kwa ajili ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu.

Fedha hizo zimewezesha kununuliwa kwa lita 1.25 milioni za viuadudu vilivyosambazwa katika halmashauri zote 184.

Mapambano hayo yamepewa msukumo zaidi kupitia Mpango Mkakati wa Taifa wa Malaria wa 2026–2030, unaoweka mkazo katika kuzuia maambukizi, kudhibiti mbu na kuhakikisha wagonjwa wanapimwa na kutibiwa kwa wakati.

Dk Magembe amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

NeST YAFUNGUA FURSA ZA ZABUNI ZA SH40.4 TRILIONI KWA WAZAWA

MFUMO wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), umewezesha kutolewa kwa zabuni 397,395 zenye thamani ya Sh40.4 trilioni, huku ukiongeza uwazi, ufanisi na ushiriki wa Watanzania katika fursa za ununuzi wa umma.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo, Dodoma.

Simba amesema tangu kuanza kutumika kwa NeST, kiwango cha uzingatiaji wa sheria katika michakato ya ununuzi wa umma kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2023/24 hadi asilimia 76 mwaka 2024/25 na kufikia asilimia 79 mwaka 2025/26.

Amesema matumizi ya mfumo huo yamewezesha pia kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, sawa na kuokoa takribani Sh27.64 bilioni.

Kwa mujibu wa Simba amesema, NeST imewaondolea wazabuni ulazima wa kusafiri kwenda kuwasilisha nyaraka za zabuni katika taasisi nunuzi, hivyo kupunguza gharama na muda wa kushiriki katika michakato ya ununuzi wa umma.

Amesema kwa sasa mzabuni anaweza kuomba zabuni akiwa mahali popote alipo, jambo ambalo limepanua wigo wa ushiriki kuanzia ngazi za juu hadi Serikali za Mitaa.

“Kwa sasa hata mafundi wa kawaida wanaweza kuomba na kupata kazi ya kushiriki ujenzi katika miradi ya Serikali,” amesema Simba.

Ameongeza kuwa mfumo huo umewezesha utoaji wa zabuni kwa uwazi na usawa katika ngazi za msingi, ikiwamo shule, vituo vya afya na ofisi za kata.

Aidha, amesema utafiti uliofanyika umeonesha kuongezeka kwa ufanisi na uwazi, sambamba na kupungua kwa uzalishaji wa hewa ya ukaa (CO₂e) kwa tani 64,768 katika kipindi cha mwaka 2023/24 hadi 2024/25.

Simba amesema utafiti mwingine unaendelea kuhusu usajili wa NeST katika biashara ya kaboni, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuchangia zaidi ya Sh20 bilioni kwa mwaka kupitia mauzo ya kaboni.

Mfumo huo umewezesha pia utekelezaji wa upendeleo wa zabuni na bidhaa za ndani kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Simba amesema zabuni zote zenye thamani isiyozidi Sh50 bilioni zimetengwa kwa wazawa pekee, huku wazabuni wa ndani wakipewa upendeleo wa hadi asilimia 10 katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa.

Vilevile, amesema bidhaa za ndani zimepewa upendeleo wa hadi asilimia 15 dhidi ya bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amesema mfumo huo umewezesha utekelezaji wa upendeleo huo kwa njia ya kielektroniki, ambapo wazabuni wa nje hawawezi kuomba zabuni zenye thamani ya chini ya Sh50 bilioni zilizotengwa kwa wazawa.

Katika hatua nyingine, Simba amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma imezielekeza taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, yakiwamo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Amesema hadi sasa makundi maalum 27,946 yamesajiliwa katika NeST, ambapo vijana ni 13,317, wanawake 13,400, wazee 643 na watu wenye ulemavu 586.

Amesema makundi hayo tayari yamepata zabuni zenye jumla ya thamani ya Sh56 bilioni kupitia mfumo huo.

Kwa mujibu wa Simba, PPRA inalenga kufikisha idadi ya makundi maalum yaliyo tayari kuomba zabuni takribani 300,000, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema mpango huo unalenga kuwapa fursa za ajira na kazi Watanzania ambao hawana uwezo wa kuwa na kampuni, lakini wanaweza kujiunga katika vikundi vya watu watatu au zaidi na kushiriki zabuni za Serikali.

“Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na uchumi jumuishi; kwamba kila Mtanzania ananufaika na anachangia pia kwenye ukuaji wa uchumi,” amesema.

Amesema kundi maalum linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh500 milioni.

Simba amesema suala hilo limepewa nafasi katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, hatua ambayo imeongeza uhamasishaji na usajili wa vikundi.

Aidha, amesema PPRA itashirikiana na Ofisi ya Rais  Wizara ya Maendeleo ya Vijana katika kuhamasisha usajili wa vikundi katika Halmashauri zote 184 nchini.

Amewataka Watanzania kujiunga katika vikundi vya watu watatu au zaidi, kuvisajili katika Halmashauri zao na baadaye kusajili vikundi hivyo katika Mfumo wa NeST ili kunufaika na fursa za zabuni za umma.

MAJI CF YATUPA ULAJI MWINGI – WAJASIRIAMALI IRINGA

Mjasiriamali eneo la Posta Iringa akipanga maji ya CF eneo lake la biashara

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA, IRINGA

BAADHI ya wafanyabiashara wadogo mjini Iringa wamesema wamehamasika kuuza maji ya CF yanayozalishwa wilayani Mufindi, mkoani Iringa, kutokana na kupata faida nzuri pamoja na mwitikio mkubwa wa wateja wanaonunua maji hayo.

Wakizungumza na Matukio Daima Media, wafanyabiashara hao, Salima Abdalah Alli, Wema Kalinga na Keni Sanga, wamesema maji ya CF yameendelea kupata soko katika maeneo mbalimbali ya mjini Iringa, hali inayowafanya kuongeza kiwango cha bidhaa hiyo katika biashara zao.

Wafanyabiashara hao wameipongeza kampuni inayozalisha maji ya CF kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa wauzaji pamoja na kuhakikisha bidhaa hiyo inawafikia kwa wakati.

Wamesema moja ya sababu zinazowavutia kuendelea kuuza maji hayo ni bei yake ya jumla, ambayo inawawezesha kupata faida nzuri wanapouza kwa wateja wao.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, katoni ya maji ya CF hununuliwa kwa bei ya jumla ya Shilingi 3,800, huku katoni ya chupa kubwa ikiuzwa kwa Shilingi 4,000, bei ambayo wamesema inawapa nafasi nzuri ya kupata faida katika biashara zao.

Wamesema katika biashara ya maji, bei ya jumla ina mchango mkubwa katika kuamua kiwango cha faida anachopata mfanyabiashara, hivyo bei ya maji ya CF imekuwa moja ya sababu zinazowafanya wafanyabiashara wengi kuyapokea vizuri.

Mbali na suala la bei, wafanyabiashara hao wamepongeza mfumo wa usambazaji wa maji hayo, wakisema magari ya kampuni yamekuwa yakifika mara kwa mara katika maeneo yao kuhakikisha hawakosi bidhaa.

Wamesema katika baadhi ya maeneo magari ya usambazaji yamekuwa yakifika zaidi ya mara tatu kwa siku kulingana na mahitaji, jambo ambalo limewasaidia kukidhi ongezeko la wateja wanaotafuta maji hayo.

Kwa upande wao, baadhi ya watumiaji wa maji ya CF wamesema wamevutiwa na bidhaa hiyo kutokana na ubora wake pamoja na namna ilivyopokelewa katika soko.

Perida Sanga, mmoja wa watumiaji wa maji hayo, amesema kwa sasa maji ya CF yameanza kutumika katika matukio mbalimbali ya kijamii, yakiwemo harusi, misiba, mikutano na sherehe nyingine.

Amesema katika baadhi ya harusi na shughuli mbalimbali, waandaaji wamekuwa wakiyapa maji hayo kipaumbele kutokana na mahitaji na mapendeleo ya wageni.

“Kwa sasa ukienda kwenye matukio mbalimbali kama harusi na misiba unakutana na maji ya CF. Watu wengi wameanza kuyapenda na kuyatumia, jambo ambalo linaonesha jinsi yalivyopokelewa vizuri sokoni,” amesema Perida.

Wafanyabiashara hao wamesema kuongezeka kwa idadi ya watumiaji ni fursa kwa wafanyabiashara wadogo, kwa sababu bidhaa inapokuwa na wateja wengi huwa rahisi kuuzwa na kuwapatia kipato.

Aidha, wameiomba kampuni kuendelea kudumisha ubora wa maji, bei rafiki kwa wafanyabiashara pamoja na mfumo mzuri wa usambazaji ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali.

Walisema bei ya chupa ndogo ya maji ni rafiki zaidi kwa ni Tsh 500 wakati chupa kubwa ni Tsh 10000 bei ambayo ni nzuri .

Maji CF ni maji yenye madini asili yanayotoka katika vyanzo salama vya asili vilivyopo wilayani Mufindi, mkoani Iringa, na kwa sasa yanasambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mawasiliano kuhusu maji ya CF, wateja na wafanyabiashara wanaweza kupiga simu +255 762 123 736 au kuwasiliana kupitia barua pepe iliyotolewa na kampuni: cfcompany100@gma.

TAZAMA VIDEO BOFYA LINK HII

PROF. KABUDI AWATAKA WANANCHI KUZINGATIA TAHADHARI ZA MAAFA

Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka wananchi kuzingatia tahadhari na maelekezo yanayotolewa na wataalamu na mamlaka husika ili kupunguza madhara yanayotokana na majanga na maafa.

Prof. Kabudi ametoa wito huo tarehe 19 Agosti, 2026 wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Misaada ya Kibinadamu Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga, huku akiwataka kuendelea kufuata taarifa na maelekezo rasmi kutoka kwa wataalamu na mamlaka zinazohusika na masuala ya maafa.”

Katika hatua nyingine, alisema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema na kujenga ustahimilivu wa jamii ili kuongeza uwezo wa wananchi kukabiliana na majanga na kupunguza madhara yanayotokana na matukio hayo.

Alisema uwezo wa nchi katika kukabiliana na majanga kwa ufanisi unategemea uwepo wa mifumo madhubuti, uratibu na ushirikiano wa karibu na wenye tija kati ya Serikali na wadau wa huduma za kibinadamu.

Prof. Kabudi pia alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kusimamia masuala ya kibinadamu na ustawi wa wananchi.

“Kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia, Serikali imeendelea kuhakikisha wananchi wanaokumbwa na changamoto za majanga wanapata msaada na faraja wakati wa dharura.”

Prof. Kabudi aliwataka watoa huduma za kibinadamu kuwekeza zaidi katika kuwawezesha wananchi kwa elimu na taarifa sahihi kuhusu vihatarishi vinavyowazunguka, pamoja na hatua za kuchukua kabla, wakati na baada ya janga.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko, amesema maadhimisho ya siku hiyo yanatoa fursa ya kutambua na kuthamini mchango wa watoa huduma za kibinadamu ambao hujitolea kwa moyo wa huruma, ujasiri na mshikamano katika kuokoa maisha na kupunguza madhara.

Alisema ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa Serikali, wadau wa huduma za kibinadamu na jamii katika kuhakikisha kuwa msaada unapatikana kwa wakati na unawafikia wale wanaouhitaji.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa katika kila hatua ya utoaji wa huduma za kibinadamu, maisha, usalama na utu wa mwanadamu vinaendelea kuwa kiini cha hatua tunazochukua.”

=MWISHO=

Dar yaongoza matumizi vipimo vya kujipima VVU

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa matumizi na idadi ya vifaa vya kujipima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) vilivyosambazwa nchini mwaka 2025 huku zaidi ya vifaa 330,000 vikifikishwa kwa wananchi.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) ya mwaka 2025. Mpango huo upo chini ya Wizara ya Afya.

Takwimu hizo zinaonesha kati ya vifaa 2,494,398 vya kujipima VVU vilivyosambazwa nchini mwaka huo, Dar es Salaam ilipokea vifaa 330,351, sawa na takribani asilimia 13 ya vifaa vyote vilivyosambazwa.

Dar es Salaam ilifuatiwa na Mbeya iliyosambaziwa vifaa 221,963, Tabora 200,784, Pwani 188,351 na Tanga 179,533.

Huduma ya kujipima VVU, maarufu kama HIV self-testing, imekuwa ikilenga kuongeza wigo wa upimaji kwa kuwapa wananchi fursa ya kujua hali zao kwa faragha na urahisi zaidi, hususan wanaume na vijana ambao wanaweza kukumbana na vikwazo vya kufika katika vituo vya afya.

Kwa mujibu wa NASHCoP, tafiti pia zimeonesha matumizi ya vifaa hivi kuwa makubwa zaidi maeneo ya mijini kuliko vijijini.

Kwa ujumla, kati ya vifaa 2,494,398 vilivyosambazwa nchini, 2,118,462 vilirejeshwa pamoja na majibu ya vipimo, sawa na karibu asilimia 85.

Hata hivyo, Dar es Salaam, licha ya kuongoza kwa idadi ya vifaa vilivyosambazwa, haikuwa miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu zaidi cha kurejesha majibu.

Katika vifaa 330,351 vilivyosambazwa jijini, 269,389 vilirejeshwa pamoja na majibu, sawa na takribani asilimia 82.

Takwimu hizo pia zinaonesha vifaa 1,292 vilirejeshwa vikiwa na majibu ya reactive, yanayoashiria uwezekano wa maambukizi ya VVU.

Majibu ya reactive kwenye kipimo cha VVU maana yake ni kwamba kipimo kimeonesha ishara inayoweza kuashiria uwepo wa maambukizi ya Ukimwi.

Kati ya watu hao, 452 pekee walithibitishwa kuwa na maambukizi na mtoa huduma za afya, sawa na asilimia 35 ya majibu ya reactive yaliyorekodiwa Dar es Salaam.

Hali hiyo inaibua maswali kuhusu hatua zinazochukuliwa baada ya mtu kupata majibu ya reactive kupitia kipimo cha kujipima, kwa kuwa kipimo hicho hakitoshi pekee kuthibitisha mtu kuwa na VVU.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu za mwaka 2025, kitaifa kulikuwa na majibu 10,867 ya reactive kutoka kwenye vifaa vilivyorejeshwa, lakini watu 5,130 pekee walithibitishwa kuwa na maambukizi na watoa huduma za afya, sawa na asilimia 47.

Tofauti kubwa pia imeonekana kati ya mikoa. Kilimanjaro ilikuwa na kiwango cha uthibitisho cha asilimia 100, Mwanza asilimia 86, Shinyanga asilimia 80 na Arusha asilimia 77. Kwa upande mwingine, Mtwara ilikuwa na asilimia nane, Morogoro asilimia 16, Mbeya 19 na Lindi asilimia mbili.

Wakati huohuo, baadhi ya mikoa ilirekodi idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na HIV iliyozidi idadi ya majibu ya reactive yaliyotokana na vifaa vya kujipima. Iringa, kwa mfano, ilikuwa na majibu 42 ya reactive lakini watu 49 walithibitishwa kuwa na HIV, huku Manyara ikiwa na majibu 63 ya reactive dhidi ya watu 91 waliothibitishwa.

Uchambuzi unaonesha tofauti hizo zinaweza kusababishwa na makosa ya uingizaji wa taarifa, kutokulingana kwa vipindi vya usambazaji wa vifaa na utoaji wa majibu, pamoja na vipimo vya uthibitisho vinavyofanyika katika vituo tofauti kutounganishwa na kituo kilichosambaza kifaa cha kujipima.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa vitambulisho vya kipekee vinavyoweza kumfuatilia mtu kutoka hatua ya kujipima, kwenda kwenye kipimo cha uthibitisho na hatimaye kuunganishwa na huduma za matibabu.

Watafiti wamekuwa wakionesha HIV self-testing inaweza kusaidia kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyowafanya wanaume kutofika kupima, ikiwamo suala la faragha, unyanyapaa na urahisi wa kupata huduma.

Hata hivyo, takwimu za mwaka 2025 zinaonesha pamoja na kuongezeka kwa usambazaji wa vifaa, bado kuna haja ya kuimarisha mfumo wa kufuatilia mtu anayepata majibu ya reactive hadi anapofanya kipimo cha uthibitisho na kupata huduma stahiki.

NI MAAJABU BEI ZA NAFAKA ZASHUKA WATEJA WAPUNGUA SOKO LA SEMTEMA SABABU YATAJWA

Na Angel Magesa (UoI), Matukio Daima Media, Iringa

HAKIKA Maajabu ni mengi na kila uchwao na maajabu yake kama hivyo ndivyo Matukio Daima Media imefunga safari na kukutana na wafanyabiashara  wa nafaka Soko la Semtema, Manispaa ya Iringa, ambao wamedai kuwa biashara ya nafaka imeendelea kudorora licha ya bei za baadhi ya bidhaa, hususan mchele, kushuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miezi iliyopita.

Wafanyabiashara hao wanaojihusisha na uuzaji wa nafaka mbalimbali zikiwemo mchele, mahindi, maharage na njegere, walisema kupungua kwa wateja kumesababisha mzunguko wa fedha kuwa mdogo na kuathiri biashara zao.

Walisema hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo wananchi wengi kuwa wamevuna mazao na hivyo kuwa na akiba ya chakula majumbani, jambo linalopunguza mahitaji ya kununua nafaka sokoni.

Sababu nyingine iliyotajwa ni wanafunzi wa vyuo, hususan Chuo Kikuu cha Tumaini, kuwa likizo, hali ambayo imepunguza idadi ya wateja waliokuwa wakitegemewa na wafanyabiashara wa Soko la Semtema.

Mfanyabiashara wa nafaka kwa jumla na rejareja katika soko hilo, Fredrick Dege, amesema bei za nafaka zimepungua kwa kiasi kikubwa, huku mchele ukitajwa kuwa miongoni mwa bidhaa zilizoshuka zaidi.

Alisema awali baadhi ya aina za mchele zilikuwa zikiuzwa hadi Shilingi 3,500 kwa kilo, lakini kwa sasa bei imeshuka hadi kufikia takribani Shilingi 2,000 kwa kilo.

“Kwa sasa bei ya nafaka imeshuka, hasa katika bei ya mchele. 

Japo mauzo yako chini kwa sababu wengi wamevuna na wana vyakula vya kutosha,” alisema Dege.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa nafaka katika Soko hilo, Neema Mushi, alisema licha ya bei kushuka, bado wafanyabiashara wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa wateja wa kutosha.

Alisema sehemu kubwa ya wateja wao ni wanafunzi wa vyuo ambao hununua nafaka kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku, hivyo kufungwa kwa vyuo kwa ajili ya likizo kumeathiri moja kwa moja biashara.

“Mzunguko wa biashara umekuwa mdogo. Wanafunzi hawapo, wapo likizo, lakini bei za bidhaa zipo chini,” amesema Neema.

Hata hivyo, kushuka kwa bei hizo kumeelezwa kuwa ni nafuu kwa upande wa watumiaji, ambao sasa wanaweza kununua baadhi ya nafaka kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kipindi kilichopita.

Mkazi wa Iringa na mteja wa nafaka katika Soko la Semtema, Melickzedeck Mboya, amesema kupungua kwa bei kumesaidia kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.

“Kwa sasa maisha yanaenda kwa utofauti. 

Awali bei za mchele zilikuwa juu sana na hali ya uchumi haikuwa vizuri, lakini kwa sasa bei imepungua,” amesema Mboya.

Wafanyabiashara hao walisema wana matumaini kuwa biashara itaimarika baada ya wanafunzi kurejea vyuoni, kutokana na kuwa kundi hilo ni miongoni mwa wateja wakubwa wa nafaka katika soko hilo.

KIJANA (19) AHUKUMIWA MWAKA 01 JELA KISA KUWATUSI VIONGOZI KUPITIA TIKTOK

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,MBEYA

Mahakama ya Mwanzo Mbeya mjini imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Ramadhan Rudabuka (19) DJ na mkazi wa Patamela Wilayani Chunya baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusambaza maudhui yasiyofaa katika mtandao wa TIKTOK.

Hukumu hiyo imetolewa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mbeya mjini Ayubu Shirima.

Ilielezwa kuwa mshitakiwa alijirekodi na kusambaza maudhui yasiyofaa kwa kutoa lugha ya matusi dhidi ya viongozi wa Serikali kwa lengo la kupata wafuasi wengi katika akaunti yake ya TIKTOK licha ya kukataa kutenda kosa lakini ushahidi uliithibitishia Mahakama mshtakiwa kutenda kosa hilo.

Baada ya hapo ndio Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Mbeya mjini alitoa adhabu kwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 kwenda kutumikia kifungo cha miezi 12 jela ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye tabia kama hiyo hasa katika mitandao ya kijamii nchini.