Mwenge wa uhuru wapongeza ujenzi wa wodi ya wazazi Kakola – HabariLeo

SHINYANGA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, ameweka Jiwe la Msingi katika jengo la wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Kakola, Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, lililogharimu zaidi ya Sh milioni 269.

Akisoma taarifa ya ujenzi huo kabla ya kuwekwa kwa jiwe hilo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk  Emanuel Boniface, amesema ujenzi ulianza rasmi Oktoba 2025 na kukamilika Julai 2026.

Amesema Serikali Kuu ilitoa Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi huo, huku halmashauri ya Msalala ikitoa zaidi ya Sh milioni 19 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kituo hicho.

Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kata ya Kakola ina takribani wakazi 51,000, ambao awali walikuwa wakitegemea zahanati kutokana na kutokuwepo kwa kituo cha afya.

Mwang’onda ameipongeza halmashauri ya Msalala kwa usimamizi mzuri wa ujenzi na wakandarasi, akisema jengo hilo limejengwa kwa kiwango kizuri.

Aidha, ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha miradi mingine inayotekelezwa inasimamiwa kwa umakini ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

*DKT. MWIGULU: TUENDELEE KULIOMBEA TAIFA NA KUDUMISHA AMANI*

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani, akisema amani ni msingi unaowezesha wananchi, taasisi za dini na Taifa kwa ujumla kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.

Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko na mitikisiko katika maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kumwomba Mungu ailinde Tanzania na kuendeleza amani ambayo imeiwezesha nchi kutekeleza shughuli zake kwa utulivu.

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumapili, Agosti 23, 2026) aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

“Tuendelee kuiombea nchi yetu. Leo hii tunaweza kufanya ibada kwa sababu nchi yetu ipo na amani. Tuna mipango mbalimbali kama nchi, katika ngazi ya familia, taasisi, Dayosisi na Kanisa, lakini hayo yote tunaweza kuyafanya kama nchi yetu ipo na amani,” amesema.

Dkt. Mwigulu amewafikishia waumini salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla, huku akitambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na Kanisa katika maendeleo ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele.

“Hauwezi ukataja maendeleo ya nchi yetu bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Goodluck Nkini, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kuabudu katika Usharika wa Kijitonyama na kwa kuendelea kujumuika na waumini katika maeneo mbalimbali.

Ibada hiyo iliongozwa na Mchungaji Anna Kuyonga wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kijitonyama.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mhe. Aggrey Mwanri; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; Mbunge wa Same Magharibi, Dkt. David Mathayo; na Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga.

Fahamu Faida na Hasara za Kutumia Gesi Kwenye Gari Kabla Hujafunga Mfumo

Matumizi ya gesi kwenye magari yanaendelea kuongezeka kutokana na gharama nafuu za uendeshaji na jitihada za kupunguza matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli. Hata hivyo, kabla ya kufanya uamuzi wa kubadili mfumo wa gari lako kutumia gesi, ni muhimu kufahamu faida na changamoto zake.

Bei ya kufunga mfumo wa gesi (CNG au LPG) kwenye gari hutegemea aina ya mfumo, ukubwa wa injini, idadi ya silinda na ubora wa vifaa vinavyotumika. Kwa Tanzania, makadirio ya bei ni kama yafuatayo:

  • Magari yenye injini ndogo (silinda 3–4): Takribani Sh milioni 1 hadi 3.5.
  • Magari yenye injini za kati (silinda 4–6): Takribani Sh milioni 3 hadi 5.
  • Magari makubwa (V6, V8 au SUV): Takribani Sh milioni 5 hadi 8 au zaidi, kutegemea mfumo unaowekwa.

Bei hiyo mara nyingi hujumuisha:

  • Tanki la gesi.
  • ECU (kompyuta ya mfumo wa gesi).
  • Injectors za gesi.
  • Pressure reducer/regulator.
  • Mabomba na vifaa vya usalama.
  • Ufungaji na majaribio ya mfumo.

Faida za kutumia gesi kwenye gari

1. Gharama nafuu za mafuta
Gesi kwa kawaida huwa na bei ya chini kuliko petroli au dizeli, hivyo hupunguza gharama za uendeshaji kwa madereva wanaosafiri mara kwa mara.

2. Rafiki kwa mazingira
Magari yanayotumia gesi hutoa kiwango kidogo cha hewa chafu, hivyo huchangia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

3. Huongeza maisha ya injini
Gesi huungua kwa usafi zaidi kuliko petroli, jambo linalosaidia kupunguza mabaki ya kaboni ndani ya injini na kuongeza maisha ya baadhi ya vipuri.

4. Huongeza chaguo la mafuta
Magari mengi yaliyowekewa mfumo wa gesi yanaweza kutumia gesi au petroli, hivyo dereva ana uhuru wa kuchagua kulingana na upatikanaji wa mafuta.

Hasara za kutumia gesi kwa upande wa injini

1. Kuongeza uchakavu wa valve na valve seats
Gesi huungua kwa joto la juu zaidi kuliko petroli katika baadhi ya mazingira ya uendeshaji. Kwa injini ambazo hazikutengenezwa mahsusi kutumia gesi, hali hii inaweza kuongeza uchakavu wa valve na sehemu zake (valve seats), na kusababisha gharama za matengenezo.

2. Kupungua kwa nguvu ya injini
Baadhi ya magari hupoteza kati ya asilimia 5 hadi 15 ya nguvu ya injini yanapotumia gesi, kutegemea aina ya mfumo na jinsi ulivyowekwa.

3. Hatari ya kuharibika kwa injini ikiwa mfumo umefungwa vibaya
Mfumo usiofungwa au usiotunzwa vizuri unaweza kusababisha mchanganyiko usio sahihi wa hewa na gesi (lean mixture), hali inayoweza kuongeza joto la injini na kusababisha uharibifu wa valve, pistoni au gasket ya kichwa cha injini (head gasket).

4. Kuongezeka kwa mzigo kwenye mfumo wa kuwasha (ignition system)
Matumizi ya gesi yanahitaji mfumo wa kuwasha uwe katika hali bora. Spark plugs, ignition coils na nyaya zake zinaweza kuchakaa haraka zaidi ikiwa hazitafanyiwa matengenezo kwa wakati.

5. Si kila injini inafaa kutumia gesi
Baadhi ya injini, hasa zenye valve seats laini au zilizotengenezwa bila kuzingatia matumizi ya gesi, zinaweza kupata uchakavu wa mapema. Ni muhimu kuhakikisha mtengenezaji wa gari au fundi mwenye uzoefu anathibitisha kuwa injini yako inafaa kufungwa mfumo wa gesi.

6. Gharama za matengenezo zinaweza kuongezeka
Iwapo mfumo wa gesi hautafungwa kwa viwango vinavyotakiwa au hautafanyiwa huduma za mara kwa mara, unaweza kusababisha hitilafu zinazohitaji matengenezo ya gharama kubwa kwenye injini.

Muhimu kufahamu

Hasara hizi si lazima zitokee kwa kila gari. Magari yenye mifumo ya kisasa ya gesi iliyofungwa kitaalamu, kutunzwa vizuri, na yanayotumia vifaa vya ubora mzuri yanaweza kufanya kazi kwa miaka mingi bila kupata uharibifu mkubwa wa injini. Jambo muhimu ni kufunga mfumo katika kituo kinachoaminika, kutumia vifaa vilivyoidhinishwa na kufuata ratiba ya matengenezo iliyopendekezwa.

Twikondele yafikisha mizinga 117 ya kisasa – HabariLeo

SHINYANGA: KIKUNDI cha Ufugaji Nyuki Twikondele kilichopo katika kijiji cha Buyange, Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala, kimefanikiwa kuongeza mizinga ya nyuki ya kisasa hadi kufikia 117 baada ya kupata ufadhili kutoka Kampuni ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Kikundi hicho kimeeleza kuwa ufadhili huo, uliokwenda sambamba na mafunzo na fursa za kutembelea maonyesho mbalimbali ya biashara, umewawezesha kuboresha ufugaji nyuki na kujifunza namna ya kutafuta masoko ya bidhaa zao.

Katibu wa kikundi hicho, Daniel Nkwande, amesema hayo leo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, alipofika katika eneo la mradi wa ufugaji nyuki na kitalu cha miti ya matunda, mradi uliogharimu Sh milioni 25.

Nkwande amesema kabla ya kufikia hatua ya kuwa na mizinga 117 ya kisasa, kikundi hicho kilianza shughuli za ufugaji nyuki mwaka 2015 kikiwa na mizinga saba ya kawaida.

Amesema Barrick Bulyanhulu pia imewapatia mafunzo mbalimbali, kuwawezesha kushiriki maonyesho ya biashara na kuwajengea uwezo wa kutafuta masoko, huku wakihamasishwa kupanda miti ya matunda kama sehemu ya uhifadhi wa mazingira.

“Kabla ya kufikia hatua ya kuwa na mizinga 117, tulianza ufugaji mwaka 2015 tukiwa na mizinga saba ya kawaida tuliyokuwa tukiifuga kwenye kikundi chetu,” amesema Nkwande.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Semkondo, amesema kampuni hiyo awali ilikifadhili kikundi hicho kwa mizinga saba kama hatua ya majaribio, na baada ya kuona kinafanya vizuri ikaongeza ufadhili kwa kuwapatia mizinga 110 ya kisasa.

Semkondo amesema kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na jamii inayozunguka mgodi kwa kuwawezesha kupitia mafunzo, vifaa na fursa za kujifunza katika maonyesho ya biashara.

Amesema ufugaji nyuki umeanza kuleta manufaa kwa wanakikundi, wakiwemo kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kutekeleza shughuli nyingine za maendeleo.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amepongeza kikundi hicho kwa kuunganisha ufugaji nyuki na uhifadhi wa mazingira kupitia uoteshaji wa vitalu vya miti ya matunda.

Mwang’onda amewataka kuendelea kutunza mazingira na kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za uhifadhi, akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Ninawapongeza kikundi hiki kwa uhifadhi na kuotesha vitalu vya miti ya matunda. Kila mmoja awe rafiki wa kuhifadhi mazingira,” amesema Mwang’onda.

WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA HOSPITALI YA MWANANYAMALA

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza leo Jumapili, Agosti 23, 2026, katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, kukagua hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alipowasili hospitalini hapo, Dkt. Mwigulu ametembelea wodi mbalimbali, zikiwemo Wodi ya Mama na Mtoto na Wodi ya Upasuaji, ambako amezungumza na wagonjwa pamoja na ndugu zao na kusikiliza maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo na changamoto wanazokabiliana nazo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na mazingira ya utoaji wa huduma hospitalini hapo.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; pamoja na viongozi wa Hospitali hiyo.

 

Jamal Bakhresa Afungiwa Kujihusisha na Mpira kwa Mwaka Mmoja

Global Publishers
August 23, 2026
1,050 views
0 Comments

Kiongozi wa Azam FC, Jamal Bakhresa, amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Agosti 22, 2026, adhabu hiyo inahusishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyodaiwa kufanywa na Bakhresa kabla na baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la CRDB uliochezwa kisiwani Pemba.

Bakhresa alifikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kujibu tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa kanuni za nidhamu. Katika mchakato wa kusikilizwa kwa shauri hilo, alisaidiwa na Wakili Alex Mushumbusi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bakhresa alikiri baadhi ya makosa yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.

Mbali na adhabu ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za mpira kwa mwaka mmoja, Bakhresa pia ameamriwa kulipa faini kutokana na makosa yaliyobainishwa. Aidha, ameahidi kutorudia vitendo hivyo.

Kamati ya Nidhamu ya TFF imesema uamuzi huo umetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 11(f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Toleo la mwaka 2021.

Adhabu hiyo inamaanisha Bakhresa hataruhusiwa kushiriki katika shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi kilichowekwa na kamati, huku uamuzi huo ukilenga kuimarisha nidhamu na kuzingatiwa kwa kanuni katika soka la Tanzania.

Stori na Florah Anderson | GPL – TUDACO

Meghan Markle Aanza Ukurasa Mpya wa Uigizaji Baada ya Kuondoka Suits

Global Publishers
August 23, 2026
486 views
0 Comments

LONDON: Meghan Markle anatarajiwa kurejea rasmi kwenye uigizaji kwa mara ya kwanza baada ya karibu muongo mmoja, huku akipokea nafasi mpya kubwa ambayo imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zilizoathiri muda wa yeye na Prince Harry kuamua kurejea Uingereza pamoja na watoto wao.

Kwa mujibu wa taarifa za PEOPLE, maelezo kuhusu mradi huo bado hayajawekwa wazi, lakini vyanzo vimeuelezea kuwa ni nafasi muhimu ambayo Meghan, 45, anafurahia kuipata. Msemaji wa Meghan na Harry hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo.

Meghan anafahamika zaidi kwa nafasi yake kama Rachel Zane katika tamthilia ya Suits, ambayo aliiacha baada ya uchumba wake na Prince Harry. Baada ya hapo, alijikita zaidi katika majukumu ya kifamilia, shughuli za hisani na uzalishaji wa maudhui.

Ingawa aliwahi kusema mwaka 2022 kwamba alikuwa amemaliza kazi ya uigizaji, hivi karibuni alianza kurejea taratibu katika tasnia hiyo. Mwaka 2025 alionekana katika filamu Close Personal Friends, akicheza nafasi ndogo kama yeye mwenyewe.

Taarifa hiyo imeibuka wakati Meghan na Prince Harry wakijiandaa kuhamia tena Uingereza pamoja na watoto wao, Prince Archie na Princess Lilibet, baada ya kuishi California kwa takribani miaka sita. Watoto hao wanatarajiwa kuanza shule nchini Uingereza mwezi Septemba.

Hata hivyo, kurejea kwao Uingereza hakumaanishi wameondoka kabisa Marekani. Wawili hao wanatarajiwa kuendelea kuwa na makazi yao Montecito, California, pamoja na kuendesha shughuli zao kupitia Archewell Productions na Archewell Philanthropies.

Wakati huo huo, Meghan anaripotiwa pia kuwa katika mazungumzo ya awali kuhusu nafasi katika mfululizo wa Netflix The Gentlemen, unaohusishwa na mtayarishaji na mwongozaji Guy Ritchie. Ikiidhinishwa, hiyo inaweza kuwa moja ya nafasi zake kubwa zaidi tangu kuondoka Suits.

Karoline Leavitt Afichua Kazi Yake Mpya Baada ya Kujiuzulu White House

Global Publishers
August 23, 2026
864 views
0 Comments

Karoline Leavitt, ambaye anatarajiwa kuondoka katika nafasi yake ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House Press Secretary.

WASHINGTON: Karoline Leavitt, ambaye anatarajiwa kuondoka katika nafasi yake ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House Press Secretary, amefichua kuwa ataendelea kufanya kazi kwa karibu na Rais Donald Trump baada ya kuondoka serikalini.

Leavitt amesema atarejea katika MAGA Inc. mwezi Septemba, ambako awali aliwahi kufanya kazi kabla ya kuwa msemaji wa kampeni ya Trump na baadaye kuteuliwa kuwa msemaji wa Ikulu.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika safari yake ya mwisho ndani ya ndege ya Rais Air Force One kuelekea kwenye mkutano wa Trump huko South Carolina Ijumaa, Agosti 21, Leavitt alisema atatumia muda kabla ya kurejea MAGA Inc. kuwa pamoja na familia yake.

Taarifa hiyo imekuja zaidi ya wiki moja baada ya Trump kutangaza kupitia mtandao wake wa Truth Social kuwa Leavitt ataondoka katika nafasi hiyo mwishoni mwa Agosti ili kutumia muda zaidi na watoto wake wadogo na familia.

Trump alisema Leavitt ataendelea kuwa mmoja wa washauri wake wakuu akiwa nje ya Ikulu na atakuwa na ushawishi ndani ya Chama cha Republican, hasa katika kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula.

Leavitt aliwahi kufanya kazi katika MAGA Inc. kabla ya kuwa msemaji wa kitaifa wa Trump na baadaye kushika nafasi ya White House Press Secretary.

Pia amerejea kazini hivi karibuni baada ya likizo ya uzazi. Yeye na mume wake, Nicholas Riccio, walipata mtoto wao wa pili mwezi Mei.

Kwa kurejea kwake MAGA Inc., Leavitt anatarajiwa kuendelea kuwa sehemu muhimu ya timu inayomsaidia Trump kisiasa, hususan katika maandalizi ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani.

Kadi Nyekundu Zatikisa Simba Wachezaji Watatu Nje, Waibua Maswali

Simba SC imeanza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kasi kubwa baada ya kushinda michezo yake yote mitatu ya mwanzo. Hata hivyo, mwenendo wa kupata kadi nyekundu katika kila mchezo umeanza kuibua maswali kuhusu nidhamu ya kikosi hicho.

Katika michezo yake mitatu ya mwanzo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2026/27, Simba SC imekumbana na kadi nyekundu katika kila mchezo, lakini jambo la kuvutia ni kwamba imeshinda yote na kufikisha alama tisa.

Mchezo wa kwanza: Kagera Sugar 0-2 Simba SC

Simba ilianza kampeni zake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Agosti 16, 2026. Ismail Touré alifunga bao la kwanza dakika ya 45, kabla ya Elie Mpanzu kuongeza la pili dakika ya 69.

Hata hivyo, dakika ya 55, beki David Kameta ‘Duchu’ alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea madhambi David Luhende. Licha ya kucheza pungufu, Simba ilifanikiwa kulinda ushindi wake.

Mchezo wa pili: Pamba Jiji 1-2 Simba SC

Katika mchezo wa pili uliochezwa Agosti 19, Simba ilishinda 2-1 dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Clatous Chama aliipa Simba bao la kwanza dakika ya 18, kabla ya Anicet Oura kuongeza la pili dakika ya 30. Pamba Jiji ilipata bao la kufutia machozi kupitia Idriss Diomande kwa mkwaju wa penalti.

Dakika ya 44, Simba ilibaki na wachezaji 10 baada ya Ibraheem Jabaar kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia tukio la kumgonga mpinzani kwa kiwiko. Pamoja na kucheza pungufu, Simba ilishikilia ushindi wa 2-1.

Mchezo wa tatu: Singida Black Stars 1-2 Simba SC

Katika mchezo wa tatu, Simba iliendeleza ushindi wake baada ya kuifunga Singida Black Stars 2-1 katika mchezo uliochezwa Agosti 22, 2026.

Clatous Chama aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 12, lakini Singida ikasawazisha kupitia Sheikhan dakika ya 22. Simba ilipata bao la ushindi dakika ya 62 kupitia Rushine De Reuck kwa mkwaju wa penalti.

Dakika ya 85, beki wa Simba Anthony Mligo alionyeshwa kadi nyekundu kufuatia rafu mbaya, na hivyo Simba kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji 10. Pamoja na hilo, ilifanikiwa kushikilia ushindi wa 2-1 na kufikisha alama tisa katika michezo mitatu.

Kwa hiyo, katika michezo hiyo mitatu, Simba imefunga mabao sita na kufungwa mabao mawili, huku wachezaji wake watatu David Kameta, Ibraheem Jabaar na Anthony Mligo wakipewa kadi nyekundu.

Mfululizo huo unaifanya Simba kuwa na mwanzo mzuri kwa upande wa matokeo, lakini pia unaweka alama ya kuuliza kuhusu nidhamu ya wachezaji, kwani katika kila mchezo timu imelazimika kucheza sehemu ya muda ikiwa na pungufu ya mchezaji.

 

Stori na Ashura Karimu

Fahamu Sababu Zinazofanya Mapera Kuwa Miongoni mwa Matunda Bora

Mapera ni miongoni mwa matunda yanayopatikana kwa urahisi lakini yana virutubisho muhimu kwa afya ya mwili. Tunda hili lina ladha nzuri, linaweza kuliwa likiwa bichi au kutengenezwa juisi, na lina virutubisho mbalimbali vinavyoweza kusaidia mwili katika shughuli zake za kila siku.

1. Husaidia kuimarisha kinga ya mwili
Mapera yana vitamini C kwa wingi, ambayo ni muhimu katika kusaidia mfumo wa kinga ya mwili kufanya kazi vizuri. Ulaji wa matunda yenye vitamini C ni sehemu ya lishe bora inayosaidia mwili kujilinda dhidi ya changamoto mbalimbali za kiafya.

2. Husaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula
Mapera yana nyuzinyuzi, ambazo ni muhimu kwa afya ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Nyuzinyuzi husaidia chakula kusafiri vizuri kwenye mfumo wa chakula na zinaweza kusaidia kudumisha choo cha kawaida.

3. Huchangia afya ya moyo
Ulaji wa matunda kama mapera, ambayo yana nyuzinyuzi na antioxidants, unaweza kuwa sehemu ya mtindo wa maisha unaolenga kulinda afya ya moyo. Lishe yenye matunda na mboga kwa wingi ni muhimu katika kudumisha afya kwa ujumla.

4. Yana antioxidants
Mapera yana aina mbalimbali za antioxidants, ambazo husaidia kulinda seli za mwili dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na molekuli hatarishi zinazojulikana kama free radicals.

5. Husaidia katika udhibiti wa uzito
Kwa kuwa mapera yana nyuzinyuzi, yanaweza kusaidia mtu kujisikia ameshiba kwa muda mrefu. Hii inaweza kuwa na mchango katika mpangilio mzuri wa ulaji kwa mtu anayelenga kudhibiti uzito.

6. Huchangia afya ya macho
Mapera yana virutubisho mbalimbali, ikiwemo vitamini A na antioxidants, ambavyo vina mchango katika kudumisha afya ya macho na mwili kwa ujumla.

7. Hutoa virutubisho muhimu mwilini
Mbali na vitamini C, mapera yana virutubisho vingine kama folate, potasiamu na vitamini B6. Virutubisho hivi vina nafasi mbalimbali katika utendaji wa kawaida wa mwili.

8. Ni bora kula tunda zima
Kula pera zima, baada ya kuliosha vizuri, kunaweza kukupa nyuzinyuzi zaidi kuliko kunywa juisi iliyotengenezwa kutokana na tunda hilo. Hivyo, kwa mtu anayependa matunda, kula pera kama lilivyo ni njia rahisi ya kupata virutubisho vyake.

Hitimisho

Mapera ni tunda lenye virutubisho mbalimbali na linaweza kuwa sehemu muhimu ya lishe bora na yenye mchanganyiko. Kula matunda kwa kiasi na kwa kuzingatia mahitaji ya mwili kunaweza kusaidia kuongeza ulaji wa vitamini, madini, nyuzinyuzi na antioxidants.

Hata hivyo, mapera hayapaswi kuchukuliwa kama dawa ya kutibu ugonjwa fulani. Afya bora inategemea mchanganyiko wa lishe bora, mazoezi, usingizi wa kutosha na mtindo mzuri wa maisha.https://www.youtube.com/watch?v=c2osqc-bV1E