VIJANA WATAKA KILIMO KIFUNGUE MILANGO YA AJIRA

Ukosefu wa mitaji, gharama kubwa za pembejeo na vikwazo vya biashara ni miongoni mwa changamoto zinazowakwamisha vijana kunufaika na fursa za ajira katika sekta ya kilimo.

Changamoto hizo zimejadiliwa katika kongamano la siku mbili linalofanyika Dodoma kuhusu ushiriki wa vijana katika mifumo ya chakula na biashara za kilimo.

Donald Mezambwa, Programu Ofisa wa Vijana, Jinsia na Maendeleo ya Ujasiriamali kutoka AGRA Tanzania, alisema kongamano hilo linalenga kubaini vikwazo vinavyowakabili vijana na kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na watunga sera.

Amesema kupitia mradi wa YEFA unaofadhiliwa na Mastercard Foundation kwa miaka mitano, vijana wanalengwa kuwezeshwa kupata ajira kupitia kilimo na mifumo ya chakula.

 “Vijana wanakabiliwa pia na ukosefu wa taarifa kuhusu taratibu za biashara za mipakani, ikiwemo utaratibu wa Simplified Trade Regime (STR), unaohusu biashara ndogo za bidhaa zenye thamani isiyozidi Sh milioni mbili kwa kuzingatia masharti husika,” Amesema Mezambwa  .

Kwa upande wake, Charles Constantine Masasi, Mkurugenzi wa Tavia Agribusiness Company Limited, alisema mitaji, ardhi na masoko ni muhimu kwa vijana wanaotaka kuwekeza katika kilimo.

Amesema kampuni yake ilinufaika na programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) tangu mwaka 2023 na kupata mkataba wa Serikali mwaka 2024 wa uzalishaji wa mbegu. Pia imeomba ekari 30 kupitia Halmashauri ya Kibaha kwa ajili ya kilimo cha mboga na matunda.

Masasi amesema gharama za pembejeo ni kikwazo, akitolea mfano wa mbolea inayouzwa kati ya Sh 80,000 na Sh 120,000 kwa mfuko, huku bei ya mahindi ikiwa haiendani na gharama za uzalishaji.

“Mifumo ya mikopo izingatie uwezo wa mwombaji na uhalisia wa mradi badala ya kutegemea historia ya mikopo pekee, akisema hali hiyo inawanyima baadhi ya vijana fursa za kuwekeza, ” Amesema.

Akizungumzia hatua za Serikali, Clephine Josephat, Msimamizi wa Programu ya BBT katika Wizara ya Kilimo, alisema Serikali inaendelea kuwawezesha vijana na wanawake kwa kuwapatia ardhi, mitaji, huduma za ugani na masoko.

Amesema kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 24 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, huku Serikali ikipanga kuanzisha mashamba 20 katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.

Josephat amesema Sh bilioni sita zimetengwa katika mwaka wa fedha husika kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) kwa ajili ya mikopo ya uwekezaji. 

Ameongeza kuwa ifikapo mwaka 2030, BBT inalenga kuchangia ajira milioni 1.6, kuweka ekari 340,000 katika uzalishaji na kupanua programu hiyo hadi vijiji 12,000 vya Tanzania Bara.

Mwisho