Global Publishers August 25, 2026 18 views 0 Comments
Uturuki imetangaza hatua ya kutaka Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akamatwe kimataifa kufuatia uchunguzi kuhusu shambulio dhidi ya wanaharakati waliokuwa wakipeleka misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Sheria wa Uturuki, Akin Gurlek, amesema hati za kukamatwa zimetolewa dhidi ya Netanyahu pamoja na mshukiwa mwingine, kwa tuhuma zinazohusisha mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mateso.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kesi hiyo inawahusisha jumla ya watu 35 na inahusiana na tukio la Israel kuingilia boti za Global Sea Flotilla katika maji ya kimataifa wakati zikiwa njiani kuelekea Gaza kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu.
Uturuki imekuwa mkosoaji mkubwa wa operesheni za kijeshi za Israel nchini Gaza, huku serikali yake ikiendelea kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya kile inachodai kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Hatua hiyo ya Uturuki inatarajiwa kuongeza mvutano wa kisheria na kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Israel, huku suala la kukamatwa kwa Netanyahu likiwa sasa likielekezwa kwenye taratibu za kimataifa kupitia Interpol.
Hata hivyo, Israel imeendelea kukataa tuhuma za kufanya ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu, jambo linalofanya hatua hiyo ya Uturuki kuwa suala linaloweza kuendelea kujadiliwa katika ngazi za kimataifa.
Global Publishers August 25, 2026 42 views 0 Comments
Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Aleksander Čeferin, amemtaka Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kujiuzulu nafasi hiyo, huku akisema hana mpango wa kugombea urais wa FIFA dhidi yake.
Čeferin ametoa kauli hiyo wakati Infantino akikabiliwa na shinikizo la kuondoka madarakani kufuatia mpango uliositishwa wa kuuza hisa katika Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.
Mashirikisho matatu ya soka ya mabara yameupinga mpango huo, yakidai kulikuwa na udanganyifu, huku UEFA ikitishia kususia baadhi ya mashindano yanayoandaliwa na FIFA.
Akizungumza katika mahojiano na podcast nchini Uingereza, Čeferin amesema Infantino amepoteza uungwaji mkono wa baadhi ya wadau muhimu wa soka, wakiwemo mashabiki, wachezaji na makocha.
Hata hivyo, Čeferin amesema hana nia ya kuwania urais wa FIFA, akieleza kuwa anaipenda nafasi yake ndani ya UEFA na pia anataka kupata muda wa kufurahia maisha nje ya majukumu ya uongozi wa soka.
Infantino amekuwa Rais wa FIFA tangu mwaka 2016. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwisho wa kuwasilisha fomu za wagombea katika uchaguzi huo ni Novemba 18.
Čeferin, mwenye umri wa miaka 58, amesisitiza kuwa licha ya kutokuwa tayari kugombea nafasi hiyo, anaamini wakati umefika kwa Infantino kuachia madaraka ya uongozi wa soka duniani.
Martin Cooper ni mhandisi wa Marekani anayefahamika duniani kama mmoja wa waanzilishi wakuu wa simu ya mkononi. Jina lake limeingia katika historia ya teknolojia baada ya kuongoza timu iliyotengeneza simu ya kwanza ya mkononi iliyoweza kutumiwa na mtu akiwa mahali popote bila kuhitaji kuunganishwa kwenye simu ya mezani.
Cooper alifanya kazi katika kampuni ya teknolojia ya Motorola, ambako alishiriki katika kuendeleza wazo la kuwawezesha watu kuwasiliana kwa simu wakiwa safarini au nje ya ofisi na nyumba.
Tarehe 3 Aprili 1973 ilikuwa siku muhimu katika historia ya mawasiliano. Siku hiyo, Martin Cooper alifanya simu ya kwanza ya mkononi hadharani mjini New York, Marekani.
Alitumia simu ya Motorola DynaTAC, kifaa kilichokuwa kikubwa na kizito sana ikilinganishwa na simu za kisasa.
Simu hiyo haikuwa na huduma tunazoziona kuwa za kawaida leo, kama kamera, intaneti, programu au ujumbe mfupi. Kazi yake kuu ilikuwa kumpa mtumiaji uwezo wa kupiga simu akiwa mbali na simu ya mezani.
Katika simu hiyo ya kwanza, Cooper alimpigia Joel Engel, mtafiti wa Bell Labs ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye teknolojia za mawasiliano ya simu.
Wazo lililobadilisha dunia
Kabla ya simu za mkononi, watu walitegemea zaidi simu za mezani zilizokuwa zimefungwa katika nyumba, ofisi au maeneo maalumu.
Cooper aliamini kuwa simu inapaswa kuwa kifaa cha mtu binafsi ambacho mtu angeweza kwenda nacho popote.
Wazo hilo lilikuwa na changamoto kubwa kwa wakati huo kutokana na ukubwa wa vifaa, gharama za uzalishaji na teknolojia iliyokuwepo. Hata hivyo, Motorola iliendelea na utafiti na maendeleo hadi kufanikisha simu hiyo.
Kutoka DynaTAC hadi smartphone
Baada ya simu ya kwanza ya mkononi kuanzishwa, teknolojia hiyo iliendelea kubadilika kwa kasi. Simu zilianza kuwa ndogo, nyepesi na rahisi kutumia.
Baadaye zikaongezewa uwezo wa kutuma ujumbe mfupi, kutumia kamera, kusikiliza muziki na kuunganishwa kwenye intaneti.
Hatua hiyo ilipelekea kuibuka kwa simu janja (smartphone) ambazo sasa zinaweza kufanya kazi nyingi, ikiwemo kupiga simu, kutuma ujumbe, kupiga picha, kutumia mitandao ya kijamii, kufanya biashara, kusoma, kutazama video na hata kutumia huduma za benki.
Kwa nini Martin Cooper ni muhimu?
Mchango wa Cooper haukuwa tu kutengeneza kifaa cha kupigia simu. Alisaidia kubadilisha namna ambavyo dunia inawasiliana.
Leo, simu ya mkononi ni sehemu muhimu ya maisha ya mabilioni ya watu duniani. Mtu anaweza kuwasiliana na mtu mwingine aliye maelfu ya kilomita kutoka kwake kwa sekunde chache.
Kutokana na mchango wake katika kuanzisha mapinduzi hayo, Martin Cooper anatajwa kama “baba wa simu ya mkononi.”
Safari kutoka kwenye simu kubwa ya Motorola DynaTAC ya mwaka 1973 hadi simu ndogo na zenye uwezo mkubwa tunazotumia leo ni ushahidi wa jinsi teknolojia ilivyobadilisha maisha ya binadamu.
Kwa hiyo, kila unaposhika simu yako mkononi, kumbuka kwamba nyuma ya teknolojia hiyo kuna historia ndefu iliyoanza na wazo la kumuwezesha mtu kubeba simu yake na kuwasiliana popote alipo.
IRINGA: WAKULIMA mkoani Iringa wamehimizwa kutumia mbegu bora na zilizoidhinishwa ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao, huku Serikali ikiimarisha mikakati ya kudhibiti mbegu bandia na kuwawezesha wakulima kupata pembejeo zenye ubora kwa wakati.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuongeza uzalishaji wa kilimo mkoani humo, hasa wakati wakulima wakijiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo, kwa kuzingatia umuhimu wa kuanza maandalizi mapema na kutumia mbegu zinazoendana na mazingira ya kilimo ya maeneo yao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Magozi, Kata ya Ilolo Mpya, Wakala Mkuu wa Mbegu za Serikali (ASA) chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds, Joseph Mgongolwa, ameipongeza serikali kwa kuendelea kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora za ruzuku huku ikiimarisha elimu ya kuzitambua na kuzitumia kwa usahihi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwakinga wakulima dhidi ya wafanyabiashara wanaouza mbegu zisizo na ubora, ambazo zinaweza kusababisha hasara kwa wakulima kutokana na kushuka kwa kiwango cha uotaji na uzalishaji.
Aidha Mgongolwa amepongeza mpango wa uwepo wa mawakala katika maeneo mbalimbali akisema utasaidia kurahisisha upatikanaji wa mbegu zilizoidhinishwa na kupunguza mianya ya wafanyabiashara wanaoweza kutumia fursa hiyo kuuza mbegu bandia.
Amesema matumizi ya mbegu bora, yakichanganywa na kanuni bora za kilimo, yana nafasi kubwa katika kuongeza tija kwa mkulima na hatimaye kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Ilolo Mpya, Oswald Kapungu, amewataka wakulima kutumia ushauri wa wataalamu wa kilimo katika kuchagua mbegu kulingana na aina ya zao, eneo na mazingira ya kilimo.
Amesema wakulima wanapaswa pia kuzingatia maandalizi ya mashamba, muda sahihi wa kupanda na matumizi sahihi ya pembejeo ili kuhakikisha mbegu bora zinatoa matokeo yanayotarajiwa.
Naye Diwani wa Kata hiyo, Patrick Muhegele, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kusikiliza changamoto za wakulima kwa kuhakikisha wanapata mbegu bora kwa gharama nafuu, akiwataka kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji.
Muhegele amewataka wakulima kuanza maandalizi ya mashamba mapema na kuhakikisha wanapata mbegu kwa wakati ili kuepuka kuchelewa kuanza msimu wa kilimo.
Baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Magozi wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mbegu bora za ruzuku, wakisema hatua hiyo imeongeza matumaini ya kuongeza uzalishaji na kipato kupitia kilimo.
Hata hivyo, wameiomba Serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao yao ili ongezeko la uzalishaji liendane na fursa za kuuza mazao kwa bei nzuri.
Ikiwa ni mwendelezo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambaye sasa anajitetea mwenyewe katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kanda ya Dar es Salaam, Lissu amefunguka namna ambavyo mchakato wa “No Reform, No Election” ulivyoanzia ndani ya chama, akieleza kuwa msimamo huo haukuwa kauli yake binafsi, bali ulikuwa msimamo wa CHADEMA ulioanzia katika maamuzi ya chama kabla ya uchaguzi wa ndani wa uongozi.
Lissu amesema kuwa tarehe 10 Desemba 2024, Mwenyekiti wa wakati huo wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ndiye aliyetamka msimamo huo, huku chama kikisubiri kwanza uchaguzi wake wa ndani uliokuwa umepangwa kufanyika Januari 2025.
Lissu amesema kuwa tarehe 20 Januari 2025, Baraza Kuu la CHADEMA lilifanya kikao chake, ambacho kwa mujibu wa utaratibu wa chama ndicho chombo kinachopokea na kupendekeza ajenda zitakazojadiliwa katika Mkutano Mkuu. Aidha, amesema kuwa Kamati Kuu iliwasilisha mapendekezo kuhusu msimamo wa “No Reform, No Election” kwa Baraza Kuu, na baada ya kukubaliwa, suala hilo likapendekezwa kuwa ajenda ya Mkutano Mkuu wa chama uliofanyika Januari 21, 2025.
Katika Mkutano huo Mkuu, Lissu amesema, pamoja na masuala mengine ya chama, mambo mawili muhimu yalifanyika. Kwanza, ulipitishwa msimamo wa CHADEMA kuhusu “No Reform, No Election”, na pili, uchaguzi wa viongozi wa chama ulifanyika ambapo yeye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA. Vilevile, Lissu amesema kuwa baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, alimteua John Mnyika kuwa Katibu Mkuu, huku Golugwa akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara na kiongozi mwingine akiteuliwa kwa upande wa Zanzibar.
Baada ya uongozi huo mpya kuingia madarakani, Lissu amesema kuwa walianza maandalizi ya mkakati wa “No Reform, No Election”, ambao ulikuwa na lengo la kuhamasisha wananchi nchini kuhusu masuala ya demokrasia na mabadiliko ya kisiasa.
Amesema kuwa mpango huo haukuwa wa kupanga kufanya uhaini, kuchoma nyumba za watu au kuvunja sheria za nchi, bali ulikuwa wa kuhamasisha umma na kuwasisitiza wananchi kudai mabadiliko ya kisiasa kwa njia za kisiasa, ikiwemo mikutano na maandamano.
Aidha, Lissu amesema kuwa katika utekelezaji wa mkakati huo, walipanga kuzungumza na Watanzania kupitia makundi na taasisi mbalimbali katika maeneo yao. Amesema miongoni mwa taasisi walizoanza nazo zilikuwa taasisi za kidini, ambapo walianza na shula za maimamu.
Hata hivyo, amesema hawakuhusika na BAKWATA wala CCM. Pia, amesema waliomba kukutana na Baraza la Maaskofu, lakini hawakufanikiwa kukutana nao, huku wakifanikiwa kukutana na Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari na kuzungumza nao kuhusu masuala hayo.
Vilevile, Lissu amesema kuwa kwa kuwa Tanzania ina uhusiano na marafiki katika nchi nyingine, waliamua kwenda Nairobi na kukutana na Raila Odinga, ambaye wakati huo alikuwa hai, pamoja na kwenda kumuona Mzee Warioba ili kuzungumza naye kuhusu “No Reform, No Election” na msimamo wao wa kisiasa.
Aidha, amesema kuwa alialikwa katika Chuo Kikuu cha Makerere kuzungumza kuhusu Mwalimu Julius Nyerere na urithi wake, na katika mazungumzo hayo alizungumzia pia changamoto za mfumo wa kikatiba nchini. Lissu amesema kuwa baada ya kurejea nchini, majukumu yaligawanywa kwa ajili ya kuanza ziara mbalimbali.
Amesema yeye alipangiwa Kanda ya Nyasa, ambako alipaswa kuzungumza katika mikutano ya hadhara. Lissu amesisitiza kuwa katika ziara hizo hawakuwa wanapanga kufanya uhaini wala kuvunja sheria za nchi.
Amesema ziara yao ya kwanza waliimaliza Iringa tarehe 30 Machi 2025. Baada ya hapo, Naibu Katibu Mkuu Golugwa alimtumia ujumbe mfupi wa simu akimtaka kuandaa watia nia kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Pia, amesema alitumiwa ujumbe kwamba tarehe 3 Aprili 2025 alitakiwa kufika Makao Makuu ya chama kwa ajili ya kuzungumza na watia nia hao kuhusu msimamo wa chama.
Lissu amesema tarehe 1 Aprili alirejea Dar es Salaam akiwa pamoja na John Heche kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo. Amesema mkutano huo uliofanyika kwa lengo la kuzungumza na watia nia na kuwaeleza msimamo wa CHADEMA kama chama.
Lissu amesema yeye ndiye alikuwa mzungumzaji katika mkutano huo, na kwamba hilo lilikuwa jukumu lake la kuzungumza baada ya mkutano kuandaliwa na taarifa kutolewa na Katibu Mkuu. Kwa msingi huo, Lissu amesema anashangaa kusikia kwamba yeye ndiye aliyeandaa mkutano huo. Amesema kama wangeuliza ni nani aliyeuandaa, wangeweza kupata majibu kuhusu mtu aliyekuwa na jukumu hilo.
Aidha, amesema yeye alipewa taarifa na Katibu Mkuu kuhusu jukumu lake la kwenda kuzungumza katika mkutano huo, hivyo kuwa mzungumzaji hakumaanishi kwamba ndiye aliyekuwa mratibu au mwandaaji wa mkutano.
Lissu amesema ushahidi uliowasilishwa mahakamani na mashahidi 17 pia unaibua maswali. Amesema kuna maneno katika ushahidi huo ambayo, ukisoma tu, hayangeweza hata kuchukua dakika moja, wakati mkutano wake ulikuwa mrefu sana. Kuhusu video ambayo anadaiwa kuichapisha kupitia Jambo TV, Lissu amesema hajawahi kuiona hadi leo.
Kwa hiyo, amesema akiulizwa alitumia dakika ngapi kwenye video hiyo, hawezi kutoa jibu kwa sababu hajawahi kuiona. Lissu amesema siku hiyo ya mkutano aliulizwa maswali mengi na alijibu maswali yote, akisisitiza kuwa mkutano huo ulikuwa wa zaidi ya saa tatu.
Aidha, amesema hakufanikiwa kuiona video hiyo kwa sababu kesho yake, tarehe 4 Aprili 2025, walielekea katika ziara mkoani Ruvuma.
Amesema tarehe 9 Aprili 2025, alipokuwa akielekea kumaliza mkutano wake jioni huko Mbinga, alikamatwa na kupigwa kabla ya kupelekwa katika kituo cha polisi Mbinga. Baadaye, amesema alihamishiwa Songea mjini, katika ofisi ya RPC.
Akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, Lissu amesema alieleza kuwa alikuwa na njaa na kuwaambia polisi kwamba alikuwa na dada yake katika eneo hilo ambaye angeweza kumletea chakula. Amesema majira ya saa nne usiku chakula kilifika na baadaye usiku alipelekwa Dar es Salaam. Lissu amesema kwa mtazamo wake, shahidi pekee aliyesema ukweli ni P17, huku akidai mashahidi wengine walitoa maelezo ambayo hayakuwa sahihi.
Amesema P17 ndiye aliyesema kuwa yeye ndiye aliyekuwa amechapisha maudhui hayo mtandaoni, siyo Lissu. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, Lissu amesema P17 alipata taarifa kutoka kwa bosi wake, John Marwa, ambaye naye alikuwa amepewa taarifa na Ofisa Habari wa chama, Brenda Rupia. Hapo ndipo Lissu anapoona mkanganyiko mkubwa katika upande wa mashtaka.
Amesema upande wa mashtaka unamhusisha yeye na uchapishaji wa maudhui hayo mtandaoni, wakati wao wenyewe walimleta P17 kama shahidi na P17 akaeleza kuwa yeye ndiye aliyerusha maudhui hayo mtandaoni. Vilevile, Lissu amesema upande wa mashtaka unadai kuwa yeye ndiye aliyeandaa mkutano, wakati kwa maelezo yake yeye alikuwa mzungumzaji tu na mkutano uliandaliwa na chama, huku taarifa kuhusu kushiriki kwake akipewa na Katibu Mkuu.
Kwa hiyo, Lissu amesema kama kweli kulikuwa na mtu aliyekuwa na jukumu la kuandaa mkutano huo, ushahidi ulipaswa kuelekeza kwa mhusika aliyekuwa na jukumu hilo, badala ya kumhusisha yeye kwa sababu tu alikuwa mzungumzaji wa mkutano.
TANGA; Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi zake kuhakikisha bunifu zinazozalishwa na Watanzania haziishii kuoneshwa kwenye maonesho, bali zinaendelezwa, zinalindwa na kupelekwa sokoni, ili zitoe suluhisho kwa changamoto mbalimbali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo, Jumatatu, Agosti 24, 2026, jijini Tanga wakati akihitimisha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, akisisitiza umuhimu wa kujenga mfumo unaowawezesha wabunifu kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa na huduma zenye tija.
Amesema Tanzania ina wabunifu wenye uwezo mkubwa katika maeneo mbalimbali, hivyo hatua inayohitajika sasa ni kuhakikisha ubunifu huo unavuka hatua ya kuoneshwa kwenye maonesho na kufikia hatua ya kutumika, kuzalishwa kwa wingi na kuuzwa sokoni.
“Ni lazima tuvuke kwenye maonesho, twende kwenye uhalisia wa maisha kwamba hivi vitu ambavyo tunavionyesha kwenye maadhimisho kama haya sasa viende kwenye utaratibu wa kila siku wa maisha, tuvitengeneze vya kutosha, vitumike na viingie sokoni,” amesema Dk Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi, ujuzi na ubunifu kwa lengo la kuyageuza maeneo hayo kuwa nguzo muhimu za uchumi wa Taifa na kuchochea maendeleo kupitia matumizi ya tafiti na teknolojia.
“Hatutaweza kuendelea bila kuwa na sayansi, teknolojia na tafiti na tukatumia matokeo ya tafiti hizo. Hatutapata tija bila kutumia matokeo ya tafiti hizo,” amesema.
Dk Mwigulu pia amesema Serikali haitakubali kushusha viwango vya elimu, akisisitiza umuhimu wa taasisi zinazosimamia ubora wa elimu kuendelea kusimamia misingi ya kitaaluma katika kuandaa wataalamu wenye uwezo unaokubalika.
“Tusitengeneze mazingira yawe rahisi ya kujifunza, yawe na alama kubwa kubwa, lakini kazini kuwe na zero kubwa kubwa. Hiyo hapana. Lazima tusimamie misingi ya elimu,” amesema.
Amesisitiza kuwa katika sekta nyeti kama afya, uhandisi na elimu, ubora wa mafunzo haupaswi kuchezewa.
“Hatuwezi kucheza na afya za Watanzania… Hatuwezi tukaandaa wataalamu kwa namna duni duni hivi, tutaharibu sekta yote. Tunataka walimu walio bora, maengineia walio bora; wakijenga daraja, wakijenga jengo, liwe jengo kweli kweli,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza mipango ya maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Tanga iangalie mahitaji ya kiuchumi na kijamii ya mkoa huo kwa kipindi cha miaka 25 ijayo, ili miundombinu inayojengwa sasa iendane na ukuaji wa uchumi, biashara, uwekezaji na ongezeko la matumizi ya usafiri wa anga.
“Lazima tunapojenga tuwaze mbele, tusijenge kwa ajili ya leo. Tuwaze mbele miaka 20 mbele, 25 mbele, kama ambavyo Dira yetu inatuambia,” amesema Dk Mwigulu.
Amesema uwanja huo unapaswa kujengwa kwa hadhi ya Tanga kama lango muhimu la shughuli za kiuchumi kutokana na miradi mikubwa inayotekelezwa katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ProF Adolf Mkenda amesema maonesho hayo yanaakisi jitihada za Serikali katika kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha elimu inayounganisha nadharia na vitendo, ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa kujiajiri na kuingia kwa ufanisi katika soko la ajira.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof Caroline Nombo amesema jumla ya taasisi 91 za umma na binafsi zimeshiriki katika maadhimisho hayo, ambayo yamehusisha maonesho ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu, mashindano ya kitaifa ya ujuzi na ubunifu pamoja na makongamano yaliyolenga kujadili mchango wa elimu, ujuzi na teknolojia katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amesema Bunge litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza elimu, ujuzi na ubunifu kupitia bajeti, sera na miongozo inayolenga kuwawezesha watafiti na wabunifu wa ndani kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Amesema kuna umuhimu wa kuzipa kipaumbele bidhaa na teknolojia zinazozalishwa nchini, zikiwemo katika taasisi za Serikali, ili kuongeza matumizi ya bunifu za Watanzania na kuchochea ukuaji wa wabunifu hao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Buriani amesema uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu umeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia mkoani humo, kuongeza miundombinu na kuchochea mafanikio ya wanafunzi, huku akipongeza maonesho hayo kwa kuibua na kuonesha uwezo mkubwa wa Watanzania katika sayansi, teknolojia na ubunifu.
Global Publishers August 24, 2026 18 views 0 Comments
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, amelipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango wake katika kuhubiri amani na utulivu nchini Tanzania.
Shigongo ametoa kauli hiyo wakati wa Jubilee ya Miaka 25 ya Upadri ya Padre Cleophace Magesa, iliyofanyika nyumbani kwao katika Kigango cha Itulabusiga, Parokia ya Mwangia ya Mwangika.
Amesema madhehebu mbalimbali ya dini yamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha amani nchini, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maisha ya jamii.
“Hivyo, tuendelee kuwaombea viongozi wa dini kwa kazi waliyonayo ya kuhubiri amani na utulivu ndani ya nchi yetu,” amesema Shigongo.
Aidha, Shigongo amesema juhudi za viongozi wa dini katika kuhubiri amani zinapaswa kuthaminiwa na kuungwa mkono kutokana na nafasi yao katika kujenga jamii yenye mshikamano na utulivu.
Global Publishers August 24, 2026 414 views 0 Comments
Yanga SC leo Agosti 24, 2026 inatarajiwa kushuka dimbani kuikabili JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 18:00 jioni.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku Yanga ikilenga kuendelea na mwenendo mzuri katika msimu huu, wakati JKT Tanzania ikisaka matokeo mazuri dhidi ya mabingwa hao.
Akizungumzia mchezo huo, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema mashabiki wamekuwa wakisubiri kwa muda kuona timu yao ikicheza katika uwanja huo.
“Mashabiki wameusubiri kwa muda mchezo huo na sasa siku imefika ya kuiona timu yao ikicheza katika Uwanja wa KMC,” amesema Ali Kamwe.
Aidha, Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kukata tiketi kupitia simu zao ili kuepuka usumbufu wakati wa kuingia uwanjani.
Mashabiki wa Yanga wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi KMC Complex kushuhudia mchezo huo, huku klabu ikiwataka kufanya maandalizi mapema kwa kukata tiketi kabla ya kwenda uwanjani.
Mchezo huo unaongeza hamasa katika mwendelezo wa Ligi Kuu ya NBC, huku macho ya mashabiki yakielekezwa KMC Complex kusubiri kuona nani ataibuka na pointi tatu.
Global Publishers August 24, 2026 6 views 0 Comments
Yanga SC leo Agosti 24, 2026 inatarajiwa kushuka dimbani kuikabili JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 18:00 jioni.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku Yanga ikilenga kuendelea na mwenendo mzuri katika msimu huu, wakati JKT Tanzania ikisaka matokeo mazuri dhidi ya mabingwa hao.
Akizungumzia mchezo huo, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema mashabiki wamekuwa wakisubiri kwa muda kuona timu yao ikicheza katika uwanja huo.
“Mashabiki wameusubiri kwa muda mchezo huo na sasa siku imefika ya kuiona timu yao ikicheza katika Uwanja wa KMC,” amesema Ali Kamwe.
Aidha, Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kukata tiketi kupitia simu zao ili kuepuka usumbufu wakati wa kuingia uwanjani.
Mashabiki wa Yanga wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi KMC Complex kushuhudia mchezo huo, huku klabu ikiwataka kufanya maandalizi mapema kwa kukata tiketi kabla ya kwenda uwanjani.
Mchezo huo unaongeza hamasa katika mwendelezo wa Ligi Kuu ya NBC, huku macho ya mashabiki yakielekezwa KMC Complex kusubiri kuona nani ataibuka na pointi tatu.