Ili kukabiliana na wadaiwa sugu kwenye vyama vya ushirika mkoani Njombe Saccos ya Walimu imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutumia wanasheria pamoja na kuwafikisha mahakamani wote watakaoshindwa kufanya marejesho yao kwa mujibu wa mkataba.
Katika mkutano mkuu wa Mwaka wa Saccos ya Walimu mkoa wa Njombe Mwenyekiti wa Bodi hiyo Humphrey Millinga amesema hatua hiyo inakuja kufuatia kuwapo kwa madeni ya zaidi ya shilingi milioni 290 ambayo yamewalazimu kutumia wanasheria ili kurejeshwa fedha hizo.
Sanjari na hayo lakini pia Bwana Millinga amewataka Watumishi wa Umma hususani wanachama wa SACCOS ya walimu kuacha tabia ya kutumia fedha yote wanayopata badala yake wawekeze hata kwa kuweka amana na kununua Hisa ili ziwasaidie katika maisha yao ya baadaye.
Awali akisoma taarifa ya kamati ya Mikopo Katibu wa Saccos hiyo Atukuzwe Mjujulu amesema licha ya maendeleo mazuri yaliyopo hivi sasa lakini bado kuna wadaiwa sugu ambao wanapaswa kurejesha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 290.
Kwa mujibu wa mkaguzi wa Nje wa vyama vya Ushirika COHASCO Bwana Vidoti Mkalinzi amesema miongoni mwa dosari zilizokutwa ni pamoja na kwenda kinyume katika utoaji Mikopo ya milioni 32.2 bila kuzingatia hisa zilizopo huku akitoa ushauri wa namna ya kushughulikia changamoto zilizopo.
Mgeni wa heshima katika mkutano huo ni mwenyekiti wa Chama cha walimu CWT Mkoa wa Njombe Mwalimu Varian Ngalioma ambaye anakiri kuwapo kwa maendeleo makubwa yaliyopigwa katika SACCOS Hiyo baada ya uongozi kubadilishwa huku haakiwataka walimu kuachana na mikopo umiza kwa kukopa kwenye taasisi za fedha za vichochoroni badala yake wakope Mwalimu Saccos.


