VIJANA WAIOMBA SERIKALI KUJENGA VIWANDA VYA MBOLEA

VIJANA wajasiriamali wa sekta ya kilimo wameiomba Serikali kuwekeza katika uanzishwaji wa viwanda vya mbolea nchini ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa pembejeo hiyo, kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha wakulima kuongeza tija.

Akizungumza kuhusu changamoto hizo, Mkurugenzi wa KSP, Frank Mustapher, amesema licha ya Serikali kuweka ruzuku ya mbolea kwa wakulima, bado kuna changamoto katika mfumo wa usambazaji, ikiwemo ucheleweshaji wa bidhaa kuwafikia wakulima na ugumu wa mawakala kuendesha biashara kutokana na gharama za usafirishaji na malipo ya fedha wanazodai.

Mustapher amesema mbolea ni muhimu katika uzalishaji wa mazao, hivyo upatikanaji wake kwa wakati na kwa bei nafuu ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza uzalishaji nchini.

Amesema Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya mbolea iliyowasaidia wakulima kupata pembejeo hiyo kwa gharama nafuu, lakini bado kuna changamoto zinazohusiana na uhusiano kati ya kampuni zinazosambaza mbolea na mawakala wanaowafikishia wakulima.

Ameeleza kuwa baadhi ya mawakala hukabiliwa na gharama za kusafirisha mbolea kwenda maeneo ya mbali, huku malipo wanayopata kwa mfuko mmoja yakiwa madogo ikilinganishwa na gharama za uendeshaji wa biashara hiyo.

Amesema hali hiyo inaweza kuwakatisha tamaa mawakala kuendelea na biashara ya usambazaji na hatimaye kusababisha wakulima kukosa mbolea kwa wakati unaohitajika.

Kutokana na changamoto hizo, Mustapher amependekeza Serikali kuweka mkakati wa kuanzisha viwanda vya kuzalisha mbolea katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza upatikanaji wake, kupunguza gharama za usafirishaji na kuwawezesha wakulima kununua pembejeo hiyo kwa bei nafuu.

Aidha, ameiomba Serikali kuboresha mifumo ya mikopo kwa vijana wajasiriamali wa kilimo, mifugo na uvuvi, akisema pamoja na kuwepo kwa fursa za mikopo, baadhi ya vijana hukumbana na vikwazo katika mchakato wa kuipata.

” Nimuhimu kuweka taratibu rahisi na zinazoeleweka ili vijana wenye miradi ya uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao waweze kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao, ” Amesema

Ameongeza kuwa uwezeshaji wa vijana kupitia mikopo na teknolojia za kisasa za kilimo utasaidia kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kutengeneza ajira.

Akizungumzia shughuli za KSP, Mustapher amesema taasisi hiyo inajihusisha na miradi ya kilimo pamoja na usambazaji wa mifumo ya umwagiliaji inayolenga kuwasaidia wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji.

Maoni hayo yametolewa katika kikao kilichowakutanisha vijana wajasiriamali na Kamati ya Bunge kwa lengo la kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara, pamoja na kujadili namna ya kuboresha mazingira ya ukuaji wa biashara zao.