Bosi NIMR asifu umuhimu wa tiba asili mfumo huduma za afya – HabariLeo

MBEYA; MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof Said Aboud, amesema asilimia 60 hadi 70 ya Watanzania huanza kutafuta matibabu ya tiba asili kabla ya kufika hospitalini, hali inayoonesha umuhimu wa tiba hiyo katika mfumo wa huduma za afya nchini.

Prof Aboud amesema kutokana na hali hiyo, NIMR inatoa huduma jumuishi katika hospitali za rufaa za mikoa 14 nchini, zinazompa mgonjwa fursa ya kuchagua kati ya tiba asili na huduma za hospitali, kwa lengo la kupanua wigo wa huduma za afya.

Amesema hayo leo wakati wa Kongamano la Tano la Kisayansi la Tiba Asili lililofanyika jijini Mbeya ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika, ambapo wataalamu wanawasilisha matokeo mbalimbali ya tafiti kuhusu tiba asili.

Amesema hadi sasa kuna takribani dawa 45 za tiba asili zilizosajiliwa katika mfumo, huku NIMR ikiwa imehusika katika dawa 11,kupitia kituo cha utafiti Mabibo, Dar es Salaam, kinachojihusisha na utafiti na uzalishaji wa dawa za tiba asili.

“Jukumu la NIMR ni kufanya utafiti ili kuangalia usalama, ufanisi na ubora wa dawa za tiba asili ambazo zimetengenezwa na NIMR, watafiti wetu au wataalamu wa tiba asili,” amesema Prof Aboud.

Amewataka wananchi kutumia dawa za tiba asili zilizohakikiwa na kuthibitishwa usalama, ufanisi na ubora wake, akisisitiza kuwa matumizi holela yanaweza kusababisha madhara.

Ameongeza kuwa Serikali imewekeza katika ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji wa dawa za tiba asili katika Kituo cha Utafiti cha NIMR Mabibo, Dar es Salaam, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa katika Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Prof Nicolao Otieno, amesema hadi sasa dawa 200 zimesajiliwa, huku zaidi ya 40 kati yake zikiwa zimepelekwa katika huduma jumuishi.

Amesema Mamlaka hiyo imeanza kufanya msako ili kubaini dawa zote zilizoingia nchini bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa huku akionya kuwa dawa ambayo haijasajiliwa hairuhusiwi kuingia sokoni wala kutumika nchini..

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI), Balozi Dk Mpoki Ulisubisya, amesema Serikali haiwezi kuruhusu matumizi ya tiba asili zisizothibitishwa ambazo zinaweza kuhatarisha afya za wananchi.

Amewataka wataalamu kuongeza kasi ya tafiti na ugunduzi katika eneo la tiba asili ili kuwezesha wananchi kupata huduma na dawa salama, zenye ufanisi na ubora unaokubalika.

Elimu zaidi inahitajika uelewa tiba asili – HabariLeo

MBEYA; Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya Wizara ya Afya, DK Winfrida Kidima,amesema jamii bado ina uelewa tofauti kuhusu tiba asili, hivyo Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa huduma hizo, hasa katika kuboresha afya ya wananchi.

Dk Kidima amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya.

Amesema tiba asili, ni maarifa ya ndani yaliyorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na ambayo yamekuwa yakitumika katika kutibu na kutatua changamoto mbalimbali za afya, lakini baadhi ya Watanzania wanahusisha tiba hizo na imani za kishirikina.

“Wizara ya Afya imejikita zaidi katika kuangalia huduma zinazohusiana na dawa, lakini kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kuangalia zile tiba na mbinu ambazo zinaweza kusaidia katika matibabu,” amesema Dk Kidima.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa tiba hizo hatua iliyowezesha kuanzisha huduma jumuishi za tiba za asili na zile zinazotolewa hospitali kwa kuzingatia miongozo ya huduma za afya.

Ameeleza kuwa ujumuishaji wa tiba asili katika mfumo wa afya unaendelea hatua kwa hatua, huku Serikali ikiendelea kujifunza na kufanya maboresho kulingana na miongozo iliyowekwa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema, amesema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha wataalamu wa tiba asili, watafiti, wasimamizi, wataalamu wa afya, wawekezaji, wazalishaji na wadau wa maendeleo kushiriki katika kuendeleza tiba asili kwa usalama na uendelevu.

Dk Nyema amewataka wananchi na wadau mbalimbali kushiriki katika shughuli zitakazofanyika katika kipindi chote cha maadhimisho hayo akisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mchango wa tiba asili katika huduma za afya unaendelezwa kupitia utafiti wa kisayansi, udhibiti, uhakiki wa ubora na ujumuishaji unaofaa katika mfumo wa afya.

Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika  Kitaifa yaliyoanza Agosti 25,2026,na kilele chake kitakachofanyika Agosti 31, 2026 yakiongozwa na kaulimbiu: “Juhudi katika Utafiti wa Tiba Asili kuelekea Huduma za Afya kwa Wote.”

 

Elimu ya uwekezaji yawaibua wananchi Karagwe – HabariLeo

WANANCHI wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wamepata elimu kuhusu umuhimu wa uwekezaji kupitia mifuko ya pamoja, huku wahitimu wa Shule ya Msingi Rwambaizi waliomaliza masomo miaka 50 iliyopita wakirejea shuleni na kuchangia maendeleo ya taasisi hiyo.

Wahitimu hao wameungana na wahitimu wa Darasa la Saba mwaka 2026 kufanya ibada ya pamoja na kuchangia maendeleo ya shule hiyo, hatua inayosisitiza umuhimu wa wahitimu kukumbuka walikotoka na kushiriki katika kuboresha mazingira ya elimu kwa kizazi cha sasa.

Zoezi la kuwaunganisha wahitimu hao limeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Pamoja wa Uwekezaji nchini UTT AMIS, Profesa Faustine Kamzora. Katika tukio hilo, wahitimu pamoja na UTT AMIS wamechangia Sh milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Shule ya Msingi Rwambaizi.

Mchango huo unalenga kusaidia shule hiyo kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, huku ukiwa mfano kwa jamii kwamba mafanikio anayopata mtu baada ya kumaliza masomo yanaweza kutumika kurudisha fadhila kwa jamii na taasisi zilizomjenga.

Ibada hiyo imeongozwa na Padre Edward Rwechungura, ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa shule hiyo miaka 50 iliyopita. Ushiriki wake pamoja na wahitimu wenzake umeonyesha namna kumbukumbu ya shule inaweza kubaki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya mtu hata baada ya miongo kadhaa kupita.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Vincent Edward, amesema Shule ya Msingi Rwambaizi ilianzishwa mwaka 1946, huku tukio hilo likiwa funzo kwa wahitimu wapya wa Darasa la Saba kwamba safari ya elimu haiishii katika kuhitimu, bali mafanikio yao ya baadaye yanaweza kuwa fursa ya kurejea na kusaidia jamii.

Baada ya ibada, Profesa Kamzora alitoa semina kwa mamia ya wananchi waliohudhuria Misa na mahafali ya Darasa la Saba kuhusu umuhimu wa kuwekeza fedha zao kupitia mifuko ya pamoja ya uwekezaji, ikiwemo UTT AMIS.

Alisema wananchi wengi huwa na hofu kuhusu namna salama ya kuhifadhi fedha, hivyo akawataka kufanya maamuzi sahihi ya kifedha kwa kuchagua maeneo yenye fursa ya kukuza fedha zao badala ya kuzitumia zote bila mpango.

Profesa Kamzora amewataka wananchi wa Karagwe kutumia vizuri mapato wanayoyapata kutokana na kilimo na mazao mbalimbali kwa kutenga sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema wananchi wanaopata fedha kwa misimu tofauti baada ya kuuza mazao wanaweza kutenga sehemu ya mapato yao na kuiwekeza kwa muda ili fedha hizo ziweze kukua na kuleta faida badala ya kutoweka katika matumizi ya muda mfupi yasiyokuwa na mpango mzuri wa kifedha.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujenga utamaduni wa kupanga matumizi ya fedha, kutenga fedha kwa mahitaji muhimu na kuweka sehemu kwa ajili ya uwekezaji wa baadaye.

Amesema uwekezaji unahitaji uvumilivu na maamuzi yenye malengo, hivyo wananchi wanapaswa kuelewa aina ya mfuko wanaochagua, masharti yake, kiwango cha hatari na matarajio ya faida kabla ya kuwekeza fedha zao.

Kwa upande wake, Padre Rwechungura amesema tukio la Rwambaizi limekuwa ujumbe mpana kwa jamii kuhusu umuhimu wa “kukumbuka nyumbani” na kurudisha mchango kwa jamii baada ya kufanikiwa.

Amesema wananchi wanaweza pia kuwekeza katika maisha yao ya baadaye na kutumia sehemu ya mafanikio yao kusaidia familia, shule na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo, uwekezaji unakuwa siyo tu njia ya kukuza fedha, bali pia sehemu ya kujenga maisha yenye mipango na kuacha alama chanya kwa vizazi vinavyofuata.

WANANCHI WAFURAHISHWA NA ELIMU YA PBPA KATIKA MAONESHO YA UTAMADUNI

 

Na Matukio Daima Media, MOROGORO

WANANCHI waliotembelea banda la Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) katika Maonesho ya Utamaduni, wameeleza kufurahishwa na elimu wanayoipata kuhusu majukumu ya Wakala katika kuratibu uagizaji wa mafuta kwa pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini.

Wananchi hao wamesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu kwao kupata uelewa kuhusu Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS), namna mafuta yanavyoagizwa nchini na nafasi ya PBPA katika kuratibu mchakato huo.

Bi. Maria Ngilisho, mmoja wa waliotembelea banda hilo, alisema elimu hiyo imemsaidia kuelewa mchakato wa upatikanaji wa mafuta nchini, ambao awali hakuwa na ufahamu wa kutosha kuuhusu.

“Nimefurahi kupata elimu hii kwa sababu tumekuwa tukitumia mafuta kila siku, lakini hatukuwa tunafahamu mchakato unaofanyika hadi mafuta yanapofika nchini. Sasa nimeelewa kuwa kuna taasisi kama PBPA inayoratibu uagizaji wa mafuta kwa pamoja,” alisema Ngilisho.

Naye, Bw. Michael Maganga, alisema mawasiliano ya ana kwa ana na watumishi wa PBPA yamewapa wananchi nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mafuta.

“Elimu tunayopata hapa ni muhimu sana kwa sababu tunapata nafasi ya kuuliza maswali yanayotuhusu kama watumiaji wa mafuta na tunapata majibu kutoka kwa wataalamu. Ni vizuri PBPA kuendelea kutumia maonesho haya kuwafikia wananchi,” alisema Maganga.

Kwa mujibu wa PBPA, miongoni mwa majukumu ya Wakala ni kukusanya mahitaji ya mafuta kutoka kwa kampuni za uuzaji wa mafuta, kuendesha zabuni za kimataifa za ununuzi wa mafuta kwa wingi, pamoja na kuratibu upokeaji na uwasilishaji wa bidhaa hizo nchini.

Ushiriki wa PBPA katika maonesho mbalimbali ni sehemu ya juhudi za Wakala za kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yake na nafasi yake katika sekta ya mafuta, huku  ukitoa fursa kwa wananchi kupata ufafanuzi kuhusu mchakato wa uagizaji wa mafuta na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizo unaendelea kuwa wa uhakika nchini.

IRINGA MANISPAA YATWAA UBINGWA WA VOLIBOLI SHIMISEMITA 2026

 

Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeibuka mshindi wa kwanza katika mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) yaliyofanyika jijini Mbeya mwaka 2026.

Ushindi huo umekuwa sehemu ya mafanikio makubwa kwa Manispaa ya Iringa baada ya kushindana na Halmashauri 177 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku timu hiyo ikifanikiwa kuibuka kidedea katika mchezo wa voliboli kwa wanaume.

Akizungumza baada ya ushindi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema mafanikio hayo yameipa heshima Manispaa hiyo na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.

“Iringa Manispaa tumeweza kuupa heshima kubwa Mkoa wetu wa Iringa. Kati ya Halmashauri 177 zilizoshiriki SHIMISEMITA 2026 tumeweza kuibuka kidedea kwa kupata ushindi wa kwanza katika mchezo wa voliboli kwa wanaume,” 

Mbali na juhudi za wanamichezo, Mlawa amesema Manispaa ya Iringa iliweka mazingira mazuri kwa timu zake kwa kuhakikisha wanamichezo wanapata sare pamoja na vifaa muhimu kwa ajili ya mashindano hayo.

“Tulianza maandalizi mapema, tukawapa t-shirt zenye nembo ya Manispaa lakini pia tukawaandalia t-shirt nyingine kwa ajili ya kubadilisha wanapokuwa kwenye mazoezi. Lakini kikubwa zaidi kilikuwa ni maandalizi na mazoezi,” 

Pia ameongeza kuwa  mafanikio hayo yametokana na maandalizi na juhudi za wanamichezo huku akieleza kuwa Manispaa hiyo itaendelea kujipanga vizuri kwa ajili ya mashindano yajayo.

“Tuko imara na tunaendelea kujipanga vema kwa ajili ya SHIMISEMITA 2027.

Mbali na ushindi wa voliboli Manispaa ya Iringa pia ilishiriki katika michezo mingine ambapo timu ya netiboli ilifika hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa kwenye mashindano hayo.

Timu ya mpira wa miguu nayo ilifanikiwa kufanya vizuri katika baadhi ya michezo ya hatua za awali kabla ya kuondolewa na wenyeji wa mashindano.

“Nawapongeza sana timu zetu zote zilizoshiriki kwa sababu haikuwa kazi ndogo Wachezaji walipambana katika michezo mbalimbali na tutaendelea kujipanga vizuri zaidi kwa mashindano yanayofuata,”

 

Ushindi huo wa voliboli umeifanya Manispaa ya Iringa kubeba kombe la ubingwa wa wanaume katika SHIMISEMITA 2026 huku matumaini yakiwa ni kuendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.

Rais Samia na Makamu Wake Ndejembi Walivyopiga Picha na Viongozi

Global Publishers
August 29, 2026
12 views
0 Comments

Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Deogratius John Ndejembi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Mkoani Dodoma tarehe 29 Agosti, 2026.
Dkt. Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Deogratius John Ndejembi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Mkoani Dodoma tarehe 29 Agosti, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepiga picha ya pamoja na viongozi wakuu wa Serikali baada ya hafla ya kumuapisha Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika picha hiyo, Rais Samia ameonekana akiwa pamoja na Makamu wa Rais Ndejembi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Lameck Nchemba.

Picha hiyo imepigwa leo, Jumamosi, Agosti 29, 2026, katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, mara baada ya kukamilika kwa hafla ya uapisho wa Ndejembi.

 

WATU WANNE WAFA MELI IKITEKETEA ZIWA TANGANYIKA

 

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

Watu wanne wamekufa na wengine watatu hawajulikani walipo baada ya Meli ya Mv  Pacific waliyokuwa wakisafiria kuungua moto katika bandari ya Kigoma mkoani Kigoma.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia August 29 mwaka huu katika bandari ya Kigoma Mjini Kigoma.

Kamanda Makungu alisema kuwa mtu mmoja alipatikana usiku wa tukio na watu wengine watatu walipatikana  mchana August 29 wakati wazamiaji walipokuwa wakitafuta miili ya abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo.

Meli hiyo iliyokuwa ikitoka Kigoma kuelekea Kalimie Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na mizigo mingine ilikuwa imebeba lita 16,000 ya mafuta ya dizeli yaliyokuwa yamewekwa kwenye matanki ambapo meli hiyo ilikuwa maalum kwa kubeba mizigo.

Meli hiyo ya abiria ilikuwa imesajiliwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu alisema ilipata ajali ikianza safari kuelekea DRC na  kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali unaendelea na taarifa zaidi itatolewa.

NDEJEMBI AAPISHWA RASMI KUWA MAKAMU MPYA WA RAIS NCHINI TANZANIA

 

Deogratius John Ndejembi,ameapishwa rasmi kuwa Makamu mpya wa rais nchini Tanzania, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi.

“Usiwe samaki, mwanetu nenda ukakue, tumekupa majukumu makubwa na ni imani yangu utaweza” alisema Rais Samia Suluhu akimpongeza makamu huyo mpya.

Hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Ndejembi mwenye umri wa miaka 43, atakuwa Makamu wa rais wa 13 tangu Tanzania ipate uhuru, akiwa miongoni mwa Makamu wa rais vijana zaidi kuwahi kushika nafasi hiyo.

RAIA WAWILI WA NIGERIA WAPELEKWA MAREKANI KUJIBU MASHTAKA YA UHALIFU WA MTANDAONI

 

Wanaume wawili kutoka Nigeria wamesafirishwa hadi nchini Marekani, kujibu mashtaka ya ulaghai wa kingono mtandaoni, katika sakata inayohusisha kifo cha kijana mmoja wa Marekani, kulingana na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X ,kwamba wanaume hao raia wa Nigeria, walikamatwa baada ya uchunguzi kufanywa.

Shirika la Nigeria la Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kifedha (EFCC) liliwataja wanaume hao wawili kuwa Mudashiru Afeez Olawale na Adebola Festus Adekunle.

EFCC ilisema wawili hao walikabidhiwa kwa mamlaka za Marekani kufuatia uchunguzi wa FBI kuhusu madai ya kuwalaghai watoto.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, shirika hilo lilisema washukiwa hao wanadaiwa kuwalenga wavulana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 17, wakitumia picha zao za uchi kuwalazimisha kutoa pesa kupitia kadi za zawadi, kuwatumia kwa benki na sarafu za kidijitali.

Kwa mujibu wa EFCC, kesi moja ilihusisha mvulana mwenye umri wa miaka 13 ambaye aliwasiliana na wawili hao kwenye mtandao wa Instagram na kubadilishana picha za uchi.

Shirika hilo lilisema baadaye mvulana huyo alitishiwa kuwa picha hizo zitasambazwa kwa watu wake wa karibu iwapo hangewatumia pesa.

“Vitisho hivyo viliendelea hata baada ya kijana huyo kusema kwamba alikuwa na nia ya kujiua,” EFCC ilisema.

Mitandao hiyo ya kuwalaghai watoto kwa kuwatishia kuvujisha picha zao za uchi zilichochea kifo cha mtoto mmoja, na uchunguzi ukapelekea kukamatwa kwa raia hao wawili wa Nigeria.