SELF YAMWAGA SH BILIONI 138, AJIRA ZAIDI YA 262,000 ZAZALIWA

 

Na Matukio DaimaMedia 

Mfuko wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 138 kwa wanufaika 131,312 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, iliyochochea shughuli za kiuchumi na kusaidia kutengeneza ajira 262,624 nchini.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa SELF, Santieli Yona, amesema mafanikio hayo yanaonesha mchango wa mfuko katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara.

Amesema katika kipindi hicho, mfuko umepata faida ya Sh bilioni 3.19 na kutoa gawio la Sh milioni 490 kwa Serikali, mafanikio yanayoonesha uwezo wake wa kuendesha shughuli zake kwa ufanisi huku ukiendelea kutekeleza jukumu la kijamii la kuwawezesha wananchi.

Yona amesema SELF imekuwa ikitoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi mengine, pamoja na kuziwezesha SACCOS na AMCOS kupata fedha za kukopesha wanachama wao. Ameongeza kuwa baadhi ya wanufaika wamepanua biashara zao na kuongeza uwezo wa kukopa, huku mfuko ukitoa pia mikopo ya makazi na kwa watumishi wa umma.

Katika kuongeza fursa za kujiajiri, amesema mfuko umeanzisha bidhaa za mikopo zinazowawezesha vijana kumiliki vyombo vya usafiri, ikiwemo bajaji, ili kujipatia kipato kupitia shughuli za kiuchumi. Hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za ajira na kuwawezesha vijana kushiriki katika uzalishaji.

Amesema upatikanaji wa huduma umeimarishwa kupitia mtandao wa matawi 12 na vituo viwili vya huduma vilivyofunguliwa mikoa ya Kigoma na Katavi, huku mfuko ukiendelea kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kuhusu mipango ya miaka mitano ijayo, Yona amesema SELF inalenga kupanua huduma za kidijitali ili wananchi waweze kupata taarifa na huduma za mikopo kwa urahisi bila kulazimika kufika katika matawi yake. Pia, mfuko unatoa mikopo ya majiko yanayotumia umeme kwa kiwango kidogo ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda mazingira.

Amesema mfuko unaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika kabla na baada ya kupata mikopo ili kuwasaidia kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, kupanga marejesho na kuendesha biashara zao kwa ufanisi, hatua inayolenga kuimarisha utamaduni wa kurejesha mikopo kwa wakati.

Hata hivyo, Yona amesema changamoto zinazoukabili mfuko ni pamoja na uelewa mdogo wa elimu ya fedha kwa baadhi ya wananchi, kutorejeshwa kwa mikopo kwa wakati na biashara nyingi za wajasiriamali wadogo kutokuwa rasmi. Amesema SELF inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha urasimishaji wa biashara ili kuongeza fursa za wananchi kupata huduma za kifedha.

Amesisitiza kuwa mfuko utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kupanua huduma za mikopo, kuongeza ajira na kukuza biashara, ili mikopo iendelee kuwa nyenzo ya kuongeza kipato cha wananchi, kukuza uchumi jumuishi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.