Global Publishers October 7, 2026 0 views 0 Comments
DAR ES SALAAM — Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuvifuatilia vyama vya siasa ambavyo havionekani kutekeleza majukumu na shughuli zao kikamilifu, akipendekeza vifutwe iwapo havikidhi matakwa ya kisheria.
Mwabukusi ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 7, 2026, wakati wa uzinduzi wa uongozi mpya na nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Amesema ni muhimu Msajili kuhakikisha vyama vya siasa vilivyosajiliwa vinafanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa, badala ya kubaki kwenye orodha ya vyama vilivyosajiliwa bila kuwa na shughuli zinazoonekana.
Aidha, Mwabukusi amesisitiza umuhimu wa kutoa nafasi kwa kizazi kipya, hususan vijana wa Gen Z, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa nchini.
Amesema vijana hao wanapaswa pia kupewa fursa ya kuanzisha vyama vyao vya siasa iwapo wanaona kuna haja ya kuwa na majukwaa yatakayowakilisha mitazamo na matarajio ya kizazi chao.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, ushiriki wa vijana katika siasa ni muhimu katika kuhakikisha mifumo ya kisiasa inaendelea kuakisi mabadiliko ya kijamii na mitazamo ya vizazi vipya.
DAR ES SALAAM — Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa nchini kusikilizwa na kueleza misimamo yao.
Prof. Kabudi amesema hayo leo, Oktoba 7, 2026, wakati wa uzinduzi wa uongozi mpya na nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Katika hafla hiyo, Prof. Kabudi pia amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya siasa kuheshimiana wanapoeleza tofauti zao za kisiasa, akisisitiza kuwa matumizi ya lugha yenye ukakasi yanaweza kudhoofisha heshima katika siasa.
Amesema si sahihi kumuita kiongozi mwenzake ambaye amechaguliwa kuwa “haramu”, akieleza kuwa kuna namna nyingine ya kueleza kutoridhishwa na uhalali wa uongozi bila kutumia neno hilo.
“Huwezi kumwita mwenzako kiongozi haramu, unaweza kusema hayupo hapo kihalali. Neno haramu katika Kiswahili lina maana ya ukakasi mkubwa sana,” amesema Prof. Kabudi.
Aidha, Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha linawashirikisha wanawake pamoja na wadau wengine katika shughuli zake.
Amesema heshima, ushirikiano na ushirikishwaji wa wadau ni miongoni mwa misingi muhimu katika kujenga mazingira mazuri ya kisiasa nchini.
Kauli hiyo imekuja wakati Baraza la Vyama vya Siasa likizindua uongozi wake mpya pamoja na nembo, hatua inayolenga kuimarisha nafasi ya baraza hilo katika kuwakutanisha vyama vya siasa na kukuza mazungumzo miongoni mwa wadau wa siasa nchini.
DAR ES SALAAM: Dk Norga Komba, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini China, anasema kwa mtazamo wake, utekelezaji wa Ilani ya chama hicho katika kipindi hiki unaonekana katika maeneo mbalimbali yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, hususan nishati, miundombinu, uwekezaji, elimu, afya na huduma za kijamii.
Katika sekta ya nishati, Dk Komba anaeleza kuwa kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere ni hatua muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania.
“Mradi huo una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 na una nafasi kubwa katika kuongeza upatikanaji na uhakika wa umeme, sambamba na kuwezesha shughuli za uzalishaji na uwekezaji,” anasema.
Kwa upande wa uwekezaji, anaona Serikali imeendelea kuweka mazingira yanayochochea uwekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Ukuaji wa uwekezaji, kwa mtazamo wake, una maana pana kwa wananchi kwa sababu unasaidia kupanua shughuli za uzalishaji, kuongeza ajira, kukuza biashara ndogo na za kati, na kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa.
“Takwimu za Serikali zinaonesha kuwa mwaka 2025 pekee zilisajiliwa zaidi ya miradi 900 ya uwekezaji, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika uchumi wa Tanzania,” anasema.
ANASEMAJE KWENYE SEKTA YA AFYA
Akizungumzia mafanikio makubwa ambayo anaona Serikali imeyapata katika kuboresha maisha ya wananchi, Komba ametaja sekta ya elimu kuwa miongoni mwa maeneo muhimu.
Anasema Serikali imeendelea kuwekeza katika upanuzi wa upatikanaji wa elimu, miundombinu ya shule na vyuo, pamoja na mikopo ya elimu ya juu.
“Hatua hizi zimewezesha Watanzania wengi zaidi kupata nafasi ya kusoma na kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye,” anasema Dk Komba.
Kwa mujibu wake, Serikali pia imeendelea kutoa elimu ya msingi bila malipo na kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu.
Katika sekta ya afya, amesema uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali, dawa, vifaa tiba na huduma za afya umeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi.
“Hili ni eneo ambalo lina umuhimu mkubwa kwa sababu afya bora ndiyo msingi wa uzalishaji na ustawi wa familia,” anasema.
VIPI KUHUSU MIUNDOMBINU NA NISHATI
Dk Komba pia anataja miundombinu ya usafirishaji kuwa eneo jingine ambalo ameona mafanikio. Anasema ujenzi na upanuzi wa barabara, madaraja, reli ya SGR na miundombinu ya usafiri wa anga umeongeza muunganiko wa maeneo mbalimbali nchini na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
“Miradi kama SGR na miundombinu ya kisasa ya usafiri pia ina umuhimu mkubwa katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema.
Katika eneo la nishati, Komba anaeleza kuimarika kwa miundombinu ya umeme na utekelezaji wa miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme, hususan Bwawa la Julius Nyerere, kunaweka msingi wa uchumi unaotegemea uzalishaji na viwanda.
CHANGAMOTO YA MAWASILIANO
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo, Komba anaeleza kuna changamoto ambazo bado zinahitaji Serikali kuongeza nguvu katika kuzitatua.
Anafafanua suala la mawasiliano ya taarifa za utekelezaji wa miradi na fursa zinazotolewa na Serikali kuwafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka.
“Serikali inaweza kuwa inatekeleza miradi na programu nyingi nzuri, lakini kama taarifa zake hazimfikii mwananchi kwa wakati, kuna hatari ya wananchi kutonufaika kikamilifu na fursa hizo au kutokuwa na uelewa wa hatua zinazochukuliwa,” anasema.
Kwa hiyo, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha zaidi mifumo ya mawasiliano ya Serikali kwenda kwa wananchi, hususan katika ngazi za vijiji, mitaa, kata na halmashauri.
Anasema matumizi ya teknolojia, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na viongozi wa jamii yanaweza kusaidia kufikisha taarifa kwa haraka zaidi.
“Nadhani tunahitaji kwenda hatua moja zaidi: siyo tu Serikali kutoa taarifa kwamba mradi umejengwa, bali kueleza wazi mradi huo umeleta faida gani, nani amenufaika, changamoto zilizopo na nini kinachofuata,” Anaeleza.
Kwa mtazamo wake, hatua hiyo itaongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi.
“Serikali yenyewe imetambua umuhimu wa taarifa za maendeleo kuwafikia wananchi kwa wakati katika mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” anahitimisha.
ANAZUNGUMZIAJE SEKTA YA KILIMO
Norga Komba anasema Serikali imeendelea kuwekeza katika umwagiliaji, upatikanaji wa mbegu bora, mbolea, huduma za ugani, mechanisation na matumizi ya teknolojia za kisasa. Pia kuna jitihada za kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mnyororo wa thamani.
Kwa mfano, katika mwaka 2024/2025, uzalishaji wa mazao ya chakula ulifikia takribani tani milioni 23.78, kutoka tani milioni 22.8 mwaka uliotangulia. Wizara pia imeweka mkazo katika kuimarisha huduma za ugani na kuhamisha teknolojia kutoka kwa watafiti kwenda kwa maafisa ugani na wakulima.
“Lakini hatua inayofuata ni kuhakikisha kwamba mkulima anapata faida zaidi kutoka kwenye kilimo. Hii inahitaji kupunguza gharama za uzalishaji, kuimarisha uhifadhi baada ya mavuno, kuongeza thamani ya mazao, upatikanaji wa masoko na kuhakikisha mkulima anaingia kikamilifu katika kilimo biashara,” anasema Norga Komba.
MTAZAMO WAKE FURSA KWA WATANZANIA
Katika eneo hili, Norga Komba anasema Serikali imechukua hatua kadhaa muhimu, hasa kupitia uwezeshaji wa vijana, wanawake na wajasiriamali.
Anasema mikopo na programu mbalimbali za uwezeshaji zimekuwa nyenzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kuanzisha au kupanua biashara zao na hivyo kujenga uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine.
Ametaja vijana na wanawake kuwa wamefikiwa kwa kiwango kikubwa kupitia mikopo na programu mbalimbali za kuwawezesha kiuchumi.
“Hata hivyo, suala la ajira linahitaji kuangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi kuliko ajira za Serikali pekee. Tunahitaji uchumi unaozalisha ajira kupitia uwekezaji, viwanda, kilimo cha kisasa, teknolojia, biashara, nishati, utalii na huduma mbalimbali,” anafafanua.
Anazungumzia pia upande mwingine, diplomasia ya Tanzania kuwa imeendelea kufungua milango ya fursa kwa Watanzania. Anasema Mahusiano mazuri na nchi mbalimbali yamekuwa yakitoa nafasi katika biashara, uwekezaji, elimu, mafunzo, teknolojia na ushirikiano wa kitaalamu.
Hivyo, diplomasia ya kiuchumi inaweza kuwa chombo muhimu zaidi cha kuwaunganisha vijana na wanawake wa Tanzania na masoko, mitaji, teknolojia na maarifa kutoka nje.
Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu amesema Tanzania imefanikiwa kutekekeza mifumo ya kikatiba na kisheria inayoongeza uwakilishi wa wanawake Bungeni na katika Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika ametoa kauli hiyo wakati akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Ausha (AICC).
“Tunajivunia kuwa uwakilishi wa wanawake katika Bunge letu umekuwa ukiongezeka kwa muda hadi kufikia 39.5% kwa sasa,” amesema
Amesema Sheria ya Vyama vya Siasa sasa inaelekeza wazi ujumuishaji wa makundi ya kijamii (vijana, wanawake na watu wenye ulemavu) ndani ya miundo ya ndani ya vyama na uteuzi wa wagombea.
WASHINGTON, Marekani — Rais wa Marekani, Donald Trump, amehusisha maandamano na vurugu zinazoendelea nchini Ufaransa na kile alichokiita uhamiaji wa kiwango kikubwa pamoja na Uislamu, akidai kuwa hali hiyo ni ishara ya changamoto zinazokabili mataifa ya Ulaya.
Trump alitoa kauli hiyo Jumanne, Oktoba 6, kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, wakati maandamano ya wanafunzi yakiendelea katika maeneo mbalimbali nchini Ufaransa.
“What’s happening in France is nothing less than out-of-control mass migration,” Trump aliandika, akidai kuwa suala hilo “si kuhusu shule” bali linahusiana na Uislamu na mabadiliko ya kijamii nchini humo.
Maandamano hayo yamekuwa yakifanyika tangu mwishoni mwa Septemba, huku wanafunzi wakifunga milango ya mamia ya shule za sekondari na kuandamana wakitaka kuboreshwa kwa mazingira ya elimu.
Baadhi ya maandamano yamegeuka kuwa makabiliano kati ya waandamanaji na vyombo vya usalama, hali iliyosababisha vurugu katika baadhi ya maeneo.
Siku ya Jumanne, takribani watu 250,000 waliandamana katika maeneo mbalimbali nchini Ufaransa, kwa mujibu wa taarifa zilizotajwa na AFP.
Hata hivyo, madai ya waandamanaji yamejikita zaidi katika masuala ya elimu na hali ya shule, huku Trump akitafsiri machafuko hayo kwa kuhusisha na uhamiaji na Uislamu.
Kauli ya Trump imekuja wakati vuguvugu lake la kisiasa la Make America Great Again (MAGA) likizidi kutumia matukio ya Ulaya kuonyesha kile wanachokiona kama madhara ya sera za uhamiaji.
Baadhi ya wafuasi wake wamekuwa wakisambaza video za maandamano ya Ufaransa kwenye mitandao ya kijamii.
Mshirika wa Trump, Glenn Beck, alisema Jumatatu kuwa vurugu nchini Ufaransa ni “onyo kwa nchi nyingine za Magharibi.”
Suala la uhamiaji limeendelea kuwa moja ya mada kuu katika siasa za Marekani, huku chama cha Republican kikisisitiza sera za kudhibiti uhamiaji kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula (midterm elections) unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Wakati huo huo, utawala wa Trump unakabiliwa na mjadala mkali kuhusu sera zake za ndani na nje, huku suala la uhamiaji likiwa miongoni mwa maeneo yanayotumika katika kampeni za kisiasa.
Kwa sasa, maandamano nchini Ufaransa yanaendelea huku mamlaka zikikabiliana na changamoto ya kudhibiti vurugu, wakati madai ya wanafunzi kuhusu hali ya elimu yakiendelea kuwa sehemu muhimu ya mjadala wa kitaifa.
MADRID: Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, ametangaza uchaguzi mkuu wa mapema utakaofanyika Novemba 29, 2026, badala ya mwaka 2027 kama ilivyopangwa awali.
Sánchez ametangaza uamuzi huo Jumatatu, Oktoba 5, 2026, baada ya serikali yake kukabiliwa na changamoto ya kupata uungwaji mkono wa kutosha bungeni kupitisha miswada muhimu.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha kwa mpango wa kukabiliana na mgogoro wa makazi, uliolenga kupunguza gharama za nyumba, kuwalinda wapangaji walio katika mazingira magumu dhidi ya kufukuzwa na kudhibiti baadhi ya shughuli za wawekezaji katika soko la nyumba.
Hispania imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la gharama za kodi za nyumba, hali inayowafanya wananchi wengi kushindwa kumudu makazi, hasa katika miji mikubwa kama Madrid.
Maelfu ya wananchi wamekuwa wakiandamana wakitaka serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo. Tukio la mwanamke mwenye umri wa miaka 87, Maricarmen Abascal, aliyefukuzwa katika nyumba yake mjini Madrid, limeongeza mjadala kuhusu haki ya kupata makazi.
Akizungumza kuhusu uchaguzi huo, Sánchez amesema ni wakati kwa wananchi kuamua mwelekeo wa kisiasa wanaoutaka kwa taifa lao.
Amesema uchaguzi huo unalenga pia kupata uungwaji mkono mpana zaidi wa kisiasa ili kuunda wingi imara wa vyama vinavyounga mkono sera za maendeleo ya kijamii, haki na uwajibikaji wa kimazingira.
Sánchez pia amekiri kuwa serikali yake imefanya makosa na kushindwa kutekeleza baadhi ya ahadi ilizojiwekea.
Uamuzi huo umefungua fursa kwa chama kikuu cha upinzani, Popular Party (PP), kinachoongozwa na Alberto Núñez Feijóo, kujaribu kuunda serikali mpya.
Chama cha PP kimekuwa kikiongoza katika baadhi ya kura za maoni dhidi ya chama tawala cha Spanish Socialist Workers’ Party (PSOE), huku chama cha mrengo wa kulia cha Vox kikitajwa kama mshirika anayeweza kusaidia upinzani kupata wingi wa viti bungeni.
Uchaguzi wa Novemba 29 unatarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa Sánchez, ambaye amekuwa Waziri Mkuu wa Hispania tangu mwaka 2018.
Wapiga kura watakuwa na nafasi ya kuamua mustakabali wa serikali yake, mwelekeo wa sera za makazi na mwelekeo wa siasa za Hispania katika miaka ijayo.
Global Publishers October 5, 2026 42 views 0 Comments
MANYARA — Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Fadhili Maganya, amewataka baadhi ya wanasiasa wanaoikosoa Serikali kutembelea maeneo mbalimbali nchini ili kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo na maboresho yanayofanyika katika huduma kwa wananchi.
Maganya ameyasema hayo Oktoba 4, 2026, wakati akiendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Manyara, akiongozana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Manyara, Janes Darabe.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Fadhili Maganya.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Wilaya ya Mbulu, Maganya amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wazazi.
Amesema ziara za kutembelea maeneo mbalimbali nchini zinasaidia viongozi na wadau kuona kwa uhalisia namna miradi ya maendeleo inavyotekelezwa na huduma zinavyoboreshwa kwa wananchi.
Maganya amesisitiza umuhimu wa kupata taarifa za maendeleo kutoka maeneo husika badala ya kutegemea taarifa za pembeni wakati wa kutoa tathmini kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za Jumuiya ya Wazazi katika mkoa wa Manyara, ambapo viongozi wameendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi na wanachama.
Wicknell Munodaani Chivayo, maarufu kama Sir Wicknell.
HARARE, Zimbabwe – Jina la Wicknell Munodaani Chivayo, maarufu kama Sir Wicknell, lilikuwa miongoni mwa majina yaliyotajwa sana katika ulimwengu wa biashara nchini Zimbabwe na sehemu mbalimbali za Afrika kutokana na shughuli zake katika sekta ya nishati, miundombinu, mawasiliano, usafirishaji na uwekezaji.
Chivayo, amefariki akiwa na umri wa miaka 43 baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Marondera, Zimbabwe Septemba 30, 2026 alikuwa akijulikana pia kwa maisha ya kifahari, magari ya gharama kubwa, mali za thamani na misaada mikubwa aliyokuwa akitoa kwa watu na taasisi mbalimbali.
Mamlaka za Zimbabwe zilisema watu wote sita waliokuwa ndani ya helikopta hiyo hawakunusurika. Mke wake, Lucy Muteke, pia alikuwa miongoni mwa waliofariki.
Chapisho la mwisho la umma la Wicknell Chivayo kwenye mtandao wa X pia limezua mjadala mkubwa baada ya taarifa za kifo chake kuibuka.
Chivayo alichapisha ujumbe huo asubuhi ya tarehe 30 Septemba, saa chache kabla ya helikopta aliyokuwa akisafiria kupata ajali.
Chivayo akionyesha saa za gharama kubwa baada ya kutembelea kiwanda cha Jacob & Co. akiwa na mmiliki wa kampuni hiyo, Jacob Arabo enzi za uhai wake.
Ulikuwa ujumbe wa kuwapongeza mawakili wawili ambao alisema walikuwa wamemuunga mkono kwa miongo kadhaa. Alianza chapisho hilo kwa maneno haya ya Kiingereza: “APPRECIATING RELATIONSHIPS BUILT OVER DECADES… SAVED THE BEST FOR LAST.”
Chapisho hilo lilijumuisha ahadi za kutoa magari ya kifahari na zawadi kubwa za fedha kwa watu aliokuwa akiwashukuru.
UTOTO ULIOJAA CHANGAMOTO
Kabla ya kujulikana kwa utajiri wake, Chivayo alieleza kupitia wasifu wake rasmi kuwa alikulia katika mazingira magumu huko Chivhu, Zimbabwe.
Kwa mujibu wa wasifu huo, alipoteza baba yake akiwa na umri wa miaka 10 na kulelewa na mama yake katika eneo la Gandami, Chivhu. Alisema aliacha shule akiwa kidato cha pili kutokana na changamoto za kifedha.
Akiwa na umri wa miaka 15, alianza kufanya kazi katika kampuni ya mabasi kama karani anayehusika na mishahara. Baadaye akaingia katika biashara na kuanza kujenga kampuni zake hatua kwa hatua. Katika wasifu wake, Chivayo alidai kwamba alipata milioni yake ya kwanza ya rand akiwa na miaka 19 na milioni yake ya kwanza ya dola akiwa na miaka 23. Madai hayo yanatokana na wasifu wake mwenyewe na hayawakilishi hesabu huru za mapato yake.
INTRATREK NA BIASHARA YA NISHATI
Moja ya kampuni zilizohusishwa kwa karibu zaidi na jina lake ni Intratrek Zimbabwe, ambayo ilijikita katika miradi ya nishati na miundombinu.
Intratrek ilipewa mwaka 2014 mkataba wa kujenga Gwanda Solar Project, mradi wa kuzalisha umeme wa jua wenye uwezo uliopangwa wa megawati 100. Mkataba wa awali ulikuwa na thamani ya takribani dola milioni 172 hadi 173 za Marekani.
Mradi huo ulipitia miaka kadhaa ya migogoro ya kimkataba na kisheria. Baadaye mahakama za Zimbabwe ziliamua kuhusu uhalali wa mkataba huo, na mwaka 2025 serikali na Intratrek zilisaini mkataba uliorekebishwa.
Mnamo Septemba 2026, Zimbabwe Power Company ilitoa Notice to Proceed, ikiiagiza Intratrek kuanza tena utekelezaji wa mradi huo. Thamani ya mkataba uliorekebishwa iliripotiwa kuwa karibu dola milioni 132, huku muda wa utekelezaji ukiwekwa kuwa miezi 24.
Ni muhimu kutofautisha thamani ya mkataba na utajiri binafsi wa Chivayo. Mkataba wa dola milioni 132 haukumaanisha kwamba fedha hizo zote zilikuwa mali yake binafsi; gharama hizo zinahusisha vifaa, ujenzi, wafanyakazi, washirika wa kiufundi, fedha za uendeshaji na gharama nyingine za mradi.
NDOA YA KWANZA NA SONJA MADZIKANDA
Chivayo alifunga ndoa na Sonja Louise Madzikanda mwaka 2017. Uhusiano wao ulidumu kwa takribani miaka saba na walipata watoto wawili.
Maisha yao ya ndoa yaliendelea kwa muda huku Chivayo akiwa akizidi kujenga biashara zake na kupata umaarufu mkubwa nchini Zimbabwe. Mwaka 2018, Chivayo aliwahi kuweka hadharani matokeo ya kipimo cha DNA kuthibitisha kwamba alikuwa baba wa mtoto wake wa kiume, John Chenjera-Chivayo.
Hata hivyo, baadaye uhusiano huo ulianza kukumbwa na migogoro na hatimaye wawili hao wakaachana. Chivayo alieleza kwamba sababu kubwa za kuvunjika kwa ndoa hiyo zilihusisha tofauti zisizoweza kutatuliwa, zikiwemo mvutano uliokuwa umejitokeza kati ya Sonja na familia yake.
TALAKA NA MGOGORO WA KISHERIA
Baada ya kuvunjika kwa uhusiano wao, suala la ndoa hiyo liliendelea kuonekana katika vyombo vya habari kutokana na migogoro kuhusu watoto na mali.
Mwaka 2026, Mahakama Kuu ya Zimbabwe ilihitimisha mzozo wa talaka kati ya Chivayo na Sonja Madzikanda kupitia makubaliano ya pande zote. Makubaliano hayo yalihusisha mpango wa malezi ya watoto wao pamoja na kifurushi cha matunzo cha dola milioni 5 za Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya The Herald, dola milioni 2.2 zilikuwa tayari zimelipwa na kiasi kilichobaki cha dola milioni 2.8 kilitakiwa kulipwa ndani ya siku 30.
Pia kulikuwa na kesi kuhusu namna Chivayo alivyokuwa akipata nafasi ya kuwaona watoto wake. Mahakama baadaye ilitoa utaratibu wa kuhakikisha anapata fursa ya kuwaona watoto hao.
KUINGIA KATIKA MAISHA YA LULU MUTEKE
Baada ya uhusiano wake na Sonja kuvunjika, Chivayo alianza uhusiano na Lucy “Lulu” Muteke.
Uhusiano huo ulianza kujulikana zaidi hadharani mwishoni mwa mwaka 2024 na mwanzoni mwa 2025. Chivayo alifanya uhusiano huo kuwa wa wazi, akimtambulisha Lulu kama mwanamke ambaye angekuwa mke wake.
Chivayo na mke wake Lucy “Lulu” Muteke.
Mwezi Machi 2025, kabla ya kufunga ndoa, Chivayo alimpeleka Lulu kumtambulisha kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, ikulu.
Katika ujumbe aliouchapisha, Chivayo alimuelezea Lulu kama “soon tobe wife” na akasema alikuwa amepata heshima ya kumtambulisha kwa Rais.
HARUSI YA WICKNELL NA LULU
Mwaka 2025, Chivayo na Lulu Muteke walifunga ndoa katika sherehe kubwa zilizofanyika Zimbabwe.
Walifanya taratibu za kimila pamoja na sherehe ya kidini ndani ya jumuiya ya Johane Masowe Echishanu, ambayo Chivayo alikuwa akiihusudu kwa muda mrefu.
Harusi hiyo ilivuta hisia kubwa kutokana na ukubwa wake, idadi ya wageni pamoja na uwepo wa watu mashuhuri. Wanamuziki maarufu akiwemo Jah Prayzah na Killer T walitumbuiza katika sherehe hizo.
Chivayo mwenyewe alielezea siku hiyo kama moja ya siku maalumu zaidi katika maisha yake, akiwashukuru familia yake na familia ya Lulu kwa kuunga mkono ndoa yao. Pia aliwashukuru wazazi wa Lulu kwa kumkabidhi binti yao na akaahidi kumpenda, kumlinda na kumtunza.
MAISHA YA NDOA NA LULU
Baada ya kufunga ndoa, Chivayo na Lulu walionekana mara kadhaa pamoja katika matukio mbalimbali, safari na shughuli za kijamii.
Lulu, ambaye pia ameelezwa katika baadhi ya taarifa kuwa alikuwa akifanya kazi katika sekta ya fashion na luxury lifestyle kama personal shopper, aliendelea kuwa mtu mwenye maisha ya faragha zaidi ikilinganishwa na mume wake ambaye alikuwa akishiriki sehemu kubwa ya maisha yake kwenye mitandao ya kijamii.
Chivayo alikuwa akimzungumzia Lulu hadharani kama mke wake na mara kadhaa alichapisha picha zao pamoja.
Taarifa zilizopo pia zinaonyesha kwamba watoto wawili wa Chivayo walikuwa kutoka katika uhusiano wake wa awali na Sonja Madzikanda. Hakuna ushahidi wa kuaminika nilioupata unaothibitisha kwamba Chivayo na Lulu walikuwa wamepata mtoto pamoja.
SAFARI YAO ILIISHIA PAMOJA
Kwa kusikitisha, ndoa ya Chivayo na Lulu haikudumu kwa muda mrefu.
Mnamo Septemba 30, 2026, wawili hao walikuwa pamoja katika helikopta iliyokuwa ikisafiri katika eneo la Marondera, Mashonaland East, Zimbabwe. Helikopta hiyo ilianguka na kusababisha vifo vya watu wote waliokuwa ndani yake.
Familia ya Chivayo ilithibitisha kwamba Wicknell na mke wake, Lucy “Lulu” Muteke, walikuwa miongoni mwa waliofariki. Mamlaka za Zimbabwe pia zilithibitisha kwamba hakukuwa na manusura katika ajali hiyo.
URITHI WA MAISHA YAKE YA FAMILIA
Historia ya ndoa ya Wicknell Chivayo inaonyesha vipindi viwili tofauti vya maisha yake binafsi. Ndoa yake ya kwanza na Sonja Madzikanda ilidumu kwa miaka kadhaa na kuzaa watoto wawili, lakini baadaye iliishia katika talaka na mfululizo wa migogoro ya kisheria kuhusu watoto na mali.
Ndoa yake ya pili na Lucy “Lulu” Muteke ilianza kwa sherehe kubwa mwaka 2025 na kuwa sehemu ya maisha yake ya hadharani hadi siku ya mwisho ya maisha yake.
Kwa upande wa Lulu, yeye ndiye aliyekuwa mke wa Chivayo wakati alipofariki, huku familia yake ikithibitisha pamoja na kifo cha mfanyabiashara huyo katika ajali ya helikopta.
BIASHARA ZAKE HAZIKUISHIA KWENYE NISHATI
Mbali na Intratrek, taarifa za biashara zinazohusishwa na Chivayo zinaonyesha maslahi katika sekta mbalimbali, zikiwemo mawasiliano, mafuta, usafirishaji na miundombinu.
Kupanuka kwa shughuli zake katika sekta mbalimbali kulimfanya kuwa mmoja wa wafanyabiashara waliokuwa na ushawishi mkubwa katika biashara nchini Zimbabwe na katika baadhi ya masoko ya Afrika.
Wakati huohuo, uhusiano wake wa karibu na baadhi ya viongozi wakuu wa Afrika uliendelea kuongeza umaarufu wake. Alionekana mara kadhaa akiwa na viongozi kama Rais William Ruto wa Kenya, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
UTAJIRI WA WICKNELL CHIVAYO
Swali ambalo limekuwa likiulizwa mara kwa mara ni: Wicknell Chivayo alikuwa na utajiri wa kiasi gani?
Jibu sahihi ni kwamba hakuna takwimu huru, zilizokaguliwa na kuthibitisha thamani halisi ya utajiri wake binafsi. Hivyo, namba mbalimbali za net worth zinazotajwa kwenye mitandao zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari. Taarifa za hivi karibuni za uchambuzi wa utajiri wake pia zinaonya kwamba hakuna takwimu iliyothibitishwa kwa uhuru inayoweka thamani kamili ya mali zake binafsi.
Hata hivyo, ukubwa wa mali na matumizi yake ulitoa picha ya kiwango kikubwa cha utajiri aliokuwa akionyesha hadharani.
Mwaka 2026, Chivayo alitangaza kununua na kuandaa nyumba ya kifahari huko Cape Town, Afrika Kusini, akisema gharama ya jumla ya nyumba hiyo pamoja na mapambo na uwekezaji wa ndani ilikuwa takribani rand milioni 160, sawa na takribani dola milioni 9–10 kulingana na viwango vya ubadilishaji vilivyotumika na vyanzo mbalimbali.
Katika maelezo yake kuhusu nyumba hiyo, Chivayo alisema nyumba yenyewe ilinunuliwa kwa bei ya karibu rand milioni 110 na baadaye akawekeza zaidi katika ukarabati, vifaa vya ndani na samani, jambo alilosema lilifikisha gharama yote karibu rand milioni 160.
Pia alihusishwa na mali nyingine za kifahari, ikiwemo nyumba kubwa nchini Zimbabwe na ndege binafsi, huku matumizi yake ya magari ya kifahari yakimfanya kuwa maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii.
MAISHA YA KIFAHARI NA UTOAJI WA MISAADA
Chivayo alikuwa akitumia mitandao ya kijamii kuonyesha sehemu ya maisha yake ya kifahari, safari, magari na mali zake.
Lakini umaarufu wake haukutokana na mali pekee. Alijulikana pia kwa kutoa zawadi na fedha kwa watu mbalimbali, wakiwemo wanamichezo, viongozi wa dini, wasanii na watu wengine waliokuwa wakimfuatilia kwenye mitandao ya kijamii.
Associated Press iliripoti kwamba alikuwa akijulikana kwa kutoa magari na fedha zenye thamani kubwa, huku pia akihusishwa na michango kwa taasisi mbalimbali.
UMAARUFU, SIASA NA UTATA
Kadiri utajiri wake ulivyoongezeka, ndivyo jina lake lilivyozidi kuhusishwa na mjadala kuhusu uhusiano kati ya biashara, serikali na siasa nchini Zimbabwe.
Chivayo alikuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, na alionekana mara kwa mara katika matukio pamoja na viongozi wa kisiasa barani Afrika. Vyombo vya habari pia viliripoti kuhusu maswali na tuhuma zilizowahi kuibuliwa kuhusu baadhi ya mikataba ya serikali na ufadhili wa shughuli za kisiasa; Chivayo alikanusha makosa katika masuala hayo.
Kwa hiyo, simulizi kuhusu maisha yake linabeba pande mbili: upande mmoja ni safari yake ya kutoka mazingira magumu hadi kuwa mfanyabiashara mkubwa; upande mwingine ni mjadala uliofuata kuhusu mikataba yake, mahusiano yake na mamlaka pamoja na namna alivyopata na kutumia utajiri wake.
KIFO CHA GHAFULA
Safari ya Chivayo ilifikia mwisho ghafla tarehe 30 Septemba 2026, baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Marondera, Mashonaland East, kusini-mashariki mwa Harare.
Mamlaka zilisema watu sita walikuwa ndani ya helikopta hiyo na hakukuwa na manusura. Familia baadaye ilithibitisha kwamba Chivayo na mke wake, Lucy Muteke, walikuwa miongoni mwa waliofariki.
Chanzo cha ajali hiyo bado kilikuwa kikichunguzwa na mamlaka wakati taarifa hizo zikitolewa.
URITHI WA WICKNELL CHIVAYO
Wicknell Chivayo anaacha nyuma historia ya maisha yenye sura nyingi kutoka kijana aliyeacha shule kutokana na changamoto za kifedha hadi kuwa mfanyabiashara aliyekuwa akihusishwa na miradi ya mabilioni ya rand na dola, mali za kifahari na mitandao ya watu wenye ushawishi barani Afrika.
Ingawa thamani halisi ya utajiri wake binafsi haijathibitishwa kwa uhuru, mali na shughuli za biashara zilizoripotiwa zinaonyesha ukubwa wa himaya aliyokuwa ameijenga.
Kifo chake kimeacha maswali kuhusu mustakabali wa biashara na miradi iliyokuwa ikiendelea chini ya kampuni zake, huku hasa Gwanda Solar Project ikiwa miongoni mwa miradi iliyokuwa ikitarajiwa kuendelea baada ya kurejeshwa kwake kwenye hatua ya utekelezaji.
ARUSHA: WAFANYABIASHARA wa bidhaa za asili jijini Arusha wameeleza kuwa ujio wa wajumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ni fursa kubwa ya kutangaza na kuuza bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Mfanyabiashara wa bidhaa za asili, Happy Mlinga, amesema leo kuwa ujio wa wageni hao umeongeza matumaini kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na bidhaa za utamaduni na sanaa za Tanzania.
Amesema wafanyabiashara hao wana bidhaa mbalimbali zikiwemo mavazi, mashati, bidhaa za ngozi, kazi za mikono pamoja na sanaa zinazobeba utamaduni wa Tanzania.
“Tunashukuru sana kwa ugeni huu mkubwa tunaouona. Tunaamini ni fursa kwetu kwa sababu tuna bidhaa nzuri, zikiwemo maguni, mashati, bidhaa za asili na kazi mbalimbali za mikono,” amesema Mlinga.
Alisema wageni wanaofika nchini wanapaswa kutumia fursa hiyo kutembelea maeneo yanayouza bidhaa za asili ili kujionea ubora wa bidhaa zinazotengenezwa na Watanzania
Mlinga amesema bidhaa hizo ni sehemu ya utambulisho wa Tanzania na kwamba ununuzi wake unasaidia kuongeza kipato kwa wafanyabiashara na wasanii wanaozalisha bidhaa hizo.
“Karibuni sana muone bidhaa za Tanzania. Hizi ni bidhaa halisi na original, tunawaomba wageni wasikose fursa ya kuziona na kununua bidhaa zetu,” amesema
Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika Jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9 huku ukiwakutanisha wabunge na viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani, hali inayotarajiwa kuongeza fursa za biashara, utalii na kutangaza bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na taasisi za dini nchini katika kutekeleza majukumu yao ya kiroho na kijamii kwa ajili ya ustawi wa Watanzania.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo (Jumapili, Oktoba 4, 2026) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu kwa Kasisi Kanoni Charles Mika Lundu kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Handeni, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme, Chanika, mkoani Tanga.
“Ni azma ya Serikali inayoongozwa na Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuimarisha ushirikiano na madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini,” amesema.
Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kuimarisha ushirikiano huo, ikiwemo kubadilisha sheria ili kurahisisha taasisi za dini kupata hadhi ya taasisi za hisani, kushughulikia madeni ya kodi yaliyokuwa yakizisumbua taasisi hizo na kutoa misamaha ya kodi kwa baadhi ya huduma zinazotolewa na taasisi za dini.
“Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi zetu hizi za dini,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea pia kushirikiana na taasisi za dini katika kugharamia sehemu ya gharama za baadhi ya huduma zinazotolewa na taasisi hizo, akisisitiza kuwa milango ya Serikali iko wazi kwa taasisi za dini.
Dkt. Mwigulu pia amewataka wazazi na taasisi za dini kuimarisha malezi ya watoto wa kike na wa kiume, akisema watoto wote wanakabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa familia, jamii na taasisi za dini.
“Kanisa pamoja na wazazi kwa sasa tuweke nguvu sawasawa kwa watoto wote wakike na wakiume kwa sababu kwa sasa wote wako hatarini,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amempongeza Askofu Charles Mika Lundu kwa kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Handeni, akisema anaamini ataendelea kulitumikia Kanisa na jamii kwa uadilifu.
Aidha, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuiombea Tanzania ili amani, utulivu, mshikamano na umoja viendelee kudumu.
“Wanufaika wa amani ni Watanzania wote. Wanufaika wa amani sio Serikali pekee yake. Wanufaika wa amani sio vyama vya siasa pekee yake. Wanufaika wa amani ni Watanzania wote,” amesema.
Dkt. Mwigulu, ambaye leo pia amesimikwa rasmi kuwa Kanoni Mlei wa Kanisa Anglikana Tanzania, alitunukiwa cheo hicho Juni 21, 2026, katika Harambee ya kukamilisha mradi wa jengo la Kitega Uchumi cha Kanisa Anglikana Tanzania, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo la Dodoma.