CHONGOLO AITAKA TOSCI KURATIBU BEI ZA MBEGU NCHINI

Na Matukio daima App 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, ameiagiza Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kuhakikisha inaratibu na kusimamia bei za mbegu nchini ili kuwawezesha wakulima kupata taarifa sahihi za bei na kununua mbegu bora kwa bei zinazozingatia taratibu zilizowekwa.

Chongolo ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha wadau wa tasnia ya mbegu akisema mbegu ni miongoni mwa pembejeo muhimu katika uzalishaji wa mazao, hivyo kuna umuhimu wa kuwepo kwa mfumo utakaomwezesha mkulima kufahamu bei ya mbegu kabla ya kufanya manunuzi.

Amesema TOSCI, kwa nafasi yake ya kusimamia ubora wa mbegu nchini, inapaswa pia kuhakikisha kampuni zia mbegu zinasambaza na kuuza mbegu kwa ushindani kwa bei ambazo TOSCI itazisimamia.

“Tumekuwa na utaratibu kwenye mbolea ambapo TFRA ndiyo inayoratibu na kusimamia bei za mbolea”. Mbegu nazo ni pembejeo za kilimo, hivyo hapa TOSCI ina wajibu wa kuratibu,” amesema Mheshimiwa Chongolo.

Aidha, amezitaka kampuni za mbegu kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima kwa wakati kupitia mawakala wanaokidhi vigezo, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini. Amesema Tanzania ina ardhi na mazingira bora yanayowezesha kuongeza uzalishaji wa mbegu ndani ya nchi na hivyo kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.

 

Waziri Mkuu Mwigulu kumwakilisha Rais Samia katika Mkutano wa Afya Moja Italia

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameondoka nchini leo Jumamosi, Septemba 19, 2026, kuelekea Roma, Italia, kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya Moja (One Health) na Mifumo ya Chakula na Kilimo.

Mkutano huo utafanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, kuanzia Septemba 21 hadi 23, 2026.

Mkutano huo unalenga kuimarisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, inayotambua uhusiano uliopo kati ya afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira, kwa lengo la kujenga mifumo endelevu ya chakula na kilimo.

Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi na Serikali, wakiwemo Marais kati ya watano hadi saba, Mawaziri kati ya 30 hadi 50, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni namna ya kuingiza dhana ya Afya Moja katika sera na uwekezaji wa mifumo ya chakula na kilimo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za kilimo, mazingira, afya, fedha na mipango miji.

Aidha, mkutano huo utajadili ukuzaji wa ubunifu, sayansi na maarifa ya ndani kwa ajili ya kuboresha uzuiaji wa vihatarishi, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali.

Pia, washiriki watajadili namna ya kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano ili kutafsiri ahadi zilizotolewa kuwa hatua madhubuti zenye matokeo yanayoweza kupimika.

Waziri Katambi Atoa Ufafanuzi kuhusu Mfumo wa Alama za leseni

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, amesema Serikali imeanza kufanya majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva kwa lengo la kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kupunguza ajali nchini.

Akizungumza kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 19, 2026, Waziri Katambi amesema mfumo huo unatokana na Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, ambazo zilirekebishwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, Waziri mwenye mamlaka ya kutunga kanuni kuhusu masuala ya usalama barabarani anaweza kuweka mfumo wa kupunguza vifo na ajali zinazotokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makosa yanayofanywa na madereva wa vyombo vya usafiri.

Serikali imeeleza kuwa imefanya kazi ya muda mrefu na imejiridhisha kuwa hakuna haja ya kuanza kutumia mfumo huo madhubuti wa kudhibiti usalama barabarani.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa pamoja na miradi ya usalama barabarani inayoendelea, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kamera za barabarani zenye uwezo wa kutumia akili unde (AI), imeanza majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mfumo huo bado haujaanza kutumika rasmi, bali hatua ya sasa ni kufanya majaribio ili kubaini namna utakavyoweza kutumika kudhibiti madereva watakaokiuka Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani.

Serikali imeonya madereva kuwa leseni zao zikiingizwa kwenye mfumo huo, alama zitakazotolewa kutokana na makosa ya barabarani zinaweza kuathiri uhalali wa leseni zao iwapo wataendelea kukiuka sheria.

Waziri Katambi amesema baadhi ya alama zinazoweza kuhusishwa na makosa ya barabarani ni pamoja na makosa ya mwendokasi, kutofuata alama za barabarani, kuzidisha abiria, kutoa mikanda, kuendesha vyombo hatarishi na makosa mengine kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi, akieleza kuwa matumizi ya mifumo kama hiyo yamekuwa yakiongezeka katika nchi mbalimbali.

Ametolea mfano Rwanda, ambayo amesema imetumia mfumo huo na kuona kupungua kwa kiwango kikubwa cha ajali na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Waziri Katambi pia amesisitiza kuwa Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, zilizorekebishwa mwaka 2025, bado hazijaanza kutekelezwa rasmi.

Amesema sababu mojawapo ya kutocheleweshwa kwa utekelezaji wake ni kuwa wataalamu wa mifumo kutoka Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato wanaendelea kuunganisha mifumo hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Waziri, ni kwamba Serikali iko katika kipindi cha utoaji elimu kwa umma kuhusu kanuni hizo. Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya madereva wa vyombo vya moto pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu mfumo huo na umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Waziri amesema Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kufikisha elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya madereva kupitia mikutano ya uelimishaji, pamoja na vyombo vya habari kama redio na Runinga, katika vituo vya mabasi, maeneo ya maegesho ya malori, mikusanyiko ya watu na maeneo mengine.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu makosa yanayoweza kupewa alama na namna alama hizo zitakavyotumika.

Waziri Katambi amesisitiza kuwa mfumo huo bado haujaanza kutekelezwa rasmi, hivyo hakuna haja ya dereva ambaye leseni yake imeondolewa alama kutokana na kosa la barabarani kuwa na wasiwasi kwa sasa.

Amesema madereva watajulishwa rasmi pindi mfumo huo utakapoanza kutumika.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, Septemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam.

Chalamila Aagiza Familia ya Mushi Itafutwe, Ikamatwe – Video

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitwinkwi, kuhakikisha wanafamilia ya David Mushi wanatafutwa na kukamatwa baada ya kutofika kwenye mkutano aliouitisha Septemba 19, 2026, kwa ajili ya kujadili mgogoro wa ardhi uliopo Mtaa wa Madale, Kata ya Wazo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Nipashe, Chalamila amesema aliwaita wanafamilia hao kwa lengo la kuzungumza nao na kutafuta namna ya kumaliza mgogoro huo kwa amani, akisisitiza kuwa Serikali haikulenga kutengua uamuzi wa Mahakama.

Amesema kutofika kwa familia hiyo katika mkutano huo, licha ya kuitwa, amekitafsiri kama dharau kwa Serikali, huku akimtaka Kamanda wa Polisi kuwatafuta na kuwahifadhi kituoni.

Chalamila amesema mgogoro huo unahusisha familia za Abdallah Kitwanga na David Mushi, ambapo Mahakama imewahi kutoa maamuzi katika vipindi tofauti. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano huo, uamuzi wa mwaka 2022 uliipa ushindi familia ya Mushi.

Mgogoro huo unahusu eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 10 katika Mtaa wa Madale, huku taarifa zikieleza kuwa kati ya kaya 13 na 15 zimehusishwa na eneo hilo.

Wakati huo huo, wawakilishi wa familia ya Mushi wamesema walinunua maeneo hayo kwa kufuata taratibu, lakini tangu Septemba 3, 2026 baadhi ya wakazi wamezuiwa kuingia katika nyumba zao na kulazimika kuishi katika mahema.

Chalamila amewataka wahusika kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhisho la mgogoro huo, huku akisisitiza kuwa matumizi ya mabango katika eneo hilo yanaweza kuongeza taharuki.

WAJASIRIAMALI WADOGO WAFAIDIKA USHIRIKI WA TBS MAONESHO YA MADINI NA FURSA ZA UWEKEZAJI LINDI 2026.

 Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuwa karibu na wajasiriamali wadogo nchini kwa kutoa elimu kuhusu viwango na ubora wa bidhaa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kuzalisha bidhaa salama, zenye ubora na zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

TBS imetoa elimu hiyo katika Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Lindi 2026, yanayofanyika Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi, ambapo wadau mbalimbali wamepata fursa ya kujifunza kuhusu viwango, taratibu za ubora wa bidhaa pamoja na umuhimu wa kuzingatia matakwa ya viwango katika uzalishaji na biashara.

Akizungumza katika maonesho hayo, Eng. Hemedy Hamim, Mkaguzi wa TBS Kanda ya Kusini, amesema TBS imeendelea kuwafikia wajasiriamali wadogo kwa kuwapatia elimu inayolenga kuwawezesha kuboresha bidhaa zao na kuingia katika masoko yenye ushindani.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, TBS imewatembelea na kuwapatia elimu wajasiriamali wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za korosho, mafuta ya mwani, sabuni za mwani pamoja na Shower Jelly zinazotokana na mwani, huku ikiwahamasisha kuzingatia viwango vya ubora katika uzalishaji wao.

Eng. Hemedy amesema elimu hiyo pia inalenga kuwawezesha wajasiriamali kuelewa taratibu za kupata Alama ya Ubora ya TBS, ambayo ni muhimu katika kujenga uaminifu wa bidhaa kwa watumiaji na kuongeza uwezo wa bidhaa kufikia masoko mbalimbali.

TBS imeeleza kuwa kwa wajasiriamali wadogo, upatikanaji wa Alama ya Ubora unatolewa bila malipo, jambo linalolenga kuwawezesha wafanyabiashara hao wadogo kupata huduma za viwango na kuimarisha ubora wa bidhaa zao.

Katika kuwafikia kwa urahisi zaidi wajasiriamali hao, TBS imeshirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), ambapo ushirikiano huo umewezesha elimu ya viwango kuwafikia wajasiriamali wadogo wanaozalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo zile zinazotokana na mazao yanayopatikana katika maeneo yao.

TBS imewasisitiza wajasiriamali kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha bidhaa zao zinafuata taratibu zinazotakiwa na kupata Alama ya Ubora, kwani hatua hiyo inaweza kuongeza uaminifu wa bidhaa kwa walaji na kuwawezesha kutafuta fursa za masoko mapana zaidi.

Mmoja wa wajasiriamali walionufaika na elimu na huduma za TBS ni Bi. Zena Adam, mbanguaji wa korosho kutoka Nachingwea, ambaye baada ya kufuata taratibu zilizowekwa na TBS alifanikiwa kupata Alama ya Ubora kwa bidhaa yake.

Bi. Zena ameishukuru TBS kwa elimu na maelekezo aliyopatiwa katika hatua mbalimbali, akieleza kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa umuhimu wa ubora na taratibu zinazotakiwa katika uzalishaji.

Kwa mujibu wa Bi. Zena, kupata Alama ya Ubora ya TBS ni hatua muhimu kwake kama mjasiriamali, kwani anaamini itasaidia kuongeza uaminifu wa bidhaa zake na kumfungulia fursa za masoko kutoka nje ya Mkoa wa Lindi hadi katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wake, Bi. Fatma Machalila, ambaye ni miongoni mwa wajasiriamali walionufaika na elimu hiyo, ameipongeza TBS kwa kuendelea kuwafikia wajasiriamali wadogo na kutoa elimu kuhusu uzalishaji wa bidhaa bora.

Bi. Fatma ameomba TBS iendelee na programu za elimu kama hiyo, hususan katika maeneo ya vijijini, ili wajasiriamali wengi zaidi waweze kupata uelewa wa viwango na kuzalisha bidhaa bora na salama.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa sababu inawasaidia wajasiriamali kuelewa namna ya kuboresha bidhaa zao, kulinda afya na usalama wa wananchi, pamoja na kukuza biashara zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Lindi 2026 umeendelea kuonyesha umuhimu wa taasisi hiyo kuwa karibu na wazalishaji na wajasiriamali, si kwa kutoa huduma za viwango pekee, bali pia kwa kutoa elimu inayowawezesha kuelewa namna ubora unavyoweza kuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa biashara zao.

Kwa wajasiriamali wadogo wanaozalisha bidhaa za korosho, mwani na bidhaa nyingine, elimu hiyo inatoa fursa ya kuelewa kwamba ubora wa bidhaa ni zaidi ya mahitaji ya kisheria; ni sehemu ya kujenga uaminifu wa mlaji, kuongeza ushindani wa bidhaa na kufungua milango ya masoko mapana zaidi.

Waziri Mkuu Afunga Mkutano wa Makambi ya Waadventista Kinyerezi

Global Publishers
September 19, 2026
6 views
0 Comments


Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba leo (Jumamosi, Septemba 19, 2026) ameshiriki Ibada Kuu na Kufunga Mkutano wa Makambi ya Kanisa la Waadventista Sabato, yaliyofanyika kwa siku saba, Kinyerezi jijini Dar es Salaam

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo Dkt. Mwigulu amewasihi waumini wa kanisa hilo kuendelea kudumisha amani na kusimamia maadili ya watoto huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda uhuru wa wananchi kuabudu kwa kadri ya imani zao.

Trump Awapiga Marufuku CNN, MS NOW na Politico Ikulu ya Marekani

Washington, D.C. — Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kuwa waandishi wa habari kutoka vyombo vya CNN, MS NOW na Politico wamepigwa marufuku kuingia Ikulu ya Marekani, huku akionya kuwa vyombo vingine vya habari vinaweza kufuatia.

Trump alitoa tangazo hilo kupitia mtandao wake wa Truth Social Ijumaa, Septemba 18, 2026. Alivituhumu vyombo hivyo kwa kile alichokiita kuripoti habari za uongo na taarifa zisizo za kweli kuhusu yeye, utawala wake na Marekani.

Trump aliandika kuwa vyombo vya habari havipaswi kuruhusiwa “kuandika au kuripoti habari za kubuni na uongo” vinapomzungumzia Rais wa Marekani au utawala wake. Pia aliongeza kuwa “vyombo vingine vya habari vya uongo” vinaweza kufuatia.

Haikufahamika mara moja kwa nini Trump alivichagua CNN, MS NOW na Politico pekee. Vyombo hivyo pia havikuwa vimetolewa maelezo ya kina kuhusu sababu maalumu za kuchukuliwa hatua hiyo.

Baada ya tangazo hilo, Brian Stelter, mchambuzi mkuu wa masuala ya vyombo vya habari wa CNN, alisema kwenye televisheni kuwa bado haikuwa wazi kama marufuku hiyo ilikuwa imetekelezwa kikamilifu.

CNN, kwa upande wake, ilisema inasimama nyuma ya timu yake ya waandishi wa habari walioko Ikulu na kwamba inaamini wana haki ya kikatiba ya kufanya kazi zao bila kuingiliwa na serikali.

Katika mahojiano yaliyofuata katika Ikulu, mwandishi alimuuliza Trump jinsi anavyoweza kuendana na Katiba ya Marekani, hasa kifungu cha Kwanza kinacholinda uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Trump alijibu kuwa anaiheshimu Katiba, huku akiendelea kuvikosoa vyombo hivyo na kuvishutumu kwa kuwa na taarifa anazoziita za uongo.

Trump alisema Marekani inahitaji habari za “uaminifu, haki na ukweli,” na akasisitiza kuwa nchi inahitaji pia vyombo vya habari vilivyo huru na vya haki.

Hatua hiyo imezua mjadala kuhusu uhusiano kati ya Ikulu ya Marekani na vyombo vya habari, pamoja na mipaka ya mamlaka ya serikali katika kuwapatia waandishi wa habari fursa ya kufikia rais na shughuli za Ikulu.

Katika kipindi chake cha pili madarakani, Trump amekuwa akikosoa mara kwa mara waandishi na vyombo vya habari vinavyoripoti kuhusu utawala wake kwa namna asiyoikubali.

Utawala wake pia umewahi kuchukua hatua zinazowazuia au kuwabana baadhi ya waandishi wa habari, huku kukiwa na mijadala na kesi za kisheria kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na haki ya serikali kudhibiti upatikanaji wa maeneo ya serikali.

Suala kubwa linalotarajiwa kujadiliwa kisheria ni iwapo serikali inaweza kuzuia chombo cha habari kupata fursa ya kuripoti kutoka Ikulu kwa sababu ya mtazamo au maudhui ya taarifa zake. Uamuzi wa mwisho kuhusu uhalali wa hatua hiyo unaweza kutegemea mahakama.

Serikali Yatoa Tahadhari Athari za El Niño Katika Mvua Za Vuli

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa athari zinazohusishwa na hali ya El Niño katika kipindi cha mvua za Vuli za miezi ya Oktoba hadi Desemba 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo, tarehe 18 Agosti 2026, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba–Desemba 2026), ambao unaashiria kuwepo kwa viwango vikubwa vya hali ya El Niño kwenye eneo kubwa la Bahari ya Pasifiki.

Hali hiyo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua za Vuli za mwaka 2026 kuwa juu ya wastani katika baadhi ya maeneo nchini.

Wizara imesema baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali hiyo ni pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, kujaa kwa mito na mifereji, uharibifu wa miundombinu ya barabara, reli, madaraja na majengo, pamoja na uharibifu wa mali na mazao.

Aidha, imeonya kuwa kuna uwezekano wa kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

Kutokana na hali hiyo, Wizara imetoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.

Maafisa hao wametakiwa pia kuwatambua wananchi walio katika mazingira hatarishi, hususan watoto, wazee na watu wenye ulemavu, pamoja na kufanya maandalizi ya utoaji wa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa wananchi watakaoathiriwa na mvua hizo.

Kwa upande wa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla, Wizara imewataka kuchukua tahadhari mapema kwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, kuepuka kuvuka mito au maeneo yaliyofunikwa na maji na kutoa usaidizi kwa watu wenye ulemavu na wazee wasiojiweza.

Wananchi pia wametakiwa kutoruhusu watoto kucheza karibu na mifereji, mitaro, mito, makalavati, madaraja na maeneo ambayo maji yanapita kwa kasi.

Aidha, wametakiwa kusafisha mitaro na mifereji ya kupitisha maji ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, pamoja na kuhakikisha wanapata maji salama ya kunywa na kupikia wakati wote.

Wizara imewataka pia wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni, karibu na mito na maeneo yenye historia ya mafuriko au maporomoko ya ardhi kuwa waangalifu zaidi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, ikiwemo kuhama mapema endapo wataelekezwa kufanya hivyo.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Charles F. Komba, Septemba 19, 2026.

Iran Yamnyonga Mtu Aliyetiwa Hatiani kwa Ujasusi wa Mossad

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

Tehran, Iran — Iran imetekeleza hukumu ya kifo dhidi ya Hoseyn Paderan, aliyepatikana na hatia ya kufanya ujasusi na kushirikiana na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti.

Hukumu hiyo ilitekelezwa baada ya rufaa ya Paderan kukataliwa na Mahakama ya Juu ya Iran kuthibitisha hukumu hiyo.

Kwa mujibu wa mahakama ya Iran, Paderan alikamatwa kwa tuhuma za kuipa Mossad taarifa za siri zinazohusiana na masuala ya kijeshi.

Mamlaka zilidai kuwa alikusanya taarifa kuhusu vituo vya kijeshi na maafisa wa kijeshi, ikiwemo baadhi ya taarifa zao binafsi, kisha kuzifikisha kwa mtu aliyekuwa akimshughulikia upande wa Mossad.

Mahakama pia ilidai kuwa Paderan alipokea malipo kwa njia ya fedha za Euro kwa ajili ya taarifa alizokuwa akitoa.

Mamlaka zilisema katika upekuzi wa nyumba yake vilipatikana vitu mbalimbali, ikiwemo daftari lenye taarifa zinazohusiana na makombora lililowekwa alama ya “siri ya juu”, vifaa vya kuhifadhi taarifa vilivyosimbwa kwa njia fiche, vifaa vya mawasiliano pamoja na vifaa vya kupiga picha na video.

Iran imekuwa ikichukua hatua kali dhidi ya watu wanaowatuhumu kwa kufanya ujasusi kwa niaba ya Israel, hasa katika kipindi ambacho mvutano kati ya Tehran na Tel Aviv umeendelea kuwa mkubwa.

MAKAMU WA RAIS AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA MTO NG’OMBE, AAGIZA TAKA ZIONDOLEWE HARAKA*

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amefanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Mto Ng’ombe, Tandale jijini Dar es Salaam, kukagua hali ya usafi wa mazingira na maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi cha mvua.

 

Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Waziri wa TAMISEMI pamoja na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Ndejembi ameelekeza Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha mto huo unasafishwa na taka zilizorundikana kandokando ya Mto Ng’ombe zinaondolewa haraka na mazingira yanaendelea kuwekwa katika hali ya usafi.

 

Amewaagiza Viongozi wa Halmshauri, kupitia maafisa mazingira na maafisa maendeleo, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuzingatia usafi na ukusanyaji wa taka. Amesema ni muhimu kwa Halmashauri kuweka miundombinu mizuri ya kukusanya taka na kuzichukua kwa wakati ili wananchi wasitupe taka hizo katika maeneo yasiyofaa.

 

Vilevile, ameelekeza mamlaka za Wilaya ya Kinondoni kuweka utaratibu wa maeneo rasmi ya kutupa taka ili wananchi wawe na sehemu zinazotambulika kwa ajili ya kuhifadhi taka, hatua itakayosaidia kudhibiti utupaji holela na uchafuzi wa mazingira.

 

Akizungumza na wananchi wanaoishi pembezoni mwa Mto Ng’ombe, Makamu wa Rais amewataka kuzingatia usafi wa mazingira na kubadili tabia ya utupaji taka holela, akisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unahitaji ushiriki wa Serikali na wananchi kwa pamoja.

 

Aidha, Makamu wa Rais ameelekeza madaraja yanayokatiza maeneo ya Pakacha na Sokoni katika Mto Kiboko yanapitika wakati wa mvua, ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila kukwamishwa na changamoto za miundombinu.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

19 Septemba 2026

Dar es Salaam.