BARABARA YA BARIADI–SINGIDA IJENGWE KWA LAMI : WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, kuhakikisha barabara inayounganisha Bariadi mkoani Simiyu na Singida inajengwa kwa kiwango cha lami ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwandoya, eneo la Kisesa, Wilayani Meatu, mkoani Simiyu, Dkt. Nchemba amemtaka Waziri wa Ujenzi kusimamia wataalamu wake kuhakikisha upembuzi yakinifu wa barabara hiyo unakamilika haraka, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha.

“Barabara hii si ya wana Mwandoya tu, bali hata Mkoa wa Mara wanaitaka, kwani ni njia fupi kuelekea makao makuu ya nchi. Pia, mkoa huu ni wa uzalishaji, hivyo barabara hii ni ya kiuchumi na ni muhimu,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amewaeleza wananchi wa Mwandoya kuwa Serikali imeanza kushughulikia utekelezaji wa ujenzi wa barabara inayotoka Salama (Magu)–Bariadi–Itilima–Mwandoya–Karatu–Hydom–Guguti–Sibiti–Mwanhuzi–Lalago hadi Maswa, kupitia makutano ya Isengwa.

Amefafanua kuwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo umeanza katika baadhi ya vipande vilivyopo mkoani Manyara, ambapo barabara ya Mbulu–Gababi yenye urefu wa kilometa 25 imefikia asilimia 52 ya utekelezaji, huku kipande cha Labay–Hydom chenye urefu wa kilometa 25 kikiwa kimefikia asilimia 25.

Amesema barabara hiyo ni muhimu kiuchumi kwa kuwa inaunganisha Kanda tatu za maendeleo, ambazo ni Kanda ya Ziwa kupitia Mkoa wa Simiyu, Kanda ya Kati kupitia Mkoa wa Singida na Kanda ya Kaskazini kupitia mikoa ya Manyara na Arusha.

Kuhusu barabara za Nyashimo–Ndutwa na Mwandoya–Isengwa Waziri Kadogosa amesema atahakikisha upembuzi yakinifu unakamilika haraka ili barabara hizo ziweze kuingizwa katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amesema mkoa huo unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kusisitiza kuwa wananchi wa Simiyu wanahitaji barabara zitakazounganisha mkoa huo na Mwanza pamoja na mikoa jirani huku akiomba kipaumbele kitolewe katika ujenzi wa barabara ya Bariadi–Magu yenye urefu wa kilometa 78.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Musa Mbuga, alimweleza Waziri Mkuu kuwa wananchi wa eneo hilo wana kiu ya kupata barabara ya Bariadi–Itilima–Mwandoya–Meatu kwa kiwango cha lami ili kufungua fursa za utalii na biashara pamoja na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji mkoani Simiyu.