Tanzania, Italia zaimarisha ushirikiano kimahakama – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sant’Anna School of Advanced Studies (Scuola) cha Italia, kinaendesha mafunzo maalumu kwa Mahakimu Wakazi na Waendesha Mashtaka kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa kushughulikia kwa ufanisi mashauri ya uhalifu unaohusu wanyamapori na maliasili.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefunguliwa Septemba 21, 2026 na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Coppola, kwa njia ya mtandao. Mafunzo hayo yanafadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia.

Wawezeshaji kutoka Italia na Tanzania wanawapatia washiriki maarifa, mbinu na uzoefu kuhusu namna ya kuchunguza, kuendesha na kutoa maamuzi katika mashauri ya uhalifu wa wanyamapori na maliasili, ikizingatiwa kuwa aina hiyo ya uhalifu mara nyingi huhusisha makosa yanayovuka mipaka.

Akifungua mafunzo hayo, Balozi Coppola amesema yana umuhimu mkubwa kutokana na kuongezeka kwa uhalifu dhidi ya wanyamapori na maliasili ambao, kwa mujibu wake, unaendelea kuwa changamoto inayovuka mipaka ya nchi.

Amesema hali hiyo inahitaji kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimahakama baina ya Tanzania na Italia, huku akiahidi kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kubadilishana uzoefu, utaalamu na mbinu za kukabiliana na uhalifu huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa IJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dkt. Paul Faustin Kihwelo, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa wa wanyamapori, misitu na rasilimali nyingine za asili.

Amesema hali hiyo inaifanya kuwa muhimu kuendelea kuimarisha mifumo ya kisheria pamoja na uwezo wa watendaji wa Mahakama katika kulinda rasilimali hizo dhidi ya uhalifu.

Dkt. Kihwelo amesema mafunzo hayo yanawalenga Waendesha Mashtaka na Mawakili wa Serikali kwa kuwaongezea uwezo katika kuandaa mashtaka, kuwasilisha ushahidi na kuendesha mashauri mahakamani, hususan yale yanayohusisha uhalifu unaovuka mipaka.

Kwa upande wa Mahakimu, amesema mafunzo hayo yanawalenga kuwaongezea uelewa kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza katika uamuzi wa mashauri yanayohusisha nchi zaidi ya moja, matumizi ya mbinu za kisasa pamoja na ushahidi maalumu.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kupata maarifa na ujuzi katika uchunguzi wa makosa, ukusanyaji na utunzaji wa ushahidi, uendeshaji wa mashtaka na uelewa wa mifumo ya sheria inayohusika na makosa hayo.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya IJA na Scuola katika kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama, Mawakili wa Serikali na Waendesha Mashtaka.

Mafunzo mengine katika ushirikiano huo yalifanyika Septemba 2025 na Machi 2026, yakijikita katika ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia uhalifu unaovuka mipaka.

Miongoni mwa maeneo yaliyofundishwa ni usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya, utakatishaji fedha, ugaidi, biashara haramu ya silaha, ujangili, uhalifu wa mtandaoni pamoja na makosa ya kimazingira.

 

Miili ya askari watano yaagawa Singida – HabariLeo

SINGIDA: Miili ya askari watano wa Jeshi la Polisi Tanzania waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Septemba 21, 2026, eneo la Sekenke mkoani Singida, imeagwa leo Septemba 22, 2026, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Shelui, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Zoezi la kuaga miili hiyo limehudhuriwa na viongozi wa mbalimbali wa Jeshi la Polisi, viongozi wa serikali, viongozi wa Taasisi za Kidini, Maafisa wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi wa Mkoa wa Singida, likiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego.

Viongozi mbalimbali wameendelea kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na Jeshi la Polisi Tanzania kufuatia msiba huo, huku wakitambua mchango wa askari hao katika kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Jeshi la Polisi Tanzania linaendelea kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, askari na Watanzania wote walioguswa na msiba huo, na kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani.

ASILIMIA KUBWA YA WANAWAKE WANASHIRIKI KILIMO, UFUGAJI – WAZIRI MKUU

*Asema uwekezaji ni lazima ili Afya Moja ifanikiwe katika ngazi ya jamii 

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema takribani theluthi mbili ya wanawake walioajiriwa katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo, hufanya kazi kwenye mifumo ya chakula na kilimo.

“FAO inakadiria kuwa wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 42 ya nguvu kazi katika mifumo ya chakula na kilimo duniani. Takwimu hizi zinaonyesha kwamba wanawake hawako pembezoni mwa mifumo ya chakula na kilimo; bali wako katika kiini cha mifumo hiyo,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akishiriki jopo la viongozi wa juu lililojadili Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima – Mtazamo wa Afya Moja, lililofanyika katika Kituo cha Sheikh Zayed, Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia. 

Waziri Mkuu ambaye anashikiri Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema yeye mwenyewe anatoka katika jamii ambako sehemu kubwa ya shughuli za uzalishaji, hasa za kilimo na ufugaji, hufanywa na wanawake.

“Katika jamii zetu nyingi, shughuli hizi mbili za kiuchumi zinaongozwa na wanawake, lakini mchango wao bado unakabiliwa na vikwazo, ikiwemo ukosefu wa fursa sawa ya kupata ardhi, fedha, teknolojia, huduma za ugani, masoko na kushiriki katika kufanya maamuzi,” alisema wakati akitoa mada yake kwenye jopo hilo llililowashirikisha mawaziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi kutoka Ufaransa na Ireland na kuongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Godfrey Magwenzi.

Akifafanua zaidi, Dkt. Mwigulu alisema: “FAO inakadiria kwamba hata pale wanawake wanaposimamia mashamba yenye ukubwa sawa na yale yanayosimamiwa na wanaume, tofauti ya uzalishaji kwa kila eneo la ardhi kati ya wanawake na wanaume ni takribani asilimia 24. Wanawake wanaofanya kazi katika ajira zenye malipo ndani ya mifumo ya chakula na kilimo hupata, kwa wastani, asilimia 78 ya kipato kinachopatikana kwa kila dola anayopata mwanaume.”

“Hizi si takwimu tu zinazoonyesha ukosefu wa usawa; zinawakilisha pia uzalishaji unaopotea, kipato kinachopotea na fursa zinazopotea za kujenga mifumo imara na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za chakula. Na hapo ndipo dhana ya Afya Moja inapopata umuhimu mkubwa,” alisisitiza.

Alisema mwanamke mkulima haoni afya ya binadamu, ya wanyama, ya mimea na ya mazingira kama sekta zinazojitegemea kwa kuwa analima chakula kwa ajili ya familia na jamii, anafuga mifugo, anasimamia maji na ardhi, anahifadhi na kusindika chakula, anafanya maamuzi kuhusu afya ya wanyama na lishe ya familia, na anakabiliana na ukame, mafuriko, wadudu na magonjwa.

“Kwa hiyo, maamuzi yake yanaweza kuathiri lishe, usalama wa chakula, kinga dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea, bioanuwai na uendelevu wa mazingira.”

“Kumwezesha mwanamke ni kuwekeza si katika kilimo pekee, bali pia katika Afya Moja. Ikiwa tunataka Afya Moja ifanikiwe katika ngazi ya jamii, ni lazima tuwekeze kwa wanawake ambao tayari wanaitekeleza katika maisha yao ya kila siku,” alisisitiza.

Akishiriki mjadala huo, Waziri wa Kilimo na Chakula wa Ufaransa, Bi. Annie Genevard alisema licha ya kuwa Ufaransa ni nchi inayohamasisha usawa kati ya wanaume na wanawake, bado kuna mazingira ambayo wanawake wanahisi kutoonekana.

“Robo ya mameneja wa mashamba nchini Ufaransa ni wanawake. Si jambo la kushangaza kusikia mwakilishi wa mauzo (sales representative) anapofika shambani na kumuuliza mwanamke anayemkuta: “Ningependa kumuona bosi wa hili shamba.” Nao hujibu: “Mimi ndiye bosi.”  

Amekiri kuwa, bado kuna safari ndefu ya kufikia usawa na kwamba hawawezi kujenga mifumo ya kilimo na chakula yenye ustahimilivu zaidi bila kuchukua hatua kwa wakati mmoja kupunguza ukosefu huo wa usawa.

Alisema alipoteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, aliamua kuanzisha mpango wa kuwainua wanawake kupitia mafunzo na kuongeza muonekano wao wa umiliki kwenye jamii yao. Lengo lake ni kuwasaidia zaidi wanawake wakulima katika maisha yao ya kila siku ili wapate taarifa bora kuhusu haki zao, hususan kuhusu uzazi, kuboresha huduma za kuchukua nafasi ya mkulima na kuboresha zaidi zana za kilimo ili ziendane na mahitaji yao.

“Na niseme wazi hapa kuwa hatuko katika hatua ya kutoa ahadi pekee; tayari tumeanza kuchukua hatua. Tumeanza kuwatambua wanawake katika kilimo na pia kuwawezesha kutambuliwa kama wakulima kamili. Zaidi ya hayo, tumehakikisha mpango huu unaweza kupimwa na kufuatiliwa kwa muda.  Kila hatua ina viashiria vya ufuatiliaji na matokeo.”

Naye, Waziri wa Kilimo, Chakula na Masuala ya Uvuvi wa Ireland, Martin Heydon aliwaeleza washiriki wa jopo hili kwamba kabla hajawa Waziri wa Kilimo, alikuwa mkulima katika shamba alilorithi kutoka kwa mama yake.

“Mimi na mke wangu bado tunaendesha shughuli za kilimo pamoja na watoto wetu wanne katika shamba letu. Shamba hilo nilirithi kutoka kwa mama yangu, kwa sababu baba yangu alifariki nilipokuwa na umri wa miaka minane tu,” alisema.

“Mwaka 1986 wakati baba anafariki, mama yangu alikuwa na miaka 43. Alikuwa mama na baba yetu kwa wakati mmoja. Wakati mwingine alikuwa mwalimu wetu, muuguzi wetu, lakini daima alikuwa mkulima. Alisisitiza kuendelea na shughuli za kilimo wakati akitulea. Alitaka kutujengea upendo, shauku na maarifa kuhusu uzalishaji wa chakula, kutunza wanyama, kutunza ardhi na mambo mengine yanayohusiana na kilimo.” 

Alisema kuwa, kwa uzoefu wa Ireland, wanawake wakulima, madaktari wa mifugo wanawake, wanasayansi wanawake wa kilimo na watafiti wanawake wa mimea wako katika kiini cha maeneo yote hayo lakini mara nyingi mchango wao hautambuliwi kwa kiwango kinachostahili. 

“Wanawake bado ndiyo walezi wakuu katika kaya nyingi za vijijini nchini Ireland, wakishiriki katika kupanga lishe ya familia, usalama wa chakula nyumbani na kubeba mzigo wa kiafya pale kipato cha shamba kinapokuwa hakina uhakika au majukumu yanapokutana na kazi za nje ya shamba. Mkakati wowote makini wa Afya Moja lazima uzingatie kazi hii isiyolipwa na ambayo kwa kiasi kikubwa haionekani kama sehemu ya mfumo huo,” alisema.

Alisema kizazi kipya nchini humo kinahusiana na maeneo yote hayo lakini kuna wakulima wachache sana ambao wana umri chini ya miaka 35. “Urithi wa mashamba nchini Ireland kwa muda mrefu umekuwa ukifuata utamaduni wa kumrithisha mwanaume. Tume yetu huru kuhusu kizazi kipya katika kilimo iliweka wazi kwamba kusaidia urithi wa mashamba na kuboresha usawa wa kijinsia ni jukumu moja, si mambo mawili tofauti. Binti yangu mwenye umri wa miaka mitano, ana nafasi sawa kabisa ya kurithi shamba letu kama ndugu zake watatu wa kiume,” alisisitiza.

Waziri huyo alisema anaamini kwamba ili kuwa na uendelevu wa kweli katika nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii, ni lazima kuhakikisha wanawake wanakuwa na nafasi sawa na wanaume katika mifumo ya chakula na kilimo. 

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amefuatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na watendaji wengine wa Serikali

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, 

JUMANNE, SEPTEMBA 22, 2026.

CLUB ZA MICHEZO SHIMIWI ZATAKIWA KUFANYA UTALII WA NDANI

Na Sixmund Begashe, Moshi

WANAMICHEZO  wa Club za  Wizara na Idara zinazoshiriki michezo ya SHIMIWI 2026 Mkoani Kilimanjaro, pamoja na mambo mengine,  wametakiwa kutumia fursa hiyo ya  michezo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani humo kama itakavyoainishwa kwenye ratiba. 

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) Daniel Mwalusamba, kwenye kikao maalumu kilichojumuisha viongozi wa Club hizo na wanamichezo waliowasili Wilayani  Moshi tayari kwa michuano hiyo. 

Bw. Mwalusamba amesema Mkoa wa Kilimanjaro umejaliwa kwa urithi adhimu wa vivutio vya utalii na ndiyo maana nafasi imetengwa kwa wanamichezo hao kutembelea vivutio hivyo wanapaswa kuitumia vizuri nafasi hiyo.

Amewasisitiza wanamichezo hao kutumia michezo hiyo katika  kuimarisha udugu, upendo na mshikamano kwa maslahi mapana ya taifa kwa ujumla.

Amewataka viongozi wa Club hizo kusimamia taratibu zote za kiutumishi na kuimarisha mshikamo na udugu miongoni mwa wanamichezo. 

Katika hatua nyingine, wanamichezo wa Club ya Michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wameendelea na mazoezi yao ili kujiimarisha zaidi katika michezo iliyo mbele yao.

 

TANZANIA YASISITIZA KUIMARISHA JUHUDI ZA KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO AFRIKA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za pamoja za kuokoa maisha ya kina mama, watoto wachanga, watoto na vijana barani Afrika, akieleza kuwa uwekezaji katika huduma bora za afya ni msingi muhimu wa kujenga familia zenye afya na mustakabali bora wa Bara la Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema Afrika imepiga hatua katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto, lakini mafanikio hayo yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kutokana na changamoto za upatikanaji wa rasilimali na mahitaji yanayoongezeka katika mifumo ya afya.

Mhe. Kombo ameyasema hayo tarehe 21 Septemba 2026 jijini New York, Marekani, wakati akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu ulioandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. John Dramani Mahama, pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA 81), uliokuwa na kaulimbiu “Marekebisho ya Accra: Kukamilisha Mzunguko kwa Kuhuisha Mfumo wa Maendeleo ya Kimataifa.”

Waziri Kombo amesema Afrika inaandaa Mpango wa Bara wa Kuokoa Maisha ya Mama na Mtoto, utakaoweka malengo yanayopimika na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji katika juhudi za kuboresha afya ya mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana. Kupitia kaulimbiu “Mother Africa Calls,” ametoa wito kwa Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Afrika katika kuhakikisha kuwa juhudi za kuokoa maisha zinawekewa rasilimali na kutekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Rais wa Ghana, Mhe. Mahama, amesisitiza umuhimu wa nchi za kusini (The Global South) kujenga uwezo wa ndani, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uzalishaji wa bidhaa muhimu, ikiwemo dawa.

Aidha, Rais Mahama amempongeza Rais Samia kwa uongozi wake katika Mother Africa Initiative, akisema mpango huo unaunganisha sera za umma na uwajibikaji wa sekta binafsi katika kuimarisha afya ya mama na mtoto.

 

Tanzania kupunguza utegemezi dawa kutoka nje – HabariLeo

MAREKANI: Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba ili kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje na kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika.

Mchengerwa amesema hayo leo jijini New York, Marekani, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028, ambapo aliiwakilisha Tanzania katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo.

Kikao hicho, kilichoandaliwa na Serikali ya Sierra Leone, kinafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa 81 (UNGA 81), unaofanyika New York.

Katika kikao hicho, Mchengerwa amesema Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030, unaolenga kufikia malengo ya ‘Zero Tatu’, ikiwemo kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani usio na wataalamu, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga pamoja na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

“Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero Tatu,” amesema.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuhakikisha huduma za afya zinapatikana karibu na wananchi, huku ikiimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote na upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama na mtoto.

Mchengerwa amesema Serikali pia inaendelea kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha katika kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, ufadhili wa vituo vya kutolea huduma za afya, mifumo ya malipo ya kielektroniki, tozo maalum na huduma za utalii tiba.

Amesema Serikali inaendelea kuongeza mgao wa bajeti kwa huduma za afya ya msingi pamoja na huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga.

Akizungumzia umuhimu wa uzalishaji wa ndani, Mchengerwa amesema Afrika hutumia zaidi ya dola bilioni 28 za Marekani kila mwaka kununua dawa na bidhaa za afya, huku sehemu kubwa ya mahitaji hayo ikitoka nje ya bara.

Amesema hali hiyo inaweza kuziweka nchi katika hatari ya kukumbwa na changamoto za minyororo ya usambazaji pamoja na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, Tanzania imeweka uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya, vifaa tiba na vifaa vya hospitali kuwa kipaumbele cha kitaifa, akisisitiza kuwa hatua hiyo si suala la uchumi pekee bali pia ni msingi wa kuimarisha usalama wa afya.

Amesema uzalishaji wa ndani utasaidia kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya vinaendelea kupata mahitaji muhimu hata pale kunapokuwa na changamoto katika minyororo ya usambazaji duniani.

Waziri huyo ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na washirika wa maendeleo kuunganisha nguvu katika uwekezaji wa sekta ya afya, uhamishaji wa teknolojia na sera za viwanda ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika.

Pia amesisitiza umuhimu wa kujenga minyororo ya thamani ya kikanda, kuimarisha mamlaka za udhibiti na kuunga mkono ubunifu unaozalishwa barani Afrika.

“Tanzania inaendelea kuhakikisha huduma muhimu za afya zinapatikana ndani ya umbali usiozidi kilomita tano kutoka kwa kila jamii, huku hospitali za rufaa zikitumika zaidi kwa wagonjwa wenye mahitaji ya huduma maalum,” amesema.

Mkutano wa UNGA 81 unawakutanisha wawakilishi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, ambapo viongozi hutumia jukwaa hilo kueleza misimamo na vipaumbele vyao kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo ni amani na usalama, vita na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, akili mnemba (AI), afya ya dunia, maendeleo na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Kaulimbiu ya UNGA 81 ni “Restoring Trust, Managing Transformation”, inayomaanisha “Kurejesha Imani, Kusimamia Mabadiliko.”

Chama Aitawala Simba, Mguu wa Kulia Wampa Mabao Manne

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama, ameonyesha ubora wa kutumia mguu wa kulia katika kufunga mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Simba SC imefunga jumla ya mabao 11 katika michezo sita, huku Chama akiwa kinara wa ufungaji ndani ya kikosi hicho akiwa amefunga mabao manne, yote akitumia mguu wake wa kulia.

Bao lake la nne alifunga katika mchezo dhidi ya Azam FC uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo Simba SC ilipata ushindi wa mabao 2-0. Chama pia alifungua akaunti yake ya mabao katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji FC uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kwa upande wa Yanga SC, Maxi Nzengeli pia ni miongoni mwa wachezaji wanaotegemea zaidi mguu wa kulia katika kufunga mabao. Nzengeli aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao akiwa nje ya eneo la mita 18 katika mchezo dhidi ya Namungo FC.

Wachezaji wengine walioonyesha uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kulia ni Maabad Maabad wa Coastal Union na Abdul Sopu wa Azam FC, ambao kwa mujibu wa rekodi za Ligi Kuu Tanzania Bara wamefunga mabao matatu kila mmoja kwa kutumia mguu huo.

Na Lunyamadzo Mlyuka



Serikali yaongeza bil 20/- upanuzi JNIA – HabariLeo

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetoa Sh bilioni 20 kwa ajili ya kuendelea na malipo ya fidia kwa wananchi wa eneo la Kipunguni wanaopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo jumla ya Sh bilioni 86 kati ya Sh bilioni 114 zinazohitajika ikiwa tayari imelipwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombakaleo, amesema fedha hizo ni sehemu ya mwendelezo wa awamu za malipo na kwamba zoezi hilo litaendelea kadiri fedha zitakavyopatikana, ambapo mpaka sasa wafidiwa 717 wamelipwa, huku wananchi wengine 1,147 wakisubiri malipo yao.

Akitoa taarifa hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari, Mombakaleo amesema leo Septemba 22, 2026 TAA imepokea Sh bilioni 20 na kwamba malipo ya awamu hiyo yataanza Jumatatu, huku utaratibu wa malipo ukitolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa mamlaka hiyo.

“Naomba niwahakikishie tumepokea Sh bilioni 20 na Jumatatu tutaanza kulipa. Maelekezo ya utaratibu wa kulipwa Mkurugenzi wa Fedha atatoa ili kila mmoja aweze kujua utaratibu na ajue kama yupo kwenye zamu ya awamu hii au awamu ijayo,”

“Naomba nichukue nafasi hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Kipunguni na wananchi wengine ambao wameamua kuvumilia kwa kuwa zoezi linaendelea na tutalipa kwa awamu. Kila mmoja atalipwa,” amesema Mombakaleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa TAA, Mohamed Seif, amesema Sh bilioni 20 zilizotolewa zitalipwa kwa wananchi waliokamilisha kujaza fomu na kufuata taratibu zilizowekwa.

Seif amewataka wananchi wanaosubiri fidia kuendelea kuwa wavumilivu, huku akisema kuwa mamlaka inaendelea na taratibu za kuhakikisha malipo yanafanyika ndani ya muda mfupi.

Amesema wananchi waliopo kwenye orodha ya malipo ya awamu hiyo watapatiwa fomu kupitia wenyeviti wa mitaa na Serikali za mitaa na baada ya kujaza fomu hizo, walengwa watazipeleka benki kwa ajili ya uhakiki na kisha kuzirudisha TAA kwa hatua zinazofuata.

Zoezi hilo ni sehemu ya mpango wa upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), unaohitaji wananchi waliopo kwenye maeneo yanayohusika kuondoka baada ya kukamilishiwa taratibu za fidia.

Dk Samia kuongoza kikao afya ya mama, mtoto – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuwaongoza viongozi wakuu wa nchi za Afrika na wadau wa maendeleo katika kujadili na kuhamasisha uwekezaji katika afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga na mtoto barani Afrika.
–
Kikao hicho cha ngazi ya juu kinatarajiwa kufanyika Septemba 23, 2026, jijini New York, Marekani, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA-81).
–
Rais Samia atakuwa mwenyeji wa kikao hicho katika nafasi yake ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto.
–
Miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa ni kupitishwa kwa tamko rasmi la kuharakisha hatua za kukomesha vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama, mtoto mchanga na mtoto, pamoja na kutangazwa kwa ahadi za uwekezaji kutoka kwa nchi na washirika wa maendeleo.
–
Uongozi wa Tanzania katika ajenda ya afya ya uzazi, mama na mtoto umejengwa kupitia utashi wa kisiasa, uwajibikaji na hatua zinazolenga kuboresha huduma za afya kwa wanawake na watoto.
–
Hatua hiyo inaendeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha masuala ya afya ya uzazi, mama na mtoto yanaendelea kupewa kipaumbele, huku Tanzania ikiwa sehemu ya juhudi za Bara la Afrika katika kuharakisha upatikanaji wa huduma bora na salama kwa wanawake na watoto ifikapo mwaka 2030.

Vita Vya Pointi Vimeanza Meridianbet Kupitia Endorphina Tournament

Mashindano mapya yameingia uwanjani na safari hii ni kuhusu pointi. Endorphina Tournament sasa inapatikana ndani ya Meridianbet, ikiwaalika wachezaji kushiriki kupitia sloti zinazostahili huku wakikusanya pointi kutokana na ushindi wao. Kila mchezo unaweza kuleta tukio jipya, na kila ushindi unaweza kuongeza alama zako kwenye safari ya tournament. Hapa, ushindi wako hauishii kwenye mchezo pekee, unaweza pia kuwa sehemu ya jumla yako ya pointi.

Ili kuanza safari, unahitaji kuweka dau lako na baada ya hapo, jambo muhimu ni kucheza kwenye sloti zinazoshiriki. Kila ushindi unahesabiwa kwa kutumia vizidishi vya ushindi, hivyo kiasi unachoshinda ukilinganisha na dau lako kinaathiri idadi ya pointi unazopata.

Vilevile, meridianbet wana michezo mingi ya kasino mtandaoni na mechi za kimataifa za kubashiri zenye ushindani mkubwa wa odds. Jiunge leo kwa kutembelea tovuti ya meridianbet au piga *149*10# kisha uanze safari yako ya ushindi.

Mfano wake unaweka picha wazi. Ukiweka Tsh. 3,000 na ukashinda Tsh. 30,000, utapewa pointi 1,000. Ukicheza tena kwa dau la Tsh. 3,000 na safari hii ukashinda Tsh. 60,000, unapata pointi 2,000. Ushindi huo wa pili unaongeza mara mbili ya pointi zilizopatikana kwenye mfano wa kwanza, na hapo ndipo umuhimu wa kila ushindi unapoonekana.

Mwisho wa mifano hiyo miwili, pointi zako zinakuwa 3,000, pointi 1,000 kutoka kwenye ushindi wa kwanza na pointi 2,000 kutoka kwenye ushindi wa pili. Kadri unavyopata ushindi mwingine kwenye sloti zinazostahili, pointi zako zinaendelea kujikusanya. Hivyo, tournament inabadilisha kila ushindi kuwa sehemu ya safari yako ya jumla ya alama.

Sasa Endorphina Tournament imefungua milango yake Meridianbet. Anza kwa kuweka dau lako, ingia kwenye sloti zinazoshiriki na anza kukusanya pointi kupitia ushindi wako. Burudani ipo, ushindani upo, na pointi zinasubiri kukusanywa.