KAMATI YA BUNGE YA EALA YAKUTANA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE, KUTATHMINI MCHAKATO WA RASIMU YA KATIBA YA FUNGAMANO LA KISIASA LA AFRIKA MASHARIKI.

Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya Kikanda na Utatuzi wa Migogoro katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Septemba 22, 2026 imekutana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, jijini Dodoma, kwa lengo la kutathmini hatua iliyofikiwa na Tanzania katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki.

Kikao hicho, kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Maina Karobia, huku Ujumbe wa Wizara ukiongozwa  na Mkurugenzi Idara ya Siasa, ulinzi na Usalama Bi.  Mwanamridu  Amiry. Wajumbe walipokea taarifa kuhusu mchakato huo na kutathmini namna wananchi wa Tanzania watakavyoshirikishwa katika kutoa maoni na mitazamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa.

Tathmini hiyo ni sehemu ya juhudi za kikanda za kuhakikisha mchakato wa kuanzishwa kwa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa unakuwa wa wazi, shirikishi na unaozingatia maoni na matakwa ya wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  

Kamati pia ililenga kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza mchakato huo.

 

TANZANIA YAALIKA WAWEKEZAJI KUTOKA VIETNAM

Tanzania imewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Vietnam kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za Uchumi ikiwemo kilimo, miundombinu, madini, teknolojia na mawasiliano na Uchumi wa buluu.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb.) wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Vietnam uliofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 22, 2026 ukilenga kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania na Vietnam.  

Alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na kampuni za Vietnam katika maeneo mbalimbali yenye fursa za uwekezaji ikiwemo kilimo, usindikaji wa mazao, biashara, teknolojia, miundombinu, madini, kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa samaki na sekta nyingine za uzalishaji, huku akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kimkakati kama Reli, Bandari, Nishati ya Umeme na Kongani za Viwanda na Usafiri wa Anga ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

“Tunawakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam kuja Tanzania na kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali ya uchumi. Tanzania iko tayari kushirikiana nao katika kukuza biashara na uwekezaji wenye manufaa kwa pande zote,” alisema Mhe. Millya.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Vietnam kwenye Mkutano huo ambaye ni Naibu Waziri wa Kilimo na Mazingira, Mhe. Nguyen Hoang Hiep, amesema nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania sio kwenye sekta ya mawasiliano peke yake bali pia katika maeneo mengine ikiwemo kukuza kilimo kupitia teknolojia ya kisasa na kwamba kinachohitajika ni pande hizi mbili kuandaa Mpango mzuri wa utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yanayofikiwa. 

Jukwaa hilo la Biashara lilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Burhani na wadau wengine kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Vietnam ambao pia walitumia nafasi hiyo kunadi fursa zilizopo kwenye maeneo yao ikiwemo TISEZA, Bodi ya Korosho, Kampuni ya Uzalishaji Kahawa ya Tanganyika (TANICA), Tume ya Taifa ya Umwagiliji (NIRC) na Kampuni za Vietnam za Intimex, VinGroup na Philimex.

 

MAKAMU WA RAIS KUHUTUBIA KIKAO CHA 81 CHA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi leo Jumanne, Septemba 22, 2026, anatarajiwa kuhutubia Mjadala Mkuu wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 81), unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

 

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano huo wa ngazi ya juu unaowakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, pamoja na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

 

Mjadala Mkuu wa mwaka 2026 unafanyika chini ya kaulimbiu, “Kurejesha imani, kusimamia mabadiliko: Umoja wa Mataifa unaowatumikia wote” (Restoring trust, managing transformation: A United Nations that delivers for all).

 

Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika mkutano huo ni changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia na namna ya kuimarisha ushirikiano katika kutafuta suluhisho la kudumu, hususan katika masuala ya amani na usalama wa kimataifa, maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, afya, utawala wa teknolojia na Matumizi ya akili unde (AI), pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa.

 

Mjadala Mkuu wa Kikao cha 81 umeanza leo, Septemba 22, na utaendelea hadi Septemba 26, kabla ya kuhitimishwa Septemba 28, 2026.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

22 Septemba 2026

New York – Marekani.

𝑴𝑨𝑲𝑨𝑴𝑼 𝑾𝑨 𝑹𝑨𝑰𝑺 𝑨𝑾𝑨𝑺𝑰𝑳𝑰 𝑵𝑬𝑾 𝒀𝑶𝑹𝑲 – 𝑴𝑨𝑹𝑬𝑲𝑨𝑵𝑰, 𝑲𝑼𝑴𝑾𝑨𝑲𝑰𝑳𝑰𝑺𝑯𝑨 𝑹𝑨𝑰𝑺 𝑫𝑲𝑻. 𝑺𝑨𝑴𝑰𝑨 𝑺𝑼𝑳𝑼𝑯𝑼 𝑯𝑨𝑺𝑺𝑨𝑵 𝑲𝑨𝑻𝑰𝑲𝑨 𝑴𝑲𝑼𝑻𝑨𝑵𝑶 𝑾𝑨 81 𝑾𝑨 𝑩𝑨𝑹𝑨𝒁𝑨 𝑲𝑼𝑼 𝑳𝑨 𝑼𝑴𝑶𝑱𝑨 𝑾𝑨 𝑴𝑨𝑻𝑨𝑰𝑭𝑨

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amewasili New York nchini Marekani, ambapo anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81) Unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Jijini New York.
 
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F Kennedy, Makamu wa Rais amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe Balozi Elsie Kanza, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa – New York Mhe. Balozi Togolani Mavura pamoja na maafisa mbalimbali.
 
Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoshirikisha Wakuu wa Nchi na Viongozi mbalimbali ni Mkutano muhimu ambao, pamoja na mambo mengine, hujadili masuala ya kiuchumi, kisiasa, mazingira na haki za binadamu.
Kikao hicho kinafanyika chini ya Kaulimbiu isemayo “Kurudisha Imani, Kusimamia Mabadiliko, Umoja wa Mataifa unaohudumia wote” (Restoring Trust, Managing Transformation: A United Nations That Delivers for All). Kaulimbiu hiyo ni wito wa pamoja wa kujenga upya uaminifu na ushirikiano wa kimataifa pamoja na kusimamia vema mabadiliko makubwa yanayoendelea ulimwenguni ikiwemo kasi ya ukuaji wa akili unde (AI).
Aidha, Mheshimiwa Makamu wa Rais anatarajiwa kuhutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kushiriki kwenye vikao mbalimbali ikiwemo Mjadala Mkuu (General Debate), Mikutano ya pembezoni na Mikutano ya pande mbili (Bilateral Meetings)

 

JALSA YA 55 AHMADIYYA KUFANYIKA DAR SEPTEMBA 25

 

Na Matukio DaimaMedia 

Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka (Jalsa Salana) wa 55, Septemba 25 hadi 27, 2026 katika eneo la Kitonga, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Zaidi ya washiriki 5,500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wenye kaulimbiu “Taqwa (Uchamungu) Ndiyo Msingi wa Kila Wema.”

Akizungumza na waandishi wa habari, Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad, amesema Jalsa hiyo inalenga kuwaimarisha waumini kiroho kwa kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu, uchamungu, huruma na upendo, huku wakijiepusha na mambo mabaya.

Amesema mkutano huo pia utajadili changamoto zinazoikabili dunia, ikiwemo migogoro na vita, huku waumini wakipata fursa ya kushiriki ibada, mihadhara na mafundisho ya dini, pamoja na Sala ya usiku (Tahajjud).

Aidha, amesema waumini wamehimizwa kushiriki shughuli za kijamii, ikiwemo kuwasaidia wenye mahitaji na kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa, huku Jumuiya hiyo ikisema ina uwepo katika nchi 212 duniani.

Kwa upande wake, Naibu Amir wa Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania, Abdurahman Mohamed Ame, amesema maadili ni msingi muhimu wa maisha ya mwanadamu na Uislamu unasisitiza kuishi kwa maadili mema katika kila hatua ya maisha.

Amesema mafundisho ya Uislamu yanamtaka mtu kusema ukweli, kuheshimu haki za wengine na kutambua kuwa katika kudai haki zake anapaswa pia kutekeleza wajibu wake bila kuvunja haki za wengine.

“Ni kweli kudai haki zetu, lakini tukumbuke wajibu wetu na tuhakikishe kwamba wakati tunadai haki, tusije tukateleza, tukavunja haki au wajibu wetu, au tukavunja haki za wengine kwa kisingizio cha kudai haki zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa maadili mema katika familia na jamii ni msingi wa amani, akisema dunia ikiheshimu haki za wengine na kuzingatia maadili, migogoro na matatizo yanaweza kupungua.

THRDC NA MAIPAC WANOA WAANDISHI WA HABARI ZA MAZINGIRA KANDA YA KATI

Na Matukio Daima Media ,Dodoma

Mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu nchini(THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Usaidizi wa Jamii za Pembezoni(MAIPAC) wamewataka wanahabari nchini, kuandika habari za mazingira zitakaleta matokeo chanya katika jamii.

THRDC na MAIPAC, wametoa wito huo,katika ufunguzi wa Mafunzo hayo yanafanywa chini ya mradi unaodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO,) katika mradi wa “Kuwawezesha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania kuwa na Athari Endelevu,” ambao unalenga kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari za mazingira kuchangia uwajibikaji wa mazingira, uelewa wa umma, ulinzi wa haki za binadamu na utawala endelevu wa mazingira kwa kuwahusisha   waandishi wa  mikoa ya Dodoma,Singida,Mbeya,Morogoro na Iringa.

Akifungua Mafunzo hayo,Mratibu wa kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa leo,Septemba 22,2026,jijini Dodoma amesema kuna changamoto nyingi za Mazingira nchini ambazo haziandikwi na kuleta matokeo.

Wakili Ole Ngurumwa anasema,tatizo la kusambaa taka mitaani,Uharibifu wa misitu na Vyanzo vya maji pamoja na uwekezaji usiozingatia athari za mazingira ni changamoto kubwa kwa sasa nchini.

“Rais Samia alisema Dar es Saalam ni chafu mimi nasema inanuka kwani uchafu umesambaa kila kona”anasrma.

Mkurugenzi wa MAIPAC,Mussa Juma anasema Dunia kwa sasa ipo katika kipindi kigumu kutokana na uharibifu wa mazingira na wanahabari wana wajibu kusaidia kutumia vyombo vyao vya habari.

Juma anasema, kwa sasa Tanzania kuna tushio kubwa la Mvua za El-Nino,lakini pia kuna maeneo ukame umeathiri maisha ya watu na mifugo lakini ni habari chache zenye tija zinazoandikwa.

“Kupitia mradi huu nendeni mkaandike habari za uchunguzi ,kubainisha changamoto za mazingira na mueleze suluhisho na ubunifu ili kusaidia jamii”amesema

Amesema Dunia inakabiliwa pia na changamoto.za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamepunguza upatikanaji wa chakula,yameleta mafuriko maeneo mengi na pia kuibua migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.

Mkuu wa Kitengo cha Utetezi,THRDC  Wakili Paul Kisabo akitoa mada katika mafunzo hayo,aliwaelimisha wanahabari sheria mbali mbali za ndani na kimataifa ambazo zinatumika katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

Wakili Kisabo aliwataka wanahabari kuandika na kuchunguza habari za mazingira bila hofu ili kusaidia jamii na kama wakikabiliwa na changamoto watapata utetezi.

Mafunzo hayo yanashirikisha wanahabari 35 ambapo awali wanahabari 35 wa mikoa ya kanda ya kaskazini walipata mafunzo na wengine 35 wa Kanda ya Ziwa walipata mafunzo hayo kupitia mradi huo wa THRDC na MAIPAC unaodhaminiwa na UNESCO.

Dereva wa Tarura Akamatwa Kwa Tuhuma Za Kutumia Silaha Bandia – (Picha+Video)

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia dereva wa TARURA Wilaya ya Dodoma, Sath John Masawa (31), kwa tuhuma za kumtishia dereva wa basi la SATCO kwa kutumia kitu kinachodhaniwa kuwa bastola.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, tukio hilo linadaiwa kutokea wakati Said Fadhili (54), dereva wa basi la SATCO lenye usajili T308 EME, akiwa anatoka kuweka mafuta katika kituo cha Total Energies.

Inadaiwa kuwa Masawa alimtishia Said kwa kitu hicho na kisha kumfuata kwa gari la TARURA lenye usajili STM 5806, aina ya Land Cruiser LX 70 Series, lililokuwa likiendeshwa na mtuhumiwa.

Baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kumkamata Sath John Masawa. Baada ya upekuzi, ilibainika kuwa kitu alichokuwa nacho na kudhaniwa kuwa bastola hakikuwa silaha halisi, bali ni kitu kinachofanana na silaha.

Aidha, Jeshi la Polisi limebaini kuwa gari la TARURA lenye usajili STM 5806 lilikuwa halitumii namba zake za usajili halali, badala yake lilikuwa likitumia namba T 881 ENZ, ambazo ni za gari mali ya mtu mwingine.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano na hatua zaidi za kisheria.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa madereva kuacha kutumia namba bandia za magari na kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara, likisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Rais Dkt. Mwinyi Ashiriki Maziko ya Marehemu Mama Fatma Karume

Global Publishers
September 22, 2026
6 views
0 Comments

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameungana na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Jeneza ya Marehemu Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar.

Sala hiyo imefanyika leo, Septemba 22, 2026, katika Masjid Jamiu Zinjibar, Mazizini, Wilaya ya Magharibi “B”, Mkoa wa Mjini Magharibi, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wanafamilia pamoja na wananchi.

Baada ya Sala ya Jeneza, Rais Dkt. Mwinyi ameungana na viongozi, wanafamilia na wananchi kuusindikiza mwili wa Marehemu Mama Fatma Karume hadi katika makaburi maalum ya familia yaliyopo Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambako amezikwa.

Usafirishaji waingiza Dola milioni 2.7, mwaka 2025 – HabariLeo

ARUSHA; SEKTA ya usafirishaji nchini imezalisha Dola za Marekani bilioni 2.7 mwaka 2025, sawa na asilimia 15.6 ya mauzo ya nje ya Tanzania, huku thamani hiyo ikiongezeka kutoka takribani dola bilioni 2.2 mwaka 2024

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ametoa takwimu hizo leo jijini Arusha alipomwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, katika Mkutano wa Nane wa Afrika wa Usimamizi wa Uendeshaji na Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM 2026), unaofanyika kwa siku mbili.

Amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa usafirishaji si sekta inayosaidia uchumi pekee, bali ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla, kwa kuwa unaunganisha wazalishaji na masoko, kuwezesha biashara na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Kihenzile amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji, ikiwemo reli, bandari, usafiri wa majini na anga, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na mizigo na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania.

“Tunapojiandaa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali imejikita katika kuimarisha usafirishaji, usafiri wa anga na mabadiliko ya kiuchumi yanayotokana na sekta ya usafirishaji,”

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Hawa Tundui, aliwataka watafiti Barani Afrika kuhakikisha tafiti zinazofanywa katika vyuo vikuu zinatafsirika kuwa suluhisho la changamoto halisi zinazokabili biashara, Serikali na jamii, badala ya kubaki katika machapisho ya kitaaluma.

Amesema vyuo vikuu vinapaswa kuendelea kutathmini kile wanachofundisha, namna wanavyofundisha na teknolojia wanazotumia ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira linalobadilika.

‎BEI YA MAHINDI YAWAPELEKA WAKULIMA WA LUDEWA KWA RC NJOMBE ‎

 

‎Wakulima wa zao la mahindi mkoani Njombe wameiomba serikali kuwapa vibali vya kuuza mahindi nje ya nchi kutokana na kuporomoko kwa soko la ndani ambalo litasababisha kupata hasara kubwa ukilinganisha na bei za uzalishaji.

‎Wakiwa kwa mkuu wa mkoa wa Njombe baadhi ya wakulima wakubwa wa mahindi toka wilayani Ludewa Akiwemo George Mkinga wamesema kitendo cha serikali kupitia wakala wa hifadhi ya chakula cha Taifa NFRA Kutangaza kuanza kununua mahindi hayo kwa shilingi 450 kwa Kilo badala ya shilingi 700 hadi 1000 kama misimu iliyopita kinawapa ugumu ukizingatia kuna hatari ya mvua kubwa za El nino ambazo zinaweza kuharibu mazao hayo.

‎Wamesema mwaka huu hususani wilaya ya Ludewa wamevuna mahindi mengi kiasi cha mkulima mmoja kuvuna hadi gunia 8000 lakini hakuna maghala ya kuhifadhia mazao na kuyauza kwa bei hiyo watapata hasara kubwa hivyo wamemuomba mkuu wa mkoa awafikishie kilio chao kwa Rais Samia.

‎Viongozi wa wilaya ya Ludewa akiwemo Mhe.Olivanus Thomas mkuu wa wilaya na Mkurugenzi Sunday Deogratias wamesema wameshafanya mazungumzo na wakulima wao na kuanza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kutafuta wanunuzi katika maeneo mengine ili kuona namna ya kuwasaidia wakulima hao.

‎

‎Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka ameahidi kufanya mawasiliano na Waziri wa Kilimo Kuona namna ya kuelekeza nguvu ya kununua mahindi hususani katika wilaya ya Ludewa ambayo imetajwa kuvuna mahindi mengi hasa katika vijiji vya Ibumi na Amani.

‎

‎Wanasema kwa ekari moja inayotumia zaidi ya shilingi milioni moja kulima zao la mahindi unaweza kupata shilingi laki saba baada ya mavuno ikiwa  hasara ni takribani shilingi laki tatu endapo mahindi yatauzwa kwa shilingi 450 kwa Kilo.