KARIAKOO FESTIVAL 2026: TBS YAWAPA WANANCHI ELIMU YA BIDHAA BORA NA SALAMA

 Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuimarisha juhudi zake za kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa kupitia ushiriki wake katika Tamasha la Kariakoo (Kariakoo Festival), lililofanyika katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.


Katika tamasha hilo lililoanza Septemba 25 na kuhitimishwa leo, Septemba 27, 2026, TBS imetumia banda lake kutoa elimu kwa wananchi waliotembelea tamasha hilo, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na kuhakikisha bidhaa zinazotumika zinakidhi matakwa ya ubora na usalama.

Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Bw. Kelvin Mtebene, alikuwa miongoni mwa wataalamu waliotoa elimu hiyo kwa wananchi, akieleza masuala mbalimbali yanayohusu viwango na umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa, kuuzwa na kutumiwa zinazingatia matakwa ya ubora na usalama.

Kupitia elimu hiyo, wananchi wamepata fursa ya kufahamu namna ya kutambua na kuchagua bidhaa zinazokidhi viwango, hatua inayosaidia kulinda afya na usalama wao pamoja na kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanapofanya manunuzi.

Ushiriki wa TBS katika tamasha hilo pia umekuwa fursa muhimu ya kulisogeza Shirika karibu zaidi na wananchi, kwa kuwapa nafasi ya kuuliza maswali, kupata ufafanuzi na kutoa maoni kuhusu huduma zinazotolewa na TBS, hususan katika eneo la udhibiti wa ubora wa bidhaa nchini.

Kupitia mazungumzo ya ana kwa ana na wananchi, TBS imeendelea kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa viwango na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa kila mdau katika kuhakikisha bidhaa zinazotumika katika jamii zinakuwa na ubora unaotakiwa.

Aidha, uwepo wa TBS katika Tamasha la Kariakoo unaonesha umuhimu wa kutumia majukwaa ya kijamii na kibiashara kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa, ili kuongeza uelewa kuhusu masuala ya viwango na kuhamasisha matumizi ya bidhaa bora na salama.

Baba Akamatwa Kwa Tuhuma za Kuwatupa Watoto Wake Kutoka Ghorofa ya Sita Japan

Mwanaume mwenye umri wa miaka 25 amekamatwa nchini Japan kwa tuhuma za kujaribu kuwaua watoto wake wawili, baada ya kudaiwa kuwatupa kutoka kwenye roshani ya ghorofa ya sita ya jengo la makazi.

Tukio hilo lilitokea mapema Jumamosi, Septemba 26, katika mji wa Kakamigahara, mkoani Gifu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Japan, mtuhumiwa huyo, Tomokazu Miura, alidaiwa kuwatupa watoto wake wawili, msichana mwenye umri wa mwaka mmoja na mwingine mwenye umri wa miaka minne, kutoka kwenye roshani ya nyumba yao.

Watoto hao walianguka kutoka urefu wa takribani ghorofa sita, lakini waliangukia kwenye mikeka iliyokuwa imeandaliwa chini na wahudumu wa dharura.

Wote wawili walinusurika na kupelekwa hospitalini. Ripoti zinasema walikuwa na fahamu wakati wakisafirishwa kwenda hospitali, huku majeraha yao yakielezwa kuwa hayakuwa ya kuhatarisha maisha.

Tukio hilo lilitokea saa 4:20 asubuhi, saa za Japan, muda mfupi baada ya polisi kufika katika nyumba hiyo kufuatia simu ya dharura iliyopigwa na mke wa mtuhumiwa usiku wa kuamkia tukio.

Majira ya saa 11:30 jioni siku ya Ijumaa, Septemba 25, mke huyo aliwapigia polisi na kuwaeleza kuwa mume wake alikuwa amemshika mkono wakati wa mabishano.

Polisi walifika katika eneo hilo na kuzungumza na mwanamke huyo nje ya nyumba. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti, Miura alikataa kushirikiana na polisi na kujifungia ndani ya nyumba.

Inadaiwa kuwa wakati polisi walipokuwa wakijiandaa kuingia ndani, ndipo watoto hao walipotupwa kutoka kwenye roshani.

Kamera za usalama zilizokuwa karibu na eneo hilo zilinasa tukio hilo, huku picha zikionyesha vitu viwili visivyoeleweka vizuri vikianguka kutoka juu ya jengo.

Baada ya tukio hilo, Miura alikamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua. Vyombo vya habari nchini Japan vimeripoti kuwa alibaki kimya wakati akihojiwa na polisi.

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyedai kushuhudia polisi wakimchukua mtuhumiwa alisema kuwa Miura alidaiwa kusema kwamba alikuwa na nia ya kufa pamoja na watoto hao.

Hata hivyo, kauli hiyo ni madai ya shahidi yaliyoripotiwa na chombo cha habari na haijathibitishwa rasmi na polisi.

Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku watoto hao wakiendelea kupata matibabu hospitalini.

England Yaanza Ligi ya Mataifa kwa Kichapo Dhidi ya Hispania

England usiku wa kuamkia leo Septemba 27, 2026 imeanza kampeni yake ya Ligi ya Mataifa kwa kichapo baada ya kufungwa mabao 3-2 na mabingwa wa dunia, Hispania, katika mchezo uliochezwa Wembley.

Hispania ilianza kwa kasi na kupata bao ndani ya dakika mbili kupitia Lamine Yamal, baada ya beki wa England, Marc Guehi, kufanya kosa lililompa nafasi mshambuliaji huyo kufunga dhidi ya kipa James Trafford.

England ilinusurika mashambulizi kadhaa ya Hispania kabla ya Anthony Gordon kuisawazishia timu yake dakika ya 36, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jude Bellingham na kumalizia kwa ustadi.

Dakika nne baadaye, Harry Kane aliipa England bao la pili kupitia kichwa chake, huku mpira ukimgonga Marc Cucurella na kuingia wavuni.

England ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, lakini mambo yalibadilika katika kipindi cha pili.

Dakika ya 55, England ilipata penalti baada ya Jude Bellingham kuangushwa ndani ya eneo la hatari kufuatia ukaguzi wa VAR.

Hata hivyo, Kane alikosa penalti hiyo kwa namna isiyo ya kawaida baada ya kuteleza wakati akipiga mpira, ambao pia uligusa mguu wake mara mbili kabla ya kugonga mwamba.

Hispania ilitumia nafasi hiyo kusawazisha dakika ya 60 kupitia Alex Baena, baada ya Nico O’Reilly kupoteza mpira.

Dakika 16 kabla ya mchezo kumalizika, Mikel Oyarzabal aliipa Hispania bao la ushindi baada ya kumalizia shambulizi la pamoja kwa mpira wa ustadi uliompita Trafford.

Ushindi huo umeifanya Hispania kufikisha michezo 39 mfululizo bila kupoteza.

Kwa upande wa England, mchezo huo umeonyesha madhara ya makosa madogo dhidi ya timu yenye kiwango cha juu, huku makosa ya Guehi na O’Reilly pamoja na penalti iliyokosa na Kane yakigharimu timu hiyo.

Anthony Gordon alikuwa miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango kizuri zaidi kwa England, huku Bellingham pia akifanya vizuri.

Kipa James Trafford, ambaye alipewa nafasi badala ya Jordan Pickford, hakupata nafasi kubwa ya kuzuia mabao ya Hispania na alifanya baadhi ya seivu muhimu katika kipindi cha kwanza.

England sasa itasafiri kwenda kukutana na Jamhuri ya Czech siku ya Jumanne, huku Hispania ikiikaribisha Croatia katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mataifa.

Manchester City Yakataa Makosa Katika Kesi Ya Mashtaka 115 Ya Premier League

Mwenyekiti wa Manchester City, Khaldoon Al Mubarak, amesema klabu hiyo bado ina imani kubwa kwamba itaweza kuthibitisha kutokuwa na hatia katika kesi inayohusisha mashtaka 115 ya madai ya kukiuka kanuni za kifedha za Premier League.

Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti kudai kuwa tume huru iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo imeikuta Manchester City na hatia katika mashtaka 114 kati ya 115.

Hata hivyo, Premier League bado haijatangaza rasmi uamuzi huo wala adhabu yoyote dhidi ya klabu hiyo.

Katika ujumbe wake kwa mashabiki Jumamosi, Al Mubarak amesema mchakato huo bado una safari ndefu na kwamba msimamo wa Manchester City wa kuthibitisha kutokuwa na hatia haujabadilika.

Amesema kuna mambo mengi ambayo angependa kuwaeleza mashabiki ili waelewe sababu ya klabu hiyo kuwa na imani katika msimamo wake, lakini masharti ya usiri yanayohusiana na kesi hiyo hayamruhusu kufichua taarifa hizo kwa sasa.

Manchester City imekuwa ikikanusha makosa hayo tangu Premier League ilipofungua mashtaka dhidi yake mwaka 2023.

Mashtaka hayo yanahusisha kipindi cha mwaka 2009 hadi 2018 na yanajumuisha madai ya kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu masuala ya kifedha pamoja na kushindwa kushirikiana kikamilifu na uchunguzi wa ligi.

Iwapo uamuzi unaoripotiwa utathibitishwa rasmi, Manchester City inaweza kukabiliwa na adhabu mbalimbali, ikiwemo kupokonywa pointi, faini au hata kuondolewa kwenye Premier League. Hata hivyo, hakuna adhabu rasmi iliyotangazwa hadi sasa.

Kesi hiyo imekuwa ikiendelea kwa zaidi ya miaka mitatu na ni miongoni mwa kesi kubwa zaidi za kinidhamu katika historia ya soka la England.

Manchester City imekuwa moja ya klabu zilizotawala soka la England katika miaka ya hivi karibuni, ikishinda mataji manane ya Premier League tangu mwaka 2012 pamoja na UEFA Champions League mwaka 2023.

Kwa sasa, klabu hiyo inaendelea kusisitiza kuwa inaamini katika msimamo wake na kwamba mchakato wa kisheria bado haujamalizika.

DKT. MWIGULU: TUNZENI UAMINIFU NA JINA LA NCHI YETU, FANYENI KAZI KWA BIDII

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi watunze uaminifu na wafanye kazi kwa bidii ili wasiliharibu jina zuri la Tanzania.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Septemba 26, 2026) wakati akizungumza na madareva wa Kitanzania zaidi ya 500 walioajiriwa na kampuni ya usafirishaji ya MOWASALAT kwenye kikao kifupi kilichofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo, zilizoko Lusail Depot nje kidogo ya Jiji la Doha, Qatar.

Dkt. Mwigulu ambaye yuko nchini Qatar kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Abdulrahman bin Jassim Al Thani alisema: “Fanyeni kazi kwa bidii ili muwe mabalozi kwa wenzenu walioko nyumbani. Kuweni waaminifu, tunzeni jina la nchi yetu ili wenzenu waweze kupata fursa za ajira katika nchi mbalimbali. Mkiaminiwa inakuwa rahisi kufungua milango kwa wenzenu.”

Waziri Mkuu alitumia fursa kuwapa picha halisi ya maendelea yaliyofikiwa nchini Tanzania katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu na akawasihi waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa amedhamiria kuwahudumia Watanzania.

Akijibu hoja za madereva hao kuhusu kutotambuliwa kwa vyeti vyao pindi wanaporudi nyumbani, Dkt. Mwigulu Nchemba alimwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani afuatilie suala hilo kwa kushirikiana na wizara husika. 

“Fuatilia uwezekano wa kulink vyeti vyao wanapohitimu mafunzo yao. Wale wanaopata distinction na wanahitajika nyumbani, tuwe na database yao ili watambuliwe kwa urahisi. Utambuzi wa elimu inayopatikana hapa unaweza kutambuliwa endapo mtu ameamua kurejea nyumbani. Kama tatizo ni sheria, basi iangalieni hiyo sheria. Mheshimiwa Rais alishasema sheria isiwe kikwazo cha Watanzania kujiletea ustawi,” alisema na kuamsha shangwe kubwa moingoni mwa madereva hao.

Kuhusu usumbufu wa kudaiwa vibali vya kazi na ushuru wa vyakula wanavyotaka kuondoka navyo, ambao wanaupata kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam wanapokuwa wanarejea kutoka likizo, Waziri Mkuu aliwahakikishia kwamba litafanyiwa kazi mara moja.

“Haiwezekeni mtu anabeba lade (matundapori) kutoka kwao ili akija huku ayatumie na kupunguza mawazo ya nyumbani halafu mnamtoza ushuru. Au msukuma amebeba unga wake ili akiwa huku asonge ugali, ajisikie yuko nyumbani halafu mnamzuia; mnataka ale tambi? Msukuma na tambi wapi na wapi? Alihoji Waziri Mkuu.

Akitoa hoja zao kwa niaba ya madereva wenzake, Calvin Isack Luo alisema: “Watanzania tunaoishi na kufanya kazi nje ya nchi tunapitia changamoto mbili zinazohusiana na safari. 

Tunapoingia Tanzania wakati mwingine tunapata usumbufu mkubwa katika ukaguzi wa mizigo, na tunaporejea nchi tunakofanyia kazi tunaweza kuhitajika kuonyesha kibali cha kazi, wakati tayari tunayo residence permit/ID halali ya nchi hiyo. Je, Serikali ina mpango wa kuweka utaratibu maalum unaotambua hadhi ya Mtanzania anayeishi kihalali nje ya nchi, ili taratibu za airport ziwe rahisi, wazi na zisizorudiwa bila sababu?”

Mapema, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi alisema atafuatilia maombi yao ya kuhuishwa kwa leseni zao za udereva ili yawe yanafanyika kwa automatic. 

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharik, Dkt. Ngwaru Maghembe alisema ataongea na benki za CRDB, NMB na Mfuko wa UTT ili wawatume watu wao wa dawati la DIASPORA waende Qatar kuwasajili wanaotaka mitaji yao iende kuwekezwa nyumbani.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amefuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Katibu Wakuu (OR-Uwekezaji), Wabunge na watendaji wengine wa Serikali.

Kifaru Avamia Gari la Watalii Namibia, Msemaji wa Wizara Afunguka

Global Publishers
September 27, 2026
12 views
0 Comments

Watalii waliokuwa katika safari ya kujionea wanyamapori nchini Namibia wamekumbwa na hofu baada ya kifaru mweusi kulishambulia gari lao katika Hifadhi ya Taifa ya Etosha.

Tukio hilo lilirekodiwa na Ebot Enow Ebot Agbor Ndip, ambaye ni mwongoza watalii, na video hiyo baadaye kushirikishwa na Storyful.

Katika video hiyo, kifaru huyo anaonekana akilikimbilia gari lililokuwa barabarani, kabla ya kuligonga kwa nguvu kwa kichwa na pembe zake upande wa kushoto wa gari.

Nguvu ya mashambulizi hayo ilisababisha sehemu ya gari kung’oka, huku kifaru huyo akiendelea kulisukuma na kuligonga. Magari mengine yaliyokuwa nyuma yalisimama baada ya kuona tukio hilo.

Baadaye, dereva wa gari lililokuwa likishambuliwa alianza kuliondoa eneo hilo, huku kifaru huyo akilifuatilia kwa muda kabla ya kusimama.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, watalii waliokuwa ndani ya gari walifanikiwa kuondoka salama bila kupata majeraha, ingawa gari lilipata uharibifu.

Ndip alisema kifaru huyo alionekana kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa na kwamba alijitahidi kuweka umbali salama wakati akirekodi tukio hilo.

Hata hivyo, alieleza kuwa baadhi ya magari mengine hayakuweka umbali huo, na akaonya kuwa watalii wanaoendesha magari wenyewe katika hifadhi wanapaswa kufahamu tabia na ishara za wanyama kabla ya kuwakaribia.

Msemaji wa Wizara ya Mazingira, Misitu na Utalii ya Namibia, Vilho Hangula, aliwahimiza watalii kuwa waangalifu wanapokuwa katika hifadhi za wanyamapori.

Hangula alisema wanyama wa porini huongozwa na tabia zao zinaweza kuwa zisizotabirika.

Mamlaka pia zimewashauri watalii kutumia waongozaji wenye uzoefu na walioandikishwa, pamoja na kujifunza tabia za wanyama wa porini ili kupunguza hatari wakati wa safari.

SIKU YA UTALII DUNIANI, NGORONGORO SI PAKUJA PEKE YAKO, NJOO NA MPENZI WAKO

Leo ni siku ya Utalii Duniani ambapo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaungana na wadau wengine duniani kusherehekea sikukuu hii ikiwa imejipanga kuendeela kuhudumia watalii kwa viwango vya kimataifa na kuendelea kuwahimiza wapendanao kuja kushuhudia maajabu ya dunia katika bustani ya Eden.

Kutokana na upekee wa Ngorongoro ambapo hadithi, fikra na mtazamo wako unakutana na uhalisia ukija bila mpenzi wako utapata tabu ya kumsimulia mwenzako kutokana na utakayoyaona kwani ni hifadhi iliyojaa kila aina ya vivutio ambavyo si  fahari ya Tanzania pekee bali dunia nzima

Akizungumzia kuhusu maajabu ya Ngorongoro kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia huduma za utalii na Masoko Mariam Kobelo amesema kwamba Hifadhi ya Ngorongoro ni urithi uliotukuka ambao unahitaji  kulindwa kwa wivu mkubwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Kobelo anaeleza kuwa katika kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani 2026, Mamlaka inawashukuru kwa  dhati  wageni waendeshaji wa utalii, mawakala wa safari, washirika ,wawekezaji, waongoza watalii, wadau wa sekta ya utalii na jamii  kwa mchango mkubwa katika utalii.

“Tunapoelekea katika mustakabali mpya wa utalii, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro inaendelea kufanya maboresho mbalimbali katika huduma za kidijitali na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) ili kuongeza ufanisi, kuboresha uzoefu wa wageni na kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku tukizingatia msingi wetu mkuu wa uhifadhi na utalii endelevu” amesisitiza kamishna Kobelo

Ameongeza kuwa Ngorongoro si eneo la kutembelea tu bali ni urithi wa dunia unaopaswa kuishi kwa faida ya vizazi na vizazi kuendelea kujifunza kutokana na historia ya asili iliyofunikwa na tabasamu la uhifadhi endelevu.  Ngorongoro inathamini utamaduni wetu, tunahifadhi maliasili zote kwa kutambua kuwa maendeleo ya utalii yanaenda sambamba na wajibu wa kulinda mazingira na kuhifadhi urithi wetu kwa ajili ya vizazi vijavyo

‘Katika siku hii muhimu, ninawaalika wote kuendelea kuwa sehemu ya safari hii, Tuitembelee Ngorongoro, Tuiheshimu Ngorongoro, Tuilinde Ngorongoro, Tuiache Ngorongoro ikiwa bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo na kuhakikisha tunaenda sambamba na kauli mbiu yam waka huu isemayo  “Ajenda ya Kidijitali na Akili Bandia Kubuni Upya Sekta ya Utalii,”

Heri ya Siku ya Utalii Duniani 2026.

TANZANIA YAENDELEA KUIMARISHA URAFIKI NA MAREKANI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha urafiki na Marekani kwa kuweka mazingira rafiki kwa raia, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini humo.

Akizungumza katika hafla ya kila mwaka ya Marafiki wa Tanzania jijini New York, Marekani, Waziri Kombo amesema Tanzania inatoa visa kwa raia wa Marekani wanapowasili nchini, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuonesha urafiki na kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Aidha, Waziri Kombo amesema Serikali iko tayari kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji katika masuala yanayohusu kanuni, sera na taratibu, huku Wizara ya Mambo ya Nje ikiwa tayari kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza, amesema hafla hiyo imelenga kuadhimisha urafiki, ushirikiano na ubia kati ya Tanzania na Marekani, pamoja na kuimarisha uhusiano wenye manufaa kwa pande zote.

Hafla hiyo imeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu nchini Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.); Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida;  Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga pamoja na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Afya na masuala ya ukimwi Dkt. Zeyana Abdallah Hamid(Mb.).

 

DKT. MUNISI AIPONGEZA SDA KUIMARISHA AMANI NA MSHIKAMANO

 Dar es Salaam

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi, amepongeza Kanisa la Waadventista wa Sabato Salasala (SDA) kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mshikamano wa kijamii, kukuza maadili ya uadilifu, uwajibikaji na upendo, pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na mshikamano wa kitaifa.

Mhe. Dkt. Munisi amesema hayo Jana, Septemba 26, 2026, katika harambee ya kuchangia ujenzi na maendeleo ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA), Salasala, jijini Dar es Salaam.

Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imejipanga kushirikiana na makundi ya kijamii katika kudumisha mshikamano, kukuza ustahimilivu, kuimarisha maadili ya kazi na kusaidia jitihada za kijamii na maendeleo endelevu.

Kadhalika, Dkt. Munisi amewapongeza viongozi na waumini wa Kanisa la SDA Salasala kwa kuandaa harambee hii ya ujenzi wa kanisa yenye lengo la kukusanya Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga jamii imara.

“Tusimame pamoja, tutoe kwa moyo wa furaha, tutashuhudia Kanisa la Waadventista wa Sabato linajengwa na kudumishwa imara kwa utukufu wa Mungu,” amesema Dkt. Munisi.

Vilevile, Dkt. Munisi amewasihi viongozi na waumini wa kanisa kuendelea kuyaenzi na kuimarisha mafundisho ya kiroho na malezi ya watoto na vijana, umoja, upendo na mshikamano, ushirikiano na Serikali, pamoja na kuwa na uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za kanisa.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Majengo, Bw. Charles Wangwe kutoka Kanisa la SDA Salasala, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha, kulinda na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano na mahusiano mema miongoni mwa Watanzania wa makundi ya imani mbalimbali katika Taifa letu.

Ameendelea kwa kusema kuwa kanisa linaendesha hospitali, kliniki, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Zahanati ya Pemba, vituo 12 vya afya, ambazo ni zahanati 11 na polyclinic moja.

Sambamba na hayo, Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa likichangia katika maendeleo ya elimu, ambapo jumla ya shule 27 za awali, 23 za msingi, 18 za sekondari, Chuo kimoja cha VETA, Chuo kimoja cha Afya na Chuo kimoja cha kati kilichopo Dodoma.

Amesema Kanisa la Waadventista wa Sabato lilianzishwa mwaka 2007 likiwa na washiriki wachache; mwaka 2010 washiriki walifika 150, mwaka 2018 waumini 400 na wengine kukaa nje, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa ujenzi wa jengo kubwa lenye uwezo wa kuchukua watu 1,500 na kukadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 3.

MWISHO