CookFund yachochea mapinduzi ya nishati safi, wanafunzi 62,000 wanufaika

Dar es Salaam. Zaidi ya wanafunzi 62,000 nchini wamenufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na usakinishaji wa majiko ya kisasa katika shule na taasisi za umma zaidi ya 45, huku idadi ya majiko ikizidi 170.

Hatua hiyo imechukuliwa kupitia programu ya CookFund, inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF).

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Machi 26, 2026, katika hafla ya makabidhiano ya msaada huo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Bunge, jijini Dar es Salaam, ikionesha hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, pamoja na kukabiliana na changamoto ya ukataji miti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha kimkakati cha Taifa katika kulinda mazingira, kuboresha afya ya jamii, na kuongeza ufanisi wa kiuchumi.

Amesema kwa kuzipatia shule na taasisi za umma teknolojia za kisasa za kupikia, Serikali inalenga kupunguza hewa chafuzi, kulinda rasilimali za misitu, na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 hadi 2034,” amesema Naibu Waziri Makamba.

Jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini zinaongozwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Wizara ya Maliasili na Utalii, na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira.

Mpango huo unalenga taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa wakati mmoja, hususan shule, ili kuondokana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira, kama kuni na mkaa.

Akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, Mkuu wa Ushirikiano nchini Tanzania, Marc Stalmans, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kusaidia mpito kuelekea matumizi ya nishati safi.

“Tunasaidia watu kuhamia kwenye mbinu endelevu zinazolinda mazingira huku zikichochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira, na kuboresha upatikanaji wa nishati katika sekta mbalimbali,” amesema.

Kwa upande wake, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kiufundi wa UNCDF, Peter Malika, amesema programu hiyo imewekeza Dola milioni 10.1 za Marekani katika biashara ndogo na za kati 102, pamoja na kusaidia taasisi 45 katika wilaya 14 za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, na Mwanza.

Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yana mchango mkubwa katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, huku yakiboresha usalama, afya, na ufanisi katika shughuli za upishi shuleni.

Kwa mujibu wa wataalamu, matumizi ya kuni na mkaa huchangia uzalishaji wa chembechembe hatarishi zinazosababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji, ikiwemo pumu na saratani ya mapafu.

Kupitia CookFund, teknolojia mbalimbali za nishati safi zimeanza kutumika, zikiwemo majiko ya umeme, majiko ya bayoethanoli, majiko banifu, pamoja na matumizi ya gesi na mkaa mbadala.

Kizimkazi yaaga kero ya maji, Rais Samia atoa neno

Unguja. Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kero ya maji iliyodumu kwa muda mrefu Kizimkazi na maeneo mengine ya Kusini Unguja, imefikia mwisho, baada ya kuzindua miradi miwili ya maji huku akiwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Agosti 13, 2026, alipozungumza na wananchi wa Kizimkazi Kibuteni, Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kuzindua miradi hiyo ikiwa ni sehemu ya shughuli za Tamasha la Kizimkazi.

Miradi hiyo inahusisha chanzo cha maji chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 2.4 kwa siku na tanki lenye ujazo wa lita milioni moja.

Rais Samia amesema Kizimkazi na Kusini kwa jumla zinakabiliwa na changamoto kubwa ya maji kwa muda mrefu, lakini utekelezaji wa miradi hiyo umeiwezesha Serikali kumaliza tatizo hilo.

“Leo tatizo la maji tumelihitimisha. Ndugu zangu wa Kusini, Kibuteni na Kizimkazi, tujipongeze sana,” amesema.

Amesema chanzo cha maji Kizimkazi kilijengwa mwaka 1974 kikiwa na tanki lenye ujazo wa lita 150,000, lakini baadaye kilishindwa kukidhi mahitaji kutokana na ukuaji wa eneo hilo na uwekezaji ulioongezeka.

Amesema Serikali haikuangalia mahitaji ya sasa pekee, ambayo ni takribani lita 500,000, bali imezingatia mahitaji ya baadaye kutokana na ongezeko la watu, miji na uwekezaji.

Rais Samia amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo, akisema Serikali imetumia fedha na utaalamu mkubwa kuitekeleza.

“Tumetengenezewa, tutunze tusiharibu. Tunajua tulipotoka, tulikuwa na tatizo kubwa la maji. Leo tumepata ufumbuzi wa maji, tutunze miundombinu hii na sisi tuwe walinzi kuilinda sisi wenyewe,” amesema.

Katika ziara hiyo, Rais Samia amepanda mti, amepokea gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kizimkazi na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Chuo cha Amali unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.

Kuhusu Kituo cha Afya Kizimkazi, amesema kinaendelea kuboreshwa na sasa kinatarajiwa kutoa huduma zinazokaribia kiwango cha hospitali ya wilaya, ikiwamo huduma za dayalisisi kwa gharama nafuu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Maji Kizimkazi katika moja ya matukio kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja Agosti 13, 2026.

Amesema kituo hicho pia kitakuwa na chumba maalumu cha mazoezi ya viungo kitakachotumiwa na wachezaji pamoja na watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali.

Amesema uwanja wa mpira wa Samia Academy unaojengwa katika eneo hilo unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu au Januari 2027, hivyo kituo hicho kitakuwa muhimu katika kutoa huduma za afya kwa wachezaji.

Pia, amesema gari la wagonjwa lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) litasaidia kuboresha huduma za afya katika kituo hicho.

Rais Samia amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kutunza miradi hiyo kwa kuwa ni uwekezaji unaolenga kuboresha maisha yao.

“Hii ni maisha yetu, fursa yetu, uchumi na ustawi wa wananchi,” amesema.

Pia, amewataka wananchi kuendelea kulinda amani na kuunga mkono maendeleo yanayotekelezwa na Serikali.

‘Maji yamefika vijiji 10,756’

Waziri wa Maji, Juma Aweso amesema Serikali imefanya maendeleo makubwa katika sekta ya maji na kufikisha huduma hiyo kwa asilimia 85 kwa wananchi nchini.

Amesema kati ya vijiji 12,333 vilivyopo Tanzania, 10,756 vimefikiwa na huduma ya maji, huku vijiji 1,575 vikiwa katika hatua za kukamilisha miradi.

“Hakuna kijiji kitakachopitwa bila kupewa maji,” amesema Aweso.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Maji Kizimkazi katika moja ya matukio kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja Agosti 13, 2026.

Amesema utekelezaji wa miradi ya Kizimkazi umetokana na maelekezo ya Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi yaliyolenga kuhakikisha tatizo la maji katika eneo hilo linamalizika.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis amesema wananchi wameanza kuona faida ya mradi huo na kuahidi kulinda miundombinu yake.

Baadhi ya wananchi wameeleza furaha yao, wakisema changamoto ya maji iliyodumu kwa miaka mingi sasa inaanza kuwa historia.

Mwachumu Haji, mkazi wa Kizimkazi, amesema hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa mbaya, lakini sasa matumaini ya kupata huduma hiyo yameongezeka.

Juma Kamis Juma amesema wananchi watahakikisha wanailinda miradi hiyo kwa sababu wanaufahamu uchungu wa kukosa maji.

Aliyedai fidia ya Sh40 milioni kwa kulea mimba ya mtoto asiye wake, agonga mwamba kortini

Singida. Omary Mgana, amegonga mwamba katika jitihada zake za kudai fidia ya Sh40 milioni kutoka kwa mke wake wa zamani, Hadija Willa, akidai alimficha ujauzito wa mwanaume mwingine wakati akifunga naye ndoa mwaka 1997.

Omary alidai Sh10 milioni alizotumia katika huduma za ujauzito na kujifungua, pamoja na Sh30 milioni alizodai kutumia kumlea na kumsomesha mtoto huyo hadi kufikia utu uzima.

Alidai aligundua mwaka 2021, kwamba mtoto huyo ambaye wakati huo alikuwa na miaka 24, hakuwa wake. Pia, aliiomba mahakama iamuru kuondolewa kwa ubini wake katika nyaraka za mtoto huyo.

Hata hivyo, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Singida imetupilia mbali rufaa yake na kusimamia uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida uliokataa madai hayo.

Katika hukumu iliyotolewa Agosti 14, 2026 na Jaji, Ayoub Mwenda na kuwekwa kwenye tovuti ya Mahakama Agosti 17, 2026, ilieleza Omary alishindwa kuthibitisha kuwa alifichwa ujauzito huo.

Jaji alisema madai ya kurejeshewa fedha yangekuwa na msingi kama Hadija angeuficha ujauzito wakati wa ndoa, lakini ushahidi ulionyesha Omary alikuwa akijua hali hiyo.

“Nimepitia ushahidi uliopo na sijaona kasoro katika hitimisho la mahakama ya chini. Kama ilivyoelezwa kwa usahihi na mahakama ya chini, mdaiwa angeweza kuhukumiwa kwa kosa la kuficha ujauzito iwapo tu, katika siku ya harusi angeulizwa kama ana ujauzito au la, jambo ambalo halikutokea,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Mwenda, kumbukumbu za kesi zinaonyesha swali aliloulizwa Hadija siku ya ndoa lilikuwa kama alikuwa tayari kufunga ndoa na Omary.

“Hakuna sheria inayomlazimisha mwanamke kusema kwa hiari kama ana mimba wakati wa kujiandaa kufunga ndoa ikiwa hajaulizwa,” alisema.

Hivyo, Jaji alisema ushahidi ulionyesha Hadija alimweleza Omary kabla ya ndoa kwamba alikuwa na ujauzito wa mwanaume mwingine.

Hadija katika utetezi wake alisema wakati Omary alipokuwa akimchumbia, alimweleza kuwa alikuwa na mwanaume mwingine aliyempa ujauzito, lakini Omary alisisitiza kumuoa akisema nyumba ya ndoa haizai mtoto haramu.

Walipofunga ndoa mwaka 1997, Hadija alikuwa na ujauzito wa miezi minne hadi mitano na alijifungua Oktoba 10, 1997.

Awali alimpa mtoto jina Mohamed Joseph, lakini Hadija alieleza kuwa Omary ndiye aliyesisitiza jina libadilishwe na baadaye mtoto akaitwa Juma Omary Juma Mgana.

Katika madai yake, Omary alisema alimtunza mtoto huyo akiamini ni wake, akigharamia huduma za ujauzito, kujifungua, malezi na elimu.

Alisema mwaka 2021 ndipo Hadija alipomweleza kuwa mtoto huyo si wake. Hata hivyo, katika shauri la talaka namba 14 la 2024, mahakama ilimwamuru kuendelea kumhudumia mtoto huyo kwa kutumia mapato ya kodi ya nyumba kugharamia matibabu na elimu hadi atakapofikia utu uzima.

Omary pia alidai kuwa mwaka 2006 Hadija alibadili msimamo na kutangaza kuwa Juma hakuwa mtoto wake, jambo lililosababisha mtoto huyo kuhamishiwa kwa mjomba wake na baadaye shangazi yake.

Juma aliyetoa ushahidi kama shahidi wa pili wa utetezi, alikanusha kupokea fedha kutoka kwa Omary kwa ajili ya elimu, akisema alisoma shule ya Serikali ambayo haikuwa na ada.

Jaji Mwenda pia alikataa madai ya Omary kwamba alitumia Sh1.5 milioni kumlipia Hadija gharama za kujifungua, akisema hakuwasilisha ushahidi kuthibitisha fedha hizo zilitumika kwa matibabu.

Kuhusu madai ya matumizi ya fedha za kodi, Jaji alisema katika shauri la talaka mahakama iligawa nyumba kwa asilimia 50 kwa 50, hivyo mapato yake hayakuwa ya mtoto huyo pekee.

“Hata kama mdaiwa asingekuwa na sehemu ya asilimia 50 ya nyumba hiyo, jambo ambalo si kweli, mlalamikaji alishindwa kuwasilisha ushahidi wowote kuthibitisha mdaiwa alikuwa akikusanya kiasi cha Sh225,000 kwa mwezi kama ilivyodaiwa,” alisema.

Jaji pia alisema Omary hakuthibitisha hasara au madhara halisi yaliyosababishwa na mwenendo wa Hadija.

“Msongo wa mawazo pekee, bila uthibitisho, hauwezi kuwa sababu halali ya kutoa fidia ya jumla,” alisema.

Aliongeza kuwa kwa kuwa Omary alijua ujauzito huo kabla ya ndoa, hakukuwa na udanganyifu uliosababisha hasara au madhara.

“Kama ilivyobainishwa kwa usahihi na mahakama, mtoto huyo alilelewa kama sehemu ya familia; hivyo, madai ya kurejeshewa gharama hayana msingi wa kisheria. Rufaa hii inakataliwa na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya unasimama,” alisema.

Hata hivyo, kuhusu gharama za kesi, Jaji alisema kwa kuwa pande hizo bado zinashirikiana katika kulea watoto wengine, haikuwa mwafaka kumuamuru Omary kuzilipa kwa kuwa hatua hiyo isingeleta amani na maelewano katika familia ambayo imesambaratika.

DCEA yateketeza ekari 603 za bangi Morogoro

Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeanza operesheni maalumu ya kuharibu mashamba ya bangi mkoani Morogoro, baada ya kubaini wakulima kuhamia maeneo ya mbali ndani na nje ya Hifadhi ya Mikumi.

Katika operesheni maalumu iliyofanyika kwa siku 14 katika vijiji vya Visengele na Lugenge wilayani Mvomero, DCEA imeteketeza ekari 603 za bangi,   kukamata magunia 49 ya bangi na watuhumiwa 13 kwa tuhuma za kujihusisha na kilimo cha dawa hizo za kulevya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu Agosti 17, 2026 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo operesheni hiyo ni mwendelezo wa kampeni maalumu ya kudhibiti dawa za kulevya zinazozalishwa nchini, hususani bangi, huku akieleza kuwa mamlaka imebaini baadhi ya wakulima wamehamia maeneo ambayo hayajawahi kufikiwa na operesheni za awali.

Amesema pamoja na operesheni kufanyika katika maeneo hayo tangu mwaka 2023, bado wananchi wameendelea kulima bangi ndani ya Hifadhi ya Mikumi na maeneo ya nje ya hifadhi.

“Katika operesheni tulizozifanya safari hii tumegundua kwamba wamelima mbali zaidi ya maeneo ambayo operesheni zilishafanyika awali, wakidhani mamlaka itashindwa kufika katika maeneo hayo,” amesema Lyimo.

Lyimo amesema ukubwa wa mashamba yaliyobainika unaonyesha kuwa kilimo cha bangi bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo ya Morogoro, hasa ndani ya hifadhi na katika vijiji vinavyozunguka maeneo ya mapori.

“Maeneo haya yako mbali sana na vijiji na makazi ya wananchi, lakini mamlaka itaweka intelijensia ya kutosha ili kuhakikisha kwamba hizi operesheni na hawa wahalifu tutaendelea kuwakamata,” amesema.

Masaji si tiba ya kila maumivu, wataalamu waonya

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameonya wananchi dhidi ya kukimbilia huduma za masaji wanapopata maumivu ya mgongo, shingo, miguu au misuli bila kwanza kufahamu chanzo cha tatizo, wakisema kufanya hivyo kunaweza kutoa nafuu ya muda huku ugonjwa ukiendelea kukua.

Wamesema baadhi ya maumivu yanayodhaniwa kuwa ya uchovu au mkazo wa misuli yanaweza kuhitaji tathmini ya kitaalamu ili kubaini chanzo na kupewa matibabu au mazoezi yanayolenga kurejesha uwezo wa mwili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Medinova, Selestine Mpiri, anasema dhana inayowachanganya wananchi ni kuamini kuwa fiziotherapia na masaji ni huduma moja.

“Massage mara nyingi inalenga kutoa unafuu wa muda mfupi. Misuli ikikaza ukafanyiwa masaji utajisikia vizuri, lakini hiyo inaweza kuwa ni ya muda mfupi. Fiziotherapia inalenga kutafuta mzizi wa tatizo na kuhakikisha unafanyiwa mazoezi au utaratibu unaoweza kusaidia tatizo liondoke na lisirudi tena,” anasema.

Anasema tatizo si masaji yenyewe, bali kuitumia kama tiba ya kila aina ya maumivu bila kufanyiwa tathmini ya kitaalamu.

Kwa mfano, anasema baadhi ya wagonjwa waliowahi kufika hospitalini wakiwa na dalili zinazofanana na kiharusi, walibainika baada ya uchunguzi kuwa hawakuwa na kiharusi wala tatizo la ubongo na walisaidiwa kwa fiziotherapia.

“Nilikuwa na wagonjwa watatu vijana ambao walikuja wakiwa wamepooza upande mmoja wa uso. Baada ya kuwafanyia uchunguzi, tulibaini hawakuwa na kiharusi wala tatizo la ubongo. Walipewa fiziotherapia na wakapona,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Mpiri, fiziotherapia haiwahusu watu waliopata ajali au kufanyiwa upasuaji pekee, bali inaweza kusaidia changamoto mbalimbali zinazohusu misuli, mifupa, mishipa ya fahamu, mfumo wa upumuaji na utendaji wa mwili.

“Fiziotherapia ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria. Kuna magonjwa ya upumuaji, kizunguzungu na matatizo ya misuli ya nyonga ambayo yanaweza kusaidiwa kwa tiba hii,” anasema.

Anasema udhaifu wa misuli ya nyonga unaweza kuhusishwa na changamoto za kudhibiti mkojo na kwamba, kwa baadhi ya watu, mazoezi maalumu yanaweza kusaidia kuimarisha misuli hiyo.

Hatari ya masaji ya nguvu

Wataalamu pia wanaonya matumizi ya nguvu kubwa wakati wa masaji, hasa kwa watu wenye maumivu ya mgongo ambayo chanzo chake hakijajulikana.

Baadhi ya watoa huduma hutumia uzito wa mwili, ikiwamo kukanyaga mgongo, kwa madai ya kumsaidia mteja kujisikia mwepesi.

Hata hivyo, wataalamu wanasema shinikizo kubwa linaweza kuwa hatari kwa mtu mwenye tatizo la mifupa, pingili za mgongo, mishipa ya fahamu au jeraha ambalo halijagundulika.

Dk Mpiri anawataka watu wenye maumivu ya muda mrefu au yanayorudia kutafuta ushauri wa kitaalamu badala ya kutegemea masaji kila wanapohisi maumivu.

Anasema hata uchovu wa mwili unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, yakiwamo kazi nzito, kukaa au kusimama kwa muda mrefu, kukosa usingizi na mkazo wa misuli.

Hata hivyo, anasema uchovu unaodumu au unaoambatana na dalili nyingine unaweza kuhitaji uchunguzi wa kitabibu.

Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa juma, mtaalamu mwingine wa fiziotherapia wa Medinova, Witney Lema, anasema huduma hiyo inahusika na tiba ya utengamao na mazoezi tiba bila kutumia dawa, huku ikilenga matatizo ya misuli na mifupa pamoja na magonjwa ya mfumo wa fahamu kwa watu wazima na watoto.

“Wengi wetu tunaonekana kusumbuliwa na matatizo ya misuli na mifupa. Tunaumwa migongo, shingo, miguu na tunapata ajali. Baada ya ajali au kuvunjika mifupa, baadhi hushindwa kutembea vizuri tena. Fiziotherapia imekuja kusaidia katika changamoto hizi,” anasema.

Anasema tiba hiyo hutumia mbinu mbalimbali, ikiwamo tiba kwa mikono na vifaa vya kielektroniki, kulingana na hali ya mgonjwa.

Dk Mpiri anawataka wananchi pia kutotumia mazoezi wanayoyaona kwenye Youtube kama mbadala wa tathmini ya mtaalamu.

“Tunatakiwa tujue kwamba mazoezi, ili yafae zaidi, yanatakiwa yawe individualized (yalengwe kwako). Mtaalamu wa fiziotherapia pia atakurekebisha unapofanya mazoezi vibaya,” anasema.

Anasema mazoezi yanapaswa kuzingatia umri, ukubwa wa mwili na hali ya kiafya ya mtu, hivyo mazoezi ya mtu mwenye miaka 20 hayawezi kutumika kwa mtu wa miaka 60 bila tathmini.

Dk Imran Asif Bajwa anasema fiziotherapia huanza kwa tathmini ya mgonjwa na wakati mwingine huhitaji ushirikiano wa wataalamu mbalimbali kulingana na tatizo litakalobainika.

“Kupona kwa mgonjwa hakutegemei daktari mmoja au wawili, bali timu kubwa. Mgonjwa anaweza kuja kwa mtaalamu, lakini wakati wa assessment (tathmini) tunaweza kubaini anahitaji kumuona daktari wa mifupa. Tutafanya kazi kwa pamoja,” anasema.

Kwa nini GB 128 za simu yako zinawahi kujaa? Fanya hivi…

Dar es Salaam. Miaka iliyopita, simu yenye nafasi ya kuhifadhi taarifa ya GB32 au GB64 ilionekana kuwa na uwezo mkubwa, lakini mabadiliko ya matumizi ya simu janja yamefanya nafasi hiyo kujaa kwa haraka.

Leo, hata simu yenye GB 128 inaweza kumlazimu mtumiaji kusafisha taarifa mara kwa mara, hasa anayepiga picha nyingi, kurekodi video, kucheza michezo mikubwa au kutumia mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa.

Sababu kubwa ni ongezeko la ukubwa wa picha, video na programu. Simu nyingi za kisasa zina uwezo wa kurekodi video za ubora wa juu, huku baadhi zikiruhusu kurekodi video zenye ubora wa hali ya juu unaofikia (4K) na hata viwango vya juu zaidi kulingana na aina ya kifaa.

Kwa mujibu wa Apple Support, kwa mfano, inaonyesha kuwa baadhi ya iPhone zinaweza kurekodi video ya 4K na kwamba teknolojia ya ProRes inaweza kutumia nafasi kubwa ya kuhifadhi, kiasi kwamba baadhi ya uwezo wa kurekodi hutegemea ukubwa wa uhifadhi ‘storage’ wa simu.

WhatsApp nayo inakula nafasi

Kwa watumiaji wengi, si kamera pekee inayojaza storage. Programu za mawasiliano kama WhatsApp zinaweza kuhifadhi kwa muda mrefu picha, video, nyaraka, sauti na faili nyingine zinazotumwa kwenye makundi na mazungumzo binafsi.

Tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kwa mtu aliye kwenye makundi mengi yanayotuma video na picha kila siku ambapo itakulazimu uzime auto-download.

Kwa upande wa Android, Google inashauri watumiaji kuingia sehemu ya Settings > Storage ili kuona ni aina gani ya faili au programu zinazotumia nafasi kubwa na kuanza kuziondoa zisizo muhimu.

Google pia inaeleza kuwa (backup) za WhatsApp kwenye Android sasa zinahesabiwa katika nafasi ya kuhifadhi ya akaunti ya Google, huku video zikiwa miongoni mwa vitu vinavyoweza kuongeza ukubwa kwa haraka.

GB 128 haimaanishi nafasi yote ipo wazi

Jambo jingine ambalo mtumiaji anapaswa kulifahamu ni kwamba namba iliyoandikwa kwenye boksi, kama GB 128, si lazima iwe nafasi yote atakayoiona akiwa anaanza kutumia simu.

Sehemu ya nafasi hiyo hutumika na mfumo wa uendeshaji, programu zilizokuja na simu na mafaili mengine ya mfumo. Kadri mtumiaji anavyoongeza programu na taarifa zake nafasi iliyobaki hupungua.

Hivyo, mtu anayenunua simu ya GB 128 kwa sababu anaona ina nafasi kubwa anapaswa kujiuliza pia ataitumia kwa shughuli gani.

Njia rahisi ni kuanza kwa kuangalia sehemu ya Storage kwenye simu ili kubaini kinachotumia nafasi kubwa.

Picha na video muhimu zinaweza kuhifadhiwa kwenye huduma za cloud au kuhamishiwa kwenye kompyuta au kifaa kingine cha kuhifadhi. Google, kwa mfano, inaruhusu watumiaji wa Android kusimamia nafasi kwa kuondoa picha na video ambazo tayari zimehifadhiwa kwenye Google photos, pamoja na faili zilizopakuliwa na programu ambazo hazitumiki.

Google Help, pia kuna simu za Android zinazoweza ku-archive programu zisizotumiwa mara kwa mara, badala ya kuzifuta kabisa. Google inaeleza kuwa hatua hiyo inaweza kuondoa sehemu ya programu inayotumia nafasi huku taarifa na ikoni yake vikibaki ili iweze kurejeshwa baadaye.

Kwa mtumiaji anayefanya matumizi ya kawaida kama kupiga picha chache, kutumia WhatsApp, mitandao ya kijamii, kusoma habari na kupiga simu, GB 128 inaweza kutosha ikiwa atasimamia vizuri taarifa zake.

Lakini kwa mpiga picha, mtengeneza maudhui, mcheza michezo mikubwa au mtu anayerekodi video nyingi, GB 256 au zaidi inaweza kuwa chaguo lenye nafasi kubwa zaidi ya matumizi ya muda mrefu.

Kabla ya kununua simu, si muhimu kuangalia storage pekee. Mnunuzi anapaswa pia kuangalia aina ya kamera, ubora wa video, ukubwa wa programu anazotumia, kama kifaa kinaunga mkono memory card na kama kina uwezo wa kutumia huduma za cloud.

Kwa kifupi, GB 128 si ndogo moja kwa moja, lakini inaweza kuwa ndogo kulingana na matumizi ya mwenye simu. Kadri simu inavyotumika kama kamera, ofisi, burudani na kituo cha kuhifadhi mafaili, ndivyo nafasi kubwa ya kuhifadhi inavyokuwa muhimu zaidi.

Asimulia alivyojifungua katikati ya tetemeko la ardhi

Dar es Salaam. Maria Florida, 39, ameeleza furaha yake baada ya kujifungua salama mtoto wake wa nne kwa njia ya upasuaji, huku tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 likitikisa eneo la Nusa Tenggara Mashariki mwa Indonesia.

Florida alikuwa tayari ameshaanza kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Nagekeo wakati tetemeko hilo lilipoanza. Hata hivyo, madaktari waliendelea na huduma huo licha ya mazingira magumu yaliyosababishwa na mtikisiko huo.

Tetemeko hilo lilisababisha kukatika kwa umeme hospitalini hapo, hivyo madaktari walilazimika kutumia mwanga wa tochi kuendelea na upasuaji hadi kufanikisha kumleta duniani mtoto huyo.

Baada ya kujifungua mtoto wa kike, Florida alimpa jina Gempita Soli Wona,   linalohusishwa na neno la Kiindonesia linalomaanisha tetemeko la ardhi.

Mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.3 na kwa mujibu wa taarifa za madaktari afya yake inaendelea kuimarika.

Tetemeko hilo lilitokea Agosti 15, 2026 na kuleta madhara makubwa mashariki mwa Indonesia, likisababisha vifo vya watu wasiopungua 54, majeruhi zaidi ya 130 na kuwalazimisha maelfu ya wakazi kuondoka katika maeneo yaliyoathirika.

Kutokana na mitikisiko kuendelea na baadhi ya miundombinu ya hospitali kuathirika, mtoto huyo amewekwa katika mashine maalumu ya kuhifadhi joto iliyowekwa nje ya jengo la hospitali.

Florida amewashukuru madaktari kwa kujitoa na kuendelea na upasuaji huo licha ya hatari iliyokuwapo.

Wakati tukio hilo likitoa simulizi ya matumaini, idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko hilo imefikia 53, huku shughuli za uokoaji zikiendelea katika maeneo yaliyoathirika.

Waokoaji wamefanikiwa kupata miili mingine sita, hali iliyoongeza idadi ya vifo kutoka 47 hadi 53.

Zaidi ya watu 135 wameripotiwa kujeruhiwa, huku nyumba zaidi ya 900 zikiharibiwa na maelfu ya watu kulazimika kuondoka katika makazi yao kutokana na hofu ya mitetemeko zaidi.

Takriban watu 5,000 wamehama makazi yao na kuhamia maeneo salama likiwa la  Kisiwa cha Flores.

Tetemeko hilo pia limesababisha maporomoko ya ardhi na kuziba baadhi ya barabara, hali iliyowapa changamoto waokoaji kuwafikia watu waliokwama katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Kukatika kwa umeme na mawasiliano kumeongeza ugumu wa shughuli za uokoaji, huku mamlaka zikiendelea kuratibu juhudi za kuwafikia waathirika na kutoa msaada wa dharura.

Misaada inayotolewa inajumuisha chakula, mahema na mahitaji mengine muhimu kwa watu walioathirika.

Jose Chameleone alivyoibua shangwe akitumbuiza kilele tamasha la Kizimkazi

Unguja. Msaanii wa kimataifa kutoka Uganda, Jose Chameleone ameibua shangwe wakati akitumbuiza katika kilele cha tamasha la Kizimkazi.

Katika tamasha hilo linalofanyika leo Agosti 14, 2026 viwanja vya Mwehe Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, msanii huyo amepata fursa kutumbuiza nyimbo zake mbili, Jamila na Mama Mia.

Katika kibao chake cha Jamila, alishuka kutoka katika jukwaa la burudani na kusogelea meza kuu walipokaa viongozi wakuu wa kitaifa kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Baada ya kufika katika jukwaa hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alishuka kutoka kwenye kiti chake alipokuwa amekaa na kuongea na msanii huyo kisha kucheza naye wimbo huo wa mbona umeniacha.

Baada ya hapo aliondoka huku akiibua shwangwe kubwa kwa wananchi na viongozi waliofurika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kusherehekea sherehe hizo.

Katika tamasha hilo pia wasanii wengine wa ndani na nje ya Tanzania wamepata fursa ya kutumbuiza.

Miongoni mwa wasanii hao ni Mrisho Mpoto, Sholo Mwamba, kikundi cha ngoma kutoka Dodoma cha Mahenza na ngoma ya asili ya Kizimkazi ya Shomoo.

Rais Samia ahimiza amani, utulivu Tamasha la Kizimkazi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewahimiza Watanzania, hususan vijana, kulinda amani, usalama na utulivu, akisema maendeleo ya Taifa hayawezi kustawi katika mazingira ya vurugu.

Amesema amani, usalama na utulivu ni nguzo muhimu zinazowezesha uwekezaji, utalii, biashara, ajira na utoaji wa huduma za jamii, ambazo haziwezi kustawi katika mazingira ya vurugu na uvunjifu wa amani.

“Niwaombe Watanzania wenzangu, hususan vijana, msikubali kuharibu amani ya nchi yenu, amani ndiyo kila kitu katika maisha yenu, niwaombe sana mumkatae kwa nguvu zote yeyote asiyeitakia mema Tanzania yetu, tulinde nchi yetu pamoja na Muungano wetu kwa mustakabali wa kizazi kijacho,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, Agosti 14, 2026, alipohitimisha Tamasha la Kizimkazi katika Uwanja wa Mwehe, Makunduchi, Zanzibar.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, akiwamo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na taasisi za umma.

Akizungumzia tamasha hilo, Rais Samia amesema limeleta chachu ya maendeleo katika wilaya za Kusini mwa Zanzibar kwa kuchochea biashara na kuongeza fursa za kiuchumi zinazoboresha maisha ya wananchi.

“Ndugu zangu, shangwe siku zote ni nzuri. Zinatuleta pamoja, zinaimarisha mshikamano na umoja, zinatusaidia kutangaza utamaduni wetu na kuvutia wageni. Kazi yetu kama viongozi ni kuhakikisha fursa zinazoibuliwa kupitia shangwe hizi zinawagusa wananchi wetu na tunaziunga mkono,” amesema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi lililofanyika leo Agosti 14, 2026, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Amesisitiza kuwa, Tamasha la Kizimkazi linapaswa kuwa lango la fursa za kiuchumi na chanzo cha ustawi wa wananchi na Taifa kwa jumla.

Amesema Wilaya ya Kusini imepata mabadiliko makubwa ikilinganishwa na mwaka 2016, kutokana na kuongezeka kwa fursa za biashara na uwekezaji.

Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu na utekelezaji wa miradi mbalimbali umeendelea kuvutia wananchi na wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo.

“Rais wa Zanzibar ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Karibuni muwekeze. Tunaendelea kujenga uwanja wa michezo ambao utasaidia kufungua fursa mbalimbali wakati wa michuano ya AFCON itakayofanyika Juni 2027,” amesema.

Ameongeza kuwa uwanja huo utatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika huduma zitakazohitajika na wachezaji pamoja na wageni watakaoshiriki mashindano hayo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha Tamasha la Kizimkazi, akisema limekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza utalii wa Zanzibar.

“Nawapongeza wananchi wote kwa mwamko mkubwa wa kushiriki tamasha hili na kutumia fursa zilizoambatana nalo, hakika mwaka huu tamasha limefana sana. Limekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha shughuli za maendeleo,” amesema na kuongeza:

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na msanii wa Uganda, Jose Chameleone wakati wa tamasha la Kizimkazi linalofanyika leo Agosti 14, 2026 viwanja vya Mwehe Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.

“Tumeshuhudia uzinduzi wa miradi mbalimbali ikiwamo ya maji, barabara, elimu, nyumba za makazi na viwanja vya michezo,” amesema.

Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha miradi yote iliyozinduliwa na itakayotekelezwa baadaye inatunzwa na kuendelezwa ipasavyo.

Hoja ya uhamiaji kutikisa mkutano wa wakuu wa SADC

Dar es Salaam. Suala la uhamiaji linatarajiwa kutawala mjadala katika mkutano wa 46 wa kawaida wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika leo, Agosti 17, 2026, jijini Durban, Afrika Kusini.

Mkutano huo unaowakutanisha viongozi wa nchi 16 wanachama unafanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Durban, chini ya uenyekiti wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Ajenda rasmi ya mkutano huo ni pana na inahusisha maendeleo ya kiuchumi, usalama, ushirikiano wa kikanda, usalama wa chakula pamoja na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya SADC.

Hata hivyo, suala la uhamiaji limeibuka kama moja ya changamoto zinazoweza kuhitaji uangalizi wa viongozi, hasa kutokana na kuongezeka kwa mvutano kuhusu wahamiaji nchini Afrika Kusini na athari zake kwa uhusiano kati ya nchi wanachama.

Mjadala huo unakuja wakati Afrika Kusini ikiendelea kukabiliana na malalamiko ya baadhi ya raia wanaodai wahamiaji wanashindania ajira, huduma za jamii na fursa za kiuchumi.

Takwimu rasmi za serikali ya nchi hiyo zinaonyesha takribani watu milioni 2.4, waliozaliwa nje ya nchi wanaishi nchini humo , na utafiti mwingine ulionyesha  idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia milioni 3.1.

Wataalamu wanaonya kuwa changamoto ya uhamiaji haiwezi kutatuliwa na Afrika Kusini pekee kwa kuwa inahusishwa kwa kiasi kikubwa na tofauti za kiuchumi, ajira na fursa zilizopo kati ya nchi za SADC.

Mtazamo huo umeungwa mkono na Taasisi ya Institute for Security Studies (ISS), inayosisitiza kuwa uhamiaji unapaswa kushughulikiwa kama suala la kikanda kutokana na utegemeano wa nchi wanachama.

Kwa mtazamo huo, hatua za nchi moja katika kudhibiti wahamiaji zinaweza kuwa na athari kwa majirani zake, hasa kwa kuwa wananchi wa nchi za SADC wamekuwa wakivuka mipaka kutafuta ajira, biashara, usalama na fursa nyingine za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Associated Press (AP), Afrika Kusini imetumia karibu dola milioni 18 kugharamia kuwarejesha  wahamiaji katika nchi zao, huku zaidi ya watu 80,000 wakirudishwa au kusaidiwa kurejea katika mataifa yao.

Serikali pia imesema imewakamata karibu watu 60,000 waliokuwa nchini humo bila vibali, wakiwamo zaidi ya 16,000 kwa Julai pekee.

Rais Ramaphosa amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuonya dhidi ya mgongano kati ya ajenda ya ushirikiano wa kikanda na matendo yanayoweza kuwabagua wahamiaji.

Katika hotuba yake ya Agosti 14, alisema Afrika Kusini haiwezi kuzungumzia ushirikiano katika mikutano ya kikanda wakati ikifanya kinyume chake mitaani, akisisitiza umuhimu wa mshikamano uliojengwa katika historia ya ukombozi wa eneo hilo.

Kauli hiyo inaweka shinikizo zaidi kwa mkutano wa Durban, ambao unafanyika wakati suala la uhamiaji likiwa tayari limezua mijadala mikali ndani ya Afrika Kusini na katika baadhi ya nchi jirani.

Imeandaliwa na Salma Hamis kwa msaada wa mitandao.