Maganya: Jumuiya ya Wazazi Yaunga Mkono Nchimbi Kuvuliwa Uanachama – Video

Global Publishers
August 28, 2026
0 views
0 Comments

Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, amesema jumuiya hiyo inaunga mkono uamuzi wa kumvua uanachama wa CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Maganya ameyasema hayo Agosti 27, 2026, akiwa Misungwi, mkoani Mwanza, wakati wa ufunguzi wa sherehe za Wiki ya Wazazi Kitaifa.

Amesema msimamo huo unatokana na hatua zilizochukuliwa na chama dhidi ya Dkt. Nchimbi, huku akisisitiza umuhimu wa wanachama kuheshimu katiba, kanuni na maamuzi ya chama.

Baada ya Kimya, Mwijaku Amtaka Maua Sama Aachie Muziki Mpya

Mjadala kuhusu kurejea kwa msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, katika muziki umeibuka upya baada ya mwanahabari na mchambuzi wa burudani Mwijaku kumtaka msanii huyo kuanza kutoa kazi mpya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo, Agosti 27, 2026, Mwijaku ametoa ujumbe mfupi lakini wenye uzito kwa Maua Sama, akisisitiza kuwa mashabiki wake bado wanahitaji kusikia muziki mpya kutoka kwake.

“Tunataka nyimbo mpya,” aliandika Mwijaku.

Kauli hiyo imeibua hisia mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakionyesha hamu ya kumuona Maua Sama akirejea studio na kuendelea na safari yake ya muziki.

Maua Sama ni miongoni mwa wasanii wa kike waliowahi kufanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva na Afro-Pop nchini Tanzania.

Alijenga jina kupitia nyimbo mbalimbali zilizopokelewa na mashabiki, ikiwemo “Iokote”, ambayo ilichangia kuongeza umaarufu wake katika tasnia ya muziki.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, mashabiki wamekuwa wakisubiri kusikia kazi mpya kutoka kwa msanii huyo, huku maisha yake binafsi yakionekana kuchukua sehemu kubwa ya muda wake.

Ujumbe wa Mwijaku umeongeza matarajio kwa mashabiki wanaotamani kumuona Maua Sama akirudi kwenye muziki.

Kwa kuwa tayari ana historia na msingi wa mashabiki katika tasnia hiyo, kurejea kwake kwa kazi mpya kunaweza kuongeza ushindani katika muziki wa kike na kutoa hamasa mpya kwa mashabiki wa Bongo Fleva.

Kwa sasa, bado haijafahamika iwapo Maua Sama amepanga kutoa kazi mpya, lakini ujumbe wa Mwijaku umeweka wazi jambo moja mashabiki bado wanaisubiri sauti yake.

Stori na Nasra Kassim | GPL -TUDACO

SERIKALI YAZINDUA ‘UGHAIBUNI LOAN’ – Matukio Daima Habari

✅Kuwezesha vijana kumudu mahitaji ya msingi anapoenda kufanya kazi nje ya nchi

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana nchini wanaendelea kunufaika na fursa za nje ya nchi na zenye staha kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 27,2026 wakati wa uzinduzi wa mkopo wa Ughaibuni Loan unaoratibiwa na Benki ya CRDB pamoja na kuwaaga vijana 130 kati ya 530 wanaotarajia kwenda kufanya kazi nje ya nchi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi amesema Serikali inatambua ajira za nje ya nchi kama nyenzo muhimu ya kupanua fursa za ajira, kuongeza kipato cha vijana, kukuza ujuzi na kuwajengea uzoefu wa kimataifa.

“Matokeo ya jitihada hizi yamewezesha Watanzania 14,613 kupata ajira nje ya nchi tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani. Kati ya Julai 2025 hadi sasa, Watanzania 8,428 wameunganishwa na waajiri nje ya nchi,” amesema Dkt. Munisi.

Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuendelea kuaminika kuwa na nguvu kazi salama na yenye staha duniani.

Kuhusu uzinduzi wa Ughaibuni Loan, Dkt. Munisi amesema mkopo huo unalenga kuwawezesha vijana waliopata ajira nje ya nchi kupata fedha nafuu za kugharamia maandalizi ya safari ikiwemo tiketi ya ndege, bima na visa.

“Ughaibuni Loan siyo msaada bali ni mkopo wa uwezeshaji. Nawasihi vijana wahakikishe wanafanya marejesho ili na wengine wapate fursa,” amesisitiza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Bw. Pendason Philemon amesema benki imetenga jumla ya Shilingi bilioni 250 kwa miaka mitano kutoa mikopo ya kati ya Sh. 500,000 hadi milioni 20 kwa kila kijana kulingana na gharama za kufika kwa mwajiri wake.

“Kigezo muhimu ni kuwa na mkataba au barua ya ajira iliyothibitishwa na wakala. Marejesho yatakuwa kwa miezi 24 na tunatoa kipindi cha neema cha miezi 2 kwa riba ya asilimia 15,” amesema Philemon.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira TRAA, Bw. Abdala Khalid amesema mkopo huo utawaepusha vijana na watu wasio na nia njema.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Zuhura Yunus amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,Ajira na Mahusiano inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya ajira ikiwemo Saudi Arabia, Oman, Qatar, Denmark na Ujerumani.

Mmoja wa wanufaika, Dickson Tadeo Mbaga amesema kupitia mkopo huo aliweza kugharamia visa, tiketi na bima. “Ninawasihi vijana wenzangu wachangamkie fursa hii,” amesema.

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana 530 wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni katika fani mbalimbali ikiwemo ujenzi wanalindwa na kazi zao zinakuwa zenye staha.

 

Droo Ya UEFA Yatoa Mapambano Makali, Barca, Man United Na Atletico Zapata Wapinzani Wazito

MONACO : Droo ya hatua ya  Ligi ya mabingwa (league phase ya UEFA Champions League) msimu wa 2026/27 imefanyika usiku wa kuamkia leo Agosti 28, 2026 mjini Monaco, huku timu 36 zikijua wapinzani wao katika hatua hiyo ya mashindano.

Kwa mujibu wa mfumo mpya wa mashindano hayo, kila timu itacheza jumla ya mechi nane dhidi ya wapinzani tofauti, nne nyumbani na nne ugenini. Timu hizo zimegawanywa katika pots nne, huku kila timu ikipangiwa wapinzani wawili kutoka kila pot.

Miongoni mwa mapambano yanayotarajiwa kwa hamu kubwa ni kati ya Barcelona na Manchester City. Barcelona pia imepangwa kukutana na Paris Saint-Germain (PSG), Aston Villa, Sporting CP, Feyenoord, Galatasaray, Como na Sabah.

Barcelona itamkaribisha Manchester City nyumbani, kabla ya kusafiri kwenda Paris kukutana na mabingwa watetezi, PSG. Pia itakuwa na safari kwenda Uturuki kucheza dhidi ya Galatasaray na Azerbaijan kukutana na Sabah.

Kwa upande mwingine, Atlético Madrid imepangiwa kukutana na wapinzani wakubwa, akiwemo Bayern Munich, Liverpool na Manchester United, jambo linalofanya ratiba yake kuwa miongoni mwa zinazotarajiwa kwa hamu kubwa katika hatua hiyo.

Mabingwa watetezi, PSG, wataingia msimu huu wakiwa na lengo la kutetea taji lao baada ya kuifunga Arsenal kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya msimu uliopita.

Hatua ya league phase ya Champions League msimu wa 2026/27 itaanza Septemba 8, 2026, huku timu nane zitakazomaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo zikifuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.

RATIBA YA LIGI YA MABINGWA ULAYA 2026/27

Hatua ya League Phase

  • Mechi za 1: 8–10 Septemba 2026

  • Mechi za 2: 13–14 Oktoba 2026

  • Mechi za 3: 20–21 Oktoba 2026

  • Mechi za 4: 3–4 Novemba 2026

  • Mechi za 5: 24–25 Novemba 2026

  • Mechi za 6: 8–9 Desemba 2026

  • Mechi za 7: 19–20 Januari 2027

  • Mechi za 8: 27 Januari 2027

Hatua ya Mtoano

  • Play-off: 16/17 na 23/24 Februari 2027

  • Hatua ya 16 Bora: 9/10 na 16/17 Machi 2027

  • Robo Fainali: 6/7 na 13/14 Aprili 2027

  • Nusu Fainali: 27/28 Aprili na 4/5 Mei 2027

  • Fainali: 5 Juni 2027, Estadio Metropolitano, Madrid.

WAPINZANI WA TIMU KUU

Barcelona

  • Manchester City

  • PSG

  • Aston Villa

  • Sporting CP

  • Feyenoord

  • Galatasaray

  • Como

  • Sabah

Manchester City

  • PSG

  • Barcelona

  • Sporting CP

  • Porto

  • Napoli

  • RB Leipzig

  • AEK Athens

  • Lens

PSG

  • Barcelona

  • Manchester City

  • Roma

  • Aston Villa

  • Galatasaray

  • Villarreal

  • Slovan Bratislava

  • Como

Real Madrid

  • Arsenal

  • Inter Milan

  • PSV

  • Roma

  • RB Leipzig

  • Shakhtar Donetsk

  • LASK

  • AEK Athens

Atlético Madrid

  • Bayern Munich

  • Manchester United

  • Liverpool

  • PSV

  • Fenerbahçe

  • Bodø/Glimt

  • Viking

  • Stuttgart

Bayern Munich

  • Arsenal

  • Atlético Madrid

  • Manchester United

  • Real Betis

  • Bodø/Glimt

  • Lille

  • Slavia Prague

  • Viking Stavanger

Liverpool

Arsenal

  • Real Madrid

  • Bayern Munich

  • Borussia Dortmund

  • Real Betis

  • Lille

  • Napoli

  • Slavia Prague

  • Sabah

MANCHESTER UNITED – CHAMPIONS LEAGUE 2026/27

  1. Bayern Munich — Nyumbani
  2. Atlético Madrid — Ugenini
  3. AS Roma — Nyumbani
  4. Sporting CP — Ugenini
  5. RB Leipzig — Nyumbani
  6. Villarreal — Ugenini
  7. Sabah FC — Nyumbani
  8. Como — Ugenini

Stori na Ashura Karimu | GPL- TUDACO

CCM KUMFUTA DKT. NCHIMBI UANACHAMA: JE, ANAKOMA MOJA KWA MOJA KUWA MAKAMU WA RAIS?

 

WAKILI PAUL KISABO ANAKUJA NA JIBU HILI  KUWA  HAPANA.

Ibara ya 47(4)(c) ya Katiba inaweka uanachama na udhamini wa chama cha siasa kama moja ya sifa za mtu kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais. Aidha, Ibara ya 47(4)(d) inamtaka mtu huyo kuwa na sifa zinazomwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hivyo, kuwa mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa ni sharti la kikatiba katika uteuzi wa Makamu wa Rais.

Hata hivyo, baada ya mtu kushika nafasi hiyo, mazingira ya kukoma kuwa Makamu wa Rais yanaainishwa na Ibara ya 50(2) ya Katiba. Kwa mazingira ya Dkt. Emmanuel Nchimbi, Ibara ya 50(2)(c) inaeleza kuwa Makamu wa Rais ataendelea kushika kiti chake hadi atakapojiuzulu, huku Ibara ya 50(2)(h) ikitambua kukoma kushika nafasi hiyo vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba.

Muhimu zaidi, Ibara ya 50(2) haisemi kwamba Makamu wa Rais anakoma kushika nafasi yake moja kwa moja anapopoteza uanachama wa chama kilichomdhamini.

Hii ni tofauti na nafasi ya Mbunge. Ibara ya 71(1)(e) ya Katiba inaeleza wazi kwamba Mbunge ataacha kuwa Mbunge iwapo ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwa mwanachama wake wakati alipochaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge.

Kwa hiyo, pale Katiba ilipotaka kupoteza uanachama wa chama kusababishe kupoteza nafasi ya kikatiba, imeeleza hivyo wazi. Masharti kama hayo hayajawekwa katika Ibara ya 50 kuhusu Makamu wa Rais.

Dkt. Nchimbi aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu tarehe 25 Agosti 2026 na kubainisha kwamba kujiuzulu kwake kutaanza kutumika tarehe 4 Septemba 2026.

Ibara ya 149(2) ya Katiba inaweka msingi muhimu kuhusu muda wa kuanza kutumika kwa kujiuzulu: pale mtu anapowasilisha kujiuzulu kwake kwa maandishi na kutaja tarehe ambayo kujiuzulu huko kutaanza kutumika, kujiuzulu huko kunakuwa na athari kuanzia tarehe aliyobainisha.

Kwa hiyo, kwa tafsiri ya masharti haya ya Katiba, kufutwa kwa uanachama wa CCM pekee hakumalizi moja kwa moja nafasi ya Dkt. Nchimbi kama Makamu wa Rais. Kwa kuwa katika barua yake alibainisha tarehe 4 Septemba 2026 kuwa ndiyo tarehe ya kuanza kutumika kwa kujiuzulu kwake, basi kujiuzulu huko kunaanza kuwa na athari za kikatiba tarehe hiyo.

Paul Kisabo

Wakili

Ayra Starr Aandika Historia Billboard, “Starrgirl” Yaingia Namba 4 Duniani

Mwimbaji wa Nigeria, Ayra Starr, ameendelea kuonyesha nguvu ya muziki wa Afrika katika soko la kimataifa baada ya album yake mpya “Starrgirl” kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard World Albums Chart.

Mafanikio hayo yanaifanya “Starrgirl” kuwa miongoni mwa miradi iliyofanya vizuri kwenye chati hiyo, huku Ayra Starr akiendelea kujenga jina lake katika soko la muziki duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ayra Starr kuingia kwenye Billboard World Albums Chart kupitia album yake kama msanii wa solo, hatua inayochukuliwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika safari yake ya muziki pamoja na kuongeza heshima kwa muziki wa Nigeria.

Album hiyo ilitolewa rasmi Agosti 14, 2026, kupitia Mavin Records na Republic Records, ikiwa ni album yake ya tatu ya studio.

“Starrgirl” inafuatia album zake mbili zilizotangulia, “19 & Dangerous” iliyotoka mwaka 2021 na “The Year I Turned 21” iliyotolewa mwaka 2024.

Album hiyo ina jumla ya nyimbo 16, huku Ayra Starr akiwashirikisha baadhi ya majina makubwa kutoka Nigeria na kimataifa, akiwemo Wizkid, Rema, ZAYN, Leon Thomas, kwn, Theodora na Danny Ocean.

Miongoni mwa nyimbo zinazopatikana kwenye album hiyo ni “Gimme Dat” akiwa na Wizkid, “Who’s Dat Girl” akiwa na Rema na “Heaven Baby” akiwa na ZAYN.

“Starrgirl” Yawa Mbele ya Album ya Tyla

Katika Billboard World Albums Chart, “Starrgirl” imeingia katika nafasi ya nne, ikiwa nyuma ya miradi mitatu ya K-pop.

Nafasi ya tano imechukuliwa na album “APOP” ya msanii wa Afrika Kusini, Tyla, hivyo Ayra Starr ameweka “Starrgirl” mbele ya album hiyo katika chati.

Mafanikio hayo yamekuja ndani ya muda mfupi tangu album hiyo itoke, jambo linaloendelea kuongeza uzito wa Ayra Starr katika muziki wa Afrobeats na soko la muziki la kimataifa.

Kwa kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard, Ayra Starr anaendelea kuthibitisha kuwa wasanii wa Afrika wana uwezo wa kushindana katika majukwaa makubwa ya muziki duniani na kuvuka mipaka ya bara hilo.

Stori na Razaku Ramadhan | GPL – TUDACO

Cardi B Avamia Jalada la Vogue Arabia, Aonyesha Mvuto wa Kiarabu

Msanii wa kimataifa kutoka Marekani, Cardi B, amepewa nafasi ya kipekee kwenye jalada la toleo la Septemba 2026 la Vogue Arabia, katika picha iliyozua gumzo kutokana na mtindo wake wa kipekee wenye mguso wa utamaduni wa Kiarabu.

Jalada hilo, lililotolewa Agosti 27, 2026, linamuonyesha Cardi B akiwa amevalia vazi la kifahari lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na kijani, huku akiwa ameshikilia tufaha.

Kinachovutia zaidi ni ujumbe ulioandikwa kwenye jalada hilo, “Assalamu Alaikum, Cardi B”, ambao umeongeza mvuto wa picha hiyo na kuonyesha namna msanii huyo anavyoendelea kuhusishwa na utamaduni wa eneo la Arabia.

Katika toleo hilo, Vogue Arabia imemzungumzia Cardi B kwa upana, ikigusa safari yake ya muziki, mitindo, umaarufu pamoja na maisha yake nje ya jukwaa akiwa mama.

Jarida hilo limemuelezea kama msanii mwenye uwezo mkubwa wa kubadilika kimtindo bila kupoteza utambulisho wake.

Cardi B naye ameonyesha furaha yake kupitia mitandao ya kijamii, ambapo amewashukuru Vogue Arabia pamoja na mpiga picha na mkurugenzi wa ubunifu Szilveszter Makó kwa kazi hiyo.

Mwonekano wake umeendelea kuzungumziwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimpongeza kwa kuonekana tofauti na vile walivyozoea kumuona kwenye matukio mbalimbali.

Cardi B si mgeni katika eneo la Mashariki ya Kati. Amewahi kutembelea Saudi Arabia na kutumbuiza katika tamasha la MDLBEAST Soundstorm jijini Riyadh.

Safari hiyo pia ilimpa nafasi ya kueleza hisia zake kuhusu watu na utamaduni wa Saudi Arabia, huku akionyesha kuvutiwa na baadhi ya vipengele vya utamaduni huo.

Kwa jalada hili la Vogue Arabia, Cardi B anaendelea kuonyesha kuwa ushawishi wake hauishii kwenye muziki pekee, bali pia unaendelea kukua katika mitindo, utamaduni na burudani ya kimataifa.

Stori na Nasra Kassim | GPL – TUDACO

Mambo 12 Usiyoyajua Kuhusu Ndejembi Hadi Kuteuliwa Kugombea Umakamu wa Rais – Video

Deogratius John Ndejembi ni mwanasiasa wa Tanzania kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Nishati.

Deogratius John Ndejembi ni mwanasiasa wa Tanzania kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Nishati.

Deogratius John Ndejembi ni mwanasiasa wa Tanzania kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa zinazopatikana katika wasifu wa Bunge, Ndejembi alisoma:
1988–1995: Cannon Andrea Mwaka Primary School.
1996–1998: Jamhuri Secondary School/Kigurunyembe Secondary School.
2002–2004: Merton College, ambako alipata elimu ya Advanced Secondary.
2006–2009: University of Lincoln, Uingereza, akisoma International Relations na kupata Shahada ya kwanza.
2009–2012: Institute of Administrative Management, ambako alipata Advanced Diploma.
Pia wasifu wa Bunge unaonyesha kuwa aliwahi kuwa kwenye masomo ya uzamili katika University of Cumbria kuanzia 2019.

Taarifa zinazoeleza tarehe yake ya kuzaliwa zinamtaja kuwa alizaliwa 12 Julai 1983. Hata hivyo, tarehe hiyo haionekani katika sehemu ya taarifa za jumla kwenye wasifu wa sasa wa Bunge, hivyo ni vizuri kuitaja kama taarifa iliyoripotiwa, si kama jambo lililothibitishwa moja kwa moja na wasifu huo

Safari yake ya kisiasa na kiuongozi imejengwa katika uzoefu wa muda mrefu ndani ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi, huku akiwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali kabla ya kupewa dhamana ya kusimamia sekta ya nishati.

1. Ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe wa CCM
Deogratius Ndejembi ni mtoto wa Mzee Pancras Mtemi Ndejembi, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wakongwe na wenye ushawishi ndani ya CCM mkoani Dodoma.

Mzee Pancras Mtemi Ndejembi alihudumu kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma kwa miaka 25, kuanzia mwaka 1982 hadi 2007, kipindi kirefu ambacho kilimfanya kuwa sehemu muhimu ya historia ya siasa za CCM katika mkoa huo.

2. Baba yake alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM kitaifa
Mbali na uongozi wake mkoani Dodoma, Mzee Pancras Mtemi Ndejembi alikuwa na nafasi muhimu katika uongozi wa CCM Tanzania Bara.
Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa Mikoa yote ya Tanzania Bara, nafasi iliyompa ushawishi na jukumu la kushirikiana na viongozi wa chama kutoka mikoa mbalimbali.

Hivyo, Deogratius Ndejembi amekulia katika familia yenye historia ndefu ya utumishi wa umma na uongozi ndani ya CCM.

3. Safari yake ndani ya CCM
Ndejembi alianza kujihusisha na shughuli za CCM akiwa kijana. Wasifu wa Bunge unaonyesha kuwa:

2007–2017: alikuwa katika uongozi wa CCM ngazi ya Wilaya.
2008–2017: alikuwa Mjumbe wa Baraza la Taifa la UVCCM.
2012–2017: alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
2012–2022: alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la CCM.
2016–2020: alikuwa katika Kamati ya Siasa.
2017–2022: alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu – Wazazi.

Kwa hiyo, safari yake ya kisiasa haikuanza akiwa Waziri; alikulia ndani ya miundo ya CCM kwa miaka kadhaa kabla ya kufika kwenye nafasi za juu za Serikali.

4. Historia yake ya uongozi ndani ya Serikali
Kabla ya kuwa Waziri wa Nishati, Ndejembi amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwemo Ukuu wa Wilaya ya Kongwa kati 2016 hadi 2020, jambo lililomjengea uzoefu katika kusimamia masuala tofauti ya kitaifa.

Amewahi kuwa Naibu Waziri na baadaye Waziri katika maeneo mbalimbali ya Serikali.

5. Aliwahi kuwa Naibu Waziri TAMISEMI
Katika hatua za awali za safari yake ya uongozi wa Serikali, Ndejembi aliwahi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kati yam waka 2023 hadi 2024.

Nafasi hiyo ilimpa uzoefu wa moja kwa moja katika masuala ya Serikali za Mitaa na utekelezaji wa huduma za umma.

6. Aliwahi kusimamia masuala ya kazi, vijana na ajira
Mwaka 2024, Ndejembi alipewa dhamana ya kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Katika nafasi hiyo, alihusika na eneo muhimu linalogusa moja kwa moja mustakabali wa vijana na nguvu kazi ya taifa.

7. Aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi
Kabla ya kuhamia Wizara ya Nishati, Ndejembi pia aliwahi kuongoza **Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Akiwa Waziri wa Ardhi mwaka 2025, alisimamia sekta yenye changamoto kubwa zinazohusisha umiliki wa ardhi, migogoro ya ardhi, makazi na maendeleo ya miji.

8. Ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino
Mbali na majukumu yake ya uwaziri, Ndejembi ni Mbunge wa Jimbo la Chamwino tangu 2020, mkoani Dodoma.
Ubunge wake unampa nafasi ya kuwakilisha wananchi wa Chamwino katika Bunge na kushiriki katika mijadala kuhusu sera, sheria na maendeleo ya taifa.

9. Sasa anaongoza Wizara ya Nishati
Ndejembi kwa sasa anaongoza Wizara ya Nishati, sekta ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania nafasi ambayo aliteuliwa na Rais Samia mwaka huu 2026.

Nishati ina nafasi kubwa katika uzalishaji viwandani, biashara, kilimo, huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

10. Safari yake ya uongozi imepitia sekta tofauti
Kinachomtofautisha Ndejembi katika safari yake ya kisiasa ni uzoefu alioupata katika maeneo mbalimbali.

Kutoka TAMISEMI, Kazi, Vijana na Ajira, Ardhi hadi Nishati, amekuwa akipewa dhamana ya kusimamia sekta zenye umuhimu mkubwa kwa wananchi na maendeleo ya nchi.

11. Anaendelea kujenga historia yake mwenyewe ya kisiasa

Ingawa ametoka katika familia yenye historia kubwa ya uongozi ndani ya CCM, Ndejembi ameendelea kujenga safari yake mwenyewe katika siasa na utumishi wa umma.

12: Maisha yake ya kazi kabla ya siasa

Kabla hajawa mwanasiasa mkubwa, Ndejembi alifanya kazi katika sekta binafsi katika nafasi mbalimbali:
2012: Manager – A1 Outdoor
2012–2014: Head of Sales – Smile Communication
2014–2015: Zonal Manager – Tigo
2016: Head of Marketing – GSM Group
2016–2020: Mkuu wa Wilaya (District Commissioner) katika Ofisi ya Rais.

Hii inaonesha kwamba kabla ya kuingia Bungeni alikuwa tayari na uzoefu katika biashara, mauzo, masoko, mawasiliano na utawala wa Serikali.

HITIMISHO
Historia ya uongozi wa baba yake, Mzee Pancras Mtemi Ndejembi, ni sehemu muhimu ya kuelewa mazingira ya kisiasa aliyokulia. Hata hivyo, nyadhifa ambazo Deogratius Ndejembi ameshika zimejenga wasifu wake binafsi ndani ya Serikali na siasa za Tanzania.
Deogratius John Ndejembi ana historia inayounganisha siasa za CCM, utumishi wa umma na uongozi wa kitaifa. Akiwa mtoto wa Mzee Pancras Mtemi Ndejembi, mwanasiasa mkongwe aliyelitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa muda mrefu mkoani Dodoma, amekulia katika mazingira yenye historia ya uongozi wa kisiasa.

Leo, Ndejembi anahudumu kama Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chamwino, akiendelea na safari yake ya uongozi katika sekta muhimu kwa uchumi na maendeleo ya Tanzania.

Safari kutoka Dodoma, kupitia nyadhifa mbalimbali za Serikali hadi kupewa dhamana ya kuongoza sekta ya nishati, inamfanya Deogratius Ndejembi kuwa mmoja wa wanasiasa ambao historia yao inafuatiliwa kwa karibu katika siasa za Tanzania.

MAKALA NA SIFAEL PAUL & NICOLAUS TRAC | GPL