Netanyahu Apata Pigo Jipya, Eisenkot Ateuliwa Kuunda Serikali

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

JERUSALEM: Rais wa Israel, Isaac Herzog, amemteua aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (IDF), Gadi Eisenkot, kujaribu kuunda serikali mpya kufuatia uchaguzi ulioacha bunge likiwa bila upande wowote wenye idadi ya kutosha ya viti kuunda serikali.

Uteuzi huo unamweka Eisenkot, ambaye ni mpinzani mkuu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, katika nafasi ya kujaribu kupata uungwaji mkono wa wabunge wengi ili kuunda serikali mpya.

Netanyahu, ambaye amekuwa kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Israel, anakabiliwa na changamoto ya kisiasa baada ya muungano wake wa vyama vya kidini na mrengo wa utaifa kushindwa kupata wingi wa viti katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27.

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (IDF), Gadi Eisenkot.

Chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu kilipata viti 27 kati ya 120 vya bunge la Israel, maarufu kama Knesset, huku muungano wake ukipata viti 53, pungufu ya viti 61 vinavyohitajika kuunda serikali yenye wingi wa wabunge.

Kwa upande mwingine, chama cha Yashar cha Eisenkot kilipata viti 21, huku muungano wake wa vyama vinne vya kisiasa ukikusanya viti 48.

Vyama viwili vinavyowakilisha jamii ya Waarabu nchini Israel vilipata jumla ya viti 19, hatua iliyovipa nafasi muhimu katika mazungumzo ya kuunda serikali.

Eisenkot ana siku 28 za kujaribu kuunda serikali, huku akiruhusiwa kuongezewa siku nyingine 14 iwapo atahitaji muda zaidi.

Miongoni mwa njia zinazoweza kumsaidia ni kuunda serikali ya wachache kwa kupata uungwaji mkono wa vyama vya Waarabu bila kuvijumuisha moja kwa moja ndani ya serikali, kushirikiana na vyama vya Wayahudi wa Kiorthodoksi au kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Netanyahu.

Hata hivyo, uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano hayo bado unakabiliwa na changamoto kutokana na tofauti za kisiasa zilizopo.

Eisenkot amekuwa akikosoa uongozi wa Netanyahu, hususan namna alivyoshughulikia operesheni za kijeshi katika Ukanda wa Gaza. Pia ameahidi kutoshiriki katika serikali inayoongozwa na Netanyahu.

Akiwa nje ya serikali, Eisenkot amekosoa pia vitendo vya vurugu vinavyofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina, ambavyo vimeongezeka tangu mwaka 2023.

Aidha, anapinga ushiriki wa viongozi wa mrengo mkali wa kulia, Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich, katika serikali ya Netanyahu.

Eisenkot, mwenye umri wa miaka 66, ni mtoto wa wahamiaji kutoka Morocco. Akifanikiwa kuwa waziri mkuu, atakuwa kiongozi wa kwanza wa Israel kutoka jamii ya Mizrahi, inayojumuisha Wayahudi wenye asili ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Aliwahi kuwa mkuu wa majeshi ya Israel na baadaye kuingia katika siasa mwaka 2022. Pia alihudumu kwa muda mfupi katika baraza la mawaziri la Netanyahu wakati wa vita vilivyoanza baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023.

Kwa upande wa familia, Eisenkot amepitia kipindi kigumu baada ya mwanawe mmoja na wapwa zake wawili kuuawa wakiwa wanapigana katika Ukanda wa Gaza.

Kabla ya kuingia kwenye siasa, Eisenkot alijijengea jina katika masuala ya usalama wa taifa, akiwahi kutekeleza mkakati wa kijeshi uliojulikana kama Dahiyeh Doctrine, unaohusisha matumizi ya nguvu kubwa za kijeshi kujibu mashambulizi.

Iwapo Eisenkot atashindwa kuunda serikali, mgombea mwingine anaweza kupewa nafasi hiyo. Endapo juhudi zote zitashindikana ndani ya muda uliowekwa, Israel italazimika kufanya uchaguzi mwingine.