Askari wa Miaka 33 Auawa Kazini, Aacha Mke na Mtoto wa Mwaka Mmoja, Wengine Watatu Wajeruhiwa

COLORADO, MAREKANI: Askari mmoja wa polisi ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika majibizano ya risasi na mtu mwenye silaha ndani ya basi katika mji wa Lakewood, jimbo la Colorado, nchini Marekani.

Askari aliyeuawa ametambuliwa kwa jina la Nic Graham, mwenye umri wa miaka 33, ambaye alikuwa akihudumu katika Idara ya Polisi ya Lakewood (LPD).

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, tukio hilo lilitokea Alhamisi, Novemba 5, 2026, majira ya saa 12:30 jioni kwa saa za eneo hilo, baada ya polisi kupokea taarifa kuhusu mtu aliyekuwa akitiliwa shaka kuhusika na tukio la kugonga na kukimbia, akijaribu kupanda basi karibu na makutano ya barabara za West Colfax Avenue na Wadsworth Boulevard.

Polisi walifika eneo hilo na kulikabili basi hilo, lakini hali ilibadilika baada ya mtuhumiwa kuanza kuwafyatulia risasi askari, ambao nao walijibu mashambulizi hayo na kusababisha majibizano makali ya risasi.

Katika tukio hilo, askari wanne walipigwa risasi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu. Hata hivyo, Graham alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata, huku askari wengine watatu wakiendelea kupata matibabu katika hali iliyotajwa kuwa thabiti.

Mtu aliyekuwa akishukiwa kufanya mashambulizi hayo naye aliuawa katika majibizano hayo, huku raia mmoja aliyekuwa eneo la tukio akijeruhiwa.

Vyombo vya habari vya nchini Marekani vimemtaja mtuhumiwa huyo kuwa Gabriel Steven Garcia, mwenye umri wa miaka 34.

Shuhuda wa tukio hilo, Teddy O’Brien, aliyezungumza na Shirika la Habari la Associated Press (AP), amesema alishuhudia magari kadhaa ya polisi yakilizunguka basi hilo kabla ya milio ya risasi kusikika.

Amesema mara tu baada ya askari kuingia ndani ya basi kupitia upande mwingine, milio ya risasi ilianza kusikika kutoka pande zote mbili.

Afisa wa Mawasiliano wa Polisi wa Lakewood, John Romero, amesema majibizano hayo yalianza ndani ya sekunde chache baada ya askari kumkaribia mtuhumiwa.

Katika kumbukumbu iliyotolewa na Idara ya Polisi ya Lakewood, Graham ameelezewa kuwa mhitimu wa mafunzo ya polisi mwaka 2019 ambaye aliwahi kufanya kazi katika kitengo cha uhalifu mkubwa na kushiriki kushughulikia jumla ya kesi 322 katika kipindi chake cha utumishi.

Graham alikuwa ametoka katika familia yenye historia ya utumishi wa polisi, ambapo baba yake alikuwa sajenti mstaafu wa polisi na mama yake alifanya kazi katika maabara ya uchunguzi wa matukio ya uhalifu.

Ameacha mke na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.

Idara ya Polisi ya Lakewood imesema imepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha askari huyo, huku ikieleza kuwa itasimama pamoja na familia yake katika kipindi hiki kigumu.