RC NYONGO AAGIZA TEMESA KUTUMIA MFUMO WA TIKETI ZA KIDIJITALI MAFIA

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, ameiagiza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuanzisha mfumo wa kidigitali wa kukata tiketi za kivuko cha Mafia–Nyamisati ndani ya siku 30, huku akieleza kuwa Serikali inatarajia kuhakikisha meli mpya inapatikana kabla ya Februari 2027, hatua zinazolenga kuimarisha ubora wa huduma za usafiri wa majini, kuondoa usumbufu kwa abiria na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Aidha, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mafia kufuatilia makusanyo ya mapato ya tiketi za kivuko hicho ili kubaini uwezekano wa upotevu wa fedha unaoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya mfumo wa zamani wa kukata tiketi kwa kuandika majina na kupokea fedha taslimu.

Mhe. Nyongo ametoa maagizo hayo wakati akisikiliza na kupokea kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Mafia, ambapo wananchi wameeleza changamoto ya kukosa uhakika wa safari kutokana na mfumo wa sasa wa tiketi unaowalazimu kufika bandarini na kuandika majina ili kujua kama watapata nafasi ya kusafiri.

Wananchi hao wameeleza kuwa mfumo huo umekuwa chanzo cha usumbufu, kuchelewa kwa safari na wakati mwingine kuwaacha abiria bila kusafiri licha ya kufika bandarini kwa wakati.

Akieleza changamoto hiyo, mwananchi wa Wilaya ya Mafia, Hasan Shomary Pango, amesema mfumo wa sasa umekuwa kikwazo kwa wananchi na wageni wanaoingia wilayani humo.

Kwa upande wake, mwananchi Jalala Iddi Omary amesema kivuko hicho kinakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya ndani, ikiwemo sehemu za lining, huku feni zikishindwa kufanya kazi vizuri, hali inayosababisha abiria kukosa mazingira bora na yenye faraja wakati wa safari. Aidha, ameomba Serikali kuhakikisha upatikanaji wa meli mpya ili kuondoa changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi wa Mafia.

Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amesema Serikali haitakubali mifumo ya kizamani iendelee kutumika wakati teknolojia ya kisasa inaweza kuboresha huduma na kuimarisha usimamizi wa mapato.

Amesema matumizi ya tiketi za kidigitali yataondoa mianya ya upotevu wa mapato, upendeleo na ubabaishaji katika utoaji wa nafasi za kusafiri, huku akisisitiza kuwa kila abiria anapaswa kupata huduma kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu.

Mhe. Nyongo amesisitiza kuwa mkoa na wilaya wataendelea kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo ili kuhakikisha huduma za kivuko cha Mafia–Nyamisati zinakuwa bora, salama na zenye ufanisi zaidi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kupatikana kwa meli mpya kabla ya Februari 2027, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto za usafiri wa majini kwa wananchi wa Mafia na kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wilaya hiyo.