Rais Samia Akutana na Balozi wa Afrika Kusini Anayemaliza Muda Wake Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Afrika Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe, aliyemaliza muda wake wa utumishi nchini.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 6, 2026, Balozi Mayende-Malepe amemshukuru Rais Samia, Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano na ukarimu alioupata katika kipindi chote cha uwakilishi wake nchini.

Balozi huyo amesema Tanzania imekuwa na nafasi ya kipekee katika kipindi chake cha utumishi kutokana na ukarimu wa Watanzania pamoja na uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini, ulioasisiwa wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.

“Tanzania ndiyo nchi niliyoifurahia zaidi kuhudumu katika kazi yangu ya ubalozi,” amesema Balozi Mayende-Malepe, akieleza kuwa anaondoka akiwa na kumbukumbu nzuri za maisha na utumishi wake nchini.

Aidha, Balozi Mayende-Malepe amepongeza mchango wa Tanzania katika masuala ya kikanda na kimataifa, akibainisha kuwa nchi hiyo imekuwa ikikaribisha makampuni ya Afrika Kusini kufanya biashara na kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Rais Samia amempongeza Balozi Mayende-Malepe kwa kutimiza vyema majukumu yake ya kibalozi nchini Tanzania na kumshukuru kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Rais Samia amesema biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini imeongezeka katika kipindi cha utumishi wa Balozi Mayende-Malepe, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia fursa zilizopo ili kuongeza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.

Balozi Mayende-Malepe amehudumu nchini Tanzania kwa miaka minne tangu alipowasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Agosti 25, 2022.