SERIKALI YATOA MILIONI 259 NISHATI SAFI MKOANI KAGERA

📌 Shule Kongwe ya Sekondari ya Kahororo na Bukoba zafungwa Mifumo ya Nishati Safi.

📌 Jumla ya shule 52 nchini kote zatajwa kunufaika na ruzuku hiyo ya Serikali.

Na Matukio App Kagara 

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imemwaga kiasi cha shilingi milioni 259.8 mkoani Kagera kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya majiko ya kisasa na mifumo ya gesi ya kupikia (LPG) katika shule tano za sekondari, ikiwa ni mkakati wa makusudi wa kulinda afya za walimu, wanafunzi, na kutunza mazingira.

Hatua hiyo imebainishwa, tarehe 13 Oktoba, 2026 na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage, wakati alipotembelea shule kongwe za sekondari za Kahororo na Bukoba mkoani humo ili kukagua mifumo hiyo mipya.

Mhandisi Advera alisema kuwa REA ilipewa maelekezo maalum ya kukuza na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Taasisi za Umma na Binafsi zinazohudumia makundi ya watu wengi kuanzia watu 100 na kuendelea. Alitaja shule zilizonufaika katika awamu hii ya kwanza mkoani Kagera kuwa ni pamoja na Ruhinda, Kahororo, Bukoba, Kabanga, na Nyakato ambazo zimefungiwa mifumo hiyo kupitia kampuni za Taifa Gas Ltd na Hunny G Investment. Kitaifa, takriban shule 52 za Tanzania Bara zimeshafaidika.

“Nitoe wito kwa Wakuu wa shule zote mkoani hapa kulinda na kuitunza miundombinu hii ya nishati safi, na kutoa taarifa haraka kwa watoa huduma waliounda mifumo hii pindi changamoto yoyote inapojitokeza,” alisisitiza Mhandisi Mwijage.

Akitaja mafanikio ya mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kahororo yenye wanafunzi 1,023, Bwana Omary Oghambage, alisema shule yake imepokea miundombinu yenye thamani ya shilingi milioni 82.5. Miundombinu hiyo inajumuisha majiko banifu 10 yenye sufuria za lita 200 kila moja, tani 16 za kuni mbadala, na mfumo wa gesi (LPG) wa tani 1.5.

Bwana Oghambage alibainisha kuwa mradi huo umesaidia kuokoa kiasi cha shilingi 560,000 kwa wiki zilizokuwa zikitumika kununua kuni za kawaida, huku ukiondoa adha ya moshi uliokuwa ukihatarisha afya za wapishi na kuongeza unadhifu na kasi ya maandalizi ya chakula.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukoba yenye wanafunzi 971, Bwana David Wilbard, alishukuru kwa kupatiwa miundombinu yenye thamani ya shilingi milioni 55.7 inayohusisha majiko banifu 9, tani 15.7 za kuni mbadala, na tani 1 ya mfumo wa gesi ya LPG.

“Uwezeshaji huu utaongeza tija kubwa kwa shule kwa kuwa chakula sasa kitaandaliwa katika mazingira safi, bora na salama, zaidi ya yote, muda wa maandalizi utakuwa mfupi sana ikilinganishwa na hapo awali,” alisema Bwana Wilbard huku akiahidi kuitunza miundombinu hiyo.

– MWISHO –