NA CHAUSIKU SAID -MATUKIO DAIMA MWANZA.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka wananchi kufahamu haki zao wanapohitaji huduma kutoka kwa watoa huduma, ikiwemo haki ya kuunganishiwa huduma ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.
Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la EWURA lililopo nje ya ofisi za mamlaka hiyo, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Musira amesema bado kuna baadhi ya wananchi ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu haki zao wanapopata huduma, hali inayofanya EWURA kuendelea kutoa elimu ili kuwasaidia wananchi kuzifahamu haki na wajibu wao.
Amesema wananchi wanapaswa kufahamu kuwa watoa huduma wana mikataba ya huduma kwa wateja ambayo inaeleza masharti mbalimbali, ikiwemo muda ambao mteja anatakiwa kuunganishiwa huduma baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa.
“Moja ya haki ambayo tumekuwa tukiielezea katika kipindi hiki cha Wiki ya Huduma kwa Wateja ni haki ya kuunganishiwa huduma ndani ya muda ambao mtoa huduma ameusema kwenye mkataba. Haki hiyo inampa mpokeaji wa huduma haki ya kupata fidia endapo itatokea hajapata huduma kwa muda uliotajwa kwenye mkataba wa huduma kwa wateja,” amesema Musira.
Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa wananchi kwa kuwa inawasaidia kutambua hatua wanazoweza kuchukua pale wanapohisi haki zao kama watumiaji wa huduma hazijazingatiwa.
Aidha, Musira amewataka wananchi wanaojihusisha na shughuli zinazodhibitiwa na EWURA kuhakikisha wanapata leseni zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imepunguza gharama za leseni kwa uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo hayo.
Amesema mwombaji wa leseni ya kituo cha mafuta kijijini hulipia Shilingi 50,000 kwa ajili ya maombi ya leseni na Shilingi 100,000 kwa ajili ya leseni ya kipindi cha miaka mitano.
Kwa mujibu wa Musira, gharama hizo ni tofauti na maeneo ya mijini ambapo maombi ya leseni ni Shilingi 500,000 na malipo ya leseni kwa kipindi cha miaka mitano ni Shilingi milioni moja.

