Wizara Yatoa Tamko la Dabi ya Simba na Yanga Oktoba 10, 2026

Global Publishers
October 8, 2026
0 views
0 Comments

Dar es Salaam. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema Uwanja wa Uhuru upo tayari kwa ajili ya kuandaa mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 10, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo Oktoba 7, 2026, maandalizi ya uwanja huo yamekamilika na hakuna sababu ya mchezo huo kuathiriwa kutokana na changamoto zinazohusu matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo vya timu.

Wizara imesema kuelekea mchezo huo, kanuni na taratibu zilizowekwa na Bodi ya Ligi kuhusu matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo, hususani masuala yanayohusu mazoezi ya timu, zimezingatiwa kikamilifu.

Aidha, imeelezwa kuwa Uwanja wa Uhuru hautatumika kwa mazoezi na timu yoyote kati ya Simba na Yanga, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa hakuna matakwa ya kifungu cha kanuni za mashindano ya ligi yatakayokiukwa.

Wizara imewataka mashabiki wa Simba na Yanga pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu, wenye amani na kuzingatia taratibu zilizowekwa kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

“Tunawashukuru kwa ushirikiano wenu na tunatawata maandalizi mema kuelekea mchezo wetu pendwa wa Dabi,” imesema Wizara katika taarifa hiyo.

Mchezo wa Simba dhidi ya Yanga unatarajiwa kuwa miongoni mwa michezo mikubwa ya msimu, huku macho ya mashabiki wa soka nchini yakielekezwa Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya Dabi hiyo ya Kariakoo.